Tuesday, August 8, 2023

MAKAMU WA RAIS DKT. MPANGO AWAASA WAZALISHAJI WA ZAO LA KAHAWA WA NCHI ZA AFRIKA.

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa nchi za Afrika wanachama wazalishaji wa zao la kahawa kuwekeza zaidi katika kupata vifaa na mashine za kisasa za uchakataji wa zao hilo ili kuongeza thamani ya kahawa kabla ya kuuzwa nje ya bara hilo.

 

Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akihutubia viongozi na wadau mbalimbali wa sekta ya kahawa Barani Afrika wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi 25 za Afrika Wanachama Wazalishaji wa Zao la Kahawa unaofanyika Kampala nchini Uganda. Amesema ili kuinua sekta hiyo ni muhimu sekta binafsi kwa kushirikiana na serikali kuweka msisitizo katika kuongeza thamani ya zao hilo pamoja na kuwekeza katika vifungashio bora.

 

Aidha Makamu wa Rais amewasihi wakulima wa zao hilo kujikita katika kilimo bora na cha kisasa kwa kutumia teknolojia rafiki ili kuhakikisha sekta hiyo inakua na mchango mkubwa kwa wananchi na uhifadhi wa mazingira.

 

Pia Makamu wa Rais ametoa rai kwa Shirika la Kimataifa la Kahawa Afrika (IACO) kuharakisha maendeleo ya kituo cha ubora cha zao la kahawa nchini Tanzania kama ilivyokubaliwa hapo awali na kuahidi kwamba serikali ya Tanzania itatoa ushirikiano wote unaohitajika katika kufanikisha jambo hilo.

 

Makamu wa Rais ameeleza kwamba licha ya bei ya kahawa kuwa na mwenendo mzuri kwa kipindi kirefu bara la Afrika limeendelea kubaki nyuma kwa kuwa na asilimia 12 tu ya uzalishaji duniani huku mwelekeo katika ukanda huo ukiendelea kupungua kwa kasi. Amesema ni muhimu kutatua changamoto zilizopo na kuchukua hatua kuhakikisha fursa ya uzalishaji kahawa inatumika vema kwa kuzingatia kuongezeka kwa bei ya zao hilo duniani na uwepo wa soko la watu bilioni 1.4 lililopo Afrika.

 

Akitaja hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuimarisha sekta ya kilimo ikiwemo kilimo cha kahawa, Makamu wa Rais amesema bajeti ya kilimo imeendelea kuongezeka katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo ya kifedha, serikali inatoa ruzuku katika mbolea pamoja na kuongeza usambazaji bure wa mbegu za kiwango cha juu za zao la kahawa. Ameongeza kwamba juhudi zingine ni pamoja na kuiwezesha benki ya maendeleo ya kilimo na kuhakikisha utoaji wa mikopo ya kilimo katika riba isiozidi asilimia tisa.

 

Aidha Makamu wa Rais amesema Tanzania imeendelea na jitihada za kuhakikisha wanawake na vijana wanashiriki katika mnyororo wa thamani katika uzalishaji wa zao la kahawa ikiwemo uanzishwaji wa Chama Cha Wakulima Wanawake wa Kahawa (TAWOCA), kuwawezesha vijana kimafunzo ili kuzalisha kahawa bora na kufanya biashara ya zao hilo.

Makamu wa Rais amesema kupitia hatua zilizochukuliwa, mafanikio mbalimbali yamepatikana ikiwemo kuongezeka kwa uzalishaji wa zao la kahawa kwa asilimia 19 kutoka tani elfu 66.5 mwaka 2018/2019 hadi tani elfu 82.5 mwaka 2022/2023. Pia kuongezeka kwa fedha za kigeni kutokana na uuzwaji wa zao hilo kutoka dola za marekani milioni 123.2 mwaka 2018/2019 hadi dola milioni 235.6 mwaka 2022/2023 huku eneo la uzalishaji likiongezeka kutoka hekta 218,966 mwaka 2018/2019 hadi hekta 265,000 mwaka 2022/2023.

