Monday, November 26, 2018

RAISI WA ZANZIBAR MHE.DK. SHEIN AHUDHURIA MKUTANO WA BLUE ECONOMY KENYA LEO

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe Dk. Ali Mohamed Shein, akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Balozi Monica Juma, alipowasili katika viwanja vya Ukumbi wa Mkutano wa Kimataifa wa Kenyatta Jijini Nairobi kuhudhuria Mkutano wa Kimataifa wa Sustainable Blue Economy) (Picha na Ikulu)

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akihutubia wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa Kwanza wa Kimataifa kuhusiana na Uchumi Endelevu wa Bahari (Sustainable Blue Economy Conference ) uliofanyika katika ukumbi wa Kmataifa wa mikutano wa Kenyatta, akiwasilisha Tamko la Serikala ya Jamuhuri ya Muungano, akimuwakilisha.

RAIS wa Jamuhuri ya Watu wa Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano Uchumi Endelevu wa Bahari (Sustainable Blue Economy Conference) uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Kenyatta Jijini Nairobi Nchini Kenya leo 26/11/2018 na kuwashirikisha Marais mbalimbali wa Nchi za Afrika.(Picha na Ikuklu)
BAADHI ya Washiriki wa Mkutano wa Kimataifa Unaozungumzia Uchumi Endelelevu wa Bahari (Sustainable Blue Economy Conference) uliofanyika katika ukumbi wa Mkutano wa Kimataifa wa Kanyatta Jijini Nairobi Kenya, leo 26/11/2018. Wakati Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akihutubia Mkutano huo akitowa Tamko la Serikali ya Jamuhuri ya Muungano, akimuwakilisha Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. John Magufuli.(Picha na Ikulu)

BRASS Band ya Jeshi la Polisi Kenya ikitumbuiza wakati wa hafla hiyo ya Mkutano wa Uchumi Endelevu wa Habari, katika viwanja vya ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Kenyatta Jijini Nairobi leo,26/11/2018.(Picha na Ikulu)
BAADHI ya Washiriki kutoka Nchini mbalimbali wakiwasili katika viwanja vya Ukumbi wa Mkutano wa Kimataifa wa Kenyatta Jijini Nairobi kuhudhuria Mkutano wa Uchumi Endelevu wa Bahari.(Picha na Ikulu)

TAKUKURU PWANI YAMFIKISHA MAHAKAMANI MTUMISHI DAWASA KWA KOSA LA KUOMBA RUSHWA YA SH. 70,000



NA MWAMVUA MWINYI,PWANI

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Pwani, imemfikisha mahakamani Romani Michael Jovin ambae ni  (volunteer surveyor )wa DAWASA kwa kosa la kuomba rushwa ya sh.70,000  na kupokea rushwa ya kiasi cha sh.50,000 .

Mtumishi huyo amejikuta akifikishwa kizimbani baada ya kwenda kinyume na kifungu cha 15(1) (a) cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba. 11 ya mwaka 2007. 

Romani Michael ambaye alifunguliwa kesi ya jinai mamba 140 ya mwaka 2018 ni volunteer Surveyor DAWASA Ubungo.

Akisoma mashtaka hayo mbele ya hakimu mkazi wilaya ya Kibaha mheshimiwa Herieth Mwailolo, mwendesha mashtaka wa TAKUKURU, Prisca Mpeka aliieleza mahakama kwamba mshitakiwa alitenda kosa la kuomba rushwa ya sh.70,000 na kupokea rushwa ya sh. 50,000 kutoka kwa mtoa taarifa  ili aweze kumsaidia mtoa taarifa kupata mita ya DAWASA.

Alisema, jambo hilo ni kosa kisheria kinyume na kifungu cha 15 (1) (a) cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa, sheria namba 11 ya mwaka 2007.

Aidha Prisca aliieleza ,mahakama kwamba mshitakiwa alipokea rushwa ya kiasi cha sh.50,000 kutoka kwa mtoa taarifa, jambo ambalo pia ni kosa kisheria  kinyume na kifungu cha 15 (1) (a) cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa, namba 11 ya mwaka 2007. 

Mshitakiwa alikana makosa yote mawili na dhamana iko wazi, hata hivyo mshtakiwa ameshindwa kutimiza masharti ya dhamana na hivyo kupelekwa magereza hadi atakapotimiza masharti ya dhamana. 

