Tuesday, March 13, 2018

NAIBU WAZIRI NISHATI, DC BAGAMOYO WATOA POLE AJALI YA MOTO CHALINZE.


Naibu waziri wa nishati Subira Mgalu, wa kwanza kulia na Mkuu wa wilaya ya bagamoyo wa pili kushoto walipofika Chalinze kujionea aja;i ya moto ambayo imesababisha vifo vya watu wanne.
....................................
Naibu waziri wa Nishati Subira Mgalu amesema serikali inasubiri uchunguzi wa tukio la moto uliotokea Chalinze ambao umesababisha vifo vya watu wanne ili kuona ni maelekezo gani ambayo inaweza kuyatoa.

Naibu waziri huyo wa nishati aliyasema hayo jumatatu Mach 12, 2018  baada ya kutembelea katika eneo la tuki la ajali ya moto katika halmashauri ya Chalinze.

Kauli hiyo ya waziri imekuja kufuatia taarifa za awali ambazo zinaonyesha kuwa, moto huo umesababishwa na hitilafu ya umeme saa saba za usiku wa jumamosi kuamkia jumapili ya Mach 11, ambapo watu wanne wamefariki dunia na wengine wawili kueruhiwa huku mtoto wa miaka miwili akiwa amenusurika.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Majid mwanga alimuagiza Afisa Tarafa ya Chalinze kufanya tathmini ya namna ya kuwasaidia walionusurika katika ajali hiyo katika kipindi hiki kigumu walinachonacho.
 Naibu waziri wa nishati Subira Mgalu, wa (katikati) na Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo wa kwanza kushoto walipofika Chalinze kutoa pole kwa familia iliyopata ajali ya moto ambayo imesababisha vifo vya watu wanne.
Muonekano wa nyumba iliyoungua moto huko Chalinze

VITUO VYA AFYA CHALINZE HAVINA VYUMBA VYA KUHIFADHIA MAITI



MBUNGE wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete ,ameweka wazi kuwa vituo vya afya katika jimbo hilo vinakabiliwana na ukosefu wa vyumba vya kuhifadhia maiti .

Amesema changamoto hiyo ni kubwa ambapo husababisha wananchi kupeleka maiti za ndugu zao kwenye Hospitali teule ya rufaa ya Tumbi na wilaya ya Bagamoyo ambako kuna mbali mrefu.

Aliyasema hayo mjini Chalinze,wakati akizungumza na baadhi ya wananchi,na kusema  shida kubwa inatokea hasa pale mgonjwa anapokuwa amefariki.

Ridhiwani alisema jimbo zima la Chalinze hakuna chumba cha kuhifadhia maiti kwenye vituo vyote vya afya hali ambayo imekuwa mtihani mkubwa kwa wananchi wa jimbo hilo .

“Hali ni mbaya kwa wenzetu wa kata ya Kibindu ambao wanapeleka maiti Hospitali ya Bwagala wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro ,”

“Wananchi wanaingia gharama kwenda kuhifadhi maiti sehemu nyingine ambako ni mbali na maeneo yao”

“Tunaishukuru serikali kwa kuendelea kuboresha huduma za afya kwenye vituo vya afya pamoja na zahanati lakini changamoto yetu kubwa ni ukosefu wa chumba cha kuhifadhia maiti ambapo tunajitahidi kufanya njia ili kuhakikisha tunajenga chumba hicho,” alisema Ridhiwani.

Hata hivyo, Ridhiwani alisema kata ya Lugoba ambapo kuna kituo cha afya serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 400 kwa ajili ya kujenga majengo yakiwemo wodi ya mama na mtoto, maabara, chumba cha kufanyia upasuaji mdogo kwa ajili ya akinamama na chumba cha kuhifadhia maiti.

Akielezea suala hilo ,mkuu wa mkoa wa Pwani ,Mhandisi  Evarist Ndikilo alisema serikali inaendelea na uboreshaji wa huduma za afya kwenye zahanati zake 292 na vituo vya afya 26 ambapo vituo 119 vimekarabatiwa ili kutoa huduma bora.

