Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Alhaji, Majid Hemedi Mwanga,
amewaonya wale wote wenye tabia ya kupitisha au kuingiza madawa ya kulevya
katika wilaya ya Bagamoyo.
Alhaji, Majid alitoa onyo hilo lep mjini Bagamoyo wakati wa
kuadhimisha siku ya kupinga madawa ya kulevya duniani, shughuli iliyofanyika
katika viwanja vya Majengo.
Alisema kamati ya ulinzi na usalama wilaya akiwa yeye ni
mwenyekiti imejipanga kuhakikisha kwamba kila aina mianya inayotumiwa na
wauzaji na waingizaji wa madawa wilayani hapa inazibwa na kwamba atakaekamatwa
hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Aidha, Mkuu huyo wa wilaya amepongeza juhudi zinazofanywa na
kituo kinachowahudumia watu walioathirika na madawa ya kulevya cha Bagamoyo
Soba House kwa kuwahudumia vijana na kurudi katika hali zao za kawaida.
Aliongeza kuwa serikali ya wilaya ya Bagamoyo itashirikiana
na Soba House katika kuokoa masiha ya vijana, ili taifa libaki na nguvu kazi
kwaajili ya maendeleo.
Aliitaka jamii kuacha kuwanyanyapaa wanaotumia madawa ya
kulevya na badala yake jamii itoe msaada wa jinsi gani ya kuwasaidia watumiaji
wa madawa ya kulevya.
Wakati huohuo amewataka viongozi wa dini wilayani hapa
kuhakikisha wanasimamia maadili ya imani zao na kuwajenga vijana kiroho ili
wasiingie katika dimbwi la matumizi ya madawa ya kulevya.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa SOBA HOUSE Bagamoyo, Karim
Banji alisema kituo hicho kimeanzishwa mwaka 2015 kikiwa na vijana 5 ambapo
mpaka sasa kina vijana zaidi ya 45 kutoka katika mikoa mbalimbali ya Tanzania.
Alisema vijana wengi waliweza kufanikiwa kuacha kabisa
matumizi ya madawa ya kulevya na kurejea katika hali zao za kawaida ambapo toka
kuanzishwa kwa kituo hicho jumla ya vijana 100 wamehudumiwa na kurejea katika
maeneo yao wakiwa katika hali nzuri akiwemo msanii wa Bongo fleva Chidi Benz
ambae kwa sasa yuko vizuri.
Aidha alisema kuwa kituo kinakabiliwa na changamoto
mbalimbali ikiwemo ukosefu wa majengo, na kuiomba serikali ya wilaya
kuwawezesha kupata eneo kwaajili ya ujenzi wa kituo kwakuwa majengo
yanayotumika sasa ni ya kukodi.
No comments:
Post a Comment