Sunday, December 23, 2018

JAFO AKABIDHI KOMPYUTA 25 KWA SHULE 14 ZA SEKONDARI WILAYANI KISARAWE

Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za miko na serikali za mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo kati kati akiwa ameshika moja ya kompyuta ambazo zmezitoa kwa niaba ya serikali, kushoto kwake ni Naibu waziri wa uchukuzi na Mawasialiano Injinia Atashasta Nditiye, na kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo. (PICHA NA VICTOR MASANGU)

Waziri wa Tamisemi Selemani Jafo akizungumza na baadhi ya walimu wa shule za sekondari katika halfa hiyo ya kukabidhi kompyuta 25 kwa shule 14 zilizopo katika halmashauri ya Kisarawe. (PICHA NA VICTOR MASANGU)

.................................................


VICTOR MASANGU, KISARAWE

WAZIRI wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo amewaagiza  wakurugenzi wote  wa halmashauri nchini pamoja na maafisa elimu kuachana  kabisa na vitendo vya kuwanyima fursa walimu ambao wanahitaji kujifunza somo la tehema na badala yake wahakikishe wanatoa vibali bila ya kuwa na ukilitimba wowote kwa lengo la kukuza teknolojia na mawasiliano.

Jafo ametoa kauli hiyo wakati wa halfa ya kukabidhi kompyuta 25 ambazo zimetolewa na serikali kupitia mfuko wa mawasilino kwa wote ambapo zitazinufaisha shule za sekondari 14 zilizopo katika halmashauri ya Kisarawe.

Jafo alibainisha  kwamba lengo kubwa la serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha inawajengea uwezo walimu ambapo hadi sasa tayari walimu  wapatao 570 wameshapatiwa mafunzo maalumu kwa ajili ya somo la tehema ili kuendana na kasi na mabadiliko ya kiteknolojia.

“Kitu kikubwa sisi kama serikali kwa sasa tumejipanga kuhakikisha kwamba somo hili la Tehama kwa walimu linapewa kipaumbele zaidi, lakini sipendi kuona walimu wananyimwa vibali kwa ajili ya kwenda kuongeza ujuzi katika somo hilo hivyo kuanzia sasa ofisi yangu italisimamia hili na kwamba wakurugenzi wote na maafisa elimu msiwanyime vibali kabisa wapeni acheni roho mbaya,”alisema Jafo.

Naye Naibu waziri wa uchukuzi na mawasiliano Injinia Atashasta Nditiye amesema kwamba kwa sasa serikali imeshaanza mchakato kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vituo 20 vya Tehama kwa upande wa Tanzania bara ambapo kwa upande wa Tanzania visiwani tayari wameshajenga vituo vya Tehama vipatavyo  10 ambavyo ni mahususi kwa wanafunzi, wanafanyakazi, pamoja na walimu.


Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo amesema kwamba katika kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano katika kuboresha sekta ya elimu wanatarajia kuanzisha kituo maalumu kwa ajili ya kufundishia somo la tehema kwa walimu pamoja na wanafunzi ili  kuweza kupanua zaidi katika Nyanja ya teknolijia.

Kwa kweli tunaishukuru sana serikali ya awamu ya tano kwa kutupatia vifaa hivi vya kompyuta 25 kwa ajili ya shule zetu za sekondari 14, bah ii itaweza kusaidia kwa kisi kikubwa kuongeza uwezo kwa walimu katika suala zima la teknolojia pamoja na mawasiliano,”alisema Jokate.

Komputa hizo  25 ambazo  zimetolewa kwa shule 14 za Wilayani Kisarawe Mkoa wa Pwani zimenunulia kwa kiasi ya shilingi milioni 43 zitaweza kuwa  ni mkombozi mkubwa kwa walimu pamoja na wanafunzi katika kusaidia suala zima la teknolojia pamoja na mawasiliano.

