Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe
25 Juni, 2016 amezindua kituo cha mawasiliano cha Jeshi la Polisi
ambacho kitarahisisha utoaji wa taarifa za uhalifu na kuharakisha askari
polisi kufika katika eneo la tukio.
Kituo hicho cha kwanza kuanzishwa na Jeshi la Polisi hapa nchini kipo
katika kituo kikuu cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam na kinafanya
kazi kwa kutumia teknolojia ya mawasiliano ya simu na mfumo wa utambuzi
wa eneo (GPS) ambapo askari polisi waliopo katika kituo cha mawasiliano
watakuwa wakipokea simu kutoka kwa wananchi wanaotoa taarifa za matukio
ya uhalifu na kisha kuwaelekeza askari walio jirani ili wafike eneo la
tukio na kukabiliana na wahalifu.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali (IGP) Ernest Mangu
amemueleza Rais Magufuli kuwa kituo hicho kina uwezo wa kupokea simu 18
kwa mpigo kutoka kwa watu wanaopiga simu ya bure namba 111 au 112 kwa
ajili ya kutoa taarifa za uhalifu na kwamba lengo la jeshi hilo ni
kuhakikisha askari wanafika eneo la tukio ndani ya dakika 15.
IGP Mangu ameongeza kuwa kituo hicho kimeanzishwa kwa msaada kutoka
benki ya CRDB iliyotoa shilingi milioni 320, kitaanza kutoa huduma
tarehe 01 Julai, 2016 kikianzia katika mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni
Kanda maalum ya Dar es salaam na polisi imejiwekea malengo ya kuwa na
vituo kama hivyo nchi nzima ifikapo mwaka 2019.
Akizungumza katika uzinduzi wa kituo hicho, Rais Magufuli amelipongeza
Jeshi la Polisi kwa kuanzisha mradi huo na ameahidi kuwa serikali
itahakikisha inaunga mkono mpango huo ikiwa ni pamoja na kulifanyia kazi
ombi la kununuliwa helkopta itakayorahisisha zaidi ufikaji eneo la
tukio.
Aidha, Rais Magufuli amelitaka Jeshi la Polisi kuwanyang’anya silaha
wahalifu kabla hawajawadhuru raia na kupora mali zao ama kusababisha
mauaji, na amewataka viongozi wa jeshi hilo kuwazawadia askari
wanaofanya kazi nzuri ya kupambana na wahalifu.
Dkt. Magufuli pia ametaka jeshi la polisi lisimame imara kuhakikisha
serikali inatekeleza ahadi zake kwa wananchi zikiwemo upatikanaji wa
maji na huduma nyingine za kijamii na kwamba hatarajii kuona mtu yeyote
anafanya vitendo vitakavyosababisha ahadi hizo kutotekelezwa.
Katika hatua nyingine, Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Aboubakar Zubeir
Ali amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli kwa juhudi kubwa anazozifanya katika kuiongoza nchi.
Mufti Mkuu Sheikh Aboubakar Zubeir Ali ametoa pongezi hizo jana jioni
tarehe 24 Juni, 2016 Ikulu Jijini Dar es salaam katika futari
iliyoandaliwa na Rais Magufuli na akatumia nafasi hiyo kuwasihi Waislamu
na watanzania wote kwa ujumla kukataa vitendo vinavyoashiria uvunjifu
wa amani.
“Niwahusie ndugu zangu watanzania wote, kwamba amani ni kitu muhimu
tuitunze amani tuliyokuwa nayo, tuienzi amani tuliyonayo, na hapo
tutakuwa tunaisadia serikali na tutakuwa tunamsadia Mhe. Rais katika
kuilinda amani” Amesema Mufti Mkuu.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
25 Juni, 2016.
No comments:
Post a Comment