Kesi hiyo itatajwa tena tarehe 27/11/2018.

Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Pwani, Suzana Raymond anaendelea kuwaasa wananchi wote kufuata taratibu kanuni na sheria za nchi ili kuweza kwenda na kasi ya awamu ya tano chini ya Raisi dk. John Magufuli.

JUMUIYA YA WAISLAMU MKOANI YATIMIZA MIAKA KUMI YAWEKA MIPANGO YA KUJENGA CHUO CHA MAFUNZO

Mwenyekiti wa Jumuiya ya waislamu iliyopo Mkoani Wilayani Kibaha Alhaji Mussa Sekule akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani mara baada ya kumalizika kwa sherehe za maadhimisho ya miaka 10  ya jumuiya hiyoo.(PICHA NA VICTOR MASANGU)
...................................................................


VICTOR  MASANGU, KIBAHA   

KATIKA kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano katika kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo kupitia sekta ya kilimo Jumuiya ya Waislamu iliyopo eneo la Mkoani kata ya Tumbi  Wilayani Kibaha imeweka mipango madhubuti ya kupambana na wimbi la umasikini na kujikwamua kiuchumi  kupitia  mradi maalumu ambao utakuwa unajikita zaidi katika  shughuli mbali mbali  za kilimo cha mazao ya biashara pamoja na  chakula.

Hayo yamebainishwa na Katibu mkuu mstaafu wa Jumuiya hiyo ya  waislamu Mkoani  Omari Hatibu wakati wa  sherehe za kilelel cha maadhimisho ya  miaka 10   ambayo yamefanyika katika msikiti wa Wipazi uliopo mjini Kibaha na kuhudhuliwa na viongozi mbali mbali wa dini pamoja na serikali.


 Aidha Katibu huyo alibainisha  kwamba  pia Jumuiya yao kwa sasa ina mipango mingine mbali mbali ikiwemo kufanya jitihada kwa ajili ya kuanzisha  ujenzi wa chuo  maalumu ambacho kitaweza kuwapa fursa waumini wa kiislamu  kujifunza mambo mbali mbali ya uongozi ikiwemo masuala ya  kuwa wazalendo na nchi yao pamoja na kudumisha amani na upendo kupitia masomo ya kidini watakayofundishwa.

“Kwanza kabisa tunapenda kumshukuru Mungu kwa jumuiya yetu hii kutimiza miaka 20 tangu kuanzishwa kwake ni hii kwetu sisi ni hatua kubwa zaidi na kitu kikubwa ni kuendelea kuisaidia jamii katika mambo mbali mbali katika sekta ya elimu, afya, maji pamoja na makundi ambayo yanamahitaji maalumu,”alisema Hatibu.


Naye Mwenyekiti wa jumuiya ya waislamu mkoani iliyopo Wilayani Kibaha Alhaji Mussa Sekule  amesema kwamba kwa kipindi chote cha miaka kumi wameweza kuisaidia jamii  katika Nyanja mbali mbali ikiwemo sekta ya elimu, afya, pamoja na kuvisaidia vituo vya watoto yatima na watu wenye mahitaji maalumu.


Kwa upande wake mmoja wa waumini walioshiriki katika maadhimisho hayo Haji Saleh ambaye pia ni Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Wipaz ambayo inajihusisha na masuala mbali mbali ya kijamii amewaasa waislamu na wananchi  wote kwa ujumla  kuhakikisha  wanaungana kwa pamoja kwa ajili ya kudumisha hali ya amani na upendo na washirikiane kikamilifu katika  kuleta  mabadiliko chanya ya kimaendeleo.


Pia alisema kuwa suala la kuwepo kwa amani na upendo ni jambo ambalo linaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa ushirikiano wa  hali na mali kutoka kwa serikali pamoja na wananchi wenyewe kuweza kupata fursa ya kushiliki  kikamilifu katika masuala ya msingi hususana katika  miradi ya maendeleo.
 
