Wednesday, February 14, 2018

MADIWANI BAGAMOYO WAIKATAA TAARIFA YA UTEKELEZAI WA ILANI.


Diwani wa kata ya Yombo, Mohamed Usinga akitoa msimamo kwa Mwenyekiti wa Halmashauri kuhusu kuiktaa Taarifa ya utekelezaji wa ilani.
............................................

Madiwani wa Halmashauri ya Bagamoyo wameikataa taarifa ya utekelezaji wa ilani ya 2017 kufuatia taarifa hiyo kuwa na mapungufu kadhaa.

Madiwani hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo, Ally Ally Issah wameikataa taarifa hiyo mara ilipofika katika utekelezai wa miradi inayohusu idara ya uvuvi ambapo miradi iliyoainishwa ndani ya taarifa hiyo haipo katika maeneo husika jambo liliwatia hasira madiwani hao na kuamua kuirudisha Taarifa yote kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ili ifanyiwe marekebisho.

Akitoa maamuzi ya Baraza Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo, Ally Ally alisema wanairudisha taarifa yote ka Mkurugenzi ili ipitiwe upya na kunyiwa marekebisho katika maeneo ambayo madiwani hawakuridhika nayo.

Kabla ya Mwenyekiti wa Halmashauri kutoa msimamo huo wa Baraza, madiwani hao walisema ifike wakati sasa wataalamu wa Halmashauri wafanye kazi kwa kuzingatia sheria na kanuni za kazi ili kila mmoja achunge mipaka yake.

Walisema katika kikao cha Baraza kuleta tarifa inayokwenda kinyume na uhalisia katika utekelezaji wa miradi ni kukiuka sheria, na kwamba baraza halitasita kumuwajibisha mtumishi yeyote anaekiuka sheriaa kwa kushindwa kutoa taarifa sahihi za utekelezaji wa ilani.

Walisema madiwani ni viongozi wanaochaguliwa na wananchi kwa lengo la kusimmamia utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa manufaa ya wananchi hivyo si vyema wataalamu wa Halmashauri wanaposhindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo ni wazi kuwa wanawatengezea mazingira magumu madiwani ambao watarudi kwa wananchi kuomba kura kwaajili ya kurudi tena madarakani.

Aidha, Madiwani hao waliwataka wataalamu wa Halmashauri wanapofika katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye maeneo mbalimbali wawasiliane na viongozi wa kata husika ili kuleta ushirikiano kati ya wataalamu hao na viongozi wa kata wakiwemo watendai wa kata na madiwani ili kuondoa sintofahamu inayoweza kujitokeza siku ya kuwasilisha taarifa.

Katika taarifa hiyo idara ya uvui imetaja kujenga kwa mabwawa ya samaki katika baadhi ya maeneo huku madiwani wakishangaa kwakuwa hawajawahi kuyaona mabwawa hayo kwenye maeneo yao.
 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo, Fatuma Latu amekiri kupokea taarifa hiyo na kwenda kuifanyia marekebisho na wataalamu wake ili baadae iwasilishwe ikiwa imekamilika.
Wakati huohuo Katibu wa CCM wilaya ya Bagamoyo, Salum kamote amewaonya wakuu wa idara ambao wanatabia ya kutoa taarifa zisizo sahihi kwani kwa kufanya hivyo wanachangia kuidhoofisha chama tawala katika mikakati yake ya kusimamia utekelezaji wa ilani uchaguzi jambo linaidhoofisha serikali iliyopo madarakani kwa ujumla.

Alisema ni vyema taarifa ikawa wazi kama kuna mradi haujatekelezwa ili chama kijue wapi kwenye madhaifu ili nguvu zielekezwe hapo na kuhkikisha miradi hiyo inateekelezwa kuliko kutoa taarifa za uongo.
Aidha, katibu huyo wa CCM wilaya ya Bagamoyo amewapongeza madiwani Halmashauri ya Bagamoyo kwa uwasilishaji mzuri wa taarifa za kata na hatua waliyochukua kuikataa taarifa ya utekelezaji wa ilani.

Alisema Madiwani ndio wasimamizi wa miradi hivyo wanapaswa kuwa imara katika kuhakikisha miradi yote iliyopangwa na kutengewa mafungu inatekelezwa kwa ukamilifu wake ili kujenga imani kwa wananchi ambao ndio walipewa ahadi za kutekeleza mambo mbalimbali.

