Thursday, July 18, 2019

Waziri Mkuu Azindua Zoezi La Uboreshaji Daftari La Wapiga Kura


*Ahimiza vijana wajitokeze kwa wingi, aonya asasi za kiraia za kutoa elimu ya mpigakura zisijihusishe na ushabiki wa kisiasa

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua rasmi zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kuwahimiza vijana waliotimiza miaka 18 wajitokeze kwa wingi kujiandikisha.

“Nitoe rai kwa vijana wote wa Kitanzania waliotimiza umri wa miaka 18 au wale ambao watatimiza umri huo ifikapo Oktoba, 2020 wajitokeze kwa wingi na kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Hawa ndio walengwa wakuu kwa sababu wanaingia kwa mara ya kwanza katika uchaguzi.”

“Ikumbukwe kwamba, bila kujiandikisha hawataweza kutumia haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi wanaowataka. Hivyo, kujiandikisha kwao kutawahakikishia ushiriki wao katika uchaguzi wa viongozi,” amesema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu ametoa rai hiyo leo, (Alhamisi, Julai 18, 2019) wakati akizindua zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lililofanyika kwenye uwanja wa Mandela, Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Waziri Mkuu ambaye amewasili mkoani Kilimanjaro leo asubuhi kwa ziara ya kikazi za siku nne, ametumia fursa hiyo kuwasisitiza vijana na wale wanaorekebisha taarifa zao kwamba hakuna mtu atakayeruhusiwa kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kama hajajiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ama hana kadi ya mpigakura.

Amesema zoezi hilo ambalo limeanza leo, linafanyika kwa mara ya kwanza tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Amesema litafanyika nchi nzima na linatarajiwa kukamilika Machi, 2020.

“Watakaohusika awamu hii ni wapigakura waliotimiza miaka 18 hivi karibuni, wale watakaotimiza miaka 18 wakati wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 2020, waliohama kata au Jimbo na kuhamia maeneo mengine ya kiuchaguzi, waliopoteza kadi au kadi zao kuharibika, wanaohitaji kurekebisha taarifa zao mfano majina ambayo hapo awali yalikuwa yamekosewa sambamba na kuwaondoa wapiga kura waliopoteza sifa kama vile kufariki,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameziasa asasi za kiraia ambazo zimepewa vibali vya kutoa elimu ya mpigakura, zijiepushe na ushabiki wa kisiasa na badala yake zizingatie mwongozo wa elimu ya mpigakura uliotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

“Nimeambiwa, Tume imetoa vibali vya kutoa elimu ya mpigakura kwa baadhi ya Asasi za Kiraia. Rai yangu kwa asasi zilizopata vibali hivyo ni kuendelea kutoa elimu hiyo kwa wananchi kwa kuzingatia mwongozo wa uliotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Niendelee kuwaasa pia kutohusisha ushabiki na mijadala ya kisiasa muda wote mtakapokuwa mkitoa elimu hiyo,” amesema.

Amesema ana imani kuwa wananchi wakipata elimu kuhusu uboreshaji kama inavyoendelea kutolewa, basi watahamasika kutumia haki yao ya kikatiba ya kujiandikisha katika daftari hilo na hatimaye kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Amesema zoezi la majaribio ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Kata ya Kibuta katika Halmshauri ya Wilaya ya Kisarawe na Kata ya Kihonda katika Halmashauri ya Manispaa ya Wilaya ya Morogoro, lilifanyika kwa mafanikio makubwa.

Mapema, akitoa maelezo kuhusu zoezi hilo, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Semistocles Kaijage, alisema katika zoezi la sasa, Tume itaendelea kutumia teknolojia ya kielektroniki ya Biometric (BVR) na imeandaa BVR kits 3,000.

Alisema kwa Tanzania Bara, Tume hiyo imeongeza vituo vya uandikishaji kutoka 36,549 vilivyotumika mwaka 2015 hadi kufikia 37,407; kutokana na zoezi la uhakiki wa vituo vya kuandikisha wapiga kura lililoendeshwa mwaka jana.

