Saturday, June 25, 2016

SERIKALI YASITISHA WAGONJWA KULIPIA CHAKULA MUHIMBILI.



Serikali imesitisha utaratibu wa wagonjwa kulipia chakula katika Hospitali ya taifa Muhimbili, mpaka hapo itakapotangazwa tena ili kuondoa hofu kwa wananchi wanaopata huduma katika Hospitali hiyo.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam, na waziri wa Afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake, wazee na watoto Ummy Mwalimu alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema kufuatia malalamiko kutoka kwa wananchi wizara yake imeamua kusitisha utaratibu wa kulipia chakula wagonjwa katika Hospitali hiyo ya taifa Muhimbili.

‘’nimepokea maoni mengi kutoka kwa Wananchi na Wadau mbalimbali kuhusiana na hatua iliyochukuliwa na Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambapo itaanzisha utaratibu utakaowezesha wagonjwa kuchangia gharama ya chakula ili chakula kiweze kuandaliwa na Hospitali badala ya utaratibu wa sasa ambapo mgonjwa huletewa chakula kutoka kwa ndugu wanaomhudumia’’.Alisema.

Alisema, kufuatia hali hiyo kuleta wasiwasi kwa wananchi na wagonjwa, wizara yake imeiagiza Hospitali ya Taifa Muhimbili kusitisha utaratibu huo mpaka hapo itakapopata taarifa za kutosha kuhusu faida na hasara za utaratibu huo mpya unaopendekezwa.

Hata hivyo alisema kuwa, uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili ulikuwa nalengo la kuboresha huduma ya chakula kwa wagonjwa ukilinganisha na sasa.

No comments:

Post a Comment