Saturday, February 24, 2018

DAWASA KUONDOA TATIZO LA MAJI BAGAMOYO.


Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga, (katikati) akiongoza Mkutano wa kujadili upatikanaji wa maji Bagamoyo pamoja na kuanzisha mfumo wa kusafirisha maji taka.
........................................................... 
Wadau wa maji wilayani Bagamoyo wamekutana kujadili namna ya kuboresha miundombinu ya maji safi pamoja na kuandaa mpango mkakati wa kuanzisha namna kusafirisha maji taka ili mji wa Bagamoyo ubaki safi na salama.

Mwenyekiti wa Mkutano huo, Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga alisema kufuatia kukua kwa mji wa Bagamoyo ipo haja ya kujadili namna bora ya kusafirisha maji taka badala ya kuwa na maeneo yasiyo rasmi kwa utupaji wa taka.

Alisema lengo la mkutano huo ni kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu mradi wa maji taka ambao DAWASA tayari wameshafanyia upembezi yakinifu juu ya utekelezaji wa mradi huo.

Akizungumza katika Mkutano huo, Mhandisi wa Miradi Chrisitian Gava alisema katika kipindi cha mwaka 2014 mpaka 2016 Mamlaka ya maji safi na maji taka Dar es Salaam (DAWASA) imeongeza uzalishaji kutoka mita za ujazo milioni 262 mpaka mita za ujazo milioni 466 kwa siku  ambazo zinazalishwa katika mitambo ya Ruvu juu na Ruvu chini iliyoko Bagamoyo.

Alisema uzalishaji huo umekuwa hadi kufikia kiwango hicho baada ya kuzinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli Mwezi Juni 2017.

Aliongeza kwa kusema kuwa,  kufuatia hali hiyo uzalishai wa maji kwa ujumla katika maeneo yanayohudumiwa na DAWASA ikiwemo wilaya ya Bagamoyo umeongezeka kutoka mita za ujazo milioni 300 mpaka mita za ujazo milioni 544,000 kwa siku.

Aidha,  alisema uzalishaji wa maji kutoka Ruvu juu, Ruvu chini, mtoni, na Visima vidogo umeongezeka kutoka lita milioni 300 mpaka lita milioni 502 kwa siku.

Alifafanua kuwa, katika kuhakikisha adha ya maji inaondoka katika wilaya ya  Bagamoyo DAWASA inaendelea na mradi wa ujenzi wa tenki la kuhifadhia na kusambaza maji katika maeneo ya mji wa Bagamoyo lenye ukubwa wa mita za ujazo 6000, ambalo lina uwezo wa kuhifadhi maji lita milioni sita.

Alisema Tenki hilo litakapokamilika litahudumia wananchi wa maeneo ya Mpii, Zinga, Kiromo, Kitopeni, Ukuni, Kerege, Buma, Mataya, Bagamoyo mjini na ukanda maalum wa ewekezaji EPZA.

Akizungumzia Mradi wa usanifu wa mpango wa muda mrefu na muda mfupi wa kujenga mfumo wa kutibu majitaka, Mhandisi Christian Gava alisema tayari muandaaji wa mpango mkakati ambae ni Mhandisi mshauri (Consultant) ameshaanza kazi  kwaajili ya kupembua na kuandaa mpango mkakati wa muda mrefu pamoja na kupendekeza  mfumo nafuu wa kutibu majitaka katika wilaya za Kibaha, Bagamoyo na eneo  maalum la uwekezaji wilayani Bagamoyo  (BSEZ).

Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa amesema mji wa Bagamoyo unakuwa kwa kasi hivyo ni vyema mikakati ya kukabiliana na majitaka iwepo ili kwenda sambamba na ukuaji wa mji.

Alisema katika kkufanya mji kuwa wa kisasa usiokuwa na taka kila mahali, ni vyema maandalizi ya kitaalamu yakafanyika mapema ili kila mwananchi ajue namna ya kusafirisha majitaka badala ya kuacha kila mtu atupe taka kwa namna anayoitaka yeye.