“Kutokana na hilo, vituo 6,208 vilibadilishwa majina, vituo 817 vimehamishwa kutoka mtaa mmoja au kijiji kimoja na kwenda kingine na vituo 19 vilihamishwa kutoka kata moja kwenda kata nyingine.”

“Kwa upande wa Zanzibar, vituo vya uandikishaji vimeongezeka kutoka 380 na kufikia 407. Kwa sasa kila kijiji au mtaa, utakuwa na kituo kimoja,” alisema.

Alisema vituo vya uandikishaji vitafunguliwa saa 2 asubuhi hadi saa 12 jioni na zoezi la uboreshaji litafanyika kwa siku saba kwa kila kituo cha kujiandikisha iwe ni Tanzania Bara au Zanzibar.

Mahakama yawaachia huru askari wanane kesi ya kutorosha dhahabu Mwanza






Damian Masyenene, Mwanza
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, imewaachia huru na kuwafutia mashtaka askari wanane waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha.
Askari hao walikuwa na mashtaka 12 yakiwamo ya  uhujumu uchumi, kuomba na kupokea rushwa ya Sh milioni 700, kuisababishia hasara Serikali na utakatishaji fedha ambapo walioachiwa ni pamoja na Koplo Dani Kasara, Matete Misana, Konstebo Japhet Kuliko, Maingu Sorry, Alex Mkali, Timoth Paul, David Ngelela na Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Moris Okinda aliyekuwa kiongozi wa askari hao na mshtakiwa wa kwanza kwenye kesi hiyo.
Uamuzi huo umetolewa leo Alhamisi Julai 18,  na Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Mwanza, Rhoda Ngimilanga aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo, ambapo amesema kutokana na ombi lililowasilishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka (DPP) kupitia kwa Wakili wa upande wa mashtaka, Castus Ndamgoba la kutokuwa na nia ya kuendelea na shauri hilo.
Washtakiwa hao ni miongoni mwa wafungwa wengine zaidi ya 200 kutoka magereza mbalimbali waliofutiwa mashtaka na kufutiwa vifungo vyao jana baada ya Rais John Magufuli kufanya ziara ya ghafla katika Gereza la Butimba, mkoani Mwanza juzi.

WAGONJWA WA MOYO 26 WAFANYIWA UPASUAJI WA KUFUNGUA KIFUA KATIKA KAMBI YA SIKU 14 KWENYE TAASISI YA JKCI



Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akimpata zawadi muuguzi wa chumba cha uangalizi maalum (ICU) kutoka shirika la CardioStart International la nchini Marekani Anasi Griffin wakati wa hafla fupi ya kuwashukuru wataalamu kutoka shirika hilo ambao kwa kushirikiana na JKC wanafanya kambi maalum ya matibabu ya moyo kwa watoto na watu wazima
Madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao wa Shirika la CardioStart International la nchini Marekani wakimfanyia mtoto upasuaji wa kuziba tundu kwenye moyo wakati wa kambi maalum ya matibabu ya siku 14 inayofanyika katika Taasisi hiyo. Jumla ya wagonjwa 26 wakiwemo watoto 13 na watu wazima 13 wamefanyiwa upasuaji na hali zao zinaendelea vizuri.
Daktari wa chumba cha uangalizi maalum kwa watoto kutoka shirika la CardioStart International la nchini Marekani Barbara Ferdman akizungumza wakati wa hafla fupi ya kuwashukuru wataalamu kutoka shirika hilo ambao kwa kushirikiana na JKC wanafanya kambi maalum ya matibabu ya moyo kwa watoto na watu wazima.(PICHA NA JKCI)
NA MWANDISHI MAALUM

WAGONJWA 26 wamefanyiwa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua katika kambi maalum ya matibabu ya siku 14 inayofanyika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Waliofanyiwa upasuaji ni watoto 13 wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu, mishipa ya damu ya moyo na valvu kutofanya kazi vizuri na watu wazima 13 ambao wamefanyiwa upasuaji wa kubadilishwa valvu moja hadi tatu ambazo hazikuwa zinafanya kazi vizuri na kupandikizwa mishipa ya damu ya moyo (Coronary artery bypass grafting - CABG).