Kikao hicho cha Baraza la madiwani Halmashuri ya Bagamoyo kimeanza leo jumatano February 14 ambapo kimejadili taarifa za robo ya pili ambapo madiwani waliweza kuwasilisha taarifa za kata zao.
 Madiwani wa Halmashauri ya Bagamoyo wakifuatilia kwa karibu uwasilishwaji wa taarifa za kata pamoja na kupokea taarifa ya utekelezaji wa ilani ambayo baadae waliikataa kwa pamoja na kumrudishia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo Fatuma Latu kwaajili ya Marekebisho.

 Madiwani wa Halmashauri ya Bagamoyo wakifuatilia kwa karibu
 uwasilishwaji wa taarifa za kata pamoja na kupokea taarifa ya utekelezaji wa ilani ambayo baadae waliikataa kwa pamoja na kumrudishia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo Fatuma Latu kwaajili ya Marekebisho.

BIL. 161.9 ZIMETUMIKA KUBORESHA VITUO VYA AFYA 170.



WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imetumia sh. bilioni 161.9 kuboresha vituo vya afya 170 nchini pamoja na kugharamia huduma ya Afya ya Mama na Mtoto kwa lengo la kuokoa maisha yao.

Amsema Serikali itaendelea kukarabati na kupanua miundombinu ya kutolea huduma pamoja na kununua vifaa vya kisasa katika Hospitali za Mloganzila, Benjamini Mkapa, Dodoma na Hosptali za Rufaa katika Mikoa na Kanda.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Februari 14, 2018) wakati akizindua jengo  jipya la mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa-Amana iliyopo wilayani Ilala jijini Dar es Salaam.

Jengo hilo la ghorofa mbili limejengwa kwa ufadhili wa kundi la kampuni za AMSONS na lina thamani ya sh bilioni 1.2.

Amesema uzinduzi wa jengo hilo  unakwenda sambamba na azma ya Rais Dkt. John Magufuli za kuimarisha sekta ya afya na kuifanya kuwa miongoni mwa sekta za kipaumbele.

Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha inasogeza huduma za afya karibu na wananchi. “Mfano, Hospitali za Rufaa za Amana, Mwananyamala na Temeke, zimeendelea kuhudumia wagonjwa kutoka Zahanati, Vituo vya Afya vya Serikali, binafsi na vya dini kutoka mikoa jirani ya Pwani, Morogoro na Lindi.

Pia amesema Serikali itaendelea kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 – 2020, kuhusu kuwapatia wananchi huduma bora za afya pamoja na kujenga hospitali nyingine za Rufaa kwa ajili ya Kanda ya Kusini, Kati na Magharibi.

Akizungumzia kuhusu changamoto ya idadi ndogo ya watumishi na ukosefu wa huduma za uangalizi maalumu (ICU) katika hospital ya Amana, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kufanyia kazi changamoto zote zilizopo katika sekta ya afya zikiwemo n aza hospital hiyo. 

Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuthamini na kutambua mchango wa wadau mbalimbali pamoja na kuendelea kushirikiana nao katika kuhakikisha kuwa huduma za afya nchini zinaboreshwa.

Hivyo, alitumia fursa hiyo  na kulipongeza kundi la kampuni za AMSON’s lililoamua kujenga jengo la mama na mtoto katika hospital hiyo kwa ushawishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Paul Makonda.

Awali, Mganga Mkuu Hospitali ya Rufaa ya Mkoa – Amana, Dkt. Meshack Shimwella alisema wazazi wanaolazwa katika hospitali hiyo kwa siku ni 180 hadi 250 na uwezo wa hospitali ni vitanda 353, ambapo vitanda 250 vinatumika wodi ya wazazi.

Alisema idadi hiyo hailingani na idadi ya wagonjwa, hivyo kusababisha wakati mwingine wagonjwa kulala zaidi ya mmoja kwenye kitanda kimoja kutokana na kasi ya ongezeko wa wagonjwa wanaolazwa hususani wodi ya watoto na akinamama.

Dkt. Shimwella alisema wamefanikiwa kuongeza jingo la kutolea huduma ya mama na mtoto lenye ghorofa mbili ilililojengwa kwa ufadhili wa AMSONS lenye uwezo wa vitanda 100, ambalo ndilo liliongeza idadi ya vitanda kutoka 253 hadi kufikia 353.