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo akizungumza jambo na baadhi ya walimu wa shule za sekondari hawapo pichani katika halfa hiyoya ugawaji wa kompyuta hizo, (PICHA NA VICTOR MASANGU)

 

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Kisarawe Mussa Gama wa kwanza kulia akishuhudia ugawaji wa kompyuta hizo ambazo zimetolewa na serikali kupitia mfuko wa mawasiliano kwa wote ambapo shule 14 za sekondari zimeweza kunufaika na msaada huo. (PICHA NA VICTOR MASANGU).

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Kisarawe Mussa Gama wa kwanza kulia akishuhudia ugawaji wa kompyuta hizo ambazo zimetolewa na serikali kupitia mfuko wa mawasiliano kwa wote ambapo shule 14 za sekondari zimeweza kunufaika na msaada huo.(PICHA NA VICTOR MASANGU)

ABDUL SHARIFU ATAKA WAISLAMU WASHIKAMANE

Na Omary Mngindo, Tanga

WAUMINI wa Dini ya Kiislamu hapa nchini, wametakiwa kuendeleza umoja, upendo na mshikamano, katika kuiendeleza dini hiyo ya Mwenyeezimungu.

Ushauri huo umetolewa na Alhaj Abdul Sharifu kutoka Bagamoyo Mkoa wa Pwani, akitoa mawaidha katika hafla ya Dhikri iliyofanyika kwenye Msikiti wa Masjid Az Hall uliopo Kijiji cha Kwenkwale, Halmashauri  ya Mkata, Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.

Aidha Alhaj Sharifu amewaomba viongozi na Waumini wote wa dini hiyo, kukemea vikali matumizi mabaya ya Dufu yaliyoshamiri maeneo nbalimbali, ambapo alisema kuna baadhi yao wanayatumia kwenye ngoma aina ya Viduku.

Wakiongozwa na Mwenyeji wao Alhaj Sheikh Juma na Ma-Alhaj kutoka mikoa mbalimbali waliohudhulia Ziara hiyo, pia Sharifu amewataka waumini hao kurudisha utaratibu uliokuwa unatumiwa na Masheikh ya kutembeleana na kukumbushana mambo yanayoihusu dini hiyo kwani hayo ndio mafundisho ya Mtume Muhammadi Swalallaahu Alayhi Wasalam.

"Waislamu wenzangu kwenye miaka ya hivi karibuni dini yetu inapoteza mwelekeo, inatupasa viongozi tusimame imara katika kuhakikisha dini yetu inarejea katika mstari wake, kuna mtindo unazidi kushika kasi wa dufu kutumika kwenye ngoma ya Viduku," alisema Alhaj Sharifu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Alhaj Juma aliwashukuru Ma-Alhaj, Mashehe na waumini wote kutoka maeneo tofauti waliohudhulia, huku akisema kwamba wamekuwa katika harakati kubwa za kuiendeleza dini, huku akitoa nasaha kwa vijana kutojiingiza katika mambo ya kidunia.

"Masheikh pamoja na juhudi tunazozifanya za kuipogania dini yetu, tunapaswa kuiendeleza umoja, upendo na mshikamano, pamoja na kuhakikisha vijana wetu wanafuata misingi imara ya dini ya kiislamu," alisema Alhaj Juma.

Waumini hao kutoka mikoa mbalimbali ndani na nje ya Mkoa wa Tanga, wameshiriki hafla ya Dhikri hiyo nwishoni kwa wiki.

Waumini wa dini ya kiislamu wakiwa katika hafla hiyo iliyofanyika katika msikiti wa Az hall, uliopo Kijiji cha Kwenkwale, Halmashauri  ya Mkata, Wilaya ya Handeni mkoani Tanga.

Saturday, December 22, 2018

SUBIRA MGALU AWAPA FARAJA PONGWE KIONA


Naibu waziri wa Nishati, Subira Khamisi Mgalu akipokelewa na viongozi wa kata na kijiji cha Pongwe Kiona.
 
Naibu waziri wa Nishati, Subira Khamisi Mgalu akizungumza na wananchi wa kijiji cha Pongwe Kiona.
.....................................

Naibu waziri wa Nishati, Subira Khamisi Mgalu amewapa faraja wananchi wa Kijiji cha Pongwe Kiona kilichopo kata ya Kimange Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo.