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Upasuaji Dkt. Anjela Muhozya alisema matibabu hayo yanafanywa na wataalamu wa Taasisi hiyo kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la CardioStart International la nchini Marekani.

Dkt. Anjela ambaye pia ni daktari bingwa wa usingizi na wagonjwa walioko katika uangalizi maalum (ICU) alisema katika kambi hiyo walipanga kufanya upasuaji kwa wagonjwa 40 kati ya hao watoto 20 na watu wazima 20 , hadi sasa wameweza kufanya upasuaji kwa wagonjwa 26 ambao hali zao zinaendelea vizuri na wengine wamesharuhusiwa kutoka ICU na kupelekwa wodini kwa ajili ya kuanza mazoezi pamoja na kuendelea na matibabu mengine. 

“Katika watoto tuliowafanyia upasuaji, mtoto mmoja alikuwa na tatizo kubwa la valvu zake tatu kutokufanya kazi vizuri, leo hii tunamfanyia upasuaji na kumwekea valvu nyingine tatu”. 

“Kuwepo kwa kambi hii kumesaidia kwa kiasi kikubwa kwa wagonjwa waliohitaji matibabu ya utaalamu wa hali ya juu kufanyiwa upasuaji wakiwa hapa nyumbani pia kubadilishana ujuzi wa kazi kati yetu na wenyeji kwani katika kambi hizi huwa tunajifunza mambo mbalimbali kutoka kwa wataalamu wageni ambao wanakuja kufanya kazi na sisi”, alisema Dkt. Anjela.

Kwa upande wake Kasilda Koka ambaye binti wake amefanyiwa upasuaji katika kambi hiyo aliishukuru Serikali na wafanyakazi wa JKCI kwa kumpokea binti yake na kumfanyia upasuaji huku akitibiwa kwa kutumia bima ya afya.

“Mwaka 1999 wakati huduma za upasuaji wa moyo hazikuwepo hapa nchini nilimpeleka mwanangu ambaye alikuwa na tundu katika moyo kutibiwa nchini India ambako nilitumia gharama kubwa” . 

“Hivi sasa binti yangu alikuwa na shida ya valvu moja kutofanya kazi vizuri ameweza kufanyiwa upasuaji hapa nchini na kuwekewa valvu nyingine kama mnavyomuona anaendelea vizuri”, alisema Kasilda.

Magufuli ampigia Ndugai ‘kampeni kiaina’ Kongwa






Rais Dk. John Magufuli
Anna Potinus
Rais Dk. John Magufuli ameonekana kumpigia ‘kampeni’ Mbunge wa jimbo la Kongwa, Job Ndugai baada ya kusema kuwa Mbunge huyo anatosha kuliongoza jimbo hilo na kwamba haina haja ya kumchagua kiongozi mwingine kwani mbunge huyo anaisaidia nchi nzima kwa nafasi yake aliyo nayo.

Ameyasema hayo leo Alhamisi Julai 18, alipokuwa akizungumza na wananchi wa Jimbo la Kongwa mkoani Dodoma, ambapo amewataka wagombea waliogombea nafasi ya ubunge 2015, kuachana na mawazo ya kutaka kugombea tena kwani nafasi hiyo ni ya Ndugai.

“Ninawashukuru kwa kumchagua Mbunge wenu Ndugai, maana wakati mwingine ni vigumu kwa mtu wa pale pale watu wakajua huyu ni mfalme ndiyo maana katika maandiko wafalme wengi walikataliwa maeneo walipozaliwa lakini ninawambia kuwa mmechagua mtu ambaye anasaidia nchi nzima kwa nafasi yake na msingemchagua kuwa mbunge kwa vyovyote asingekuwa spika,” amesema.

“Ninafahamu wakati wa kampeni kulikuwa na wengine waliohitaji ubunge na nilipofika hapa niliwaambia kazi si ubunge na ukweli ni kwamba wale wote waliogombea niliwateua nafasi mbalimbali wengine wakawa wakurugenzi na wengine wakuu wa mikoa hivyo nitashangaa sana kama 2020 watakuja tena kugombea hapa na wakija wajue hizo nafasi zilizowapa hawataziona tena labda wajitokeze wengine,” amesema.

