Sunday, November 25, 2018

MAGAZETI YA LEO NOVEMBA 25, 2018.

TAARIFA KWA UMMA KUTOKA BENKI KUU.YA TANZANIA.

HALMASHAURI YA KISARAWE KINARA UKUSANYAJI MAPATO 2018/19

HALMASHAURI ya Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2018/19, ndio imekuwa kinara wa makusanyo kwa Halmashauri zote nchi. 

Halmashauri hiyo imeshika nafasi ya kwanza kiasilimia kwenye mapato yake kwa kukusanya kwa asilimia 53 katika kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka huu na ndio iliyoongoza kiujumla.

Mafanikio hayo yametokana na sababu kuu nne ikiwemo fursa ya ujenzi wa Reli ya kati ya kisasa(SGR).

Ujenzi huo umekuwa ni fursa kubwa kwa Halmashauri hiyo kutokana na kifusi kingi kimekuwa kikitoka Kisarawe na kuwezesha makusanyo makubwa ya mapato nje ya matarajio ya awali.
 
Sababu nyingine ni kuongezeka kwa mapato ni kutokana na kuzuia uvujaji wa mapato kwa kuisimamia vyema mifumo ya kielektroniki.

Hiyo imedhihirika hata katika Hospitali ya wilaya Kisarawe hapo awali ilikuwa inakusanya mapato yasiyozidi Sh.Milioni sita kwa mwezi lakini kwasasa baada ya mifumo kuimarishwa na kuongezeka kwa umakini katika ujazaji wa fomu za bima ya afya,  sambamba na kuanzisha duka maalum mapato yameongezeka na kufikia wastani wa Sh.Milioni 45 kwa mwezi.

Kadhalika, usimamizi mzuri wa mapato katika vituo vya kukusanyia mapato vijijini umeimarika kutokana na watendaji kupewa onyo kwa kuonesha uzembe katika ukusanyaji wa mapato.

Pia Halmashauri hiyo kwasasa inakamikisha ujenzi wa Kituo cha mabasi ambacho kitazidi kuongeza mapato ya Kisarawe.

Novemba 24, mwaka huu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI)Selemani Jafo akitoa taarifa kuhusu taarifa ya ukusanyaji mapato ya robo mwaka wa fedha wa 2018/2019 alitangaza kuwa Halmashauri hiyo imeongoza kwa upande wa Halmashauri za wilaya kwa kukusanya kwa asilimia 53.

Anasema kwa upande wa majiji, Halmashauri ya Jiji la Arusha ndilo lililoongoza kiasilimia ambapo limekusanya kiasi cha Sh.Bilioni 4.1 kati ya Sh. Bilioni.15.6 sawa na asilimia 26 ya malengo yao ya makusanyo kwa mwaka wa Fedha 2018/19.

Aidha, Waziri Jafo anabainisha kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeongoza kwa wingi wa kukusanya mapato ghafi ambapo limefanikiwa kukusanya kiasi cha Sh. Bilioni 14.4 kati Sh. Bilioni 68.6, sawa na asilimia 21 ya  malengo waliyojiwekea.

Anaongeza kuwa kwa upande wa Halmashauri za Manispaa iliyofanya vizuri zaidi ni Manispaa ya Musoma  na kwa Halmashauri za Mji zimeongozwa na Mbinga.

Jafo anaeleza kuwa makusanyo hayo kwa mikoa, Mkoa wa Simiyu unaongoza ukifuatiwa na Manyara, Lindi, Mara, Pwani, Arusha, Njombe,Dodoma, Mwanza na Geita.

Waziri huyo anataja Halmashauri zilizofanya vibaya zaidi kwa kukusanya chini ni Halmashauri ya Wilaya ya Masasi DC, Nanyamba TC, Nanyumbu DC, Newala DC,Tandahimba DC,Songea DC,Madaba DC, Rorya na Morogoro DC.

Aidha, kwa Upande wa Mikoa iliyofanya vibaya kwa kukusanya mapato kidogo ni Mkoa wa Mtwara, Ruvuma na Kigoma.

Anasema kwa mwaka wa Fedha 2018/19 Halmashauri zilipangiwa kukusanya Sh.Bilioni 735.6 kutoka kwenye vyanzo vyake vua ndani na hadi kufikia Septemba 30, mwaka huu Halmashauri zilikusanya jumla ya Sh.Bilioni 143.6 sawa na asilimia 20 ya makisio ya mwaka. 