Wananchi wa Pongwe Kiona wamepata faraja hiyo baada ya kumuona naibu waziri kuwasili katika kijiji hicho ambacho hakina historia yakufikiwa na kiongozi mkubwa wa wizara.

Akifungua mkutano mbele ya Naibu waziri wa Nishati, Mwenyekiti wa Kijiji cha Pongwe Kiona alisema mara ya mwisho kijiji hicho kilitembelewa na waziri wa mambo ya ndani mwaka 1960 na kwamba toka wakati huo mpaka sasa hajawahi kufika waziri wala naibu waziri.

Aliendelea kusema kuwa, kwa ujio wa Naibu waziri wa Nishati, Subira Mgalu wananchi wa kijiji cha Pongwe Kiona wamepata faraja kubwa ya kuona serikali inawajali, inawathamini na kuamini kuwa matatizo yao yatasikilizwa.

Naibu waziri wa Nishati, Subira Khamisi Mgalu, amefika katika kijiji hicho kuangalia changamoto inayowakabili wananchi wa kijiji hicho kuhusu nishati ya umeme ambapo amewahakikishia kuwa, kazi ya kufikisha umeme katika kijiji hicho itaanza Tarehe 01 mwezi Julai 2019.

Alisema katika kipindi hicho vijiji vyote vya kata ya Kimange ambavyo vipo katika mpango wa usambazaji umeme vijijini (REA) awamu ya tatu vitafikiwa na kupatiwa umeme.

Aliongeza kwa kusema kuwa serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli inaendelea na mpango wake wa kufikisha umeme vijijini hivyo wananchi waondoe hofu kila kijiji kitapata umeme.

Alifafanua kuwa Tanzania ina vijiji 12, 268 ambapo wakati serikali ya awamu ya tano inaingia madarakani imekuta vijiji 8,783 havina umeme na kwamba utekelezaji umeanza na vijiji 3,559 na baadae kumalizia vijiji vilivyobaki ili umeme upatikane kijiji hadi kijiji.

Aidha, Naibu waziri huyo wa Nishati amewataka wananchi wanaosubiri miradi kutekelezwa kwenye vijiji vyao kufanya maandalizi ya kuupokea umeme ili miradi itakapoanza iswachukue muda mrefu wawe wamepata umeme kwa gharama nafuu ya 27,000 tu.

Kufuatia hali hiyo wananchi wa kijiji cha Kimange wamempongeza Naibu waziri huyo kwa kazi kubwa anayofanya ya kuleta mabadiliko katika sekta ya umeme.

Aidha, wamemzawadia mbuzi kwa furaha ya kufikiwa na Naibu waziri katika kijiji hicho toka miaka hamsini iliyopita.

Awali, akimkaribisha Naibu waziri, Diwani wa kata ya Kimange Hussein Hading'oka alisema vijiji vya kata ya Kimange vinakabiliwa na changamoto ya kukosa umeme na kufanya mazingira ya utendaji kazi kuwa magumu hasa katika Zahanati wakati wa kujifungua kinamama nyakati za usiku.

Alimuomba Naibu waziri wa Nishati kuangalia uwezekano wa kuondolea adha ya kukosa umeme wananchi wa vijiji vya kata ya Kimange.

Meneja wa TANESCO Chalinze Zakaria Masalu akitoa ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa Mradi wa umeme katika vijiji vya Pongwe Kiona na Pongwe Mnazi.
Naibu waziri wa Nishati, Subira Khamisi Mgalu akipokea zawadi ya Mbuzi kutoka kwa wazee wa Pongwe Kiona baada ya furaha yao ya kumuona Naibu waziri katika kijiji hicho baada ya kipindi cha miaka 58 kupita.

NAIBU KATIBU MKUU MAMBO YA NDANI AFANYA UKAGUZI KITUO CHA MABASI YA UBUNGO

Naibu  Katibu  Mkuu  wa  Mambo  ya  Ndani  ya  Nchi, Ramadhani Kailima,  akizungumza  na  abiria  katika  Kituo Kikuu  cha  Mabasi  Ubungo, wakati  wa  ziara  ya ukaguzi  wa mabasi  yanayosafirisha  abiria  kwenda  mikoa  mbalimbali nchini.