“Kutokana kukamilika kwa jengo hilo kwa sasa akinamama wanaonyonyesha wanalala wakiwa mmoja mmoja, watoto wachanga wanahudumiwa katika mazingira mazuri yanayofanana na viwango Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.”

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Makonda aliwashukuru wafadhili waliojenga jengo hilo kwa sababu si kila mtu anayekwenda hospitali na kukuta changamoto na akaamua kuzifanyia kazi.

Bw. Makonda alisema awali akinamama walikuwa wanalala hadi watatu katika kitanda kimoja, hivyo madhumuni ya ujenzi wa jego hilo ni kupunguza msongamano katika wodi ya wazazi.

MADIWANI CHALINZE WAMUOMBA RAIS AINGILIE KATI KILIO CHA MAJI.



BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Chalinze ,limemuangukia rais Dkt. John Magufuli kwa kumuomba aende kujionea mradi wa maji awamu ya tatu WAMI-CHALINZE ambao umekwama huku wananchi wakiwa hawana maji kwa takriban miezi mitatu sasa.

Wamesema Rais ,ndio mwenye mamlaka za mwisho kwani waziri mkuu alishafika kujionea mradi huo ambapo mkandarasi aliongezewa muda lakini mkataba umekwisha na hakuna kilichofanyika.

Wakitoa kilio hicho ,wakati wa kikao cha bajeti ,baadhi ya madiwani akiwemo diwani wa Talawanda ambae pia ni mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Saidi Zikatimu alisema kuna kila sababu serikali ikaingilia kati na kutoa tamko ili kurejesha imani kwa wananchi.

Alieleza tatizo hilo ni kubwa kwani zipo baadhi ya shule hazina maji safi na salama na wanahofiwa wanafunzi kupata magonjwa ya mlipuko.

“Maji ni tatizo mradi wa WAMI -CHALINZE, kamati ya fedha tulishaenda lakini majibu ya meneja wa CHALIWASA Christer Mchomba  hayakuturidhisha “

“Baraza hili linaimani na Mh.Rais jambo hilo lichukuliwe ufumbuzi wa haraka zaidi ya miezi miwili ama mitatu hakuna maji, serikali itoe tamko kuhusiana na mradi huo “; alisema Zikatimu .

Zikatimu alisema zipo shule za sekondari ya Kikalo ,Miono ,Chalinze hazina maji na wanafunzi wameshaanza kusumbuliwa na magonjwa ya matumbo kutokana na ukosefu wa maji.

Aliomba serikali kuu,CCM na halmashauri ishirikiane kwa hilo ili kupata ufumbuzi.

Zikatimu alieleza kwasasa, wamechukua hatua ya kuzungumza na watu wenye maboza ya kusambaza maji kwenye maeneo muhimu ya kijamii kama mashuleni kwani meneja wa CHALIWASA  aliwaambia kuna uwezekano wa kuchukua maji katika chanzo chao cha maji ambayo yatawasaidia wakati suluhu ikiendelea kutafutwa .

Nao diwani wa kata ya Miono Juma Mpwimbwi,Diwani wa Lugoba Rehema Mwene na diwani wa Kimange Hussein Hading’oka walisema hali ya mradi mkubwa wa aina hiyo iliyofikia ni mbaya na haileti taswira nzuri kwa jamii.

Diwani wa kata ya Miono ,Juma Mpwimbwi,alisikitika kutokuwa na maji ya uhakika kwa miaka mingi hali ambayo inakatisha tamaa wananchi.

“Rais aje kujionea labda kauli yake itasaidia kutatua changamoto ya mradi huu:;”Mradi huu sio rafiki tena na jamii shule hazipati maji na unasababisha usumbufu kwa wanafunzi ambao wakati mwingine inabidi waache masomo wakatafute maji ;” alifafanua Mpwimbwi.

Mpwimbwi alisema ,amehamasisha kila kaya katika kata ya Miono kutoa 2,000 itakayosaidia kulipia maboza yanayosambaza maji yatakayowezesha kusaidia wanafunzi .