Alisema mbali ya hilo pia inahakikisha upatikanaji wa dawa unakuwa mkubwa.
Ndikilo alieleza kwa sasa ni kunahakikishwa kunakuwa na ongezeko kutoka asilimia 73.3 hadi kufikia asilimia 85 hali ambayo amesema inawezekana kutokana na mikakati iliyowekwa ya upatikanaji wa dawa.

MKOA WA PWANI WAJIPANGA KUDHIBITI MAGHALA YA KOROSHO YA VICHOCHORONI



Mkuu wa Mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo (wa pili kushoto) alipotembelea ghala linalomilikiwa na kampuni ya RK Chudasama Ltd wilayani Mkuranga,(wa kwanza kushoto)mkurugenzi kampuni hiyo ,Sundeep Chudasama ,wa kwanza kulia Katibu wa CCM Mkuranga, Shilla na wa pili kulia mkuu wa wilaya hiyo,Filberto Sanga
...............................................

SERIKALI mkoani Pwani, inatarajia kuchukua mbinu mbadala ya kukodi ghala lenye ubora na kuendelea na ujenzi wa maghala ya kuhifadhia korosho ili kupambana na vyama ushirika vya msingi (AMCOS) vilivyokuwa vikitumia maghala ya vichochoroni na majumbani yasiyo na viwango.

Aidha ,imesema haitokubali kutumia maghala ya vyama hivyo katika msimu ujao na kudai mkoa umechoka kudang’anywa na kuchafuliwa sifa ya nchi kwenye soko la nje.

Mkuu wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo, aliyasema hayo wakati alipotembelea ghala la kisasa linalomilikiwa na kampuni ya RK CHUDASAMA Ltd, wilayani Mkuranga.

Alieleza,serikali imeshamlipa malipo ya awali sh.bilioni moja mkandarasi wa ujenzi wa ghala la kuhifadhia korosho wilayani Mkuranga, inalojengwa na kampuni ya BQ Contractors Ltd .

Ndikilo alisema endapo ghala hilo litakamilika mwezi sept ,litatumika lakini kama litachelewa ,watakodisha ghala la uhakika kwa ajili ya wakulima wa Mkuranga ambapo wanatarajia kuwa na tani 15,000 hadi 20,000 za korosho kwa msimu unaokuja.

Anasema’,”Ghala hilo linajengwa na bodi ya korosho Tanzania.lengo kubwa ni kuwa na maghala makubwa yatakayohifadhi korosho Kibiti, Mkururanga na Kibaha.

Kwa mujibu wa Ndikilo,lengo ni kupambana na udanganyifu wa zao korosho maana kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani mkoa huo haukuwa ukitumia maghala rasmi .

“Ghala hili mnalojenga RK CHUDASAMA lipo kwenye kiwango ,limekamilika kwa asilimia 90 tunaomba muache milango wazi,kama tutakuja kukodisha kuhifadhi korosho zetu mtupokee”alisisitiza Ndikilo.

Hata hivyo ,alisema serikali imeona ianze kuchukua hatua mapema ili kuepukana na udang’anyifu na hujuma zilizojitokeza msimu huu unaomalizika .

Ndikilo alielezea, kuna baadhi ya AMCOS zilihusika kuchakachua na kutelemsha ubora wa korosho pamoja na kuweka mawe na michanga kwenye magunia ya korosho zilizokuwa zinauzwa kwenye minada .

“Hali hii imetia doa ,,Kuna watu wachache wanataka kuwaharibia wakulima ambao ni asilimia 80 ambayo wanajishughulisha na kilimo,lakini nawapa taarifa serikali haitakubali hata kidogo kuona ubabaishaji huu ukiendelea”alisema Ndikilo.

Mkurugenzi wa RK CHUDASAMA Ltd ,Sundeep Chudasama alikubali kushirikiana na serikali kwa kutoa ghala lake kulingana na makubaliano watakayowekeana.

Alieleza yupo tayari kupangisha ghala hilo ambalo ujenzi wake unakaribia kukamilika na kampuni yake inaendelea kujenga maghala ikiwemo jijini Dar es salaam ambako anayapangisha.

Sundeep alifafanua,mipango yake ni kuendelea kujenga viwanda na ameshajenga maghala mawili wilayani Mkuranga na anawasiliana na wawekezaji wengine ili waje kuwekeza nchini.