Naibu  Katibu  Mkuu  wa  Mambo  ya  Ndani  ya  Nchi, Ramadhani Kailima,  akitoa elimu  kwa   abiria  katika  Kituo Kikuu  cha  Mabasi  Ubungo, wakati  wa  ziara  ya ukaguzi  wa mabasi  yanayosafirisha  abiria  kwenda  mikoa  mbalimbali nchini.

Naibu  Katibu  Mkuu  wa  Mambo  ya  Ndani  ya  Nchi, Ramadhani Kailima,  akimsikiliza Mkaguzi wa magari kutoka Kikosi cha Usalama Barabarani, Inspekta Ibrahim Samwix (kulia),  wakati  wa  ziara  yake ya  ukaguzi  wa mabasi  yanayosafirisha  abiria  kwenda  mikoa  mbalimbali nchini.

Naibu  Katibu  Mkuu  wa  Mambo  ya  Ndani  ya  Nchi, Ramadhani Kailima(kulia),  akishuhudia ukaguzi wa magari katika  Kituo Kikuu  cha  Mabasi  Ubungo, wakati  wa  ziara  ya ukaguzi  wa mabasi  yanayosafirisha  abiria  kwenda  mikoa  mbalimbali nchini.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Friday, December 21, 2018

JESHI LA POLISI LATAKIWA KUJENGA UCHUMI WA KISASA.

Na.Immaculate Makilika – MAELEZO

Jeshi la Polisi nchini limetakiwa  kuwa na mwelekeo mpya  wa kujenga uchumi wa kisasa, kwa kushiriki katika shughuli za ujenzi wa viwanda sambamba na sera ya Serikali ya Awamu ya Tano ya ujenzi wa viwanda na kufikia nchi yenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2020.

Akizungumza  leo jijini Dar es salaam, wakati alipokuwa mgeni rasmi katika hafla ya kuwatunuku vyeo wahitimu 513  waliofaulu zaidi mafunzo ya  Uofisa na Ukaguzi, katika Chuo cha Taaluma ya Polisi kilichopo Kurasini jijini Dar es salaam, Rais Magufuli alisema kuwa imefika wakati Jeshi  la Polisi kuwa na mwelekeo mpya wa uchumi wa kisasa ili kusaidia majeshi hayo kuwa na uwezo wa kujiendesha vizuri bila kutegemea sana Serikali.

“Mtafute mwelekeo mpya wa majeshi yetu, unaolenga kujenga uchumi wa kisasa, mjipange kushiriki shughuli za uchumi hasa ujenzi wa viwanda, pamoja na kupanua wigo wa kutengeneza sare zenu, na bidhaa mbalimbali za viatu au maji hali itakaosadia kuwa na bidhaa za ziada badala ya kununua  na kuweza kujiendesha” alisema Rais Magufuli
Rais Magufuli alitolea mfano baadhi ya majeshi kushiriki katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo barabara ,ambapo alisema  Jeshi la nchi ya China  limejenga mji mkubwa nchini humo.

Aidha, Rais Magufuli amelitaka Jeshi la Magereza kushirikiana na majeshi mengine nchini likiwemo Jeshi la Polisi kwa kutengeneza bidhaa mbalimbali pamoja na kusaidiana masuala kadhaa.

Sambamba na hilo, Rais Magufuli ameahidi kukipatia Chuo cha Taaluma ya Polisi nchini kiasi cha shilingi milioni 700 kabla ya ijumaa wiki ijayo kwa ajili ya kukarabati chuo hicho kwa kujenga mabweni na madarasa ya kisasa kwa lengo la kuboresha hali ya chuo na kuongeza ufanisi kwa wahitimu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro, alisema  ujenzi wa makazi ya Polisi unaendelea kwa kutumia fedha walizopewa  na Serikali kiasi cha shilingi bilioni 3.7, na wanatarajia  kukarabati nyumba 400 za Polisi mara baada ya kupewa kiasi cha fedha kilichobaki ikiwa ni  ahadi ya Rais Magufuli, aliyoitoa mapema mwaka huu ya kuwapa  Jeshi hilo shilingi bilioni 10 ambazo ameahidi kuwapa ndani ya  kipindi cha wiki moja.