Baadhi ya viongozi wa Jumuiya ya waislamu Mkoani wakijadiliana jambo wakati wa kilele cha sherehe za  maadhimisho hayo ya kutimiza miaka 10 tangu kuanzishwa kwake. (PICHA NA VICTOR MASANGU)
 
Mmoja wa waumini wa kiislamu Haji Saleh ambaye pia ni mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Wipaz akizungumza jambo na waandishi wa vyombo mbali mbali vya habari wakati wa maadhimisho hayo ya jumuiya ya waislamu Mkoani yaliyofanyika katika msikiti wa Wipaz mjini Kibaha. (PICHA NA VICTOR MASANGU)

SERIKALI YAZINDUA VIZA NA VIBALI VYA UKAAZI VYA KIELEKTRONIKI

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amezindua huduma za viza na vibali vya ukaazi vya kielektroniki na amewataka watu wote watakaopewa vibali hivyo kutii sheria kwa kufanya shughuli ambazo wameelekezwa kwa mujibu wa vibali vyao na si vinginevyo.

Amesema utoaji wa huduma hizo ni miongoni mwa jitihada za Serikali katika kuvutia uwekezaji, hususan katika sekta ya viwanda kwani hatua hiyo itarahisisha upatikanaji wa vibali hivyo kwa raia wa kigeni na kuchochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Novemba 26, 2028) wakati akizindua huduma za viza na vibali vya ukaazi vya kielektroniki katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam na kwamba hatua hiyo itasaidia kuondoa urasimu na ucheleweshwaji wa huduma pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi.

Amesema Idara ya Uhamiaji inatarajia kuanza kutoa huduma tajwa kwa raia wa kigeni muda wowote kuanzia sasa na kwa kupitia huduma hiyo, raia wa kigeni wataweza kuomba vibali hivyo kwa njia ya kielektroniki wakati wowote na mahali popote walipo.

Waziri Mkuu amesema watakaopewa vibali wanatakiwa kufanya shughuli zao kwa mujibu wa vibali vyao kwa sababu kufanya shughuli tofauti na ilivyoainishwa kwenye kibali ni kosa kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Uhamiaji.

Amesema matumizi ya mtandao katika utoaji wa huduma za viza na vibali vya ukaazi ni hatua ya mfano, kwani inakwenda sambamba na mabadiliko ya sayansi na teknolojia na sera ya Serikali ya matumizi ya TEHAMA katika shughuli za Serikali (e-government).

Amesema Serikali inatarajia kuwa, matumizi ya mifumo hiyo itaongeza ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kwa kuwa mteja ataweza kulipia huduma hizo mwenyewe moja kwa moja pasipo kupitia kwa mawakala au mtu yeyote.

“Natoa wito kwa Maafisa, Askari pamoja na Watumishi wote wa Idara ya Uhamiaji kuhakikisha kuwa mifumo hiyo inatunzwa pamoja na kuendeleza miundombinu yote ya kiutendaji.”

Waziri Mkuu amesema kwa kuzingatia ahadi ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli ya kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi na raia wa kigeni, Maafisa Uhamiaji wanatakiwa kutoa huduma hiyo kwa wakati, weledi na kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Uhamiaji.

Amesema mfumo wa huduma hizo utaunganishwa na mifumo mingine ya Serikali, ambayo inatoa huduma kwa wananchi na wageni kama vile Mifumo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Idara ya Kazi – Ofisi ya Waziri Mkuu, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mfumo wa Malipo ya Serikali Kimtandao (GePG).

Sunday, November 25, 2018

MHE HASUNGA AWAONYA WASAMBAZAJI WA MBEGU FEKI

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga akikagua shamba la mahindi wakati wa ziara yake ya kikazi Mkoani Morogoro alipotembelea Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI).
............................................

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Morogoro

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga, 24 Novemba 2018 ametangaza kiama kwa wafanyabiashara wa mbegu nchini wanaouza Mbegu feki zilizopigwa marufuku na serikali.

Amewataka wafanyabiashara wote wa mbegu ambao wamekuwa wakifanya biashara hiyo kwa kuwauzia wakulima mbegu feki zilizopigwa marufuku na serikali kuacha haraka iwezekanavyo kwani serikali itawachukulia hatua za kisheria wale wote watakaobainika kukiuka maagizo ya serikali.

Ametoa agizo hilo akiwa ziarani Mkoani Morogoro ambapo pamoja na mambo mengine alitembelea Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), Taasisi iliyopewa jukumu na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la usajili wa wafanyabiashara wa mbegu (Seed Dealers).