Jafo anasema kwa mwaka wa fedha 2017/18 Halmashuri zilipangiwa kukusanya Sh.Bilioni 687.3 na hadi kufikia septemba 30 mwaka 2017 ziliweza kukusanya Sh.Bilioni 126.8 sawa asilimia 18 ya makisio ya mwaka.

“Kutokana na Takwimu hizo inaonyesha kwamba Halmashuri zimeongeza wingi wa mapato kwa kiasi cha Sh.Bilioni 16.7 na ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani umeongezeka kwa asilimia 2,” anasema Jafo.

Waziri Jafo anasema ukusanyaji wa mapato ndio kitakua kigezo cha kupimwa katika utendaji kazi wa viongozi hivyo kila mtu ajitathmini kulingana na mapato ya Halmashauri au Mkoa wake.

Saturday, November 24, 2018

WAZIRI MGALU ATAKA NYARAKA KUJIONEA MATUMIZI YA FEDHA

Naibu waziri wa nishati Subira Mgalu akisisitiza jambo katika baraza la madiwani.
......................................

Na Shushu Joel,Chalinze.
NAIBU waziri wa Nishati Subira Mgalu ameahidi kwenda ofisini kwa mkurugenzi wa halmashauri ya chalinze katika wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani kwa lengo la kujionea matumizi yanayofanyika na ofisi hiyo ili kuona fedha za serikali kuu zinavyotekelezeka matumizi yake.
Hayo aliyasema alipokuwa katika kikao cha baraza la madiwani ambapo madiwani wengi walikuwa wakihoji juu ya matumizi yanayofanyika bila wao kushirikishwa na baadae wanasomewa tu kwenye vikoa kitu ambapo ni hatari katika ukaguzi na uendeshaji wa miradi .
Aliongeza kuwa lengo la kwenda kwenye ofisi ya mkurugenzi ni kujionea kile kinacholalamikiwa na madiwani wenzake na kukosa majibu yenye uhakikia kutoka kwa wataalamu wa halmashauri hiyo.
“Kumekuwepo na matumizi ambayo si sahihi kutumika kwa kuchukua fedha za miradi hivyo mimi kama mtaalamu wa fedha nitaenda ofisini kwa mkurugenzi kwa kuwa ni mtaalamu ili kujionea kile wanachokifanya kupitia fedha za serikali na zile za ndani kama kwamab vile fedha zinapokopwa kwenda sehemu zingine wanarudisha na kwenda kule zilikopangiwa”Alisema Mgalu.
Hivyo amemtaka mkurugenzi kuhakikisha anaandaa nyaraka ili akifika ofisini hapo aweze kujionea kile kinachotekelezwa na ofisi yake juu ya matumizi ya fedha za serikali kuu na zile za makusanyo ya ndani.
Aidha waziri Mgalu amewashauri madiwani kuwa na tabia ya kumuomba mkurugenzi nyaraka za ndani ili kujionea hali halisi ya matumizi katika halmashauri yao,kupata nyaraka ni haki ya madiwani hivyo watumie fursa hiyo katika kujiletea maendeleo ya halmashauri yao.
Kwa upande wake diwani wa kata ya kimange Hussein Hading oka amempongeza naibu waziri huyo wa nishati Subira Mgalu kwa kuwasaidia madiwani hao juu ya kuomba kutambua umuhimu wa kuona nyaraka za siri juu ya matuimizi yanayoyafanya katika ufanikishaji wa maendeleo ya halmashauri yao ya chalinze.
Aidha amemuomba kuendeleo kuja na kuwapatia elimu kwani madiwani walio wengi wamekuwa hawana elimu juu ya uombaji wa nyaraka ingawa kumbe ni haki yao ya msingi katika kutambua kile kilichofanyika katika halmashauri yao.
Naye mkurugenzi wa halmashauri hiyo Amina Kiwanuka amemkaribisha Naibu waziri huyo wa Nishati ofisini kwake ili kujionea jinsi walivyo na matumizi bora nay ale yanayolingana na kile kilichopangwa na madiwani pamoja na wataalamu kwa lengo la kuhakikisha chalinze inazidi kuwa halmashauri bora hapa nchini kwa watu mbalimbali kuendeleo kuja kujifunza katika halmashauri hiyo.