 

Mkutano wa Pili wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi 25 za Afrika Wanachama Wazalishaji wa Zao la Kahawa umebeba kauli mbiu isemayo “Mageuzi katika sekta ya kahawa kwa kuongeza thamani”. Mkutano huo umelenga kuendelea kusimamia ajenda ya kahawa katika orodha ya bidhaa za kimkakati chini ya umoja wa Afrika kupitia mpango wa Maendeleo ya Afrika (AU Agenda 2063). Pia kuongeza thamani na matumizi ya ndani ya zao hilo, kupanua wigo wa biashara ya kahawa kupitia eneo huru la biashara Barani Afrika (AfCFTA) pamoja na kubadilisha uzoefu kuhusu za mabadiliko ya tabianchi na UVIKO19 katika sekta ya Kahawa.

 

Aidha Mkutano huo ni mwendelezo wa Mkutano wa kwanza uliofanyika Mei mwaka 2022 Jijini Nairobi nchini Kenya huku Mkutano wa Tatu ukitarajiwa kufanyika nchini Tanzania.

 

Kando ya mkutano huo Makamu wa Rais amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Uganda Mheshimiwa Jessica Alupo.

 

Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais

08 Agosti 2023

Kampala – Uganda.



PROFESA MKENDA ATOA MAELEKEZO KWA TAASISI KUENDELEZA UBUNIFU


 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ametoa maelekezo kwa taasisi mbalimbali nchini kuendeleza bunifu na kuziingiza sokoni ili ziweze kushindana katika soko la dunia.


Akizungumza baada ya kutembelea banda la Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya, Profesa Mkenda amesema maendeleo ya teknolojia yanayofanywa na taasisi za Serikali ni makubwa.


“Tunachohitaji vile vilivyogundulika visiwe tu vya maonesho mwaka huu au mwakani, tunataka tuvione vinaingia sokoni vinaanza kuuzwa,” amesema Profesa Mkenda.


Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu Veta, Anthony Kasore, amesema wanawafundisha vijana ili kuwaandaa kuingia kwenye soko la ajira katika nyanja mbalimbali za uwekezaji, viwanda, kilimo na ufugaji.

Tumekuja na bunifu kwa ajili ya kuwasaidia wakulima kufanya shughuli zao za kilimo na ufugaji kwa urahisi,” amesema Kasore.


Kwa mujibu wa Kasore, kupitia mradi wa sumu kuvu vijana 420 kutoka katika wilaya 20 wamepatiwa ujuzi wa kutengeneza vihenge ambapo Serikali itawapatia vifaa bure kuweza kujiajiri.


Kaimu mkurugenzi huyo, amesema pia ujenzi wa vyuo vipya katika wilaya 64 na kimoja katika Mkoa wa Songwe utaongeza wigo wa mafunzo ya ufundi stadi kutolewa kote nchini.


DKT. MPANGO ASHIRIKI MKUTANO WA PILI WA WAKUU WA NCHI NA SERIKALI WA NCHI 25 ZA AFRIKA, WANACHAMA WAZALISHAJI WA ZAO LA KAHAWA

 


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi 25 za Afrika Wanachama Wazalishaji wa Zao la Kahawa unaofanyika Kampala nchini Uganda leo tarehe 08 Agosti 2023.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiongozana na viongozi mbalimbali wa Afrika kuelekea katika Ukumbi wa Mikutano wa Speke Munyonyo uliopo Kampala nchini Uganda kushiriki Mkutano wa Pili wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi 25 za Afrika Wanachama Wazalishaji wa Zao la Kahawa leo tarehe 08 Agosti 2023.




Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiungana na viongozi wengine pamoja na wadau wa zao la kahawa katika kuimba wimbo wa Taif awa Uganda wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi 25 za Afrika Wanachama Wazalishaji wa Zao la Kahawa unaofanyika Kampala nchini Uganda leo tarehe 08 Agosti 2023.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango na Rais wa Uganda Yoweri Museveni wakifuatilia mawasilisho mbalimbali wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi 25 za Afrika Wanachama Wazalishaji wa Zao la Kahawa unaofanyika Kampala nchini Uganda leo tarehe 08 Agosti 2023.