Akizungumza wakati wa kufunga mkutano huo, Mwenyekiti wa mkutano huo ambae  ni Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga alisema anamshukuru Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya maji safi na maji taka (DAWASA) kwa kushirikiana na serikali ya wilaya ya Bagamoyo katika kuboresha miundombinu ya maji safi na maji taka ndani ya Wilaya ya Bagamoyo. 
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo, Fatuma Latu akiwatambulisha washiriki wa mkutano huo mbele ya Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo ambae ndiye Mwenyekiti wa Mkutano huo. 
Mhandisi wa Miradi kutoka mamlaka ya maji safi na maji taka (DAWASA) Christian Gava akiwasilisha Taarifa ya Miradi ya kusambaza maji safi pamoja na kutibu maji taka katika wilaya ya Bagamoyo.
Wahandisi kutoka DAWASA wakisikiliza kwa makini mapendekezo kutoka kwa washiriki wa mkutano huo uliofanyika ukumbi wa Halmashari ya Bagamoyo.
Madiwani wa Halmashauri ya Bagamoyo pamoa na watalamu wa Halmashauri hiyo wakisikiliza Taarifa ya wataalamu wa DAWASA. 
Mwenyekiti wa mkutano huo ambae ni Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga (katikati) kulia ni Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa, Kushoto ni Makamo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo,  Saidi Ngatipula.

Thursday, February 22, 2018

NAIBU WAZIRI WA NISHATI AWASHA KITUO CHA UMEME MBAGALA.



Naibu waziri wa nishati awasha umeme kituo cha Mbagala baada ya mradi huo kukamilika.

Kufuatia kuwashwa kwa kituo hicho, Wananchi wa Mbagala ,Kigamboni ,Tandika na Mkuranga na Wenye Viwanda watapata Umeme wenye Nguvu na wenye uhakika ambao hautokatika.

Naibu waziri wa Nishati, amewapongeza wananchi wakazi wa maeneo hayo Kwa kuwa na subira huku akiwapa pole kwa kero ya umeme ya muda Mrefu.

Aidha, alisema amewashukuru Waheshimiwa Wabunge wa Majimbo ya Kigamboni Dk Ndungulile na Mhe Mangungu na Wakuu wa Wilaya Kwa kufuatilia Jitahada za kuondosha Kero hiyo ya Upatikanaji wa Nishati ya Uhakika katika Maeneo hayo.

Alisema Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Pombe Magufuli imefanya juhudi kubwa kutekeleza mradi huo ili wananchi waondokane na kero hiyo.

Alisema kufuatia ushirikiano alionao yeye pamoja na Waziri wa nishati Dk Medard Kalemani wameweza kufanikisha Miradi mbalimbali ya Nishati ya umeme hapa nchini hali inayopelekea wananchi kujenga imani na serikali yao ya awamu ya tano katika utekelezaji wa miradi.

Aliongeza kwa kusema kuwa, kufuatia ushirikiano na Waziri wa nishati, imepelekea kuwa karibu na Wataalam wote wa TANESCO pamoja na Wakandarasi na hatimae kufanikisha mradi huo na miradi mingine iliyo chini ya wizara hiyo.

MAKAMU WA RAIS AHUDHURIA MAHAFALI YA 34 YA CHUO KIKUU HURIA


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akishiriki matembezi ya mahafali ya 34 ya Chuko Kikuu Huria pamoja na Mkuu wa chuo hicho Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda (kulia) kuelekea kwenye uwanja wa Halmashauri ya  Bariadi kwenye sherehe za mahafali ya 34 ya Chuo Kikuu Huria Tanzania.
..............................................................

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewakumbusha wahitimu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kuwa Vyeti walivyotunukiwa  ni tuzo halali kwa juhudi na jitihada walizoonesha darasani.

Makamu wa Rais aliyasema hayo wakati wa sherehe za mahafali ya 34 ya Chuo Kikuu Huria yaliyofanyika kwenye uwanja wa Halmashauri Bariadi mkoani Simiyu.

Makamu wa Rais alisema “ Jamii inategemea mtaipatia tuzo ya utendaji bora na ufanisi katika fani zenu utakao akisi viwango vilivyoainishwa kwenye vyeti vyenu”.

