Ugonjwa
usiofahamika ulioripotiwa katika wilaya za Chemba na Kondoa mkoani Dodoma
umechukua sura mpya baada ya wagonjwa kuongezeka kutoka 21 June 19 na kufikia
32 June 24 mwaka huu.
Akitoa Taarifa
kwa waandishi wa Habari leo jijini Dar es Salaam, Waziri wa afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wanawake, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu, alisema kuwa idadi hiyo
imeongezeka baada ya kuripotiwa wagonjwa 11 katika kipindi cha wiki moja na
kufanya jumla ya wagonjwa hao kufikia 32 huku watu waliofariki kutokana na
ugonjwa huo kubakia 7 kama ilivyoripotiwa awali.
Alisema tangu
ugonjwa huo kuanza wagonjwa 12 walipatiwa huduma ya matibabu katika Hospitali
ya mkoa wa Dodoma, na wagonjwa 18 walipatiwa matibabu katika Hospitali ya
wilaya ya Kondoa huku wagonjwa 2 hawakuwahi kulazwa Hospitali.
Aliongozea
kuwa, hadi kufikia jana Hospitali ya mkoa wa Dodoma imebakiwa na wagonjwa 9 na
Hospitali ya wilaya ya Kondoa imebaki na wagonjwa 14 ambapo wagonjwa 3
waliolazwa katika hospitali ya Mkoa wa Dodoma na 2 Hospitali ya wilaya ya
Kondoa hali zao ni tete.
Alisema, atika
jitihada za kutambua kiini cha ugonjwa huu, Wizara imepeleka jopo la Wataalam
huko Dodoma ili waweze kushirikiana na wenzao walioko huko kufanya uchunguzi wa
kina wa ugonjwa huo
Aidha, waziri
Mwalimu, alisema sampuli mbalimbali zikiwemo damu, haja ndogo, haja kubwa,
vinyama vya ini, na sampuli za vyakula zilipelekwa katika maabara za Mkemia
Mkuu wa Serikali, Maabara ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Maabara ya
Taifa ya Magonjwa ya Binadamu na Maabara ya Hospitali ya KCMC (KCRI). Vile vile
sampuli nyingine zimepelekwa nchini Marekani katika maabara ya Kituo cha
Udhibiti wa Magonjwa cha Marekani (CDC) jijini Atlanta kwa ajili ya uchunguzi
zaidi.
Alisema kuwa,
hadi sasa, ni sampuli za nafaka pekee, zilizofanyiwa uchunguzi katika Maabara
ya TFDA ndio zilizoonyesha kuwepo kwa uchafuzi wa sumukuvu (Aflatoxin) katika
sampuli za nafaka hizo,
Waziri
Mwalimu alizitaja sampuli hizo na kusema kuwa,
a) Jumla ya sampuli 13 kati ya 27 (48%) zilikuwa na
uchafuzi wa sumukuvu (aflatoxins) kwa kiasi kisichokubalika kwenye nafaka kwa mujibu wa
viwango vya kitaifa na zote zilitokana na mahindi;
b) Kati ya sampuli hizo zenye sumukuvu, 12 zilitoka
wilaya ya Chemba na sampuli 1 ilitoka wilaya ya Kondoa.
c) Sampuli saba (7) kati ya hizo 12 zilikuwa na kiasi kikubwa cha sumukuvu kinachozidi 150 µg/kg (micrograms per kllogram) kwa total aflatoxins, ambapo wigo wa aflatoxin B1 katika sampuli hizo ni
kati ya 157.1 – 194.4 µg/kg.
d) Kiasi kama hicho kiliwahi kuhusishwa na madhara
yatokanayo na sumukuvu
(aflatoxins) katika nchi za
India, China na Kenya.
e) Dalili za madhara ya sumukuvu
(aflatoxins) zinafanana na dalili za ugonjwa usiofahamika
uliojitokeza katika Wilaya za Chemba na Kondoa
Kufuatia
uchunguzi huo waziri Ummy Mwalimu alisema upo uwezekano mkubwa kwamba ugonjwa
huu umesababishwa na ulaji wa chakula kilichokuwa na sumukuvu na kuleta
madhara.
Aliongeza
kuwa, Ili kuwa na uhakika wa jambo hilo Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wanawake, Wazee na Watoto inasubiri matokeo ya vipimo vya damu na haja
ndogo vilivyopelekwa kwa uchunguzi zaidi katika Maabara ya CDC, Atlanta iliyopo
nchini Marekani ambapo majibu hayo yanatarajiwa kupatikana katika kipindi
kisichozidi wiki moja.
Aidha,
alisisitiza kuwa hayo ni matokeo ya awali ya uchunguzi unaondelea kufanyika ili
kubaini hasa ni ugonjwa gani na unasababishwa na nini huku wizara ikiendelea
kufanyia kazi matokeo hayo.
Alisema wizara itaendelea kutoa
taarifa za mara kwa mara kwa wananchi kuhusu ugonjwa huo kadri taarifa muhimu
zitakavyokuwa zikipatikana.
Waziri Mwalimu alitoa wito kwa jamii,
kuendelea kushirikiana na wataalamu wanaoshughulika na ugonjwa huo, na pale
atakapopatikana mgonjwa apelekwe haraka katika kituo cha Afya cha karibu, ili
aweze kusaidiwa.
No comments:
Post a Comment