“Serikali imepokea malalamiko mengi kwa wananchi kuhusu Ubovu wa mbegu jambo ambalo limepelekea kwa kiasi kikubwa kuwa na mavuno kidogo pasina kukidhi matakwa ya wakulima wetu nchini” Alikaririwa Mhe Hasunga

Waziri huyo pia ameiagiza Taasisi ya udhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) kutimiza majukumu yao kwa kuwabaini wafanyabiashara wanaokiuka maagizo ya serikali pamoja na taratibu na sheria za nchi.

“Kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusu mbegu feki jambo hili serikali haiwezi kukubaliana nalo hivyo TOSCI wanapaswa kusimamia kwa weledi ukaguzi na usajili wa Mbegu bora, pia ni lazima kuwabaini wasambazaji feki wa mbegu ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao” Alisisitiza Mhe Hasunga

Alisema Wizara ya Kilimo imepewa jukumu mahususi la kuhakikisha sekta ya kilimo inaimarika kwa usimamizi madhubuti wa sera, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali hivyo kunapokuwa na kelele za wananchi kuhusu mbegu feki ni dhahiri kuwa Taasisi zenye jukumu hilo hazitekelezi kazi yake kwa weledi.

Mhe Hasunga alieleza kuwa serikali imejipanga kuhakikisha kuwa inaongeza thamani ya mazao yote yanayozalishwa nchini, sambamba na kutafuta masoko mazuri.

Vilevile, ameitaja Wizara ya Kilimo kuwa ina wataalamu wengi hivyo unaandaliwa mfumo mzuri wa kuwaunganisha watalaamu hao ili kujadili kwa pamoja namna ambavyo kilimo kinaweza kubadilika kutoka kilimo cha kujikimu na kuwa kilimo cha kibiashara ili kutoa malighafi za kutosha zitakazohuisha serikali ya viwanda.

 



MAHAFALI KIDATO CHA NNE 2018 YEMEN DYCCC, WADAU WATAKIWA KUWEKEZA KWENYE ELIMU.



Wahitimu wa kidato cha nne 2018 na elimu ya awali katika shule za Yemen DYCCC Chang'ombe jijini Dar es Salaam.

Mgeni rasmi katika mahafali hayo, Muhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Pazi Mwinyimvua akizungumza katika mahafali ya wahitimu wa kidato cha nne na elimu ya awali katika shule za Yemen DYCCC, kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Elimu ya shule za Yemen DYCCC, Hassan Akrabi na kulia ni Mwalimu Mkuu wa sekondari Hamisi Togwa.
................................................


Wadau wa Elimu wametakiwa kuwekeza kwenye elimu ili kuwawezesha vijana kujiondoa kwenye fikra potofu.


Akizungumza kwenye mahafali ya wahitimu wa kidato cha nne 2018 na elimu ya awali,  katika shule za Yemen DYCCC, mgeni rasmi katika mahafali hayo Muhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dkt. Pazi mwinyimvua alisema uwekezaji katika elimu ndio msingi mzuri kwa vijana utakaowasaidia katika maisha ya dunia na akhera.

Alisema uislamu umehimiza elimu zote zenye manufaa bila ya kuchagua, hivyo vijana wanapaswa kujengewa katika misingi ya kutafuta elimu.

Alifafanua kuwa, Nabii Adam alianza kufundishwa majina ya vitu vyote na baadae kupokea muongo kutoka kwa mola wake, hii dalili ya kuwa katika elimu ni lazima upate elimu ya mazingira itakayokusaidia katika maisha ya dunia na ile ya muongozo itakayokuongoza katika maisha ya akhera.

Dkt. Pazi alisema ili kuyafikia hayo ni wazi kuwa waanzilishi wa shule wanatakiwa kusukumwa na nia iliyo thabiti ya kujua kuwa wanachokifanya ni katika sadaka inayoendelea kwa jamii.

Aidha, alitumia nafasi hiyo kuipongeza Taasisi ya DYCCC inayomiliki shule za Yemen kwa kutengeneza mazingira mazuri ya kusomea hali inayopelekea mtoto kupata hamu ya kusoma.

