Wednesday, December 5, 2018

SERIKALI IMETOA KIPAUMBELE MATUMIZI YA TEHAMA NCHINI-MAJALIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi Tuzo Mshindi wa Kwanza wa Mashindano ya TEHAMA ya HUAWEI, Emmanuel  Chaula wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam katika sherehe za kukabidhi Tuzo hizo kwenye hoteli ya Hayyat Regency jijini Dar es salaam, Desemba 5, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipokabidhi Tuzo za Mashindano ya TEHAMA ya HUAWEI kwenye hoteli ya Hayyat Regency jijini Dar es salaam, Desemba 5, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
............................................
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imetoa kipaumbele kwenye matumizi ya TEHAMA ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utendaji kazi wa shughuli za Serikali za kila siku.

Hivyo, amewataka wananchi kutumia vizuri teknolojia hiyo ya habari na mawasiliano kwenye shughuli za uzalishaji mali na utoaji huduma katika sekta mbalimbali kwa lengo la  kukuza uchumi na kuwapunguzia wananchi umaskini pamoja na kuongeza ajira.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Desemba 5, 2018) katika sherehe za utoaji tuzo za mashindano ya TEHAMA ya HUAWEI yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, ambapo ametumia fursa hiyo kuwaonya watu wote wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii nchini.

“Nawaonya watu wote wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii waache. Ni vema wakatumia mitandao hiyo kwa kuhamasishana mambo mema zikiwemo shughuli mbalimbali za maendeleo. Na kwa wataokiuka sheria ipo na inaendelea kufanya kazi.”

Amsema Serikali inaamini kuwa matumizi ya TEHAMA yataongeza ufanisi katika kuwahudumia ipasavyo wananchi, mfano katika sekta ya elimu mwalimu mmoja anaweza kufundisha wanafunzi wengi kutoka katika shule tofauti kwa wakati mmoja. 

Waziri Mkuu ameongeza kuwa “Matumizi ya TEHAMA kwa kiasi kikubwa yatapunguza gharamaza za uendeshaji kwani yanaweza kufanikisha mawasiliano binafsi, warsha na maelekezo mbalimbali kuwafikia walengwa bila ya kusafiri nje ya vituo vyao vya kazi.”

Ametoa mfano Juni 2017 Rais Dkt. Magufuli alizindua mfumo wa ukusanyaji Mapato ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na Ushuru wa Bidhaa (Excise Duty) kwa njia ya kielektroniki na kudhihirisha kuwa, sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano ni muhimili muhimu wa maendeleo kwenye sekta zote, ikiwemo viwanda, utalii, ujenzi, elimu, afya, kilimo, uvuvi na ufugaji.

“Kwa kuzingatia hayo, mwezi Juni 2018 wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Serikali ilizindua mifumo tisa ya TEHAMA, ambayo inalenga kuimarisha utendaji wa Serikali hususan katika kuwahudumia wananchi kwenye sekta mbalimbali ikiwemo afya, ukusanyaji mapato na utoaji wa taarifa.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika kutengeneza mifumo ya TEHAMA ili kutekeleza kwa vitendo azmaya kuwapatia wananchi maendeleo hususani waishio maeneo ya vijijini huduma bora na kwa wakati.

Amesema kwa sasa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) inauwezo wa kuona na kubaini makusanyo yanayoendelea kukusanywa katika halmashauri mbalimbali nchini na kiasi kinachoingizwa benki kwa kupitia TEHAMA.

Pia, Waziri Mkuu amsema Serikali imeendelea kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwenye taasisi zake ili kufanikisha azma ya kutumia Serikali mtandao, zoezi ambalo linakwenda sambamba na kuunganisha baadhi ya shule za msingi, shule za Sekondari, Ofisi za Wakuu wa Wilaya, Polisi, Hospitali za Wilaya, Vyuo Vikuu na Vituo vya Posta.

Wakati huo huo,Waziri Mkuu ameipongeza kampuni ya HUAWEI kwa uzinduzi wa program yao ya Seed of the Futureambayo inalengo la kuwajengea uwezo wa TEHAMA wanafunzi mbalimbali nchini katika hatua za awali kabisa. 