“Mie ni mtanzania halisi,nimesoma hapa ,sina tatizo tutashirikiana pamoja na nina ahidi kutoa ghala hili ,kwa mipango na utaratibu tutakaojiwekea,ili kila upande unufaike”alisema Sundeep.

Nae katibu tawala msaidizi uchumi na uzalishaji,mkoani Pwani ,Shangwe Twamala alisema kwasasa mkoa umejiwekea mkakati wa kujenga maghala makubwa matatu ambayo yataondoa changamoto zilizojitokeza hivi karibuni.

Alisema ,wajibu wa serikali ni kuwaunga mkono wakulima ,kwa kuhakikisha wanapata manufaa na tija kupitia jasho wanalolitoa kwa kujishughulisha na kilimo chao.

Twamala ,aliwaasa wale wote wanaojiingiza katika udalali badala ya kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani na kuvitaka vyama vya msingi vya ushirika kuacha kujiingiza kwenye wizi na kuwakandamiza wakulima.

Mwishoni mwa mwezi desemba mwaka 2017,viongozi wa vyama vya ushirika vya msingi (AMCOS) kumi ,walikamatwa na kuhojiwa kutokana na kosa la kufanya udanganyifu wa ubora na uzito wa korosho ,na uchunguzi unaendelea .

Thursday, March 8, 2018

SUBIRA MGALU ATOA MIFUKO 300 YA SARUJI, RUFII, KIBITI NA MKURANGA.



Naibu Waziri Wa Nishati Subira Mgalu ambae pia ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Pwani amekabidhi Mifuko ya Saruji Mia Tatu kwa Viongozi wa Wilaya za Rufiji, Kibiti na Mkuranga katika hafla fupi iliyofanyika terehe 6/3/2018 Ikwiriri.

Msaada huo wa Saruji ni kwa ajili ya Ujenzi unaoendelea kwa nguvu za Wananchi kwenye Vituo vya Afya Wadi za Wazazi Mloka na Nyamwinywili kata za Mwaseni na Kipugira upande wa Wilaya ya Rufiji .

Aidha, kwa upande wa Wilaya ya Kibiti Saruji hiyo inakwenda kutumika katika Ujenzi wa Kituo cha Afya Nyamatanga Rualuke na Sekondari ya kata ya Dimani ambapo Mkuranga Mifuko hiyo itatumika katika ujenzi wa Zahanati ya Kazole na Shule mpya ya Msingi Kisemvule.

Mhe Mgalu ametoa Msaada huo wa Mifuko 300 ya Saruji kufuatia Ziara yake katika wilaya hizo Mwezi Desemba 2017 ambapo alijionea ujenzi wa Miundombinu hiyo kwa nguvu za Wananchi na Wahisani mbalimbali.

Kwa kutambua Umuhimu wa Wilaya hizo hasa maeneo ambayo mradi Mkubwa wa Rufiji Hydropower utatekelezwa mfano Mloka Mwaseni ambapo kuna haja ya kuwa na MiundoMbinu imara ya Huduma Wezeshi Mfano Zahanati na Vituo vya Afya ili kuufanya Mradi utekelezeke Kirahisi na kwa Wakati .

Akizungumza na viongozi hao mara baada ya kukabidhi msaada huo, Mhe Mgalu amewaasa Viongozi wa Maeneo hayo kusimamia vizuri ili Saruji hiyo itumike kama ilivyokusudiwa .

Pia amewaomba Wadau Mbalimbali kujitokeza Kusaidia Ukamilishaji wa MiundoMbinu hii kwa Maslahi ya wananchi wa Maeneo hayo.

Wakipokea Saruji hiyo waheshimiwa Wabunge wa Maeneo hayo wamemshukuru Mhe Mgalu na Kumuahidi kuwa watahakikisha Saruji hiyo itafanya Kazi iliyokusudiwa .

Viongozi hao akiwemo Mkuu wa Wilaya Rufiji Mhe Juma Njwayo amempongeza Mhe Subira kwa kazi nzuri anazofanya na michango yake ya Mara kwa mara katika Sekta mbalimbali .

Naibu Waziri Nishati alikuwa Wilayani Rufiji kuhudhuria Mkutano wa Wadau wa Mradi mkubwa wa Rufiji Hydropower.
 Naibu Waziri Wa Nishati Subira Mgalu, akimkabidhi Saruji Mhe. Mbunge wa jimbo la Mkuranga, Mhe Abdallaah Ulega.