WAZIRI LUKUVI AWASIMAMISHA KAZI MAAFISA ARDHI WATATU WA JIJI LA ARUSHA

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amewasimamisha kazi watumishi watatu wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya Jiji la Arusha  kwa tuhuma  ya kushirikiana na matapeli wa viwanja katika jiji hilo.

Aidha, Lukuvi ameagiza maofisa hao waliosimamishwa kazi kutokanyaga katika eneo la ofisi za Jiji mpaka hapo uchunguzi utakapofanyika na maamuzi dhidi ya tuhuma zao yatakapotolewa.

Lukuvi alichukua uamuzi huo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika ofisi za Jiji la Arusha jana kufuatia kuwepo tuhuma nyingi  za matapeli ya viwanja kushirikiana na baadhi ya maofisa wa ardhi wasiokuwa waaminifu kufanya utapeli kwa wamiliki halali wa viwanja.

Maafisa  ardhi waliosimamishwa kwa tuhuma hizo za kushirikiana na matapeli kudhulumu viwanja kwa wamiliki halali katika jiji la Arusha ni Elizabeth Mollel, Lassen Mjema na Zawadi Mtafikikolo.

Mbali na kusimamishwa kazi kwa watumishi, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliagiza maafisa Ardhi wa Jiji la Arusha kuhakikisha matapeli wote wa viwanja wanaoshirikiana na watumishi hao wasipatiwe huduma katika masuala yoyote ya ardhi kufuatia  kuonekana kujihusisha na mipango ya utapeli wa viwanja kwa kushirikiana na baadhi ya watumishi wa sekta ya ardhi katika  jiji la Arusha.

Katika ziara yake hiyo ya kushtukiza pamoja na kuelezwa na Afisa Ardhi Mteule wa Jiji la Arusha Dicley Nyato uwepo wa watumishi wawili Lassen na Zawadi huku Elizabeth akiwa katika likizo ya uzazi, watumishi hao walipotea ghafla ofisini bila taarifa mara baada ya kuelezwa wanahitajika kwa waziri na hata pale walipopigiwa simu za mkononi  hazikupatikana.

Kwa mujibu wa Lukuvi, watumishi hao wa sekta ya ardhi katika jiji la Arusha wamekuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na matapeli wa viwanja katika jiji hilo jambo linalotia mashaka utendaji wao wa kazi na kubainisha kuwa  maafisa hao wamekuwa na tabia ya kufuatilia kesi zilizopo katika Mabaraza ya Ardhi kwa nia ya kuwasaidia  matapeli.

Kufuatia kadhia hiyo, Lukuvi ameagiza kuanzia sasa hati zote za wito wa Mahakama nchini kusainiwa na Afisa Ardhi Mteule au Msajili wa Hati ama Kamishna Msaidizi wa Ardhi wa Kanda na Mwanasheria wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi lazima afahamishwe uwepo wa kesi husika.

“Kuanzia sasa summons zote zipokelewe na Maafisa Ardhi Wateule, Makamishna au Wasajili wa Hati wa Kanda na watumishi wengine wasipokee wala kujihusisha” alisema Lukuvi

Lukuvi alisema matapeli wa viwanja wamekuwa wakifungua kesi  katika Mabaraza ya Ardhi dhidi ya wamiliki halali na wakati mwingine matapeli hao hawawafahamu hata wamiliki  lengo lao likiwa kuwakatisha tamaa pale kesi inapochukua muda mrefu hasa ikizingatiwa baadhi ya wamiliki hawana uwezo wa kuweka mawakili na hivyo kuwa na uwezekano mkubwa wa kupoteza haki zao.

Alisema, tabia hiyo haiwezi kuvumiliwa na kusisitiza kuwa mtandao wote wa matapeli wa viwanja katika jiji la Arusha ataukomesha kama alivyofanya katika jiji la Dar es Salaam ambalo huko nyuma lilishamiri sana kwa tabia hiyo ili kusaidia haki za wanyonge.

Kwa upande wake Afisa Ardhi Mteule wa Jiji la Arusha Dicley Nyato alimueleza waziri Lukuvi kuwa wamekuwa wakisumbuliwa sana na matapeli wa viwanja katika jiji hilo na wakati mwingine matapeli hao huwashitaki lengo likiwa kujipatia viwanja kwa njia ya udanganyifu na kuviuza.