Aidha, Rais Magufuli amesema kuwa muda umefika wa kulienzi Jimbo la Kongwa kutokana kubeba historia ya Tanzania katika ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika

“Unapotamka Kongwa kwenye nchi ambazo zimepata uhuru kutokana na kujitolea kwenu wanaelewa, wapo walioacha hata damu zao hapa na wengine walizikwa hapa, baba wa taifa alipoamua kuzikomboa nchi zote za kusini mwa Afrika alitumia Kongwa kwa hiyo hapa kuna historia ya ukombozi.

“Ninakubaliana na ombi la spika kuwa wakati umefika wa kuienzi Kongwa hata kama ni kwa kuwa na jengo ambalo litakumbusha haya au uwanja wa ndege alioutumia Rais wa Misri na Algeria na nitakapokutana na marais hawa nitawaeleza kwamba kuna uwanja waliutumia viongozi wenu lakini bado haupo vizuri, nitachomekea chomekea,” amesema Rais Magufuli.

AIR TANZANIA YAZINDUA SAFARI YA KWANZA YA MUMBAI


 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Injinia Isaack Kamwelwe akikata keki wakati wa hafla fupi ya uzinduzi rasmi wa safari ya Mumbai nchini India kwa ndege ya Air Tanzania ikiwa ni safari ya kwanza kwa ndege za Air Tanzania kutoka nje ya Bara la Afrika na ni safari ya moja kwa moja kutokea Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam.Ndege ya kwanza ya Air Tanzania imeondoka Julai 17, 2019 kuelekea Mumbai, nchini India.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Injinia Isaack Kamwelwe akikata utepe wakati wa hafla fupi ya uzinduzi rasmi wa safari ya Mumbai nchini India kwa ndege ya Air Tanzania ikiwa ni
safari ya kwanza kwa ndege za Air Tanzania kutoka nje ya Bara la Afrika na ni safari ya moja kwa moja kutokea Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam. Ndege ya kwanza ya Air Tanzania imeondoka Julai 17, 2019 kuelekea Mumbai, nchini India.

 Mkurugenzi Mtendaji wa Air Tanzania, Ladislaus Matindi akizungumza wakati wa hafla fupi ya uzinduzi rasmi wa safari ya Mumbai nchini India kwa ndege ya Air Tanzania ikiwa ni safari ya kwanza kwa ndege za Air Tanzania kutoka nje ya Bara la Afrika na ni safari ya moja kwa moja kutokea Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam. Ndege ya kwanza ya Air Tanzania imeondoka Julai 17, 2019 kuelekea Mumbai, nchini India.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Injinia Isaack Kamwelwe akizungumza wakati wa hafla fupi ya uzinduzi rasmi wa safari ya Mumbai nchini India kwa ndege ya Air Tanzania ikiwa ni safari ya kwanza kwa ndege za Air Tanzania kutoka nje ya Bara la Afrika na ni safari ya moja kwa moja kutokea Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam. Ndege ya kwanza ya Air Tanzania imeondoka Julai 17, 2019 kuelekea Mumbai, nchini India.