“Kuna shule hizi za sekondari ya Miono na Kikalo zinapata shida,walimu wanaogopa kuchangisha wanafunzi kutokana na suala la elimu bure,kila trip moja ya boza kwa wiki ni sh.100,000 ,mkuu gani wa shule atamudu kulipia ama diwani ” alisema Mpwimbwi.

Mkazi wa Bwilingu,Chalinze Zulfa Hassan alieleza wanalazimika kununua madumu ya maji matano hadi kumi kwa siku kwa ajili ya matumizi ya familia.

Alisema uwezo wa kutoa sh.2,500 na 5,000 kila siku hawana hivyo wnaiomba serikali itatue changamoto ya maji Chalinze.

Kwa upande wake ,mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Bagamoyo alhaj Abdul Sharif ,alisema ukienda kwa meneja wa CHALIWASA hupati majibu ya kuridhisha hivyo viongozi kukosa majibu mazuri ya kuwaeleza wananchi.

Alisema ni vyema wizara ya maji ikaeleza kinaga ubaga kinachofuata kwenye mradi baada ya mkataba wa ujenzi wa mradi wa maji WAMI-Chalinze kuisha.

Alhaj Sharif alisema, serikali inafanya juhudi kubwa kuendeleza viwanda na Chalinze ni moja ya halmashauri yenye viwanda na wawekezaji lakini kukosekana kwa maji miezi mitatu anahofu ya kukatisha tamaa baadhi ya wawekezaji .

Meneja wa Chaliwasa alielezea serikali inaendelea kuchukua hatua na kufanya jitihada za kuondoa tatizo la maji tangu mwaka 2001 ,ilipoanza kutekeleza mradi wa maji Chalinze kwa awamu mbalimbali.

Mapema sept mwaka jana Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitembelea baadhi ya viwanda mkoani Pwani ,na kutoa agizo la wiki mbili kwa waziri wa maji kutathmini matokeo ya mwenendo wa mradi wa maji wa mradi wa WAMI CHALINZE ,;:      ili kutoa utaratibu na kama sheria ingeruhusu kuvunja mkataba ikiwa mkandarasi ameshafikia kiwango cha asilimia 50 ya utekelezaji.

Monday, February 12, 2018

MAKAMU WA RAIS AZINDUA MRADI WA KUENDELEZA UTALII UKANDA WA KUSINI (REGROW)


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla kabrasha lenye Andiko la  mradi wa REGROW na Mikataba ya Fedha na utekelezaji wa mradi mara baada ya kuuzindua mradi huo katika eneo la Kihesa Kilolo mkoani Iringa.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa mradi wa kuendeleza utalii ukanda wa kusini mwa Tanzania (REGROW) ,Kihesa Kilolo mkoani Iringa.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipata maelezo ya mpango wa uwekezaji katika miundo mbinu ya mradi wa kuendeleza utalii ukanda wa kusini mwa Tanzania kutoka kwa Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla wakati alipotembelea mabanda ya maonyesho kabla ya kuzindua mradi wa REGROW. 

Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais.

WAZIRI WA NISHATI AZINDUA HUDUMA YA UMEME KIGWE



Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amezindua rasmi huduma ya umeme katika Kata ya Kigwe iliyopo wilayani Bahi, Mkoa wa Dodoma.

Uzinduzi huo uliofanyika mwishoni mwa Juma, Jumamosi Februari 10 mwaka huu, ulienda sambamba na ufunguzi wa Mtambo wa Maji ambao umeweza kufanya kazi kutokana na upatikanaji wa huduma hiyo ya umeme.
Waziri Kalemani alifanya uzinduzi huo akiwa katika ziara ya kazi wilayani Bahi kukagua miradi ya umeme inayotekelezwa wilayani humo.

Awali, akiwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge kumweleza nia ya ziara yake, Waziri alisema kuwa wananchi zaidi ya 200 wataanza kupata umeme kufuatia tukio la kurasimishwa kuwashwa kwa nishati hiyo Kigwe.

“Tunatoa kipaumbele sana kwa Mkoa wa Dodoma kwa sasa kwani ni Makao Makuu. Tunaweka juhudi za makusudi kuhakikisha kwamba wananchi wengi wanapata umeme na huduma hiyo inakuwa ya uhakika,” alisema Dkt. Kalemani.

Akifafanua zaidi, alisema kuwa, Serikali imeanzisha harakati za kufanya ukaguzi kwenye utekelezaji wa Miradi yote ya umeme mkoani humo. 