Tuesday, March 6, 2018

MARUFUKU MKAA KWENYE GARI ZA ABIRIA- DC BAGAMOYO.


Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga akiangalia Basi la abiria ambalo limebeba mkaa kwenye buti. 
 Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga akiangalia Basi la abiria ambalo limebeba mkaa kwenye buti. 
...............................................

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga amepiga marufuku ndani ya wilaya yake kupita mabasi ya Abiria ambayo yamebeba Mkaa.

Mkuu huyo wa wilaya ametoa kauli hiyo kwenye oparesheni maalum ya kukagua mazao ya misitu ambayo yanasafirishwa bila ya kuwa na kibali na kukwepa ushuru hali inayopelekea kuikosesha serikali mapato.

Alisema kila mwenye kusafirisha mazao ya misitu ikiwemo Kuni, Mbao, Mkaa na Miti ya ujenzi anapaswa kuwa na kibali kinachomruhusu kuvuna na kusafirisha huku akisisitiza kuwa ndani ya vibali hivyo yapo maelekezo ya wapi muhusika anapaswa kuvuna Mbao, Mkaa au Kuni.

alisema kwa kuzingatia sheria zilizowekwa ndio kutapelekea kulinda mapato ya serikali ambayo faida ya mapato hayo inarudi kwa wananchi kwa kuwatekelezea miradi mbalimbali ya maendeleo.

Katika Oparesheni hiyo maalum, mkuu wa wilaya ya Bagamoyo amebaini mabasi kadhaa Abiria yanayobeba mkaa hali inayohatarisha usalama wa abiria.

Alisema licha ya kukiuka sheria za usalama barabarani, ubebaji wa Mkaa katika mabasi ya Abiria ni hatari kwa usalama kwakuwa baadhi ya magunia ya mkaa yanakuwa na cheche za moto hali itakayopelekea gunia la mkaa kuwaka moto na hatimae Gari lote kuungua na kupoteza maisha ya watu wasio na hatia.

Aidha, aliwataka Abiria kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi kubaini mabasi yote ya Abiria yanayobeba magunia ya mkaa ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheia zitakazokomesha tabia ovu katika sekta ya usafirishaji.

Kwa upande wao Abiria wa mabasi hayo walisema wanakerwa vitendo vya kupakia magunia ya mkaa kwenye mabasi ya abiria kwakuwa hutumia muda mrefu kupakia mkaa njiani.

Walisema katika safari kila mtu anamahitai na umuhimu wake wa kuwahi hivyo kitendo cha kucheleshwa kwasababu ya kupakia mkaa ni kutokujali umuhimu wa safari kwa abiria.

Nao makondakta wa mabasi yanayofanya safari katika barabara ya Chalinze Segera walisema wanalazimika kupakia mkaa ili kufidia kwakuwa kuna shida ya abiria ambapo Gari hutumbea bila ya kujaza na kupelekea kushindwa hata pesa ya kujaza mafuta.

Walisema gunia moja la mkaa wanasafirisha kwa bei ya shilingi elfu kumi ambayo ukizidisha kwa magunia kumi unaweza kupata pesa ya kuongezea kipato.
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga, akiangalia magunia ya mkaa marefu yanayojulikana kwa jina la Shanga mbili, ambayo yapo kando ya barabara ya Chalinze Segera kwaajili ya kusubiri kupakiwa kwenye mabasi ya abiria, pamoja nae kulia ni Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFSA) Halmashauri ya Chalinze, David Ntemi, na wa pili kulia ni Kaimu meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFSA) kanda ya Mashariki, Suleiman Bulenga.
Basi hili limekutwa limepakia magunia kumi ya mkaa makubwa (shanga mbili) kutoka Kimange kuelekea Dar es Salaam, ambapo kila gunia moja hulipiwa shilingi Elfu kumi.

Monday, March 5, 2018

JK. ACHANGIA UJENZI WA SHULE KIBINDU WILAYANI BAGAMOYO.


 Rais Mstaafu wa awamu ya nne nchini Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete akiwasili shule ya msingi Kibindu, kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Alhaj, Majid Mwanga, kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete.

