Tuesday, January 28, 2020

KINONDONI YA SAINI MKATABA NA JWTZ UJENZI WA UWANJA WA KISASA, JENGO LA UTAWALA, MEYA SITTA ASEMA MKURUGENZI KAGURUMJULI NI MSIKIVU.


 Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Mhe. Benjamini Sitta katikati mwenyesuti, akiwa na Kaimu Mkurugenzi Mahudu Kazi wa kwanza kulia,   Luteni Kanali wa JWTZ David Luoga wakipitia nyaraka za mkataba wa ujenzi wa Jengo la Utawala pamoja na Uwanja wa kisasa wa mpira wa miguu.
 Luteni Kanali wa JWTZ David Luoga, akiwaonyesha Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Benjamini Sitta, Kaimu Mkurugenzi Mahudu Kazi, mchoro wa uwanja wa mpira wa miguu utakavyokuwa.  Mwenye shati la kijani kulia ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kinondoni Mhe. Harlod Muruma.

Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Mhe. Benjamini Sitta mwenyesuti akipeana mkono na Luteni Kanali David Luoga wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) mara baada ya kusaini mkataba na ujenzi wa miradi miwili mikubwa  ya Jengo la Utawala pamoja na Uwanja wa mpira wa miguu.
...................................


Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imesaini mkataba na Jeshi la Wananchi Tanzani (JWTZ) kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa kisasa wa mpira wa miguu pamoja na Jengo la kisasa la Utawala la Halmashauri hiyo.
Mkataba huo umesainiwa jana Januari 27, 2020 na Mstahiki Meya wa Halmashauri hiyo Mhe. Benjamini Sitta pamoja na Luteni Kanali David Michael Luoga na kushuhudiwa na watendaji wa Halmashauri hiyo pamoja na Mwenyekiti wa Chama Cha  Mapinduzi CCM Wilaya ya Kinondoni Harlod Maruma.

Akizungumza na wandishi wa habari wakati wa utiaji saini wa mkataba huo, Mhe. Meya Sitta amesema kuwa mradi wa ujenzi wa jengo la utawala utagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 1.6 huku ujenzi wa uwanja wa kisasa wa mpira wa miguu ukigharimu kiasi cha shilingi Bilioni 2.7.

Amefafanua kuwa uamuzi wa kutumia JWTZ umetokana na kufuata ushauri uliokuwa unatolewa na Mhe. Rais Dk. John Pombe Magufuli wakutumia Locol Fundi (Foce Account).

Mhe. Meya amesema kuwa miradi hiyo mikubwa miwili iliyosainiwa  itajengwa na Jeshi la Wananchi kwakuwa wana amini watafanya kazi hiyo kwa umakini mkubwa na wa haraka kulingana na mkataba huo ulivyoeleza.
 “ Tunamshukuru Mhe. Rais wetu mpendwa, Dk. Magufuli kwa kutuonyesha njia ya kufanya kazi kwa kutumia wanajeshi kwa kuwa itakamilika kwa wakati, hapa hakuna michakato, miradi hii mikubwa itafanywa na jeshi la JWTZ” amesema Meya Sitta.

Aidha Mhe. Meya Sitta alisema wanampongeza Mkurugenzi Aron Kagurumjuli kwa kuwa msikivu na kufuata maelekezo.

“tunampongeza Mkurugenzi wetu Aron Kagurumjuli, kwakweli tuna mkurugenzi makini, msikivu ,ambaye anafuata maelekezo na ni mchapakazi ndio mana leo Kinondoni yetu ipo hapa” alisema.

Kwa upande wake Luteni Kanali Luoga ameipongeza Manispaa ya Kinondoni kwa kuwaamini kufanya kazi hiyo na kuahidi kukalimisha ujenzi huo kwa muda wa miezi sita.

Luteni Luoga amesema katika ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu, awamu ya kwanza itakamilika kwa kipindi cha miezi mitatu na nusu na awamu ya pili itatumia miezi miwili na nusu.

Ameongeza kuwa katika ujenzi huo, licha ya kwamba Jeshi la Wananchi litafanyakazi hiyo, lakini pia litatoa nafasi kwa watu wengine ikiwemo Mama ntilie pamoja na vijana wengine lengo likiwa ni kila mwananchi apate kipato.

“ Tunampongeza Mhe. Meya Sitta, Mkurugenzi Kagurumjuli kwa kutuamini, nasisi tunawahakikishia kuwa Jengo la utawala pamoja na uwanja tutakamilisha kwa kipindi cha miezi sita kama ilivyo kwenye mkataba wetu”amesema Luteni Kanali Luoga.

Kwa upande wake  Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kinondoni Mhe. Harlod Muruma amefafanua kuwa ujenzi huo wa miradi mikubwa miwili iliyotiwa saini leo ni utekelezaji wa ilani  CCM.

Imetolewa na Kitengo Cha Habari na Uhusiano
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.
 


 

VULU ATAKA KIPAUMBELE VYOO VYA WASICHANA

Na Omary Mngindi, Kisarawe.

MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Pwani Zaynab Vulu, amewataka mafundi wanaojenga vyoo kwenye shule mbalimbali mkoani hapa, kuweka kipaumbele maalumu katika vyumba upande wa wasichana.

Vulu ametoa rai hiyo katika Kijiji cha Kisangile Kata ya Marui wilaya ya Kisarawe mkoani hapa, alipokwenda kuhamasishaji zoezi la uboreshaji wa daftari la wapigakura, linalotarajiwa kuanza Februali Mosi mpaka saba mwaka huu, huku Mkoa wa Pwani ikiwa ni moja ya mikoa itakayoanza zoezi hilo.