Amesema iwapo TEHAMA itatumika vizuri itatoa fursa kwa watu wote kupata elimu, kuleta usawa katika elimu, kujenga mazingira na mbinu bora za ufundishaji na kujifunza, kuongeza weledi wa walimu, kuimarisha usimamizi wa masuala ya elimu, uongozi na utawala.
  
Mashindano hayo ya TEHAMA ya HUAWEI yaliasisiwa mwaka 2015 na baadaye mwaka 2016 yakazinduliwa huko Afrika Kusini, ambapo hadi kufikia mwaka 2017 tayari wanafunzi wapatao 40,000 wameshiriki mashindano hayo. 

Kwa upande wa Tanzania, yamezinduliwa mwaka huu, ambapo wanafunzi 500 walishiriki na baadaye kubaki 50, ambapo  waliokabidhiwa tuzo ni saba na watatu kati yao na mkufunzi mmoja wamepata fursa ya kushiriki hatua inayofuata ya mashindano hayo nchini Afrika Kusini. 

Sherehe hizo zimehudhuliwa na Balozi wa China nchini Tanzania, Balozi Wang Ke, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, Naibu Wazri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye, Mkurugenzi Mtendaji wa HUAWEI Tanzania Frank Zhou na wawakilishi mbalimbali wa taasisi za Umoja wa Mataifa nchini.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Balozi wa China Nchini, Mhe. Wang Ke wakati alipowasili kwenye Hoteli ya Hayyat Regency jijini Dar es salaam, Kutoa Tuzo za Mashindano ya TEHAMA ya HUAWEI, Desemba 5, 2018.  Wapili kushoto ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Profesa  Joyce Ndalichako   na kulia ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na viongozi walioshiriki katika sherehe za Utoaji Tuzo za Mashindano ya TEHAMA ya HUAWEI kwenye hoteli ya Hayyat Regency jijini Dar es salaam, Desemba 5, 2018. Kutoka kushoto ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi, Atashasta Nditiye, Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Profesa Joyce Ndalichako, Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya HUAWEI nchini, Frank Zhou na  Balozi wa China nchini, Mhe. Wang Ke. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Viongozi wa Kitaifa na Kimataifa wakiwa katika picha ya pamoja na washindi wa Mashindano ya TEHAMA ya HUAWEI baada ya kuwakabidhi tuzo za ushindi washindi hao kwenye hoteli ya Hayyat Regency jijini Dar es salaam, Desemba 5, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

OPERESHENI NZAGAMBA AWAMU YA PILI YAONDOA WATUMISHI WAZEMBE KIBAHA.

 Baadhi ya Maafisa wa Polisi walioshiriki  Operesheni Nzagamba awamu ya pili  wakifuatilia kwa makini Hotuba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Luhaga Mpina (hayupo pichani).
........................................

Na Frank Mvungi- MAELEZO

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina ameagiza Kuondolewa mara moja kwa watumishi wa Wanaosimamia Kituo cha Ukaguzi Kibaha Mkoani Pwani kwa kushindwa kusimamia rasilimali za Sekta ya Mifugo na Uvuvi. Akizungumza leo Jijini Dodoma wakati  wa kikao cha Tathmini ya Operesheni Nzagamba Awamu ya Pili iliyofanyika  kati ya mwezi Oktoba na Novemba 2018 ikilenga Kuinua mchango wa Sekta ya Mifugo katika Pato la Taifa Waziri Mpina amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali yatokanayo na biashara ya Mifugo na Mazao yake.

“ Watumishi wote walioshiriki katika Operesheni Nzagamba Awamu ya Pili wamefanya kazi kubwa na kwa uzalendo mkubwa hivyo nawapongeza kwa kuwa mmeonesha kuwa tunao uwezo wa kusimamia rasilimali zetu ili zitoe mchango stahiki katika pato la Taifa”.Alisisitiza. 

Mhe. Mpina. Akifafanua amesema watumishi wasio waadilfu na wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao hawana nafasi katika Wizara hiyo ndio maana ameagiza kuondolewa mara moja kwa watumishi wanaofanya kazi ya ukaguzi wa rasilimali hizo katika kituo cha Kibaha.