Rais Mstaafu wa awamu ya nne nchini Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete, akizungumza katika shule ya msingi Kibindu iliyopo kata ya Kibindu Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo, wa kwanza kulia ni Mkewe Mama Salma Kikwete, wapili kulia ni Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Alhaj, Majid Mwanga na kushoto ni Mbunge wa jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete.
......................................................
Rais Mstaafu wa awamu ya nne nchini Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete amechangia mifuko 450 ya Saruji ambapo kati ya hiyo mkewe mama Salma Kikwete amechangia mifuko 150 katika uenzi wa shule za Msingi Kibindu, Kweikonje, na Pera katika Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo.

Rais huyo mstaafu wa Tanzania ametoa mchango huo baada ya kutembelea shule hizo ambazo zinaendelea na ujenzi wa kuongeza vyumba vya madarasa ili kukabiliana na msongamano wa wanafunzi ambao wamekuwa wakiandikishwa kwa wingi kila mwaka.

Akitoa mchango huo Rais huyo Mstaafu amewapongeza viongozi wa wilaya, Mbunge pamoja na wananchi kwa kujitolea katika kuhakikisha shule hizo zinaongeza vyumba vya madarasa.

Alisema shule hizo zinamahitaji ya vyumba vya madarasa hivyo ushirikiano ndio njia pekee itakayoweza kusaidia ujenzi wa madarasa hayo.

Hata hivyo ametoa ushauri kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chalinze kuona uwezekano wa kuigawa shule ya Msingi Kibindu ili kuondoa msongamano wa wananfunzi uliopo kwa sasa.

Aidha, alitumia fursa hiyo kumshukuru Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa (TANAPA) Allan Kijazi, kwa kutoa milioni 160 kwaajili kuchangia ujenzi wa shule mbili ikiwemo shule ya msingi Kibindu na Kweikonje.

Dkt. Jakaya alimuomba Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa (TANAPA) Allan Kijazi, kuangalia uwezekano wa kuongeza msaada katika shule ya Msingi Kibindu ili kuwaondolea adha ya msongamano wananfunzi wa shule hiyo.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete alisema anaipongeza Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Shule ya msingi kibindu imeanzishwa mwaka 1952 ambayo kwa sasa ina jumla ya wanafunzi 1407 ambapo mahitaji ya vyumba vya madarasa ni 32 na madarasa yaliyopo kwa sasa ni saba tu.
 Rais Mstaafu wa awamu ya nne nchini Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete akipokelewa na Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Alhaj, Majid Hemed Mwanga mara baada ya kuwasili shule ya msingi Kibindu ambapo alienda kujionea ujenzi wa upanuzi wa shule hiyo.

 Rais Mstaafu wa awamu ya nne nchini Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete
akijenga ukuta wa madarasa yanayoendelea kujengwa katika shule ya msingi Kibindu, huku Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete akiwa saidia fundi kwa kumpa udongo Rais Mstaafu ili kazi ya ujenzi iendelee.
 Mke wa Rais Mstaafu wa Tanzania, Mama Salma Kikwete, ambae pia ni Mbunge wa kuteuliwa akishiriki kujenga ukuta wa madarasa yanayoendelea kujengwa katika shule ya msingi Kibindu.
 Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Alhaj, Majid Hemed Mwanga, (kulia) na Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete (kushoto) wakibeba mawe kwaajili ya kujaza kwenye vyumba vya madarasa vinavyotakiwa kumwagwa zege la jamvi katika shule ya Kibindu.
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Alhaj, Majid Hemed Mwanga, akijenga ukuta wa madarasa yanayoendelea kujengwa katika shule ya msingi Kibindu.

Mbunge wa jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete, akijenga ukuta wa madarasa yanayoendelea kujengwa katika shule ya msingi Kibindu, wakati walipotembelea shuleni hapo pamoja na Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Kikwete.

MAKATIBU WAKUU 15 KUTAFUTA SULUHU ZA CHANGAMOTO ZINAZOKABILI ZIWA MANYARA NA TISHIO LA KUKAUKA KWAKE


Baadhi ya Makatibu Wakuu wakitizama kwa mbali Ziwa Manyara.

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii,Meja Jenerali ,Gaudence Milanzi akiwanesha baadhi ya Makatibu Wakuu namna ambavyo athari za kimazingira zimeanza kuonekana katika Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara .


Mkuruenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa (TANAPA) Allan Kijazi (Mwenye kofia) akiwaonesha Makatibu Wakuu waliotembelea Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara maeneo ya Ziwa Manyara ambayo yameanza kukauka.
Eneo moja wapo la Vivutio vya Utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara likionekana kuanza kukauka kutokana na Athari za kimazingira zinazosababishwa na shughuli mbalimbali za kibinadamu zikiwemo ,Kilimo Uchimbaji wa Madini katika maene ya jirani na Ziwa hilo.

Tuesday, February 27, 2018

VIONGOZI WALIOKULA FEDHA ZA WAKULIMA WA KOROSHO WARUDISHE.



WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema viongozi wa Vyama vya Ushirika waliokula fedha za wakulima wa korosho wilayani Masasi wazirudishe na wakishindwa mali zao zikiwemo nyumba zitauzwa ili kufidia.

Pia Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Bw. Gelasius Byakanwa ahakikishe anawasaka viongozi wa chama Ushirika cha Msingi cha Nanyindwa wilayani Masasi ambao wamekula fedha za wakulima na kisha kutoroka.

Amesema viongozi wa vyama vya Ushirika katika wilaya hiyo si waaminifu, ambapo mwaka wa fedha 2016/2017 jumla ya sh. bilioni 2.3 za wakulima ziliibiwa na viongozi hao, ambapo mwaka 2017/2018 sh. bilioni 1.7 zimeibiwa.

Waziri Mkuu alitoa maagizo hayo jana (Jumatatu, Februari 2018) alipozungumza kwa nyakati tofauti na wananchi pamoja na watumishi wa wilaya akiwa kwenye ziara yake ya kikazi mkoani Mtwara.

Alisema viongozi wa Ushirika wa Nanyindwa ambao wametoroka ni Michael Mkali, Yusuph Mataula, ambapo alimuagiza Bw. Byakanwa kuwasaka na kuwafikisha kwenye vyombo vya dola ili waweze kuchukuliwa hatua zinazostahili.

Pia Waziri Mkuu aliwaagiza Wakuu wa wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuvichunguza vyama vya Msingi katika maeneo na wakikuta kuna kiongozi amekula fedha za wakulima wamkamate na kumchukulia hatua za kisheria.

Alisema wakati wa watu kuomba kuchaguliwa kuongoza vyama vya Ushirika kwa lengo la kujitajirisha umepita na Serikali imedhamilia inawasimamia wakulima wa mazao mbalimbali nchini wakiwemo wa korosho ili kuhakikisha nao wananufaika.

Waziri Mkuu alisema vyama vya Ushirika wilaya hiyo vinaongoza kwa ubadhilifu wa fedha za wakulima ambapo wiki iliyopita Bw. Byakanwa aliwakamata viongozi 36 wa Vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS) wilayani Masasi.

Viongozi hao ambao ni wenyeviti na makatibu wanakabiliwa na tuhuma za ubadhirifu wa fedha za wakulima wa korosho ambazo ni zaidi ya sh bilioni 2.3, ambazo ni malipo ya zao hilo kwa msimu wa ununuzi 2016/2017 na 2017/18.

Alisema mbali na wafanyabiasharahao, pia Meneja wa benki ya NMB tawi la Masasi, Aidan Msuya anaye alikamatwa kwa tuhuma za kufanya muamala wa fedha za malipo ya wakulima sh milioni 45 kwa zaidi ya mara 11 kwa siku moja.

Waziri Mkuu alimpongeza  Bw. Byakanwa kwa hatua alizozichukua dhidi ya viongozi hao na kumuagiza ahakikishe viongozi wote waliosababisha ubadhirifu huo wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Monday, February 26, 2018

WATOTO 6 WAWASHIWA VIFAA VYA USIKIVU (COCHLEAR IMPLANT).



Mtaalam wa Huduma ya Usikivu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Mathayo Majogoro Alfred (katikati) akiunganisha kifaa cha usikivu cha nje na cha ndani ili mtoto Matilda Katobesi aweze kusikia kwa mara ya kwanza. Kulia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Pua, Koo na Masikio, Dkt. Edwin Liyombo akifuatilia na kushoto ni mama wa mtoto huyo, Angelina Cosmas.
................................

