Na Mwamvua Mwinyi,Mkuranga.
MKOA wa Pwani ,tayari umeuza tani 19,815 ambazo zimeingiza zaidi ya
bilioni 39 tofauti na msimu uliopita ambapo uliuza tani 13,000 na kupata
bilioni 33.##
Mkoa huo umejiwekea lengo la kuuza tani 25,000 hadi 30,000 kwa msimu huu
ambao minada yake ya korosho ikiwa bado inaendelea .
Mkuu wa Mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo ,aliyasema hayo Mkuranga
,wakati akizungumzia changamoto na mafanikio waliyoyapata msimu wa korosho
2017/2018 .
Alieleza ,mbali ya hayo wakulima wa korosho mkoani Pwani wakiwa bado
wanadai zaidi ya bilioni tano.
Mhandisi Ndikilo alisema ,kuuza tani 19,815 hadi sasa ni mwanzo mzuri wa
kufikia malengo yao waliyojiwekea msimu huu.
Alisema ,hatua hiyo imetokana na serikali kutoa pembejeo bure katika
msimu huu na mfumo wa stakabadhi ghalani.
Alibainisha ,licha ya mafanikio hayo lakini kuna changamoto zimejitokeza
tangu kuanza kwa minada mwaka huu ikiwemo uhaba wa magunia .
Kero nyingine ni ile iliyojitokeza sasa ya kuchakachua ubora wa korosho
unaofanywa na baadhi ya vyama vya msingi vya ushirika (Amcos).
“Changamoto ya magunia inaweza kuwa historia endapo tutakubaliana kwa
kukaa na mikoa ya Lindi na Mtwara ili kuhamasisha wawekezaji waje wawekeze
kiwanda cha magunia lengo likiwa ni kukabiliana na tatizo hili” alifafanua .
Akizungumzia kuhusu tatizo la ubora wa korosho, mhandisi Ndikilo ,alisema
baadhi ya Amcos zimejiingiza kwenye kuhujumu minada hiyo kwani baadhi yao
wameweka michanga na mawe kwenye magunia ya korosho .
Alisema huo ni wizi,uhujumu uchumi na kuaibisha sifa ya nchi ya Tanzania
nje ya nchi kwani magunia hayo yangefika India na nchi nyingine ingekuwa aibu
na fedheha.
Kutokana na upuuzi huo ndio maana nimeamua kutoa maagizo kuwa Amcos 10
zilizojihusisha na ubabaishaji huo viongozi wake wakamatwe na kuhojiwa.
Kwa mujibu wa mhandisi Ndikilo ,kuwepo kwa maghala makubwa itainua soko
la korosho msimu ujao na kuondoa ubabaishaji wa maghala ya vichochoroni
yanayoleta dosari .
Alisema mfumo wa stakabadhi ghalani ni mkombozi kwa wakulima hivyo
anawashangaa wale wanaobeza na kuyumbisha mfumo huo.
Mhandisi Ndikilo ,aliwataka wakulima wa korosho
kuacha kukubali kurubuniwa na madalali ama wanunuzi wachache hali
inayosababisha kukosa mapato kulingana na korosho zao.
Serikali mkoani humo imewatoa shaka wakulima wa korosho ambao bado
hawajalipwa fedha zao na kudai itasimamia makampuni na wanunuzi kulipa kwa
wakati na changamoto zinazojitokeza.