Tanzania yajiandaa kuzalisha dawa SADC





MWANDISHI WETU
Tanzania, kupitia Wizara ya Viwanda na Bishara na Bohari Kuu ya Dawa (MSD), imeandaa mkakati malumu wa uzalishaji wa dawa, kwa ajili ya kuhudumia nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano wa Mradi wa Uzalishaji Dawa na Vifaa Tiba kwa Ubia wa Sekta ya Umma na Sekta Binafsi jana, Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa alisema mchakato huo unaanza wakati Tanzania ikijiandaa kuwa mwenyeji wa mkutano wa SADC, hatua inayoaksi juhudi za Serikali katika kujenga uchumi imara.
Alisema hatua ya ujenzi wa viwanda vitatu vya kutengeneza dawa na vitendanishi nchini itasaidia kunusuru sehemu ya Sh Trilioni 1.2 zinazokwenda nje ya nchi kwa ajili ya ununuzi wa dawa zinazosambazwa nchini na katika nchi za SADC chini ya MSD.
“Kimsingi, wakati Tanzania inakwenda kuwa mwenyeji na kushika uenyekiti wa SADC kuanzia Agosti mwkaa huu, tunahitaji pia kuifanya iwe mzalishaji wa dawa na vitendanishi kwa ajili ya nchi zote 16 wanachama, Afrika Mashariki na Afrika.
“Kwa hiyo tumeweka mazingira rafiki kwa ajili ya uwekezaji mkubwa katika sekta hii ya uzalishaji wa dawa na vitendanishi. Serikali pia inaendelea kupitia sheria ambazo ni kero kwa uwekezaji, ambazo tutazipeleka katika bunge lijalo kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho,” alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu alisema tayari andiko maalumu kw ajaili ya kuanzisha viwanda vya dawa kwenye maeneo matatu nchini limeshakamilika na sasa wanafanya jitihada za kukaribisha wawekezaji.
Alisema katika wazo hilo jipya la kuanzisha viwanda vya dawa kwa kushirikisha sekta binafsi, ujenzi wa viwanda hivyo vya za hospitali umegawanywa katika maeneo matatu, ambayo ni Mwanza ambapo kutajengwa kiwanda cha bidhaa za pamba, Mbeya kwa ajili ya kiwanda cha maji-tiba na Pwani kwa ajili ya kiwanda cha bidhaa mchanganyiko.
“Kwa sasa MSD  ndiyo inayosambaza dawa katika nchi za SADC, lakini asilimia 85 ya dawa zote zinanunuliwa nje ya nchi. Afrika Kusini ndiyo inayoonekana kinara katika nchi hizi kwa mauzo ya dawa, lakini bado ina uhitaji mkubwa kwa sababu inaweza kuhudumia asilimia 25 tu ya watu kwake kwa bidhaa za ndani.
“Kwa hiyo wakati tukielekea katika utani ujao wa SADC, moja ya mambo muhimu ni kuhamaisha uwekezaji wa viwanda hivi vya dawa, ili fedha inayokwenda nje, ambayo kwa sasa inafikia Sh Trilioni 1.2 kwa mwaka ibaki katika nchi hizi,” alisema.
Alisema uwekezaji katika viwanda hivyo nchini utasaidia kupungua gharama za usafirishaji na uhifadhi wa dawa ambazo huchukua hadi miezi tisa kufika nchini, pia utaongeza ajira na kupanua wigo wa teknolojia.
Kamishna wa Ushirikishaji wa Seta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), Dk John Mboya alisema maandiko ya uwekezaji huo utakaogharimu zaidi ya Sh Trilioni 1.1 tayari yameshakamilika, ambapo unatarajiwa kuzalisha zaidi ya ajira rasmi 800.
“Sheria ya PPP pia imeweka wazi kwamba uwekezaji wowote lazima ushirikishe wazawa, kwa hiyo mwekezaji yeyote atakayejitokeza kama akipatikana kutoka nje, atalazimika kushirikisha pia wazawa,” alisema.
Akitoa ufafanuzi, Meneja wa Mradi huo wa Uwekezaji katika Viwanda vya Dawa kwa ubia na PPP, Fred Pondamali alisema hatua ya kupata wawekezaji hadi kusaini mikataba rasmi inatarajiwa kuchukua muda wa miezi sita, hivyo wawekezaji wanatarajiwa kuingia rasmi kwenye ujenzi kuanzia Juni 2020.
“Miradi hii inashindanishwa na watakaoshinda ni wale wenye uwezo wa kifedha na teknolojia. Kwa hiyo utaratibu wa kuwashindanisha hadi kuwakabidhi washindi maeneo ya uwekezaji utachukua muda mrefi kidogo,” alisema.
Alisema katika uwekezaji huo, kiwanda cha bidhaa za hospitali zinazotokana na pamba kinachotarajiwa kujengwa Mwanza kitazalisha bidhaa za aina tatu, cha bidhaa za maji-tiba huko Mbeya kitazalisha bidhaa za aina 10 na cha dawa mseto huko Pwani kitazalisha bidhaa za aina 223.