Akiwa kijijini hapo, Vulu alichangia shilingi laki moja na elfu themanini ya kununulia mifuko 10 ya saruji, itayokajengea matundu kumi ya vyoo kwenye shule shikizi kijijini hapo, yenye vyumba vitano, vyoo matundu matatu, walimu wawili na wanafunzi 380.

Alisema kuwa katika ujenzi wa matundu kumi unaotarajiwa kuanza, ni vyema mafundi wakazingatia mazingira ya wasichana, kulingana na hali wanayokabiliana nayo katika kila kipindi, hivyo ni vizuri wakaweka chumba maalumu kwa ajili ya kujisitiri.

"Sisi kina Mama tuna muda maalumu tunaoutumikia, ambao hata katika vitabu vya dini vimeandikwa, hivyo ni vyema kwa viongozi kukaa na mafundi, mkawapatia maelekezo kuhusiana na ujenzi utakaozingatia mahitaji hayo," alisema Vulu.

Kwa upande wake Abdallah Mapanya alisema kuwa shule hiyo yenye vyumba vitano, vinne vimejengwa kwa nguvu za wananchi, huku halmashauri ya wilaya ya Kisarawe ikijenga darasa moja linalotumiwa na wanafunzi wa shule ya awali.

"Masikitiko yetu wana-Kijiji cha Kisangile ni hatua ya kutopatiwa kibari kwa shule hii pia walimu, kwani hapa kama mlivyoona kuna mwalumu mmoja na mwingine wa pili anajitolea tu, tumepeleka maombi yetu lakini hakuna taarifa zozote," alisema Mapanya.

Diwani wa Kata hiyo Salehe Mfaume alisema kwamba shule yao ni shikizi, na kwamba tayari wataalamu wa elimu kutoka halmashauri wameshafika, na kuwaambia wachimbe shimo la matundu kumi ya vyoo kama ilivyo utaratibu wa serikali.

"Nimekutana na wataalamu wanaohusika na elimu, nikawaelezea juhudi za wana-Kisangile, wamefika wakatueleza tuchimbe shimo la vyoo lenye matundu kumi, zoezi ambalo tayari limeshaanza," alisema Mfaume.

Akizungumzia juhudi za wakazi wake kwenye suala la maendeleo, Mwenyekiti wa Kijiji hicho Ally Korongo alisema kuwa, wananchi wamejitolea katika ujenzi huo kwa kuchangia michango ya hali na mali.

MNADA WA 11 WA KOROSHO GHAFI WAAHIRISHWA LINDI.

NA HADIJA HASSAN, LINDI

CHAMA kikuu cha Ushirika cha Lindi Mwambao kinachojumuisha wakulima wa Halmashauri ya Kilwa, Mtama na Manispaa ya Lindi Mkoani humo kimejikuta kikilazimika kusitisha kuendelea na mnada wake wa 11 wa mauzo ya korosho ghafi kwa kile kilichodaiwa kukosekana kwa watoa maamuzi.

Mnada huo ulifanyika katika chama cha msingi Tulieni Amcos Manispaa ya Lindi ambapo jumla ya tani 305 na kg 212 za korosho ghafi zilifikishwa kwenye mnada huo.

Kwa mujibu wa Kaimu meneja Mkuu wa chama hicho Mohamed Mchekenje alisema kuwa kati ya tani 305 na kg 212 , kg 5,720 za Daraja la kwanza na kg 6,074 Kutoka ghala la Buco Manispaa ya Lindi huku kg 10548 za daraja la kwanza na kg 282,870 za daraja la pili zikitoka katika ghala la Nangurukuru kilwa.

Wakati mnada huo unafanyika katika Manispaa ya Lindi, mnunuzi aliejitokeza kwa siku hiyo aliomba kununua korosho za Ghala la Nangurukuru tani 10 na kg 548 kwa bei ya shilingi 1,560 kwa korosho daraja la kwanza na tani 1 na kg 168 kwa shilingi 1,168 kwa korosho daraja la pili.

Baada ya majadiliano ya muda mrefu baina ya Mrajisi wa vyama vya ushirika Mkoa wa Lindi Robert Nsunza, Afisa kutoka Bodi ya Korosho Ayub Mumi wajumbe wa bodi wakapendekeza mnada huo kuahirishwa mpaka pale watakapotangaza tena ili kuwapa fursa wanunuzi wengi kuja kununua korosho hizo pamoja na kuwapa fursa wakulima wa maeneo husika kutokea maamuzi ya kuuzwa kwa korosho zao.

"mnunuzi kuomba kununua korosho za kilwa wakati mnada unafanyika Manispaa haikuwa tatizo kwa wakulima wa hapa kutolea maamuzi endapo bei ingekuwa nzuri lakini kutokana na mazingira haya tumelazimika kusitisha mpaka pale tutakapopanga tena" alisema Mohamed Masudi makamu mwenyekiti.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Ndani wa Bodi ya Korosho Tanzania Ayub Mumi aliwashauri viongozi wa chama hicho kuandika barua na kuiwasilisha bodi ya korosho itakayoeleza sababu ya kuahirisha mnada huo pamoja na tarehe watakayoipendekeza kufanya mnada wa marudio.

"Kama mnakumbuka bodi ya korosho ilishatoa barua kwa vyama kikuu vyote kuwaeleza kuwa tarehe 26 ndio msimu wa korosho unafungwa rasm hivyo ni vyema muandike barua ili kuwajulisha hali halisi na wao wakafahamu kinachoendelea vinginevyo mnaweza kuendesha mnada ambao ni batili" alisisitiza Mumi