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa Afrika mara baada ya ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi 25 za Afrika Wanachama Wazalishaji wa Zao la Kahawa unaofanyika Kampala nchini Uganda leo tarehe 08 Agosti 2023.


VIJANA 70 WAFUNGISHWA NDOA NA AL-HIKMA

Jumla ya vijana 70 wasiokuwa na uwezo wa kutoa mahari wamefungishwa ndoa kwa pamoja jijini Dar es Salaam kwa msaada wa Taasisi ya Al hikma Foundation.


Ndoa hizo zimefungwa kwenye ukumbi wa DYCCC, Chang'ombe na kushuhudiwa na maelfu ya watu pamoja na viongozi mbalimbali akiwemo Naibu Spika wa bunge la Tanzania, Mussa Azan Zungu, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi na Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Sheikh Dkt. Abubakar Zubeir Bin Ally


Mkurugenzi wa Taasisi iliyoratibu ndoa hizo, Al Hikma Foundation, Sheikh Nurdin Kishki amesema kilichowasukuma kuwasaidia vijana hao kwa kuwatolea mahali ni kutokana na gharama za ndoa kuwa juu kulinganisha na uwezo wa maisha yao...


"Tulipokea ujumbe zaidi ya 1000 baada ya kutangaza jambo hili mwezi wa nne, waliojaza fomu za kutaka kusaidiwa kuoa walikua zaidi ya 200 lakini baada ya usaili tumepata 70 ambao leo wameoa", alisema Kishki.


Moja ya vigezo muhimu vilivyotumika kuwapata vijana hao ni nia yao ya kuoa, uwezo wa kumudu ndoa na wale ambao hawaongezi mke wa pili.


Mbali na kupewa nasaha za uvumilivu kwenye ndoa kutoka kwa viongozi karibu wote walioshiriki, mmoja wa vijana aliyeoa leo, Ally Ismail Mwaluka, mlemavu pekee katika kundi la waliooa anasema ni ndoto iliyotimia.


"Sikutarajia, wakati mwaka unaanza sikua hata na ndoto ya kuoa, leo nmeoa bure na nimepata vitu vingine juu kutoka kwa viongozi wa serikali, bajaji, mafuta ya bajaji kwa mwaka mzima na fedha mbalimbali, sina cha kusema namshukuru Mungu", alisema Ally.


Vijana hao wametoka mikoa 12 ya Tanzania bara na Visiwani na mahari waliozosaidia zimegharimu shilingi zaidi ya milioni 70 za kitanzania.



 

WAZIRI JAFO AWAASA WAKULIMA

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akizungumza wakati alipokuwa akitembelea mabanda ya Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Kati yanayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mjini Morogoro leo Agosti 08, 2023.

........................

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ametoa wito kwa wakulima na wafugaji kuendelea kutunza mazingira ili shughuli ziwe endelevu.


Amesema hayo wakati akitembelea mabanda ya Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Kati yanayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mjini Morogoro leo Agosti 08, 2023.


Dkt. Jafo alisema kuwa endapo mazingira yataharibiwa ni dhahiri kuwa sekta za kilimo na ufugaji zitaathirika kutokana na ukame uliosababishwa na shughuli za kibinadamu.


“Ndugu zangu tunapokata miti ovyo na kufanya shughuli za kibinadanu kwenye vyanzo vya maji tunasababisha mito yetu kukauka na mito ikikauka kilimo chetu kinachotegemea mvua hakitakuwa na tija, nawaomba tutunze mazingira,” alisisitiza.


Aidha, Waziri Jafo alipongeza waandaaji wa maonesho hayo yanayojumuisha mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam na Pwani maandalizi mazuri ambayo yanatumika kutoa elimu kwa makundi hayo na wananchi kwa ujumla.