BASHUNGWA AKUTANA NA WAFANYABIASHARA KARIAKOO, ATAKA LIWE SOKO LA MFANO UKANDA WA SADC NA EAC,

Na Selemani Magali; Dar es salaam.
Waziri wa Viwanda na biashara Innocent Bashungwa amewataka wafanyabiashara soko la Kariakoo kujiendesha kisasa ikiwamo kufuatilia fursa mbalimbali ambazo serikali imekuwa ikizitengeneza dhamira ikiwa ni kulifanya soko hilo kuwa la kimataifa na kimbilio kwa Nchi zote za ukanda wa SADC na EAC.
Akizungumza na wafanyabiashara hao, jana 18 Julai 2019 katika ukumbi wa Anatoglo Manispaa ya Ilala jijini Dar es salaam, Bashungwa amesema lazima wafanyabiashara waamke na kufuatilia fursa hizo kwa manufaa yao binafsi na Taifa kwa ujumla.
Amesema Serikali imejipanga kuweka mazingira wezeshi yatakayosaidia kulifanya soko la Kariakoo kuwa la kimataifa, ni wajibu wa wafanyabiashara kutumia mazingira hayo kwa faida ya TAIFA.
“Kama mnavyofahamu kuwa tunatarajia kuwa na ugeni Mkubwa nchi za SADC ambapo Mh Rais John Pombe Magufuli anatarajiwa kupokea kijiti cha kuwa Mwenyeikiti wa umoja huo, kuanzia  tarehe 5 -9 Agosti 2019 tuna wiki ya viwanda ya SADC sasa ni fursa kwa wafanyabiashara kutangaza biashara zao. Wiki hiyo itafanyika ukumbi wa Mwalim Nyerere Dar salaam.” Alisema
Pia amewataka wenye  viwanda kujipang kwa kuonyesha kazi zao, lakini pia kukutana na wafanyabiashara wenzao kutoka nje ya Tanzaniakwani hiyo ni fursa adhimu inayopaswa kutumiwa ipasavyo.
Aidha akizungumzia mkutano wake na wafanyabiashara wa Kariakoo, Bashungwa amesema wafanyabiashara wameibua changamoto nyingi zinazorudisha nyuma maendeleo ya biashara Kariakoo ikiwamo zuio la watu gari za IT kufanya manunuzi yta bidhaa katika soko hilo
Amesema suala hilo limekuwa kero kubwa na linashangaza kuona watu wanazuiliwa kununua bidhaa badala ya kufurahia suala hilo.
Pia amesema katika mazungumzo yake kumeibuka suala kodi,  katika kutatua changamoto hizo amemua kuitisha kikao na Mkurugenzi Mtendaji wa mamlaka ya mapato Tanzania TRA sambamba na wafanyabiashara wa Kariakoo ili kukaa pamoja kuangalia namna ya kuondoa changamoto hizo.
“Mkoa wa Daresalaam ndio moyo wa uzalishaji wa uchumi wa Nchi kibiashara, kiwanda na kimapato ya serikali, nimetoa maelekezo kuangalia njia ya kutatua changamoto za kibiashara ikiwamo tozo mbalimbaliambazo si rafiki kwa ustawi wa biashara, Wafanyabiashara tunawajali, na selikali imejipanga kuahikikisha inatatua kero zote zinazoikabili sekta hiyo.
Amesema mipango ya kuifanya Kariakoo kuwa kituo kikubwa cha biashara kiasi ambacho wananchi wanachama wa SADC na EAC wanakikimbilia, badala ya kwenda Duabai, Hong Kong kutafuata bidhaa wazipate hapahapa Tanzania.
“Sisis tumezungukwa na Nchi ambazo hazina bahari, tukijipanga vizuri tutaweza kuwahudumia ndugu zetu, tulifanye hilo, ndio kariakoo niyaotaka kuiona, yeney kila kitu Serikali inaweka mazingira wezeshi ya kufikia huko.