Vilevile, IGP Sirro, alisema kuwa nchi iko salama kwani hali ya uhalifu imepungua kwa kuwa Jeshi la Polisi  limeendelea kufanyakazi kwa kuzingatia nidhamu na weledi

“Hali ya uhalifu imepungua nchi nzima,makosa ya barabarani yamepungua kwa asilimia 32.6, ajali zimepungua kwa asilimia 30.8, kwa ujumla kumekuwepo na upungufu wa matukio ya uhalifu kwa sababu Jeshi la Polisi linashirikiana na wananchi katika kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao”alisema IGP Sirro

Naye, Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi, Anthony Rutashugurugukwa, alisema kuwa  mafunzo hayo yanayotolewa kwa lengo la kupanda daraja na vyeo  yalidumu kwa muda wa miezi sita, ambapo wanafunzi 513 walihitimu masomo hayo yaliyogawanyika katika  sehemu mbili za mafunzo ya Ukaguzi na Uofisa.

Wahitimu wa mafunzo ya Uofisa walikuwa 120 ikiwa wanaume 106 na wanawake 14. Aidha, katika mafunzo ya Ukaguzi kulikuwa na wahitimu wanaume 393 na wahitimu wanawake 60.

Naibu Kamishna huyo wa Polisi alisema kuwa wahitimu hao wamepata mafunzo mbalimbali yakiwemo stadi za upelelezi, medani za kivita na masuala mengine mtambuka.

VULLU ATOA MSAADA KATIKA WODI YA UZAZI KISARAWE NA SARUJI MIFUKO 80 KWA AJILI YA UKARABATI WA ZAHANATI NA SHULE


NA MWAMVUA MWINYI, KISARAWE 

MBUNGE wa viti maalum mkoani Pwani, Zainab Vullu ametoa msaada wa mapazia mazito yanayotumika kusaidia kuweka usiri kwa akinamama wanaokwenda kujifungua katika wodi ya uzazi hospital ya wilaya ya Kisarawe. 

Msaada huo unaelezwa kuwaondolea kero waliyokuwa wakiipata akinamama hao kipindi cha nyuma ambapo walikuwa wakikataa kujifungua hospitalini hapo kwa kuhofia kukosa faragha wakati wa kujifungua. 

Mbali ya msaada huo pia ametoa mifuko 80 ya saruji kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya ,zahanati na shule vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya sh.milioni mbili.

Akitoa msaada huo ,Zainab alieleza kipindi cha nyuma akinamama wanaojifungua walikuwa wanakaa sehemu ambayo haijazibwa  jambo ambalo limemsukuma kujitolea mapazia hayo.

“Faragha inaanza tangu pale anapoanza kutafutwa mtoto hadi anapozaliwa lazima usiri uwepo,” alifafanua Zainab.

Nae mkuu wa wilaya ya Kisarawe ,Jokate Mwegelo alimshukuru mbunge huyo na kudai suala la ukosefu wa mapazia hayo ilikuwa ni changamoto kwa akinamama wanaojifungua.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Hamis Dikupatile alisema, serikali imekuwa ikijitahidi kuboresha mazingira ya kutolea huduma lakini bado jitihada zinapaswa kufanywa na kila mmoja.

Mganga mkuu wa halmashauri ya Kisarawe, Jonathan Budenu alibainisha kutokana na changamoto hiyo baadhi ya akinamama walikuwa wakikataa kujifungulia hapo kutokana na hali hiyo.

ALIYOYASEMA NAIBU WAZIRI WA NISHATI, SUBIRA MGALU KATIKA MAHOJIANO NA KINGS FM RADIO MKOANI NJOMBE LEO TAREHE 21/12/2018

# Ziara yangu mkoani Njombe imelenga kukagua miradi ya umeme vijijini ili itekelezwe kwa kasi na kuweza kuunganisha vijiji 125 vya Mkoa wa Njombe vilivyopangwa kuunganishwa na umeme kupitia mradi wa usambazaji umeme wa awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza unaokamilika Juni, 2019.

