Wednesday, October 4, 2023

NG'OMBE WA BBT WAKO SALAMA - ULEGA

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema ng'ombe walio katika programu ya Jenga kesho iliyo bora (BBT) Mifugo, katika Kituo cha Shamba la Serikali Mabuki Mkoani Mwanza wako salama na vijana wanaendelea na shughuli zao za unenepeshaji wa ng'ombe hao.


Waziri Ulega amesema hayo alipotembelea katika kituo hicho kwa lengo la kuona maendeleo ya shughuli za unenepeshaji wa mifugo zinazoendelea kituoni hapo leo Oktoba 4, 2023.


Mhe. Ulega amesema pamoja na kutokea jaribio la wizi katika kituo cha Mabuki kilichopo Wilayani Misungwi Mkoani Mwanza ambalo lilizua taharuki, ng'ombe wote wako salama, huku akitumia nafasi hiyo kuushukuru uongozi wa Mkoa wa Mwanza, Wananchi na Vijana kwa ushirikiano na kazi kubwa wanayoifanya kituoni hapo.


Amesema kuwa Serikali ya Rais, Dkt. Samia mwaka huu itaendelea kuongeza vituo vingine vya BBT ili vijana wengi zaidi wapate fursa ya kupata elimu hiyo na waweze kujikwamua kimaisha.


Ameongeza kuwa mwaka huu wanakwenda kuongeza vituo vingine kama hivyo katika mikoa ya Tabora, Morogoro, Pwani na Arusha.


Awali, Waziri Ulega ameielekeza Idara ya masoko iliyopo katika Wizara yake kuhakikisha inaendelea kutafuta masoko ya ng'ombe hao wa BBT ili vijana hao waweze kuendelea kufanya biashara na kutimiza lengo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kutengeneza fursa nyingi za ajira kwa vijana nchini. 




No comments:

Post a Comment