Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania leo, Mjini Dodoma limepitisha
muswada wa marekebisho ya sheria ya Elimu kifungu kinachoeleza kuwa mtu
anayempatia ujauzito mwanafunzi wa shule ya msingi au sekondari kuwa adhabu
yake ni faini isiyozidi shilingi laki tano au kifungo kisichozidi miaka
mitatu.
“Muswada unapendekeza kuwa kifungu hicho kifutwe na badala yake
kitungwe kifungu kipya cha 60A ili kuweka masharti yanayojitosheleza kuhusu
zuio la kuoa au kumpatia ujauzito mwanafunzi wa shule ya msingi au sekondari,
kinapendekeza adhabu yake iwe kifungo cha miaka 30 gerezani,” alifafanua
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Masaju.
Vile vile mtu atakayebainika kusaidia, kushawishi au kuacha mwanafunzi
wa shule ya msingi au sekondari kuolewa au kuoa anatenda kosa la jinai ambalo
adhabu yake ni faini isiyopungua shilingi milioni tano au kifungo cha miaka
mitano gerezani au vyote kwa pamoja.
Mhe. Masaju aliendelea kwa kufafanua kuwa, sheria hiyo imependekeza
kuwa pale ambapo kosa hilo litafanywa na mtoto basi adhabu yake itakuwa kwa
mujibu wa masharti ya sheria ya motto,
Alifafanua kuwa, kwa sababu sheria ya mtoto inakataza mtoto anayetiwa
hatiani kufungwa gerezani.
Aidha marekebisho hayo katika sheria ya Elimu yanalenga kumjengea
mwanafunzi wa shule ya msingi au sekondari mazingira mazuri ya kumaliza
ipasavyo elimu yake kwa ngazi hiyo.Hivyo basi kila Mkuu wa shule au Mwalimu
Mkuu atawasilisha kwa Kamishna wa Elimu taarifa ya robo mwaka kuhusu matukio ya
ndoa na mimba kwa wanafunzi katika shule yake na hatua zilizochukuliwa.
Sheria ya Elimu inamruhusu mwanafunzi aliyepewa ujauzito kuendelea na
masomo mara tu anapojifungua. Sheria hiyo inasubiri kuwekwa saini na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli ili ianze
kutumika.
No comments:
Post a Comment