Akizungumzia misingi ya elimu Dkt. Pazi alisema inaanzia kwenye majengo, vitendea kazi, walimu wenye moyo wa kujituma, wanafunzi waliopata malezi mazuri ya wazazi na wazazi au walezi wenye kufuatilia maendeleo ya vijana wao na kuongeza kuwa kwa mkusanyiko wa aina hiyo ndipo inapatikana elimu bora yenye manufaa kwa vijana.

Kwa kuzingatia hayo aliwataka wamiliki wa shule kuwajali walimu kwa kutoa motisha kwa wanaofanya vizuri ikiwa njia ya kumfanya mwalimu aongeze juhudi na kupata matokeo mazuri kwa wanafunzi.

Akizungumzia, wajibu wa mwalimu alisema mwalimu ana wajibu wa kutumia taaluma yake kwa kuchunga kanuni na misingi ya kazi yake huku akitakiwa kuhakikisha kile anachokifundisha kinafika kwa mwanafunzi kama ilivyokusudiwa,

Katika hatua ya kujenga muhimili mmoja amewataka wazazi na walezi kusimamia malezi ikiwa ni pamoja na nidhamu na maadili kwa kushirikiana na walimu kuhakikisha watoto wanapata elimu iliyokuwa sahihi huku watoto wakitakiwa kuwatii wazazi wao na kuzingatia kile wanachofundishwa na walimu wao.

Mwenyekiti wa Bodi ya shule za Yemen Hassan Akrabi aliwataka wahitimu kuzingatia kile walichofundishwa shuleni hapo ili waendelee kuwa na tabia njema.

Alisema katika jamii kuna vishawishi vingi vinavyopelekea vijana wengi kutoka nje ya maadili hivyo ni wajibu wao kuwa makini ili kulinda heshima yao.

Aliongeza kwa kusema kuwa, kwa muda mrefu waliokuwepo shuleni wamejifunza mabo mbalimbali kwa lengo la kwenda kendelea na kile walichokipata katika masiha ya kawaida.

Awali akisoma taarifa kwa mgeni rasmi kwa niaba ya meneja wa shule za Yemen, Mwalimu Mkuu wa Sekondari, Hamisi Togwa alisema shule za Yemen kuanzia ngazi ya awali hadi kidato cha sita zimeanzishwa kwa lengo la kuwalea watoto kimwili na kiroho katika maadili mema yanayozingatia haki na uadilifu ili waje kuwa viongozi bora kwa Taifa.

Alisema shule za Yemen ni miongoni mwa shule zenye wastani wa kati hapa nchini na zinaendelea kufanya vizuri katika kiwango hicho tangu kuanzishwa kwake katika ngazi ya wilaya, Mkoa, Kanda na Taifa kwa ujumla.

Jumla ya wanafunzi wa elimu awali 95 wamemaliza ngazi ya awali kwa kipindi cha miaka mitatu na wahitimu 65 wamehitimu elimu ya kidato cha nne 2018


  
Mwenyekiti wa Bodi ya Elimu ya shule za Yemen DYCCC, Hassan Akrabi akiongea katika mahafali hayo.

 
Mwalimu Mkuu wa sekondari Hamisi Togwa akizungumza katika mahafali hayo.
 Wahitimu wa kidato cha nne shule ya sekondari Yemen DYCCC wakipunga mikono kama ishara ya kuaga.
 Wahitimu wa elimu ya awali katika shule ya awali ya Yemen DYCCC, Chang'ombe jijini Dar es Salaam wakionyesha baadhi ya vitu walivyofundishwa.
 
Wahitimu wa kidato cha nne shule ya sekondari Yemen DYCCC wakionyesha miongomi mwa masomo waliyofundishwa shuleni hapo.
 
Wahitimu wa kidato cha nne shule ya sekondari Yemen DYCCC wakionyesha namna mitandao ya kijamii invyo athiri jamii.



Meza kuu wakifuatilia maonyesho mbalimbali yalikuwa yakitolewa na wahitimu katika shule za Yemen DYCCC Chang'ombe jijini Dar es Salaam.

WAKAZI WA BAGAMOYO, DAR ES SALAAM KUPATA MAJI YA UHAKIKA- ENG. KALOBELO.