Aliongeza kuwa Operesheni Nzagamba awamu ya Pili, 2018 imedhihirisha kwamba usimamizi thabiti wa Sheria, Kanuni na Taratibu katika Sekta ya Mifugo unaweza kuleta tija kwa kuongeza uzalishaji bora wa mazao ya mifugo ambayo ni malighafi ya Viwanda na hivyo kuchangia ipasavyo katika kuendeleza uchumi wa Viwanda.

“ Ni mategemeo yangu kuwa wananchi mtakuwa wazalendo kwa nchi yetu kwa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za Kufanya biashara ya mifugo pia kutoa taarifa pale mnapobaini utoroshaji wa mifugo kwenda nchi jirani bila kulipiwa ushuru na tozo stahiki ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya watu hao”. Alibainisha Mhe. Mpina. 

Pia aliwaasa Watumishi wa Wizara hiyo na wale wa Halmashauri kuhakikisha kuwa wanasimamia kwa makini utekelezaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu zote zinazosimamia biashara ya Mifugo na Mazao yake hususan mabadiliko ya Kanuni mpya iliyotolewa mwezi Agosti, 2018.

Katika kuhakikisha minada yote ya awali na ile ya Upili pamaoja na ile ya mipakani inatoa matokea chanya, Waziri Mpina amesema kuwa  usimamizi utaendelea kuimarishwa ili kuwezesha biashara ya mifugo kufanyika kwa ufanisi na hivyo kurahisisha ukusanyaji wa maduhuli, tozo na ushuru wa Serikali. 

Alizitaka Mamlaka zinazotoa Leseni kwa wafanyabishara wanaosafirisha Mifugo nje ya nchi kuweka utaratibu rafiki utakaosaidia  kundi hilo kutoa mchango wake katika ujenzi wa Taifa na kuondoa au kupunguza vitendo vya biashara ya magendo. 

Aidha Waziri Mpina aliagiza kufunguliwa kwa Ofisi za Kanda ili kuimarisha usimamizi wa rasilimali za mazao ya mifugo hapa nchini.

Kwa Upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema kuwa Operesheni hiyo ilishirikisha watendaji 152 waliogawanyika katika timu 14 zilizofanya kazi katika nchi nzima. 

Akizungumzia mafanikio ya Operesheni hiyo amesema kuwa kwa mfano katika Mji wa Bunda zilikuwa zikikusanywa shilingi milioni mbili na nusu  (2.5) hapo awali ambapo kwa sasa baada ya kuimarisha ukusanyaji mapato katika eneo hilo yamefikia milioni nane  (8)kwa siku.

Udhibiti wa Biashara ya Mifugo na Mazao yake uliofanyika kupitia Operesheni Nzagamba II kuanzia tarehe 11 Oktoba, 2018 hadi tarehe 30 Novemba, 2018 (siku 50) umeiwezesha Wizara yangu kupitia Sekta ya Mifugo kukusanya kiasi cha shilingi Bilioni 5,773,074,768. Makusanyo haya yanapelekea Wizara hiyo katika sekta ya Mifugo tu kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 9,764,241,926.28 kwa kipindi cha Julai hadi Novemba, 2018 sawa na asilimia 52.87 ya lengo lililowekwa na Wizara ya Fedha.
 Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Luhaga Mpina akifuatilia uwasilishwaji wa Taarifa ya Tathmini ya Matokeo ya Operesheni Nzagamba awamu ya pili  leo Jijini Dodoma.Kulia kwake ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof Elisante Ole Gabriel,Naibu Waziri Mifugo na Uvuvi Mhe.Abdallah Ulega na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Prof Siza Tumbo.
Viongozi mbalimbali wa “Comand Post” zilizotumika kuongoza Operesheni Nzagamba awamu ya pili  (Mstari wa mbele) wakifuatilia uwasilishwaji wa Taarifa ya Tathmini ya Matokeo ya Operesheni kutoka kwa Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko Dk Felix Nandonde kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi(hayupo Pichani) katika Ukumbi wa St.Gasper  Jijini Dodoma.
 Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Luhaga Mpina akiwa pamoja na Naibu Waziri wa  Mifugo na Uvuvi Mhe.Abdallah Ulega na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof Elisante Ole Gabriel wakati wa uwasilishwaji wa Taarifa ya Tathmini ya Matokeo ya Operesheni Nzagamba awamu ya pili  leo Jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof Elisante Ole Gabriel akizungumza wakati wa uwasilishwaji wa Taarifa ya Tathmini ya Matokeo ya Operesheni Nzagamba awamu ya pili  katika ukumbi wa St.Gasper Leo Jijini Dodoma. 
Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko Dk Felix Nandonde kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi akiwasilisha Taarifa ya Tathmini ya Matokeo ya Operesheni Nzagamba awamu ya pili  leo Jijini Dodoma.
Viongozi  14  wa timu zilizokuwa zinaongoza utekelezaji wa Operesheni Nzagamba awamu ya pili  wakieleza makusanyo waliyofikia mara baada ya Operesheni hiyo kuisha, leo katika ukumbi wa St.Gasper leo  Jijini Dodoma. 
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Luhaga Mpina akizungumza wakati wa uwasilishwaji wa Taarifa ya Tathmini ya Matokeo ya Operesheni Nzagamba awamu ya pili leo Jijini Dodoma.
Picha na MAELEZO.

