Rais mstaafu wa awamu ya nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amewapongeza waandaaji wa Tamasha la 40 la kimataifa la sanaa na utamaduni kwa kuweka utaratibu wa kuwatembeza wageni kwenye vivutio mbalimbali ikiwemo historia ya mji wa Bagamoyo.
Dkt. Jakaya alitoa pongezi hizo wakati wa kufunga Tamasha la 40 la kimataifa la sanaa na utamaduni Tarehe 30 Oktoba 2021, katika viwanja vya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) ambapo alisema historia ya Bagamoyo ni kubwa sana na wananchi wa ndani na nje ya Bagamoyo, na wageni kutoka nje ya nchi wanapaswa kuijua historia hiyo.
Alisema kutokana na umuhimu wa historia ya Bagamoyo, imempelekea Rais Samia Suluhu Hassan kufika Bagamoyo wakati wa maandalizi ya filamu ya Royal tour na kwamba hiyo ni heshima kubwa kwa Bagamoyo ambapo wizara husika inapaswa kuendelea kuielezea historia ya Bagamoyo kwa wageni.
Aliongeza kwa kusema kuwa, ili wageni waweze kuvutiwa kusikiliza na kuelewa historia hiyo, ni vyema wakapatikana watembeza watalii wenye uwezo wa kuelezea historia halisi ya Bagamoyo yenye kueleweka kwakuwa maelezo mazuri yanamvutia msikilizaji na kupata hamu kutaka kujua zaidi.
Aidha, alipongeza maandalizi yaliyofanyika katika Tamasha hilo la 40 kwa namna lilivyofana kwa kuwakusanya wasanii mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi ambapo kila mmoja alionyesha uwezo wake jukwaani huku wahudhuriaji wakiwa na furaha kutokana na burudani zilizokuwa zikitolewa.
Alisema katika nchi yetu swala la utamaduni ni muhimu sana kwakuwa linawarudisha watanzania kwenye burudani zao za asili na kwamba siku zote anaekataa asili yake ni mtumwa.
Aliendelea kusema kuwa, kutokana na umuhimu huo ndiomana seikali ya Tanzania kuanzia awamu ya kwanza hadi sasa wizara ya utamaduni ilikuwepo na bado ipo ili watanzania waone umuhimu wa kutunza utamaduni wao.
Alisema utamaduni ni kielelezo cha utashi na uhai wa Tanzania hivyo kila panapofanyika Tamasha watanzania wanaendelea kukumbushana na kusisitiza umuhimu wa utamaduni katika jamii yetu na Taifa kwa ujumla.
Alisema Rais Samia ameendelea kutambua na kusisitiza umuhimu wa utamaduni kwakuwa utamaduni unabeba ujumbe halisi wa jamii husika kwa kipindi hicho.
Rais mstaafu wa awamu ya nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, (katikati) Naibu waziri wa Utamaduni , Sanaa na Michezo, Pauline Philipo Gekul, (kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge (kulia) wakiangalia vikundi vya sanaa wakati wa kufunga Tamasha la 40 la kimataifa la sanaa na utamaduni lilifanyika katika viwanja vya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) Tarehe 30 Oktoba 2021.