# Sijaridhishwa na kasi ya mkandarasi kampuni ya Mufindi katika usambazaji umeme vijijini, hata hivyo tayari nimeshazungumza naye na ameahidi kuongeza kasi.

# Nimekagua yadi ya mkandarasi huyo iliyopo Makambako mkoani Njombe na nimekuta ameleta mita za umeme zaidi ya 4000, transfoma zaidi ya 50 na vifaa vingine vinavyohitajika katika kazi ya usambazaji umeme hivyo tunaamini kasi yake sasa itaongezeka.

# Katika mradi wa Makambako- Songea, jumla ya vijini 121 vinasambaziwa umeme katika Mkoa wa Ruvuma na Njombe huku Njombe ikiwa na Vijiji 55.

# Kati ya Vijiji 121 vilivyopangwa kupelekewa umeme katika mradi wa Makambako- Songea, Vijiji 78 tayari vimeshapata umeme.

# Kuhusu changamoto ya uunguaji wa transfoma mara kwa mara mkoani Njombe na wananchi kukosa umeme kwa muda mrefu, nimeagiza TANESCO kuleta kikosi kazi kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa changamoto hii.

# TANESCO izingatie agizo la Waziri wa Nishati, la kuwa na vifaa vya akiba ili linapotokea tatizo la kifaa kuharibika kuwe na marekebisho ya haraka ili kutowakosesha wananchi umeme kwa muda mrefu.

# Vitengo vya manunuzi vya TANESCO katika Kanda mbalimbali vitathmini utendaji kazi wake hasa katika suala la kuwa wabunifu wakati zinapojitokeza changamoto za wananchi kukosa umeme kwa muda mrefu kwa sababu ya vifaa kuharibika.

# Kazi ya usambazaji umeme ilenge pia vituo vya afya 300 vinavyojengwa nchini na kama maeneo hayo yapo nje ya wigo wa wakandarasi wanaosambaza umeme, wakandarasi wawasilishe andiko serikalini ili kuweza kufanyia kazi suala hilo.

# Mkoa wa Njombe ni mdau mkubwa katika mradi wa Umeme wa Rufiji kwani kuna vyanzo vinavyopeleka maji katika mito inayotiririsha maji katika Mto Rufiji hivyo wananchi wahakikishe kuwa hawafanyi shughuli zitakazoathiri vyanzo hivyo.

# Serikali inaendelea kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali ikiwemo gesi asilia ambapo katika zaidi ya megawati 1500 zinazozalishwa nchini, zaidi ya asilimia 50 ya megawati hizo zinazalishwa kwa kutumia gesi.

# Kazi ya usambazaji gesi majumbani imeanza katika mikoa ya Dar es Salaam na Mtwara na itaendelea katika mikoa mingine nchini.

NAIBU WAZIRI WA NISHATI ATAKA WAKANDARASI WASICHELESHE KAZI.

Asema Hali ya hewa isiwe kisingizio cha kuchelewesha miradi ya umeme vijijini.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amewataka wakandarasi wanaosambaza umeme vijijini kutochelewesha utekelezaji wa miradi hiyo kwa kisingizo cha mabadiliko ya hali ya hewa kama vile uwepo wa mvua. 

Aliyasema hayo wilayani Makete mkoani Njombe wakati alipokuwa akikagua kazi ya usambazaji umeme vijijini inayotekelezwa kupitia mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu (REA III) mzunguko wa kwanza.

“ Kabla ya Serikali kuwakabidhi kazi hii ya usambazaji umeme vijijini, mlishafanya upembuzi wa maeneo mnayoenda kufanyia kazi na mnayafahamu vizuri, hivyo basi, iwe Jua au mvua, tunataka kuona kazi hii inaendelea kutekelezwa ili wananchi wengi wapate huduma ya umeme,” alisema Mgalu

Aliongeza kuwa, wakandarasi hao wanapaswa kuwa na mipango mbalimbali ya utekelezaji wa kazi kulingana na hali ya hewa ya maeneo wanayofanyia kazi ili kuweza kusambaza umeme katika vijiji vyote walivyopangiwa na Serikali ifikapo Juni 2019.