Alieleza kuwa lengo la kufanya hivyo siyo tu kwa sababu Dodoma ni Makao Makuu bali pia kama Mkoa, imebainika kuwa miundombinu yake katika baadhi ya maeneo imepoteza ubora, hasa nguzo. 

Hii ni kwa sababu eneo hili ni tambarare na hivyo mvua ikinyesha maji yanatuama na kuharibu nguzo mara kwa mara.
“Kwa hiyo tunaendelea na ukaguzi wa miundombinu ili kuhakikisha Dodoma inaendelea kupata umeme wa uhakika muda wote.”

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa pamoja na kupongeza jitihada ambazo Wizara ya nishati imekuwa ikifanya nchi nzima katika kuhakikisha huduma ya umeme inapatikana katika maeneo mbalimbali, pia alimwomba Waziri Kalemani kuupa upendeleo Mkoa huo kwa kuwa ni kitovu cha nchi.

Akiwa katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Bahi katika ziara yake, Waziri Kalemani aliwasisitiza wananchi kufanya maandalizi ili umeme utakapounganishwa katika maeneo yao waweze pia kuunganisha katika makazi yao na katika maeneo yao mbalimbali ya kazi.

Aidha, alitumia fursa hiyo kuwataka viongozi wa Halmashauri mbalimbali za vijiji kote nchini, kuhakikisha wanajiandaa kwa ajili ya kuunganishiwa umeme katika taasisi zote za umma zikiwemo Shule, Vituo vya Afya, Miradi ya Maji, Masoko na nyinginezo.

Vilevile, alikumbushia umuhimu wa kila mmoja kuhakikisha baada ya kuunganishiwa umeme katika eneo lake anakumbuka kulipa bili za huduma hiyo muhimu.

“Usipolipa, Serikali itakukatia umeme hivyo kurudisha nyuma maendeleo yako,” alisisitiza.

Jambo jingine ambalo Waziri Kalemani alisisitiza ni kwa wakandarasi kuhakikisha wanawagawia bure wateja 200 wa kwanza watakaojitokeza kuunganishiwa umeme wa REA, kifaa cha Umeme Tayari (UMETA) kama ilivyoelekezwa na Serikali na siyo vinginevyo.

“Kifaa hicho hakiuzwi kwa sasa hadi wateja 200 wa mwanzo wakamilike na kugawiwa bure ikiwa ni njia ya kuhamasisha wananchi wengi vijijini kujitokeza kuunganisha umeme. Mkandarasi yeyote atakayebainika kuwauzia wananchi au kutowapatia kifaa hicho wale wateja 200 wa kwanza kama tulivyoelekeza, tutamchukulia hatua.”

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Bahi Elizabeth Kitundu na Mbunge wa Jimbo hilo, Omari Baduel walipongeza jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Nishati katika kuhakikisha wananchi, hususan wa vijijini wanafikiwa na huduma muhimu ya umeme.

Akiwasilisha taarifa ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kwa Waziri Kalemani katika ziara hiyo, Meneja wa Shirika hilo wa Wilaya ya Bahi, Kitila Bryceson alisema kuwa, Wilaya hiyo ina jumla ya wateja 1498 wa umeme hadi kufikia mwezi Januari mwaka huu na kwamba ina laini ya umeme yenye urefu wa jumla ya kilomita 78.8 na jumla ya Mashine Poozo (Transfoma) 35 zinazohudumia wananchi, taasisi na viwanda.

Saturday, February 10, 2018

RAIS DKT. JOHN MAGUFULI AMPANDISHA CHEO MOHAMED HASSAN HAJI.


WAZIRI MKUU AMJULIA HALI MWENYEKITI WA CWT SINGIDA



WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemtembelea na kumpa pole Mwenyekiti wa Chama Cha Walimu (CWT) mkoa wa Singida Mwalimu Aron Jumbe aliyelazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).
Akiwa hospitalini hapo leo (Jumamosi, Februari 10, 2018), Waziri Mkuu amefarijika baada ya kumkuta Mwenyekiti huyo na wagonjwa wengine waliolazwa kwenye taasisi hiyo wakihudumiwa vizuri.

