Sunday, October 1, 2023

MADIWANI LINDI WAKANUSHA KUMKATAA MEYA.


Na Mwandishi wetu.

MADIWANI wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi mkoani Lindi wameshangazwa na waraka uliotumwa kwa Mkurugenzi wa Manispaa ukidai hauna imani na Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Frank Magali wakisema hawautambui na saini zinazoonekana humo hazikuwekwa kwa malengo hayo.


Wakizungumza kwa njia ya simu na Mwandishi wa habari hizi, baadhi ya madiwani hao wameonesha
kushangazwa kwao na madai hayo waliyoyaita ni ya uzushi unaosukumwa na
tamaa ya madaraka zaidi kuliko wanachokidai.

Waraka huo wa Septemba 26/2023 ambao  nakala yake tunayo ulikuwa na kichwa kisomekacho “Kutokuwa na imani na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi Mh.Frank R. Magali”.


Juma Lunda diwani wa Makonde Manispaa ya Lindi alisema licha ya jina lake kuorodheshwa kwenye waraka huo wa kumkataa Meya, lakini hana taarifa zozote za kina juu ya sababu za kufikia hatua hiyo.


“Sikiliza mwandishi, ninachokiona mimi ni kwamba, kuna badhi ya
madiwani walitumia fedha nyingi katika uchaguzi uliopita wakiwinda
nafasi ya U-Meya na wakaikosa, sasa wanachofanya ni kutapatapa tu,
maana kama huo mkopo waliousema, hakuna diwani asiyejua maana sisi
kamati ya Fedha tulihusika kwaniaba ya Madiwani” alisema Lunda ambaye
pia ni mjumbe wa kamati ya Fedha ya Manispaa ya Lindi.

Naye diwani wa Kata ya Rasibula bwana Abdallah Kikwei akizungumza na
Mwandishi wa habari hizi alisema Naibu Meya wa Manispaa hiyo Salum Ng’ondo ndiye kinara wa harakati hizo akidaiwa kumsaidia kigogo mmoja kuusaka Ubunge
jimbo la Lindi mjini.

Ng’ondo amekiri kuongoza kikosi cha madiwani na kuandika barua hiyo
wakimtaka Meya huyo kujiuzulu kwa madai ya kukiuka  kanuni mbalimbali
za uendeshaji wa Manispaa ya Lindi.

Kwa upande wake Meya Magali alisema madai hayo si ya kweli bali
yanachochewa na baadhi ya madiwani wanaotumika na wanasiasa wasio na
huruma na wanachi wa Lindi.

“Madiwani wetu wanahitaji ziara ya mafunzo (Tour), na katika vikao vyetu tulikubaliana bajeti ya shilingi Milioni 16, lakini madiwani wakaja na pendekezo la kwenda Dodoma, Bwawa la Mwalimu Nyerere na Ngorongoro ambako bajeti yake ni zaidi ya sh. Milioni 90.


“Nikawauliza pesa hizi zote haziwezi kutumika kutatua baadhi ya changamoto za wanachi kwenye kata zetu? Na je, Mkuu wa mkoa anaweza kuidhinisha matumizi haya makubwa ya fedha kwa ajili ya kutembea
tu”,alisema Magali.

Aidha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi Juma Mnwele licha
ya kukiri kupokea barua hiyo ambayo haikusainiwa, alisema ameshaijibu na kuwakabidhi wahusika na kuwataka wazingatie kanuni za kudumu za Halmashauri katika mchakato wa kumuondoa Meya na wala si kwa utaratibu huo waliofanya.

“Kuhusu Mkopo, Halmashauri ilipata Mkopo wa Mzunguko kwa Halmashauri
zote nchini kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi
tarehe 10.6.2023 pamoja na Halmashauri zingine za Kigamboni Chamwino
Kishapu na Maswa, hafla ilifanyika Dodoma chini ya Tamisemi na Ardhi”,alisema Mnwele na kuongeza.

“.Madai ya  bei ya viwanja vimewekwa na kuridhiwa na baraza la Madiwani, Kuhusu vikao, vikao vya Halmashauri huendeshwa kwa kuzingatia kanuni za kudumu za Halmashauri za mwaka 2014 kifungu 42(1) cha sheria za serikali za mitaa (mamlaka za miji) sura 288. Hakuna ukiukwaji wa kanuni uliotajwa wowote uliofanyika kwenye eneo hilo.


“Kikao cha Mkutano wa Mwaka kinatekelezwa ipasavyo kwa vile mambo na
hadidurejea zote zilizoainishwa kwenye kanuni hiyo vinatekelezwa bila
dosari yoyote”.

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Lindi bwana Bakari Bwatamu alisema
haamini kama walioandika barua hiyo kwa Mkurugenzi ni madiwani wa
Halmashauri ya Manispaa ya Lindi wanaotokana na CCM.

“Awali barua yenye saini kama hizo waliileta kwetu chama wakidai wanahitaji kukutana na Mkurugenzi. Sasa tena tunaona barua ileile yenye saini za watu walewale inaelekezwa kwa Mkurugenzi wakidai hawana imani na Meya”


Kwa muda mrefu madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi yenye majimbo ya Lindi na Mchinga wamekuwa katika misuguano na Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo kwa upande mmoja na Mkurugenzi wake kwa upande
mwingine wakidai kupunjwa posho na marupurupu mengine.

No comments:

Post a Comment