Awali, Mkuu Wilaya ya Makete, Veronica Kessy, alimweleza Naibu Waziri kuwa, jumla ya vijiji 29 vimepangwa kuunganishiwa umeme kupitia mradi wa REA III mzunguko wa kwanza ambapo mkandarasi anaendelea na kazi ya usambazaji umeme vijijini, ingawa uongozi wa Wilaya hiyo umekuwa na wasiwasi na kasi yake katika usambazaji umeme.

Kuhusu hali ya upatikanaji umeme, alisema kuwa Wilaya hiyo inapata umeme kutokea mkoani Mbeya lakini laini hiyo ni ndefu na inapelekea changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara hivyo aliomba Wilaya hiyo ipate laini nyingine ya umeme kutokea mkoani Njombe.

Kuhusu suala hilo, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, alisema kuwa, Serikali ilishaona changamoto hiyo ya umeme wilayani Makete na kueleza kuwa Wilaya hiyo ipo katika mpango wa kupelekewa umeme kupitia mradi wa Makambako- Songea ambao umekamilika.

Akiwa wilayani humo, NaibuWaziri aliwasha umeme katika kijiji cha Bulongwa na kukagua miundombinu ya umeme katika Kijiji cha Usagatikwa na Usungilo ambapo alimsisittiza mkandarasi kuongeza kasi ya kusambaza umeme.

Wilaya ya Makete ina Vijiji 96 ambapo vijiji 29 tayari vimeshasambaziwa umeme, vijiji 29 vinasambaziwa umeme kupitia REA III mzunguko wa kwanza na Vijiji 38 vinavyosalia vitasambaziwa umeme kupitia mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu unaotarajiwa kuanza Julai mwakani.



TANZANIA NA UGANDA ZAKUBALIANA KUIMARISHA BIASHARA

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Joseph Kakunda (kulia) na Waziri wa Viwanda, Biashara na Ushirika wa Uganda, Mhe. Amelia Kyabambadde wakibadilishana taarifa ya mkutano kati ya Tanzania na Uganda uliojadili namna ya kuimarisha biashara na kuondoa vikwazo vya kibiashara na visivyokuwa vya kiforodha uliofanyika Mutukula, Uganda tarehe 19 Desemba 2018.
.....................................


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Tanzania na Uganda zakubaliana kuimarisha Biashara
Mkutano kati ya Tanzania na Uganda kujadili namna ya kuimairisha mahusiano ya kibiashara na kiuchumi ulifanyika Mutukula, Uganda kuanzia tarehe 17 hadi 19 Desemba 2018.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Joseph Kakunda na Waziri wa Viwanda, Biashara na Ushirika wa Uganda, Mhe. Amelia Kyabambadde waliongoza ujumbe wa nchi zao katika mkutano huo.

Mkutano huo ulihitimishwa kwa Mawaziri kusaini taarifa ya makubaliano ambayo pamoja na mambo mengine, waliafikiana kuvitafutia ufumbuzi vikwazo vya kibishara na vile visivyo vya kiforodha vinavyozorotesha biashara baina ya nchi hizo mbili.

Mkutano huo ulianza kwa ngazi ya Wataalamu na Makatibu Wakuu ambapo ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Joseph R. Buchwaishaija.

Aidha, Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Mhe. Dkt Aziz Ponary Mlima na Balozi wa Uganda nchini Tanzania, Mhe. Richard Kabonero walishiriki mkutano huo.

Imetolewa na: Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya

Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mutukula, Uganda 20 Desemba 2018

 

KWAMBWA ATOA GARI KUKABILI TEMBO MWAVI

Na Omary Mngindo, Fukayosi

BUNGE wa Jimbo la Bagamoyo Mkoa wa Pwani Dkt. Shukuru Kawambwa, amekubali kutoa gari yake inayotumika kwa kazi za kiofisi, ili itumike kwa doria kwa wakazi waishio kwenye Vitongoji vinavyopakana na Hifadhi ya Mbuga ya Saadani wilayani humo.