Pia Waziri Mkuu amewajulia hali mabinti pacha walioungana Consolata na Maria Mwakikuti ambao nao wamelazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwapa pole wagonjwa hao na kuwaeleza kwamba Serikali inadhamira ya dhati kuhakikisha inaboresha huduma za afya na kwamba madaktari wataendelea kuwahudumia vizuri ili kuhakikishia afya zao zinaimarika na kurejea katika shughuli zao za kila siku

Kwa upande wake, Mwalimu Jumbe alimshukuru Waziri Mkuu kwa kutenga muda wake na kwenda kumjulia hali. Aliwashukuru madaktari na wauguzi wa taasisi ya JKCI kwa huduma nzuri wanazompatia tangu alipofika hospitalini hapo.

Kwa upande wao Maria na Consolata walishukuru kwa msaada wa huduma za matibabu wanazozipata na kwa sasa wanaendelea vizuri. Pia walimshukuru Waziri Mkuu kwa kwenda kuwajulia hali na kumtakia kheri katika shughuli zake

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, FEBRUARI 10, 2018.

DC BAGAMOYO AWAONYA BODABODA.


Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Alhaj, majid Hemed Mwanga, amewaonya waendesha pikipiki (Bodaboda) kuzingatia sheria za uslama barabarani ikiwa ni pamoja na kuvaa kofia ngumu ili kuepuka ajali za mara kwa mara na zenye madhara.

Mkuu huyo wa wilaya alitoa kauli hiyo alipofanya Mkutano wa hadhara katika kitongoji cha Maji Coast kata ya Magomeni katika utaratibu wake wa kuhutubia kila kata zilizopo ndani ya wilaya yake.

Alisema mwendo kasi, upakiaji wa mishikaki pamoja na kutovaa kofia ngumu ni miongoni mwa sababu zinazopelekea ajali zenye madhara kwa bodaboda.

Alisisitiza kuwa boda anapaswa kovaa kofia ngumu kila aendeshapo bodaboda na kumuagiza Mkuu wa polisi wilaya ya Bagamoyo kufuatilia waendesha bodaboda wote wilayani humo kama wanafuata sheria.

Aidha, alisema wazazi na jamii kwa ujumla wanapaswa kuwaelimisha vijana wao wanaoendesha boda boda juu ya kujifunza sheria za barabarani na kuzifuata wakati wa kuendesha kwani madhara yatokanayo na ajali za bodaboda si ya familia tu bali ni Taifa kwa ujumla kwa kupoteza nguvu kazi ya Taifa.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa wilaya ambae pia ni Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya amewataka waendesha Bodaboda wote wilayani humo kuacha kujihusisha na ubebaji mali za magendo ikiwa ni pamoja ubebaji wahamiaji haramu,

Alisema vijana wengi wa Bodaboda wanabeba bidhaa za magendo ikiwemo sukari, mafuta ya kula na vinginevyo na kupelekea kuikosesha serikali mapato huku wahamiaji haramu wakitumia bodaboda kupitishwa njia zisizo rasmi kufika wanapotaka.

Wakati huo huo amepiga marufuku mgambo kukamata Bodaboda kwakuwa Mgambo hawajui sheria za barabarani na ukamataji wao pia unakiuka sheria.

Alimtaka Mkuu wa polisi kusimamia hilo kuhakikisha kuwa bodaboda zote zinazokiuka sheria za usalama barabarani na zile zinazojihusisha na biashara za magendo polisi wahusike kuzikamata na sio mgambo.
Kwa upande wake Mkuu wa Polisi Wilaya ya Bagamoyo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Adam Maro alisema kila mwananchi anapaswa kutii sheria bila ya shuruti.

Alisema jeshi la polisi kazi yake kulinda usalama wa raia na mali zao na kuzuia uhalifu hivyo kila mwananchi anapaswa kuisaidia polisi katika kuhakikisha kuwa uhalifu hautokei kwenye mitaa mbalimbali.

Alisema ameandaa utaratibu wa kutoa elimu kwa raia juu ya utii wa sheria hivyo kupitia wenyeviti wa vitongoji mikutano ya hadhara itaandaliwa na jeshi la polisi litafika kutoa elimu ya utii wa sheria bila ya shuruti na jinsi ya kukabiliana na uhalifu kwenye maeneo wanayoishi.