Lukuvi alifanya ziara hiyo ya kushtukiza katika ofisi za jiji Arusha akitokea wilayani Babati mkoa wa Manyara ambako huko aliweza kutoa faraja iliyopotea kwa muda mrefu kwa wananchi wa vijiji vya Singu na Endasago  kwa kuamuru kubaki katika maeneo yao kufuatia mgogoro wa muda mrefu wa takriban miaka hamsini kati ya wana kijiji na wamiliki wa mashamba ambao ni kampuni za Agric Tanzania Ltd na  Endasago Co Ltd.

MAGAZETI YA LEO NOVEMBA 24, 2018.

Friday, November 23, 2018

JESHI LA POLISI LAKAMATA SHEHENA YA SILAHA NA MILIPUKO NDANI YA MWEZI MMOJA, OPERESHENI MIKOA YA KUSINI.

Mkuu wa Operesheni Maalum za Jeshi la Polisi Nchini, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Liberatus Sabas, katikati akiwa amenyanyua silaha aina ya AK 47 zilizopatikana katika Operesheni maalum ya kupambana na uhalifu iliyofanyika kuanzia Octoba mwaka huu mpaka Novemba mwaka huu katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma.
Mkuu wa Operesheni Maalum za Jeshi la Polisi Nchini, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Liberatus Sabas, katikati akiwa amenyanyua Bomu moja (1) la kurushwa kwa mkono (Hand Grenade – Defensive) lililoko mkono wa kulia na milipuko mingine iitwayo Explosive – Gel V6 iliyokamatwa katika Operesheni maalum ya kupambana na uhalifu iliyofanyika kuanzia Octoba mwaka huu mpaka Novemba mwaka huu katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma.
Mkuu wa Operesheni Maalum za Jeshi la Polisi Nchini, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Liberatus Sabas, katikati akionyesha  mbolea aina Ammonium Nitrate  na Potassium Nitrate zinazotumika kutengenezea milipuko mbalimbali, mbolea hizo zilipatikana katika Operesheni maalum ya kupambana na uhalifu iliyofanyika kuanzia Octoba mwaka huu mpaka Novemba mwaka huu katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma. (Picha na Jeshi la Polisi)

WADAU WA KILIMO WATAKIWA KUTOA USHIRIKIANO.

Waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizundua Kongani ya tatu ya Centre Limited (SCL) Sagcot-Kilombelo katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Flomi mjini Morogoro tarehe 23 Novemba 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal-Wizara ya Kilimo)
............................................


Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Morogoro

Mageuzi ya kilimo nchini Tanzania yanapaswa kutiliwa mkazo na wadau wote wa sekta ya kilimo wakiwemo wananchi, wadau wa maendeleo na serikali kwa ujumla.

Waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo tarehe 23 Novemba 2018 wakati akizundua Kongani ya tatu ya Centre Limited (SCL) Sagcot-Kilombelo katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Flomi mjini Morogoro.

Mhe Hasunga alisema kuwa Sekta ya kilimo imeendelea kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania kwani imekuwa ikichangia kwa Kiasi kikubwa katika kutoa ajira, kuchangia karibu nusu ya mauzo yote ya nje na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuleta fedha za kigeni.

Alisema kuwa Serikali imeendelea kuweka juhudi zake katika kuwezesha sekta ya kilimo kwa kufanya mabadiliko mbalimbali ya kisera yenye lengo la kuweka mazingira wezeshi kwa sekta ya kilimo kukua.

Pia serikali imezindua Mpango wa pili wa Maendeleo ya Kilimo (ASDP II) wenye lengo la kuhakikisha sekta ya kilimo inakuwa na inachangia katika maendeleo ya uchumi na kuongeza kipato cha mkulima mdogo.

Mhe Hasunga amesisitiza kuwa mpango wa SAGCOT ulianza toka mwaka 2010 kwenye mkutano wa Baraza la Uchumi la Dunia kwa Africa (World Economic Forum of Africa WEF-A) uliofanyika Jijini Dar es Salaam ambao utatekelezwa kwa miaka 20 mpaka mwaka 2030.

Alisema mpango wa SAGCOT umepangwa kutekelezwa kwa awamu katika mgawanyo wa kongani sita. Kongani hizo Ihemi, Mbarali, Kilombero, Rufiji, Ludewa na Rukwa hivyo ili kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao ameitaka SAGCOT kuongeza ufanisi na weledi katika kukamilisha kongani zote sita kama mtazamo ulivyo.