Tuesday, December 4, 2018

MFUMO WA KIELECTRONIC KUITAJIRISHA CCM.

MNEC wa mkoa wa Pwani Haji Jumaa akifafanua jambo mbele ya viongozi wa chama hicho kutoka Taifa na watendaji wa Ccm Mkoa huo juu ya matumizi ya Electronic katika ukusanyaji wa mapato ya chama.
.....................................................

Na Shushu Joel, Kibaha.
KUTOKANA na mabadiliko ya mfumo wa kimawasiliano  kuwa ni makubwa nchini na duniani kumempelekea mjumbe wa halmashauri kuu ya ccm(MNEC) Haji Jumaa kuwaleta wataalam wa mfumo kutoka makao makuu ya ccm ili kuwanoa makatibu wa chama na jumuiya ili waweze kutumia fursa hiyo kwa ajili ya kuwaingiza wanachama wote wa ccm katika mfumo wa kielectronic ili kurahishia utendaji na mawasiliano baina ya wanachama na chama.

Akizungumza na watendaji wa chama hicho mara baada ya utambulisho mjumbe wa mkutano mkuu wa taifa (MNEC) Haji Jumaa  amewataka watendaji wa chama hicho kuhakikisha wanatumia nafasi hiyo ili kuwaelimisha wanachama wetu mabadiliko ya kidunia yaliyopo duniani kwa sasa.

Aliongeza kuwa mfumo huo wa ukusanyaji wa mapato ya chama utasaidia kuongezeka kwa kipato kwa cjhama hicho na kukifanya kuwa chama tajiri duniani kutokana na raslimali zake zilizopo kote nchini.

“Usajili wa wanachama ni mara moja tu kwani pale unapomaliza kujazo fomu za kitambulisho hicho taarifa zako zitakuwa ni kama zile za kitambulisho cha kitaifa”Alisema Jumaa.

Aliongeza kuwa mfumo huu utaondokana na usumbufu uliopo wa kuwa na kadi ya karatasi na nyepesi kuchanika hivyo wanachama wakipata kitambulisho hiki chenye mfano wa kadi za benki kitarahisisha vitu vingi hapa nchini.

Aidha Jumaa aliwataka watendaji wote walioajiliwa na chama kuwa wabunifu katika ukusanyaji wa mapato ili chama hicho kiweze kujiongezea mapato kwani cc mina vyanzo vingi kila maeneo katika nchi hii.

Akitoa mafunzo hayo mkuu wa idara ya uchumu kutoka ccm makao makuu Dkt Seleman Selele amempongeza mjumbe wa mkutano mkuu wa ccm kutokea mkoa wa pwani kwa juhudi zake za kuhakikisha watendaji wote wa chama katika mkoa huo wanapatiwa elimu juu ya umuhimu wa ukusanyaji na uongezaji wa mapato ya chama.