Makamu wa Rais aliupongeza uongozi wa chuo kwa jitihada zake katika kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais hasa katika sula la Uchumi wa Viwanda ambapo chuo hicho kimefanya Kongamano kubwa la Elimu ya Juu na Uchumi wa Viwanda mjini Bariadi lakini pia chuo hicho kipo kwenye mchakato wa Kigoda cha kiprofesa cha Viwanda na Maendeleo.

Makamu wa Rais aliwakumbusha uongozi wa chuo katika jitihada zake za kutekeleza majukumu ya chuo , uendelee kujikita kwenye kauli mbiu yake Elimu Bora na Nafuu kwa Wote .

Katika Mahafali hayo ambayo zaidi ya wanafunzi 941 wamehitimu kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na nchi za jirani ambapo wanafunzi saba (7) walihitimu Shahada ya Uzamivu ya Udaktari wa Falsafa ya Chuo Kikuu Huria.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Huria Tanzania Profesa Rwekaza Mukandala wakati wa mahafali ya 34 ya chuo hicho yaliyofanyika kwenye uwanja wa Halmashauri ya Bariadi mkoani Simiyu.



Sehemu ya Wanafunzi waliohitimu katika Chuo Kikuu Huria wakiwa kwenye sherehe za mahafali ya 34 ya chuo hicho.
Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais

Wednesday, February 21, 2018

NAIBU WAZIRI WA NISAHATI AKAGUA MITAMBO YA UMEME ITAKAYOFUNGWA MTWARQ



Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amekagua mitambo miwili ya umeme yenye uwezo wa kuzalisha megawati 2 kila mmoja itakayofungwa katika kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia cha Mtwara.

Amekagua mitambo hiyo tarehe 21 Februari, 2018 katika eneo la Mkandarasi, jijini Dar es Salaam ambapo kampuni ya Mantrac ndiyo iliyopewa kazi ya kufunga mitambo hiyo.

Baada ya kukagua mitambo hiyo, Naibu Waziri alisisitiza kuwa, Serikali inafuatilia kwa karibu utekelezaji wa  kazi  hiyo lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa  mitambo hiyo inafikishwa na kusimikwa mkoani Mtwara mapema iwezekanavyo ili kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme katika mkoa wa Mtwara pamoja na Lindi.

Kabla ya kukagua mitambo hiyo, Naibu Waziri Mgalu alifanya kikao na watendaji wa kampuni hiyo ya Mantrac pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) lengo likiwa ni kufahamu maendeleo ya kazi hiyo.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa Mantrac, Ahmed Saleh alimweleza Naibu Waziri kuwa mpaka sasa mitambo hiyo tayari imewasili jijini Dar es Salaam na kinachosubiriwa kwa sasa ni kuwasili kwa kontena maalum zitakazotumika kuwekea mitambo hiyo kabla ya kusafirishwa kuelekea mkoani Mtwara.

Aliongeza kuwa, kazi ya usafirishaji wa mitambo hiyo kwenda mkoani Mtwara itafanyika mwanzoni mwa mwezi Aprili mwaka huu na kwamba kazi ya kufunga mitambo hiyo, majaribio na makabidhiano itafanyika tarehe 9 hadi 30 mwezi Aprili mwaka huu.

Kituo cha kuzalisha umeme kwa Gesi asilia mkoani Mtwara kina mitambo Tisa yenye uwezo wa kuzalisha megawati 2 kila mmoja. Kituo kwa sasa kinazalisha umeme wa kiasi cha megawati 16 kufuatia mtambo namba Tisa kuwa nje kwa matengenezo.

Kuongezeka kwa mashine hizo mbili mpya (4 MW) kutafanya uwezo wa kituo hicho kuongezeka na  kufikia megawati 22 na hivyo kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Lindi na Mtwara.



Sunday, February 18, 2018

NAIBU WAZIRI NISHATI ATOA WIKI MOJA KWA WAKANDARASI WA REA.


Naibu waziri wa Nishati Subira Mgalu ametoa wiki moja kuanzia leo Tarehe 18 February 2018,  kwa  wakandarasi wote nchini wanaofanya kazi ya kusambaza umeme kupitia Mradi wa Umeme vijijini (REA) kuhakikisha wanapima (survey)  kwenye taasisi za uma zikiwemo Vituo vya Afya, Zahanati, na Shule .