Naye Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba akizungumza katika hafla hiyo alisema kuwa wizara ya kilimo ina ziada ya kutosha kwenye mazao ya chakula huku akisisitiza kuwa mkakati wa kutafuta masoko unaendelea ili kuwanufaisha wakulima nchini.

Alisema nchi ina fursa kubwa kwenye sekta ya kilimo hivyo wananchi wanapaswa kujikita zaidi katika kilimo kwani ndio sehemu pekee yenye uwezo wa kuwanufaisha wananchi wengi kwa wakati mmoja.

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Innocent Bashungwa alisisitiza kuwa SAGCOT inapaswa kufanya haraka katika kuanzisha kongani ya nne na hatimaye mpaka ya sita ili kuajiri vijana na wananchi wengi.

Ameongeza kuwa wataalamu wengi wa kilimo wamenufaika na elimu nchini lakini ajira zimekuwa chache hivyo kuongezwa kwa kongani nyingine ajira zitaongezeka na wananchi wengi watanufaika na kipato kwa ajili ya maendeleo ya kaya na Taifa kwa ujumla wake.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa SAGCOT Ndg Geofrey Kirenga alieleza kuwa malengo ya mpango wa SAGCOT yanakwenda sambamba na Dira ya maendeleo ya Taifa ya 2025, mpango wa maendeleo wa miaka 5, utekelezaji wa mpango wa pili wa maendeleo ya kilimo (ASDP II) na mpango wa uwekezaji kwenye kilimo kwa ajili ya usalama wa chakula na lishe (TAFSIP) ambao unatumika kutekeleza programu kabambe ya maendeleo ya kilimo barani Afrika (CAADP).

Alitaja lengo kuu la mpango wa SAGCOT kuwa ni kuhakikisha kuwa kilimo katika maeneo ya SAGCOT kinachangia katika kuongeza tija, kuhakikisha kuna usalama wa chakula, kupunguza umaskini, kuhakikisha wakulima wadogo wanatoka kwenye kilimo cha kujikimu na kwenda kwenye kilimo cha kibiashara na kuhakikisha mazingira yanatuzwa kwa maendeleo endelevu ya kilimo.
Waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizundua Kongani ya tatu ya Centre Limited (SCL) Sagcot-Kilombelo katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Flomi mjini Morogoro tarehe 23 Novemba 2018. 
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Innocent Bashungwa akisisitiza jambo wakati wa uzinduzi wa Kongani ya tatu ya Centre Limited (SCL) Sagcot-Kilombelo katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Flomi mjini Morogoro tarehe 23 Novemba 2018. 
 Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kongani ya tatu ya Centre Limited (SCL) Sagcot-Kilombelo katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Flomi mjini Morogoro tarehe 23 Novemba 2018.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe Albert Chalamila akitoa ushuhuda toka kongani ya Ihemi na Mbarali wakati wa uzinduzi wa Kongani ya tatu ya Centre Limited (SCL) Sagcot-Kilombelo katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Flomi mjini Morogoro tarehe 23 Novemba 2018.
Mkurugenzi Mtendaji wa SAGCOT Ndg Geofrey Kirenga akieleza mwelekeo wa jinsi SAGCOT itakavyoendesha shughuli zake wakati wa uzinduzi wa Kongani ya tatu ya Centre Limited (SCL) Sagcot-Kilombelo katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Flomi mjini Morogoro tarehe 23 Novemba 2018. 
 
Muwakilishi wa Benki ya Dunia Bi Emma Isinika Modamba akiwasilisha taarifa fupi toka kwa wadau wa Maendeleo wanaowezesha mpango wa SAGCOT wakati wa uzinduzi wa Kongani ya tatu ya Centre Limited (SCL) Sagcot-Kilombelo katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Flomi mjini Morogoro tarehe 23 Novemba 2018. 

TUTAENDELEA KUSHIRIKIANA NA VYUO VIKUU VYOTE NCHINI-MAJALIWA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na Maafisa Afya wa mikoa nchini, wakati alipofungua rasmi mkutano wa maafisa hao kwenye ukumbi wa mipango jijini Dodoma Novemba 23, 2018.
.....................................