Aliongeza kuwa mfumo uliopo kwa sasa katika ukusanyaji wa mapato ya chama ni wa kisasa na wenye tija kubwa katika ufanikishaji wa maendeleo ya chama.

Aidha Dkt Selele aliwataka watendaji wote wa chama kuendana na mabiliko yaliyopo ndani ya chama kwani lengo la chama hicho ni zuri na lenye maana kubwa kwa wanachama wake.

Mmmoja wa makatibu walioudhuria kikao hicho kutokea katika wilaya ya kibaha vijijini Janeth Mnyaga ameupongeza uongozi wa chama hicho katika ngazi ya mkoa kwa kuona umuhimu wa kuwaleta viongozi wa kitaifa walio bobea katika masuala ya uchumi ili kuwaelekeza jinsi ya kukiongezea chama hicho mapato.

Hivyo amewataka viongozi wenzake kuwa wawazi katika zoezi linaloendelea nchini katika kuorodhesha mali za chama na jinsi zilivyopangishwa .
Wajumbe wa mkutano huo wakisikiliza elimu inayotolewa na wataalam kutoka makao makuu ya ccm juu ya umuhimu wa kutumia mfumo wa electronic katika ukusanyaji wa mapato ya chama hicho.

MAGAZETI YA LEO DESEMBA 04,2018.

Monday, December 3, 2018

WANAUME LINDI WATAKIWA KUWASINDIKIZA WAKE ZAO CLINIC.

NA HADIJA OMARY, LINDI

Mkuu wa Mkoa wa Lindi  Godfrey Zambi awataka wanaume wa Mkoa huo kuhusika moja kwa moja katika kuwasindikiza wenza wao  Clinic  wanapokuwa wajawazito pindi wanapokwenda kupata huduma, Huku akiwataka Wakuu wa wilaya kulisimamia jambo hilo



Zambi ameyasema hayo juzi katika uzinduzi wa Kampeni ya Jiongeze tuwavushe salama” yenyelengo la kuongeza kasi ya uwajibikaji kwa kupunguza vifo vya akinamama wajawazito na watoto wachanga uliofanyika katika manispaa ya Lindi Mkoani humo



Alisema kuna baadhi ya wanaume wa maeneo mengi wanawageuza wanawake wao kama chombo cha kuwapatia wanaume watoto jambo ambalo sio sawa



Alisema ili kuweza kupata takwimu za wanaume wangapi wametekeleza agizo hilo ni muhimu kwa Waganga Wakuu wa Wilaya kuwa na Dafutari la kumbukumbu maalumu  litakaloonyesha ni wanawake wangapi wamekenda clinic na wanaume wao



“ni lazima tuweke kumbukumbu za namna hiyo na kama tunaona mama mjamzito anaudhuria clinic zaidi ya mara tatu au mara nne, mume ajaonekana na mwanaume wake  yupo ila hataki kwenda kwa makusudi , lazima mwanaume huyo afuatwe na serikali tuchukuwe hatua hili ni agizo langu” alisema Zambi



“serikali tupo mahari pote haiwezekani tukawatumia tuu mama zetu kama chombo cha kutuletea watoto wakati sisi wenyewe tunawajibu, ni kazi muhimu ambayo wamepewa na mwenyezimungu  kwahivyo lazima tuwasamini wake zetu ”aliongeza Zambi 

WAKAZI WA GAMA BAGAMOYO WAMUOMBA WAZIRI LUKUVI


Na Omary Mngindo, Makurunge Bagamoyo

WAKAZI wa Kitongoji cha Gama Makaani, Kata ya Makurunge Bagamoyo Mkoa wa Pwani, waliomo ndani ya eneo la mradi wa Bagamoyo Sugar, wanamuomba Waziri William Lukuvi afike kusikiliza kilio chao.

Wakizungumza na waandishi wa habari kitongojini hapo, wakazi hao walisema kuwa, wanamtaka Waziri huyo ili wampatie kilio chao, kilichodumu kwa miaka zaidi ya mitano sasa, huku kukikosekana majibu ya uhakika.