Watoto sita ambao wamewekewa vifaa vya usikivu Januari mwaka huu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) leo wameanza kusikia kwa mara ya kwanza baada ya kuwashiwa vifaa hivyo. 

Kuwashwa kwa vifaa hivyo kumeleta furaha kwa wazazi kwani wameshuhudia watoto wao wakisikia sauti kwa mara ya kwanza na hivyo kuwajengea matumaini ya watoto hao kuanza maisha mapya.

Zoezi la kuwawashia vifaa hivyo (Switch On) limefanyika leo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili  kwa kushirikiana na wataalaam kutoka Medel Austria ambao ndio wasambazaji wa vifaa hivyo.

Akizungumza na waandishi wa habari , Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Pua,  Koo na Masikio Dkt. Edwin Liyombo amesema watoto hao walifanyiwa upasuaji wa upandikizaji kifaa cha usikivu Januari mwaka huu ambapo zaidi ya asilimia 80 ya upasuaji huo ulifanywa na watalaam wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili .

 ‘’Watoto hawa wataanza maisha mapya ya kusikia sauti mbalimbali katika mazingira yanayowazunguka baada ya kuunganisha vifaa hivi na kuviwasha’’. Amesema Dkt. Liyombo.

Akifafanua amesema mbali na watoto hao sita lakini pia watoto wengine watano ambao walifanyiwa upasuaji huo mwaka jana  na  wengine sita  ambao walifanyiwa upasuaji huo nchini India nao wamekuja kufuatiliwa maendeleo yao ili kubaini changamoto zinazowakabili  na kupewa ushauri wa kitaalam.  

Akielezea ukubwa tatizo  Dkt. Liyombo amesema takwimu za Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) zinaonesha kuwa katika watoto 1,000 wanaozaliwa,  inakadiriwa kuwa watoto watano wanazaliwa na tatizo kubwa la usikivu .
Pia amesema MNH ipo kwenye mchakato wa kuanzisha utaratibu wa kuwachunguza watoto wachanga ili kubaini mapema wenye matatizo yakutosikia. 

Kwa upande wake Muwakilishi kutoka Medel Fayaz Jafar amesema upasuji huo umekua na mafanikio makubwa kwakua  katika awamu hiyo kumekua na mabadiliko  kwani asilimia kubwa  ya upasuaji umefanywa na watalaam wa MNH  na kwamba hatua hiyo ni ya kuridhisha.

Huduma ya Upandikizaji wa kifaa cha usikivu (Cochlear Implant) ilizinduliwa Juni 7 , 2017 na  Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii , Jinsia , Wazee na Watoto Mheshimiwa Ummy Mwalimu hivyo Tanzania imekuwa nchi ya pili kutoa huduma hiyo katika nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki baada ya Kenya. Aidha Tanzania imekuwa nchi ya kwanza kutoa huduma hiyo  kupitia Hospitali ya Umma ambayo ni Muhimbili yenye hadhi ya ubingwa wa hali ya juu.

Mtoto Matilda kwa mara ya kwanza tarehe 24, Januari, 2018 akianza kutamka baadhi ya maneno baada ya kufundishwa na mtaalamu wa sauti kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Wazazi wa watoto wenye matatizo ya kusikia wakiwa kweny mkutano huo.

Sunday, February 25, 2018

NAIBU WAZIRI ANGELINA MABULA ASHUHUDIA UZINDUZI WA HUDUMA ZA KISASA KITUO CHA AFYA NYAMWAGA TARIME


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula akiangalia vifaa vilivyopo katika kituo cha afya cha Nyamwaga kilichopo wilaya ya Tarime mkoa wa Mara. 
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula akitoa nasaha wakati alipokwenda kushuhudia uzinduzi wa huduma za kisasa katika kituo cha Afya cha Nyamwaga kilichopo Wilaya ya Tarime mkoa wa Mara.
Baadhi ya wananchi wakisikiliza nasaha zilizokuwa zikitolewa na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula wakati wa uzinduzi wa kituo cha afya cha Nyamwaga kilichopo Tarime mkoa wa Mara.
Sehemu ya majengo ya kituo cha Afya cha Nyamwaga kilichopo Tarime mkoa wa Mara .

PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI-WANMM