Hatua hiyo imetokana na kuwepo kwa adha kubwa ya Tembo, ambao mara kadhaa wamekuwa wakiingia kwenye mashamba ya wakulima hao na hufanya uharibifu mkubwa wa mazao ya wananchi hao.

Dkt. Kawambwa ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki katika Kitongoji cha Segwa, wakati wa mkutano uliohusisha Maofisa wa Idara ya Misitu kutoka Kanda ya Mashariki Makao Makuu jijini Dar es Salaam, waliofika kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi hao. 

Ahadi ya Kawambwa imefuatia wazo jema lililotolewa na Abraham Jullu Ofisa Wanyamapori Kikosi dhidi ya ujangili Kanda ya Mashariki kutoka Makao Makuu jijini Dar es Salaam, ambaye alianza kuwapa pole wakazi hao kwa adha hiyo na kusema kuwa, kuna Chuo Maalumu kinachotoa mafunzo kwa ajili ya wananchi kuwa na elimu ya kudhibiti wanyama hao. 

Kabla ya kauli ya mbunge huyo, Jullu alisema kuwa tatizo la Tembo lipo maeneo mengi hapa nchini, hivyo kutokana na changamoto hiyo kuwa kubwa, wana mpango wa kuwapatia elimu wananchi ya kukabiliana na wanyama hao, wakati askari wao wakiwa wanakwenda maeneo husika kwa msaada zaidi.

"Kama mtakuwa tayari ofisi yetu itawapatia mafunzo ya muda mfupi yatakayosaidia kuwapatia elimu ya kudhibiti wanyama hao, sisi tupo wachache eneo tunalolifanyiakazi ni kubwa, hivyo wakati mnaathiriwa na Tembo mpaka tutoke Dar es Salaam kuja huku athari inaweza ikawa kubwa zaidi," alisema Jullu.

Jullu aliyeambatana na Maofisa wenzake Samsoni Saye na Hemed Matiko, pia wamewahakikishia wakulima hao kwamba wapo nje ya Hifadhi ya Saadani, huku akiwaambia kuwa wakipokea wazo hilo watafika katikati ya wiki hii kwa ajili ya kuanza mafunzo hayo. 

"Katika kufanikisha hili changamoto itakuwa moja, ofisi yetu haina gari za kutosha, zoezi tunakotaka kulifanya linahusika kutembelea maeneo ambayo Tembo huwa anaonekana au kupita, kwa hiyo hatuwezi kutembea kwa miguu lazima ipatikane gari," alisema Jullu. 

Kikao hicho kilichokuwa chini ya Mwenyekiti wa Kitongoji cha Segwa Abdi Amani na wa Kijiji Shaabani Mkumbi, 
Mtendaji wa Kijiji Zahra Swalehe na Maofisa kutoka Bagamoyo, ndipo Dkt. Kawambwa akasema kuwa gari yake inayotumika kwa shughuli za kiofisi itakuwa tayari kwa ajili ya zoezi hilo. 

"Gari yangu ya ofisi ipo itakuja kwa ajili ya zoezi hilo la kuhakikisha mafunzo yanafanyika, ili wananchi wetu waweze kupata elimu ya namna gani ya kuwakabili wanyama hao wanaoharibu mazao yetu," alisema Dkt. Kawambwa. 

Mwenyekiti wa Kitongoji hicho Amani alisema kuwa walivamiwa na tembo tarehe 21 mwezi wa 8, wakarudi tena tarehe 18 wakarejea tena tarehe 20, yena 23 na kwamba tarehe 10 mwezi wa 9 wakarudi kwa mara nyingine wakiwa wawili.

Akitoa neno la shukrani, Mkumbi alianza kwa kumpongeza Dkt. Kawambwa kwa kuguswa na changamoto hiyo, ambayo aliiwasilisha kwa Waziri husika, kisha kupatikana kwa Maofisa hao kufika na kutoa elimu hiyo.