Alisema lengo la Mradi huo ni kuhakikisha wananchi wa vijiini wanapata umeme huku sehemu zao za kupata huduma, Vituo vya Afya, Zahanati na shule  zikipewa kipaumbele katika kufikisha umeme.

Naibu waziri huyo wa Nishati ametoa kauli hiyo Wilayani Bagamoyo alipokuwa akizindua mradi wa umeme vijijini (REA) awamu ya tatu kitongoji cha Migude kata ya Kiromo. 

Aliwataka wakandrasi hao kuhakikisha maeneo yote ya Zahanati, Vituo vya Afya, Shule na Miradi ya maji yanapimwa (yanafanyiwa  survey) kwakuwa agizo la serikali maeneo hayo yafikiwe na huduma ya Nishati katika utekelezaji wa REA awamu ya tatu. 

Alisema maeneo hayo yanapaswa kufanyiwa matayarisho ya miundombinu ikiwa ni pamoja na upimai (survey) ili yafikiwe na Umeme.

Aliongeza kwa kusema kuwa,  Mkandarasi atakaeshindwa kufuata maelekezo ya serikali atakuwa ameshindwa kazi na mkataba wake utasitishwa ili apatikane mkandarasi atakaeweza kufanya kazi kwa mujibu wa maelekezo ya serikali.

Kauli hiyo imekuja kufuatia Diwani wa kata ya Kiromo Wilayani Bagamoyo, Hasan Usinga (Wembe) kutoa taaraifa ya hali ya umeme katika kata yake ambapo alisema umeme huo haujafikishwa kwenye Zahanati.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo Dkt. Shukuru Kawambwa amepongeza utendaji kazi wa wizara ya Nishati chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kwa namna inavyoweza kufikisha umeme vijiini.

 Naibu waziri wa Nishati Subira Mgalu (katikat) akikagua utekelezaji wa Miradi ya Umeme Vijijini (REA) awamu ya tatu katika Kitongoi cha Migude kata ya Kiromo Wilayani Bagamoyo, kulia ni Diwani wa kata ya Kiromo, Hassan Usinga (Wembe) na kushoto ni Mwenyekiti wa kitongoji cha Migude, Kitumboy Bushiri.
 Diwani wa kata ya Kiromo, Hassan Usinga (Wembe)wa kwanza kulia akifurahia ambo na Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa.
Madiwani wa viti Maalum wa Halmashauri ya Bagamoyo wakifuatilia hutuba ya naibu waziri wa Nishati ( hayupo pichani) kutoka Kulia ni Hafsa Juma Kilingo, wa katikati ni Shumina Ismail Rashid na wa kwanza kushoto ni Togo Omari Hega.
Wananchi waliohudhuria kumsikiliza Naibu waziri wa Nishati kitongoji cha Migude 
 Naibu waziri wa Nishati Subira Mgalu, akipeana mkono na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Migude, Kitumboy Bushiri ikiwa ni ishara ya kuzindua Mradi wa REA awamu ya tatu katika kitongoi hicho.

Wananchi wa Kitongoji cha Migude wakifurahi umeme baada ya Naibu waziri wa Nishati, Subira Mgalu kuwahakikishia umeme utapatikana katika eneo hilo na nchi nzima.

JAFO AAGIZA MKANDARASI KUFANYA KAZI KWA BIDII KUKAMILISHA DARAJA LA KIMALAMISALE



Waziri wa  Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Selemani Jafo amemuagiza mkandarasi anayejenga daraja wa Kimalamisale wilayani Kisarawe kufanyakazi usiku na mchana ili daraja hilo liweze kukamilika kabla ya Mvua za masika hazijaanza.

Waziri Jafo ametoa agizo hilo alipotembelea kukagua mradi wa ujenzi wa daraja hilo ambao unagharimu kiasi cha Sh.Milioni 390.

Hatua hiyo ya Jafo imetokana na mradi huo kuchelewa hapo awali kutokana na Mvua kubwa za vuli zilizokuwa zinanyesha.