Akizungumzia swala la ulinzi shirikishi SSP. Adam Maro alisema ulinzi shirikishi unambulika kisheria hivyo utekelezaji wake unapaswa ufanyike kwa makubaliano ya wananchi wenye na njia zipi na wakati gani wafanye huo ulinzi shirikishi.
Wananchi wa Kitongoji cha Maji Coast kata ya Magomeni wilayani Bagamoyo wakifuatilia Mkutano ulioitishwa na Mkuu wa wa Wilaya.

WATOTO WASIRUDISHWE NYUMBANI SABABU YA MICHANGO-MAJALIWA



*Asisitiza ni kinyume na maelekezo ya Serikali.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kitendo cha watoto kurudishwa nyumbani kwa sababu ya mzazi au mlezi kuto changia michango shuleni ni kinyume na maelekezo ya Serikali.

Amesema Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilitoa Waraka wa Elimu Namba 3 wa mwaka 2016 ambao pamoja na mambo mengine, ulipiga marufuku michango ya aina yoyote isiyo ya lazima katika Elimumsingi. 

Waraka huo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 sambamba na maelekezo ya Ibara ya 52(a) ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015-2020 inayosisitiza utoaji wa Elimumsingi bila malipo.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Februari 9, 2018) bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa 10 wa Bunge la 11. Bunge limeahirishwa hadi Aprili 3, mwaka huu.

Amesema katika siku za hivi karibuni kumejitokeza malalamiko kuhusu baadhi ya shule kuchangisha michango mbalimbali kutoka kwa wazazi na walezi na kusababisha watoto kurudishwa nyumbani kwa sababu ya mzazi au mlezi kuto changia michango shuleni.

“Napenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa watendaji wa elimu kuanzia Wakurungezi wa Halmashauri pamoja na wadau wote wa elimu kuzingatia maelekezo ya Waraka uliotolewa na Serikali, ambapo majukumu ya kila mdau katika kutekeleza Mpango wa Elimumsingi Bila Malipo yamefafanuliwa.”

Akizungumzia fedha zilizotolewa katika utekelezaji wa mpango huo, Waziri Mkuu amesema katika kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba, 2017, Serikali imetuma moja kwa moja shuleni jumla ya sh. bilioni 124.8.
“Fedha zinazopelekwa moja kwa moja shuleni kwa mwezi ni shilingi bilioni 20.8 na shilingi bilioni 3.06 hupelekwa Baraza la Mitihani kwa ajili ya fidia ya gharama za mitihani kwa wanafunzi wa shule za Serikali. “

“Ruhusa ya michango shuleni ipo, kutoka mtu mmoja mmoja, vikundi au Taasisi. Hata hivyo, michango yote sasa itafikishwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ili ashirikishe Kamati ya Shule za Msingi na Bodi kwa Shule za Sekondari. Walimu wasisumbuliwe na michango ili wajikite na taaluma.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kukusanya taarifa kutoka shule mbalimbali za Sekondari za Serikali kwa lengo la kujua hali ya umiliki wa ardhi katika shule hizo. 

Hatua hiyo imekuja kufuatia kuwepo kwa changamoto ya umiliki wa ardhi kutokana na baadhi ya shule kutokuwa na hati miliki, ambapo inatarajia   kuhusisha shule za Sekondari Kongwe zipatazo 89. 

Amesema zoezi hilo litakapokamilika litawezesha Serikali kuandaa hati miliki kwa shule zenye umiliki wa Serikali na pia kufanya maamuzi kwa shule ambazo umiliki wake uko chini ya taasisi za dini. 

Waziri Mkuu amesema kupitia zoezi hilo maeneo ya mipaka ya shule ikiwemo viwanja vya michezo vitatambuliwa na kujumuishwa kwenye ramani za shule. “Zoezi la ufuatiliaji wa umiliki wa ardhi kwa shule za msingi na shule za Sekondari zilizobaki za Serikali litaendelea kufanyika ili kuondoa changamoto za migogoro ya ardhi.”


IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,
1.     L. P. 980,
41193 – DODOMA.

IJUMAA, FEBRUARI 9, 2018.

Friday, February 9, 2018

NSSF YATOA MSAADA MASHUKA 600 HOSPITALI YA BAGAMOYO.



Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga (wa tatu kutoka kulia) akipokea Mashuka 600 ikiwa ni msaada kutoka Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) anaemkabidhi ni Kaimu Meneja Masoko wa NSSF ( wa pili kulia) Salim Khalfani, kutoka  kushoto ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo, Fatuma Latu, Mwenyekiti wa kamati ya huduma za jamii Dickson Makamba, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo, Ally Ally Issa. 

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga, Timu ya usimamizi wa Afya Halmashauri ya Bagamoyo (CHMT) Madiwani wa Halmashauri ya Bagamoyo, kwa pamoja wakipokea msaada wa mashuka 600 kutoka Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) anaekabidhi wakipeana mikono na Mkuuu wa wilaya ya Bagamoyo ni Kaimu Meneja wa Masoko NSSF, Salim Khalfani.
.........................................
Shirikia la Taifa la hifadhi ya jamii (NSSF) limetoa msaada wa mashuka mia sita (600) kwa Hospitali ya Bagamoyo.

Akizungumza wakati wa kukabidhi mashuka hayo Kaimu Meneja wa Masoko na uhusiano, Salim Khalfani, alisema shirika la NSSF ni shirika linalohudumia jamii hivyo kutoa misaada ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yao katika kujenga mahusiano mema na jamii.

Aidha, alimtaja Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo kuwa ni kiongozi anaejali watu wake anaowaongoza hali iliyompelekea kuomba msaada wa mashuka kwa shirika la NSSF.

Akizungumza wakati wa kupokea msaada huo Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Alhaj, Majid Mwanga aliwashukuru NSSF kwa msada huo ambao ni muhimu katika sekta ya Afya.

Alisema Hospitali ya Bagamoyo inakabiliwa na changamoto kadhaa na kwamba serikali ya wilaya kwa kushirikiana na ofisi ya Mkurugenzi wa Bagamoyo imejipanga kutatua changamoto hizo kupitia wadau mbalimbali waliopo ndani na nje ya Bagamoyo.

Mkuu huyo wa wilaya ya Bagamoyo, alimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo kuhakikisha anafanya utaratibu wa ununuzi wa mashine ya kufulia ili mashuka hayo yadumu katika hali ya usafi muda wote.

Aidha, alitumia nafasi hiyo kuwataka Madaktari na manesi katika Hospitali ya wilaya ya Bagamoyo kuacha kutoa lugha chafu kwa wagonjwa na kwamba watekeleze majukumu yao kwa mujibu wa maadili ya kazi yao.

Alisema uboreshaji wa vitanda vya wagonjwa kwa kuweka mashuka mapya uende sambamba na uwajibikaji ili kuleta faraja kwa Hospitali hiyo ambayo inahudumia watu kutoka ndani na nje ya Bagamoyo.

Nae Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Dkt. Salvio Wikesi alisema anamshukuru Mkuu wa wilaya kwa juhudi ya kutafuta wahisani ili kuweza kusaidia matatizo mbali mbali katika Hospitali ya Bagamoyo.

Dkt. Salvio alisema Hospitali ya wilaya ya Bagamoyo ina jumla ya vitanda 100 ambapo kwa mujibu wa muongozo wa wizara ya Afya kila kitanda kimoja kinahitaji mashuka nane na hivyo mashuka yanayohitajika ni 800 huku Hospitali ikiwa na mashuka 325 na hivyo kufanya Hospitali hiyo kuwa na upungufu wa mashuka 475 .

Alisema kufuatia msada huo wa mashuka 600 Hospitali hiyo ina ziada ya mashuka 125 kwa sasa na kwamba tatizo la mashuka litakuwa limekwisha kabisa katika Hospitali hiyo.

 Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga, akizungumza mara baada ya kupokea mashuka 600 kutoka Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii, katika Ukumbi wa Halmashauri ya Bagamoyo, kulia ni Kaimu meneja masoko wa NSSF, Salim Khalfani na kushoto ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo, Ally Ally Issa.

Kaimu meneja masoko wa NSSF, Salim Khalfani, akizungumza wakati wa makabidhiano ya mashuka 600 yaliyotolewa na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii, (NSSF).

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo, Fatuma Latu, akizungumza wakat wa makabidhiano ya mashuka 600 kutoka Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Timu ya Usimamizi wa Afya Halmashauri ya Bagamoyo (CHMT) wakifuatilia kwa karibu hafla fupi ya kupokea mashuka 600 kutoka Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii, (NSSF) iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Bagamoyo.