Wakijitambulisha kwa majina ya Samwel Almass, Hassani Lungwa, Shufaa Nyakoki na Halima Kiongole, kwa niaba ya wenzao walisema kuwa, kwenye eneo lao awali waliingia makubaliano na kampuni EccoEnergy ambayo walikubaliana kuwapatia viwanja sanjali na kuwajengea nyumba.

"Lakini baadae Serikali ikavunja mkataba na EccoEnergy ikakabidhiwa eneo hili Kampuni ya Bagamoyo Sugar, wakati wa Kampuni ya awali ikifanya tathimini, wengine hatukufikiwa kwa kuwa kipindi kilikuwa cha mvua, wengi wetu hatukufikiwa na zoezi hilo," alisema Lungwa.

Nae Shufaa alisema kwamba wiki iliyopita walifika viongozi kutika ngazi ya halmashauri wakawaambia wahame maramoja wapishe mradi huo, huku wengine wakidai kwamba hawajapitiwa na zoezi la tathmini.

"Kinachoendelea hivi sasa ni vitisho kutoka kwa baadhi ya viongozi, wanatuambia tuvunje nyumba tupishe mradi, sisi wengine hatujapitiwa naa tathmini sasa tutakwenda wapi? alihoji Shufaa.

Shufaa aliongeza kwamba hivi karibuni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (MNEC) Haji Abuu Jumaa, Mwenyekiti wa chama hicho Bagamoyo Abdul Sharifu na viongozi wengine, walifika wakaahidi kufuatilia suala hilo, hivyo wanasubiri majibu lakini wanashangaa kutakiwa waondoke .ara moja.

Nilipomtafuta MNEC Haji alisema kuwa katika mkutano uliofanyika kijijini hapo hivi karibuni baada ya kupokea kutoka kwa wananchi hao wametoa kauli kwamba waliolipwa wapishe mradi, kwa ambapo hawajalipwa wasubiri malipo yao.

Nilimtafuta Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo Fatuma Latu atolee ufafanuzi kuhusu suala hilo, alijibu kwa mkato tu kwamba hana neno la kuzungunza juu ya suala hilo

VIFO 893 VYA KINA MAMA WAJAWAZITO NA WATOTO WACHANGA VYARIPOTIWA MKOANI LINDI 2017/2018.

NA HADIJA OMARY- LINDI

Jumla ya vifo(893) vya akinamama wajawazito na watoto wachanga vimetokea Mkoani Lindi kutokana na sababu mbali mbali  ikiwemo kutokwa na Damu nyingi wakati wa kujifungua kipindi cha January 2017-oktoba 2018 



Hayo yameelezwa na mganga mkuu wa Mkoa wa lindi (RMO) Dkt. John Sijaona, alipokuwa anatoa taarifa ya mkoa huo kwenye uzinduzi wa kampeni ya “jiongeze tuwavushe salama” yenyelengo la kuongeza kasi ya uwajibikaji kwa kupunguza vifo vya akinamama wajawazito na watoto wachanga uliofanyika katika manspaa ya Lindi Mkoani humo



Alisema vifo hivyo vikiwemo na vya watoto wafu vimetokea kwa kipindi cha mwezi januari-disemba 2017 na January-oktoba mwaka 2018



Alifafanua  katika kipindi hicho vifo vya akinamama wajawazito vilikuwa 88 watoto wachanga vilikuwa 449 huku watoto waliozaliwa wakiwa wafu vilikuwa 207

Aidha aliongeza kuwa  kwa kipindi cha mwezi January hadi Disemba mwaka 2017 pekee  akina mama waliofaliki kwa uzazi walikuwa 49 watoto wachanga waliokuwa na siku 1-28 walikuwa 290 huku watoto waliozaliwa wakiwa wafu wakiwa 207



Hata hivyo sijaona aliongeza kuwa katika kipindi cha mwezi January-oktoba mwaka 2018 vifo vya akina mama wajawazito vilikuwa 39 na watoto wachanga waliochini ya siku 1-28 walikuwa 396



Akieleza sabubu zilizochangia vifo hivyo Dk, Sijaona alisema kuwa miongoni mwa sababu zilizopelekea vifo hivyo ni kutokwa na damu nyingi wakati wa kujifungua,(PPH) kwa asilimia 31, upungufu wa damu, kuchelewa kufika katika kituo cha Afya na kifafa cha uzazi