 Naibu Katibu Mkuu wizara ya Maji,  Mhandisi Emmanuel Kalobelo, (katikati) akifafanua jambo wakati alipotembelea Mradi wa ujenzi wa Tenki la kuhifadhia maji kata ya Magomeni wilayania Bagamoyo,  wa tatu kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi, Cyprian Luhemeja, wa pili kushoto ni Mkurugenzi wa Maji na Usafi wa Mazingira kutoka wizara ya Maji ambae pia ni mjumbe wa Bodi ya DAWASA, Mhandisi Nadhifa Kemikimba.
....................................................

Wialaya ya Bagamoyo na Jiji la Dar es Salaam sasa kufaidika na huduma ya maji ya uhakika kutokana na mradi mkubwa unaotekelezwa na Mamlaka ya Maji safi na maji taka Dar es Salaam, (DAWASA) wilayani Bagamoyo.

Hayo yamebainishwa na Naibu Katibu Mkuu wizara ya Maji,  Mhandisi Emmanuel Kalobelo alipokuwa katika ziara ya kutembelea miradi ya upanuzi wa huduma ya maji inayotekelezwa na DAWASA.

Alisema kutokana na kuimarishwa kwa miundombinu ya maji na DAWASA na utekelezaji wa Mradi Mkubwa wa Tenki la kuhifadhia maji linalojengwa kata ya Magomeni mjini Bagamoyo ni wazi sasa kero ya maji itakuwa historia kwa wakazi wa maeneo ya Bagamoyo na Dar es Salaam.

Mhandisi Kalobelo alisema kuwa, Tenki hilo la Bagamoyo lina ukubwa wa mita za ujazo 6000, ambalo lina uwezo wa kuhifadhi maji lita milioni sita ambapo litahudumia watu wengi zaidi na kuondoa shida ya maji.

Aidha, alitumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wananchi kuomba huduma ya maji ya DAWASA ili kila mtu apate huduma hiyo ya maji.

Alisema lengo la serikali ni kuwaondolea adha wananchi katika swala la upatikanaji wa maji hivyo ni vyema wananchi walio karibu na miundombinu ya maji kuomba kusogezewa huduma hiyo majumbani mwao ili lengo la serikali lifikiwe.

Mhandisi Kalobelo, ameipongeza DAWASA kwa kazi nzuri ya utekelezaji wa miradi jambo ambalo linaleta matumaini kwa wananchi kuendelea kutumia huduma ya maji kutoka DAWASA.

Alisema kwa sasa ndani ya DAWASA kuna mabadiliko makubwa sana ya kiutendaji kuwataka waendelee hivyo ili kufikia malengo.

Aliongeza kwa kusema kuwa, wizara peke yake haiwezi kutekeleza miradi hiyo bila ya kuwepo kwa mamlaka za maji hivyo uwepo wao (DAWASA) unaleta ufanisi pia katika kazi za wizara na kupelekea malalamiko kuhusu maji  kupungua.

Naibu Katibu Mkuu wa wizara ya maji ameipongeza DAWASA pia kwa kuimarisha kitengo cha kupokea malalamiko kwani wanachukua hatua haraka mara tu wanapopata malalamiko kutoka kwa wateja au yale yanayotumwa kutoka wizarani.

Naibu Katibu Mkuu huyo wa wizara ya maji alikuwa katika ziara ya kutembelea miradi ya upanuzi wa huduma ya maji inayotekelezwa na DAWASA miradi ambayo ni Ujenzi wa matenki na upanuzi wa mtandao.

Miradi hiyo itanufaisha Manispaa za Kinondoni na Ubungo na Halmashauri ya Bagamoyo.
 
Naibu Katibu Mkuu wizara ya Maji,  Mhandisi Emmanuel Kalobelo, akikagua ujenzi wa Tenki la kuhifadhia maji kata ya Magomeni wilayania Bagamoyo.
 
Naibu Katibu Mkuu wizara ya Maji,  Mhandisi Emmanuel Kalobelo, (wa tatu kushoto) akifafanua jambo wakati alipotembelea Mradi wa ujenzi wa Tenki la kuhifadhia maji kata ya Magomeni wilayania Bagamoyo,  wa pili  kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi, Cyprian Luhemeja, wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Maji na Usafi wa Mazingira kutoka wizara ya Maji ambae pia ni mjumbe wa Bodi ya DAWASA, Mhandisi Nadhifa Kemikimba. 

Sehemu ya muonekano wa Tenki kubwa la kuhifadhia maji mjini Bagamoyo mradi unaoetekelezwa na DAWASA.