Friday, October 27, 2023

DKT. TULIA ACKSON ACHAGULIWA KUWA RAIS WA MABUNGE DUNIANI.

 

Spika wa Bunge la Jamahuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson amechaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) katika uchaguzi uliofanyika leo Oktoba 27, jijini Luanda nchini Angola.


Dkt. Ackson amechaguliwa kwa kupata kura 172 kati ya kura 303 zilizopigwa na anarithi mikoba ya rais aliyemaliza muda wake, Duarte Pacheco kutoka Ureno aliyekuwa rais wa IPU kwa mihula mitatu.


Tulia alipata ubunge nchini Tanzania mwaka 2015, na baadae kuchaguliwa kuwa Naibu Spika na hatimae Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Akizungumza mara baada ya uchaguzi huo, Dk Tulia Ackson amesema, “Asanteni kwa kuniamini kwa kunichagua, naipokea nafasi hii kwa unyenyekevu huku nikitambua majukumu yote yanayoambatana na nafasi hii, napenda kuwathibitishi tena kuwa,  jitihada zangu za kufanya kazi mkono kwa mkono na wote ili kuifanya IPU iwe na ufanisi zaidi, yenye kuwajibika na uwazi.”

Wabunge wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) walipiga kura ya siri, huku kukiwa na wagombea wanne, ambapo rais mpya Dkt. Tulia Ackson, alipata kura 172 sawa na asilimia 57 ya kura zote zilizopigwa, huku wagombea wengine ni Catherine Gotani Hara kutoka Malawi, aliyepata kura 61, Adji Diarra Mergane Kanouté, kutoka Senegal, aliyepata kura 59, na Marwa Abdibashir Hagi kutoka Somalia aliyeambulia  kura 11. Wote wakiweka historia ya kuwa wabunge wanawake kutoka Afrika, waliogombea nafasi hiyo.

Dkt. Tulia Ackson anakuwa Rais wa 31 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na anakuwa mwanamke wa tatu kushika nafasi hiyo baada ya Najma Heptulla kutoka India (1999–2002) na Gabriela Cuevas kutoka Mexico (2017–2020), pia Dkt. Dulia Ackson anakuwa mwanamke wa kwanza kutoka Afrika kushika nafasi hiyo.



Umoja wa Mabunge Duniani IPU inachagua Rais baada ya kila miaka mitatu na lazima anaechaguliwa awe mbunge katika kipindi atakachokuwa Rais.
Rais mpya wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) Dkt. Tulia Ackson akihutubua mara baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa IPU.
Dkt. Tulia Ackson akipongezwa mara baada ya kutangazwa mshindi.
Baadhi ya wabunge wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) wakimpongeza Dkt. Tulia Ackson kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Umoja huo.







No comments:

Post a Comment