Alibainisha kuwa ili kukabiliana na changamoto ya ukame Serikali ya Awamu ya Sita imejipambanua katika uwekezaji kwenye kilimo na mifugo kwa kuhakikusha sekta hizo mbili zinakuwa na tija na manufaa.


Hali kadhalika Waziri Jafo ametoa wito kwa Watanzania kuungana kwa pamoja na kuhakikisha wanalinda rasilimali zilizopo hapa nchini ili ziwe na manufaa kwa jamii nzima.


Kwa upande Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima amesema changamoto ya ukosefu wa mvua inatokana na ukataji miti holela hasa katika maeneo ya milima.


Hivyo, amesisitiza kuwa kila mwananchi mkoani humo ashiriki kikamilifu katika zoezi la upandaji miti na huku akiwataka wakulima kuacha kulima kwa kuharibu mazingira.


“Miti imekatwa ndio maana kuna changamoto ya athari za mazingira mvua hazinyeshi kwa wakati au hazinyeshi kabisa na kusababisha mtu anashindwa kupanda na akipanda anapata hasara,“ alisema Malima.


Ili kukabiliana na hali hiyo alisema Kanda ya Mashariki wamekuja na mkakati wa kutengeneza ajenda ya kilimo itakayomsaidia mkulima katika kufanya kilimo endelevu na chenye mafanikio












MAGAZETI YA LEO TAREHE 08 AGOSTI 2023.

 














Monday, August 7, 2023

RAIS DKT SAMIA AWASILI MKOANI MBEYA KWAAJILI YA SIKUKUU YA NANENANE


 Rais wa Jamhuri ya Muungano *Dkt, Samia Suluhu Hassan* leo August 07, 2023 amewasili *Uwanja wa Ndege wa Songwe* kwaajili ya kushiriki maadhimisho ya Siku ya wakulima *(Nanenane)* yatakayofanyika Siku ya Kesho *August 08* Mkoani Mbeya.


Baada ya kuwasili *Mhe. Samia* amepokelewa na kusalimiana na *Viongozi* mbalimbali waliojitokeza Uwanjani hapo kwaajili ya kumpokea.


Maonyesho ya Siku ya Wakulima *Nanenane* kwa mwaka 2023 yameambatana na kauli mbiu isemayo *“Vijana na Wanawake ni msingi imara wa mfumo endelevu wa chakula”.*


Fuatilia mitandao yetu ya kijamii 

Instagram: @mamakajatz

Twitter @mamakajatz

Facebook: Mamakajatz

YouTube: Mama kaja tz 


#Mamakaja






 



HONGERA KISARAWE KWA KUHAKIKISHA HEWA SAFI NA SALAMA DAR ES SALAAM


 MWANDISHI WETU 

 *Morogoro* 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Dkt. Selemani Saidi Jafo amepongeza jitihada zinazofanywa na Halmashauri ya Wilaya kisarawe katika kuhakikisha inatunza Mazingira na kuhakikisha inafuga ngombe vizuri kanda Mashariki,

Mhe. Jafo, ametoa pongezi hizo leo Agosti 7,2023 alipotembelea Banda la Kisarawe kwenye maonesho ya Nanenane kanda ya Mashariki yanayoendelea katika viwanja vya Julius Kambarage Nyerere mkoa Morogoro Kanda Mashariki,

Aidha, ameitaka kisarawe kuendelea kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira ikiwa ni pamoja na elimu ya kuzuia shughuli za kibinadamu zinazofanyika pembezoni mwa vyanzo vya maji ili kuepusha kujaa kwa uchafuzi katika msitu wa Kazimzumbwi ambalo ni chanzo mama cha hewa safi kwa wakazi wa Dare es Salaam na Pwani.