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kutoa ushirikiano na miongozo kwa vyuo vikuu vyote nchini, vya binafsi na vya umma ili viendelee kutoa elimu ya juu yenye ubora na viwango vinavyotakiwa kwa lengo la kukidhi matakwa na ushindani kwenye soko la kitaifa na kimataifa. 

Amesema suala hilo ni muhimu likapewa uzito unaostahili kwani wahitimu hao wakitoka vyuoni wanakwenda kutoa huduma katika jamii ya Watanzania na pia ya kimataifa, hivyo ni muhimu elimu inayotolewa ikazingatia ubora na viwango vinavyostahiki.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Novemba 23,2018) kwenye mahafali ya tisa ya chuo kikuu cha Mtakatifu Yohana cha Tanzania Kampasi ya Chifu Mazengo, Dodoma yaliyofanyika kwenye ukumbi wa CCM.

Amesema Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli, inatambua na kuthamini mchango wa Sekta Binafsi hususan wa vyuo vikuu binafsi kama Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yohana cha Tanzania, katika maendeleo ya elimu ya juu. 

“Serikali inatambua mchango wa vyuo hivyo katika kupanua fursa kwa Watanzania wengi kupata elimu ya juu, ambapo hadi sasa udahili wa wanafunzi wa elimu ya juu kwenye vyuo vikuu binafsi nchini ni takriban asilimia 25 ya wanafunzi wote.”

Amesema Serikali inatambua mchango wa chuo kikuu cha Mtakatifu Yohana cha Tanzania katika kutayarisha watalaamu wa fani mbalimbali. Aidha, tangu kuanzishwa kwake mwaka 2007, chuo hicho kimetoa wahitimu zaidi ya 10,000.

Amesema kati ya wahitimu hao wapo Wafamasia, Wauguzi, Walimu wa Sayansi, Walimu wa Sanaa, Wataalamu wa Maabara, na Wasimamizi na Waendeshaji wa fani mbalimbali kama Utawala, Masoko na Wahasibu, mchango ambao unahitajika kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa uchumi wa Taifa katika nyanja tajwa.

Waziri Mkuu amesema baadhi ya wahitimu watapata ajira lakini si kila mhitimu atapata fursa ya kuajiriwa, hivyo Serikali itaendelea kuunga mkono azma yao kama chuo kikuu ya kutoa wahitimu wenye tabia, utashi na uwezo wa kutengeneza kazi na siyo watafuta kazi tu.

Akizungumzia kuhusuchangamoto zinazokabili sekta ya elimu ya juu, amesema baadhi ya changamoto zinafanana katika vyuo vikuu vyote nchini na pia zipo changamoto zinazokabili vyuo vikuu binafsi na wakati mwingine zipo changamoto zinazohusu chuo kikuu kimoja kimoja. 

Amesema moja ya changamoto kubwa katika elimu ya Juu ni uhaba wa Wahadhiri wenye sifa stahiki ili kuendana na ongezeko la wanafunzi wanaojiunga na vyuo vyao. “Nafahamu jitihada ambazo vyuo vikuu binafsi vinafanya katika kuendeleza Rasilimali Watu wao na hasa katika eneo la taaluma ili viwe na Wahadhiri na Maprofesa wa kutosha.” 

Hivyo, Waziri Mkuu ametoa wito vyuo vingine binafsi nchini viwekeze katika eneo la kuendeleza Rasilimali Watu kwa bidii zaidi na kwa upande wa Serikali, ipo mikakati mbali mbali ya kuajiri lakini pia kusomesha wale waliopo kazini ili kufikia viwango vinavyokubalika Kitaifa na Kimataifa. 

Waziri Mkuu amesema changamoto nyingine inayovikabili vyuo vikuu ni miundombinu ya kufundishia na kujifunzia kama vile mabweni na nyumba za watumishi, hivyo kusababisha baadhi ya vyuo  kushindwa kukidhi matakwa ya ithibati zao na kuzuiwa kufanya udahili au kufungiwa kabisa.

“Ni kweli tunahitaji Watanzania wengi wapate elimu ya juu kwenye vyuo vyetu vikuu. Hata ninyi wanafunzi, mngependa kupata elimu iliyo bora itakayoweza kuwasaidia maishani na itakayowakomboa kifikra, itakayowapa ujuzi na maarifa ya kupambana na changamoto za maendeleo. Kila mmoja anataka elimu bora na si bora elimu.” 

