Thursday, June 23, 2016

KIKUNDI CHA WAFUGAJI CHALINZE (KIUNG’OMA) CHAKOSA USHIRIKIANO NA AFISA MIFUGO WA KATA .






Katibu wa Kikundi cha Ufugaji Ng'ombe wa Maziwa Chalinze (KIUNG'OMA) Bw. Joel Kibindu.
Kikundi cha wafugaji wa Ngombe wa Maziwa, kinachojumuisha kata ya Bwilingu na Pera, katika Halmashauri ya Chalinze, kimelalamikia kukosa ushirikiano na Afisa mifugo wa kata ya Bwilingu.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, katibu wa kikundi hicho Joel Kibindu alisema mara kadhaa Ng’ombe wamekuwa wakipatwa na ugonjwa na kupelekea kufa kwasababu ya kukosa ushirikiano na Afisa mifugo wa kata hiyo.

Alisema kufuatia hali hiyo wanalazimika kumwita daktari kutoka kata ya jirani ili kutoa huduma jambo ambalo linakwamisha juhudi ya kikundi hicho.

Aliongeza kuwa swala la ufugaji ni swala kitaalamu, hvyo linahitaji kuwa karibu na wataalamu ili kuweza kujua mambo muhimu yanayohusu ufugaji ikiwemo namna bora ya malisho muda wa kuwapa chanjo na kuwatibu wanapopatwa na magonjwa.

Kibindu alisema kikundi hicho kilianzishwa mwezi wan ne mwaka 2015 kina wananchama watano ambapo kwa sasa kina Ng’ombe 10 wa maziwa.

Aidha, alisema kuwa, licha ya kufanikiwa kuwa na Ng’ombe kumi na kupata maziwa,kikundi kinakabiliwa na changamoto ya kukosa soko la uhakika la maziwa na sehemu ya kuhifadhia maziwa pindi wanapokosa wateja.

Kufuatia hali hiyo wameiomba serikali kuwawezesha kupata eneo na vifaa vya kuhifadhia maziwa ili kuepuka hasara wanayoipata sasa.

Katibu huyo wa kikundi alitoa wito kwa jamii kujiunga na vikundi vya ufugaji ili kukabiliana na changamoto za maisha, huku akiwataka maafisa mifugo kutoa kutoa elimu ya ufugaji kwa jamii.

Juhudi za kumpata afisa mifugo wa kata ya Bwilingu kuelezea sababu zinazopelekea kushindwa kutoa ushirikiano na kikundi hicho hazikufanikiwa baada ya simu yake ya mkononi kutopatikana.

No comments:

Post a Comment