Sambamba na hilo amesisitiza juu ya utoaji wa elimu kuhusu athari ya vitendo vya uchomaji moto wa misitu iliyopo katika Milima ya Uluguru ili kuhifadhi mazingira na vyanzo maji Mkoa Morogoro,

Kisarawe inashiriki maonesho ya nanenane huku ikisogeza karibu huduma mbalimbali zinazotolewa na halmashauri hiyo pamoja na utoaji wa elimu ya umuhimu wa utunzaji wa Mazingira na vyanzo vya maji na utumzaji wa Mazingira,kulima Chikichi,kwa wananchi wanaojitokeza katika maonesho hayo pamoja na Kutoa elimu kuhusu ufugaji, Kilimo.


Aidha kwa upande wake mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe Adam malima alifurahishwa na Mdau wa Maendeleo wa Kilimo Cha Chikichi kutoka kampuni ya Ina mwanga na kumtaka abaki Morogoro baada ya Nanenane ili Kutoa elimu ya Kilimo hicho kwa Wakulima wa Morogoro,

Nae kwa upande wake pia Msimamizi wa Inamwanga alikubali Ombi la mkuu wa Mkoa kubaki Morogoro ili Kutoa elimu ya kulima zaidi Chikichi kisasa kwa mwalimu wa mkuu huyo. 

FEDHA ZA MIRADI ZIKAGUSE CHANGAMOTO ZA WANANCHI VIJIJINI

Na WAF- Kagera 

NAIBU Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel ametoa wito kwa Wadau na watendaji wote wa Serikali kuhakikisha fedha zote zinazoingia nchini na zinazotoka Serikalini kupitia ziara za nje za Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan zikatatue changamoto zilizokusudiwa za wananchi katika vijiji kuliko kwenye semina na warsha. 


Dkt. Mollel ametoa wito huo leo Agosti 07, 2023 wakati akizindua kampeni ya ugawaji wa vyandarua katika maeneo yote ya mikoa ya Kagera na Tabora inayoambatana na elimu itayosaidia katika mapambano dhidi ya maambukizi ya Ugonjwa wa Malaria katika mikoa hiyo.


"Niwaasa taasisi zote za Serikali na zisizo za Serikali, Rais wetu anapoenda kuzunguka kwenda kwenye makampuni makubwa na mashirika makubwa duniani ili kutafuta fedha, vipaumbele vyake ni kwenda kumfikia Mtanzania mnyonge kutatua changamoto katika vijiji". Amesema Dkt. Mollel. 


Sambamba na hilo, Dkt. Mollel amewataka Wadau kupunguza semina, warsha na mafunzo na fedha hizo ambazo zimetumika huko zielekezwe katika kuongeza nguvu kutatua changamoto zinazowagusa Watanzania wenye uhitaji ikiwemo changamoto za afya.


Aidha, Dkt. Mollel ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Kagera kutumia vyandarua vilivyo na dawa na kusikiliza vizuri maelekezo na ushauri kutoka kwa Wataalamu wa afya hasa kwenye afua mbalimbali za mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria ili kufanikisha dhamira ya Serikali ya kuutokemeza ugonjwa huo nchini. 


Kwa upande wake mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mhe. Erasto Sima ameomba Serikali kupitia Wizara ya Afya kuupa Mkoa wa Kagera kipaumbele kwenye eneo la rasilimali fedha na watu ili kuhakikisha wanatokomeza ugonjwa wa Malaria kwani Mkoa huo ni moja kati ya mikoa inayoongoza kuwa na maambukizi ya Ugonjwa wa Malaria. 


Pia, amewashauri wananchi kujenga tabia ya kupima ugonjwa wa Malaria kabla ya kutumia dawa ili kuondoa usugu wa dawa, huku akibainisha kama mkoa wataendelea kutekeleza juhudi za mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria ikiwemo kusafisha mazingira na kutoa elimu ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo. 


Nae, Mkurugenzi wa afya ,Ustawi wa jamii na lishe OR-TAMISEMI Dkt. Ntuli Kapologwe amesema kama wasimamizi wa Sera watahakikisha Halmashauri zote zinatekeleza ununuzi wa viududu kupitia kiwanda cha Kibaha kwani tayari TAMISEMI imetenga bajeti kwaajili ya ununuzi wa viuadudu hivyo kwenye Halmashauri zote nchini.