Waziri Mkuu amesema kuwa dhamira hiyo ndiyo inayoifanya Serikali kupitia Tume ya Vyuo Vikuu kuhakikisha kuwa vyuo vyote visivyokidhi matakwa ya ithibati yao haviendelei kutoa mafunzo ya aina yoyote. 

“Nitoe rai kwa vyuo vikuu vyote vizingatie matakwa ya ithibati zao ili viweze kutoa elimu iliyo bora itakayokidhi matamanio ya Watanzania na ushindani wa soko la ndani na nje.”

Kuhusu Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yohana cha Tanzania ambacho kimeomba kuruhusiwa kufanya udahili baada ya kufungiwa, Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako kujiridhisha iwapo chuo hicho kimekidhi vigezo kabla ya kukipa kibali cha kudahili wanafunzi wapya.

MABORESHO YA MWONGOZO WA UTOAJI HUDUMA ZA KIELIMU KUSAIDIA WENYE UONI HAFIFU

Mwanasheria wa Shirika la kimataifa la kutetea haki za watu wenye ualibino (Under The Same Sun) nchini Tanzania, Bw. Madulu William, akifafanua jambo wakati wa warsha hiyo ya kupitia na kurekebisha mwongozo wa utoaji elimu kwa wanafunzi wenye ualbino na uoni hafifu iliyofanyika Novemba 22 na 23, 2018 Dodoma Hoteli Jijini Dodoma.
........................................

Maboresho ya mwongozo wa utoaji huduma za kielimu kusaidia kutatua changamoto za mazingira ya kielimu kwa wenye ulemavu wa ngozi (ualbino) na uoni hafifu.

Akizungumza Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Wenye Ulemavu Bi. Magreth Malunda alisema kuwa Serikali imekuwa ikisirikiana kwa karibu na Shirika la Kimataifa la Kutetea haki za wenye ualbino Duniani (Under the Same Sun) pamoja na wadau mbalimbali katika harakati za kutatua changamoto za kielimu zinazowakabili wanafunzi wenye ualbino, hususan suala la uoni hafifu.

“Mwongozo huo utakuwa ni nyenzo muhimu katika utoaji huduma za kielimu kwa watoto wenye ualbino na uoni hafifu hapa nchini, maana utasaidia kutambua mahitaji yao muhimu,” alisema Malunda.

Kwa upande wake Mwanasheria wa Shirika la Under the Same Sun, Bw. Madulu William alisema kuwa matatizo wanayokumbana nayo wanafunzi wenye ualbino ni pamoja na kushindwa kusoma vizuri mitihani na mwandiko ubaoni wanapokuwa madarasani, hivyo kusababisha wengi wao kushindwa kufanya vizuri katika masomo.

“Jambo la msingi ni kuhakikisha mwongozo unakuwa na njia bora ya kuwawezesha walimu kujua jinsi watakavyoweza kuwajumuisha wanafunzi wenye ualbino na uoni hafifu wanapata fursa sawa kama walivyo wanafunzi wengine,” alisema William.

Naye Meneja Mradi Jumuishi wa Watu wenye Ualbino (KCBRP) Bw. Florence Rugemalira alisema kuwa ni vyema jamii ikaelimishwa juu ya watu wenye ulemavu ualbino na uoni hafifu ili waweze kutambua kuwa wanaouwezo kama wengine katika kupata elimu.

Warsha hiyo imehusisha Wizara mbalimbali na wadau wanaofanya kazi kwa ukaribu na watu wenye ualbino ambapo walikutana kwa siku mbili kupitia na kurekebisha mwongozo wa utoaji elimu kwa wanafunzi wenye ualbino na uoni hafifu.
Mratibu wa Elimu Maalum Kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Bi. Janneth Mwocha akionesha kitabu cha mwongozo wa utoaji wa huduma za kielimu kwa Watoto wenye ulemavu wa Ngozi.

Afisa Ustawi wa Jamii Bi. Oliver Njogopa, akichangia mada wakati wa warsha hiyo.

Mwanasheria wa kujitegemea Bi. Neema Ndemno akiwasilisha mada kwa washiriki waliohudhuria warsha hiyo iliyofanyika Jijini Dodoma.

Baadhi ya washiriki wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa katika warsha hiyo.Baadhi ya washiriki wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa katika warsha hiyo.