Sijaona pia alitaja sababu zilizopelekea vifo kwa watoto wachanga ni pamoja na kushindwa kupumua baada ya kuzaliwa(birthasphyxia) kuzaliwa wakiwanjiti(premuturity) na kupata maambukizi 



Akizungumza baada ya kuzindua kampeni hiyo Mkuu wa mkoa wa Lindi Godfrey Zambi amesema kuwa ili kampeni hiyo ya “jiongeze Tuwavushe salama” iweze iweze kuleta tija na kufikia malengo yake ni lazima kuwepo na uwajibikaji  kwa kushirikiana na watumishi wa umma katika Nyanja mbali mbali za huduma



Hata hivyo Zambi alisema kuwa vifo vingi vya akinamama wajawazito na watoto wachanga vinaweza kuepukuka kama jamii itashirikiana kwa pamoja katika kuweka na kuongeza jitihada za kudhibiti vifo hivyo


ZAYNABU VULLU AKABIDHI MIFUKO 20 UJENZI UWANJA WA JKT

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Pwani Zaynabu Vullu akikabidhi mifuko 20 ya Saruji kwa Mwenyekiti wa Kamati ya ujenzi wa Uwanja wa Mpira wa miguu wa JKT Ruvu Mlandizi Meja James kwaajili ya ujenzi huo
.........................................

Na Omary Mngindo, Mlandizi

MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Pwani Zaynabu Vullu amekabidhi mifuko 20 ya saruji ikiwa ni kuunga mono juhudi za ujenzi wa uwanja wa Moira wa JKT Ruvu uliopo Mlandizi Kibaha Pwani.

Vullu amekabidhi mifuko hiyo Mwenyekiti wa Kamati ya ujenzi wa uwanja huo Meja James ambaye ndio Kaimu Mkuu wa Kikosi cha Ruvu, ambapo alisema mifuko hiyo ni kuunga mkono juhudi hizo.

"Nimefarijika na juhudi zinazoendelea za ujenzi wa uwanja wetu wa JKT Ruvu Maarufu Mabatini, ambapo kwa ushawishi wa viongozi na wadau wameeeza kuanzisha ujenzi wa uzio wa ukuta, nami nakabidhi mifuko 20," alisema Vullu.

Vullu aliongeza kwamba juhudi hizo za uongozi kwa kusbirikisha wadau zinapaswa kuunga mkono katika kufanikisha wengine kwa lengo la kufanikisha zoezi hilo muhimu.

Mbali ya Mbunge Vullu, pia Madiwani walioambatana na mbunge huyo wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti Fatma Ngozi diwani wa Kaata ya Kikongo wemekabidhi mifuko mitano na kufanya mifuko yoye kuwa 25.

Ngozi alisema kuwa uwanja huo ambapo ni fahari kwa wana- Mlandizi, nao wameshawishika kuchangia ujenzi huo na kwamba pia watakwenda kushaweshi wadau wengine waongezee nguvu ili kukamilisha ujenzi huo.

Akizungumza baada ya kupokea mifuko hiyo, Meja James alisema kwamba ujenzi huo unataraji kuchukua tofari elfu 35 kwa gharama ya zaidi ya sh. Mil. 150 na kwamba kwa sasa wamefikisha tofari 6,000.

"Haya matofari mnayoyaona yamefikia 6,000 bado tunaendelea kupokea michango kutoka kwa wadau mbalimbali wanaojitokeza kuchangia ujenzi huo, with wangu watu wengine wajitokeze kusaidia chochote ili kukamilisha ujenzi," alisema Meja James.
 Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu wa JKT Ruvu Mlandizi, Meja James akitoa ufafanuzi juu ya matofali yaliyoanza kufyatuliwa tayari kwa ujenzi wa uzio huo.
  Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu wa JKT Ruvu Mlandizi, Meja James akitolea ufafanuzi moja ya vyumba vya kisasavilivyopo ndani ya uwanja wa JKT Ruvu Mlandizi.

 

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Pwani Zaynabu Vulluakizungumza na kamati ya ujenzi wakiongozwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Meja James (Picha zote na Omary Mngindo)