Amesema mradi huo unatarajiwa kuwa kiungo muafaka kwa barabara ya Kimalamisale ambapo kukamilika kwa daraja hilo kutakuwa ukombozi mkubwa kwa wananchi.

Amebainisha kuwa kwasasa mvua zinaponyesha magari yanashindwa kupita kutokana kujaa maji mengi katika mto Muyombo unaotenganisha wilaya ya Kibaha na Kisarawe mkoani Pwani. 

Katika ukaguzi huo, Mkandarasi wa mradi huo amemwambia Waziri Jafo kuwa ameshanunua jenerata kubwa ambalo watalitumia wakati wa usiku ili aweze kukamilisha ujenzi huo.

Ameahidi kwamba watajitahidi kufanyakazi kwa kasi kubwa ili kuwahi  Mvua za masika na wasipate hasara ya kuchelewesha mradi.

Wananchi wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI Selemani Jafo.

SERIKALI KUFANYA UCHUNGUZI WA KIFO CHA MWANAFUNZI ALIYEPIGWA RISASI.



Waziri wa Elimu na Mafunzo Profesa Joyce Ndalichako na Naibu waziri wa Mambo ya Ndani Injinia Hamad Yusuph Masauni wakimfariji mama mzazi wa marehemu Akwiline Baftaha Mwanafunzi wa Cho cha Usafirishaji NIT aliyefariki kwa majeraha  baada ya kujeruhiwa na  risasi juzi. 

Akiwa kwenye daladala. Kufuatia vurugu za maanamano ya wafuasi wa Chadema ,Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Dk. John Pombe Magufuli ametuma salami za rambirambi kwa familia kufuatia kifo hicho.
....................................

Serikali imewahakikishia Watanzania kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vinafanya uchunguzi kufuatia kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT) Akwilina Baftaha Akwilini, aliyefariki kwa kupigwa risasi mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, leo jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Hamad Masauni amesema kuwa Serikali itahakikisha uchunguzi huo unafanyika kwa weledi na utaalamu ili haki iweze kupatikana na yeyote aliyehusika atachukuliwa hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.

“Nawasihi watanzania kuwa na subira ili uchunguzi ufanyike na tutahakikisha uchunguzi huo unafanyika haraka iwezekanavyo na baada ya kukamilika wote waliohusika watachukuliwa hatua za kisheria”, alisisitiza Masauni.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Joyce Ndalichako alisema kuwa Serikali imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha mwanafunzi huyo ambacho kilitokea wakati wa kudhibiti maandamano yaliyokuwa yakifanyika katika eneo la Mkwajuni, wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.

“Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli amepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha mwanafunzi Akwilina na anaungana na wazazi, familia, ndugu, jamaa na watanzania wote kuwapa pole za dhati kutokana na msiba huo”, alisema Ndalichako.

Aidha Ndalichako alibainisha kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia itagharamia shughuli zote za mazishi ya mwanafunzi huyo na amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo kusimamia shughuli zote za msiba huo.
Pia Ndalichako alitoa rai kwa watanzania kujiepusha na vitendo vyote ambavyo vinaweza kusababisha maafa kwa watu wasio na hatia.

Wednesday, February 14, 2018

WAZIRI KALEMANI ATOA WIKI MOA KWA MKANDARASI ANAYESAMBAZA UMEME VIJIJI


Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Chato,Dk Medard Kalemani akitoa maagizo ya utekelezaji wa usambazaji wa umeme kwenye maeneo ya vijiji na Kata za  Iparamasa pamoja  Kalembela wakati alipokuwa akizungumza na wananchi kwenye mojo kati ya ziara zake za kukagua utekelezaji wa usambazaji wa umeme wa REA awamu ya tatu.
...............................................
Waziri wa Nishati,Dkt Medard Kalemani amemwagiza mkandarasi
shirika la White City  International ambaye anasambaza umeme wa rea
awamu ya tatu kwenye Vijini na kata za Iparamasa na Kalembela kuhakikisha anafanya kazi hiyo kwa haraka zaidi ili kuwasaidia wananchi ambao wamekuwa na kilio cha muda mrefu cha uhitaji wa nishati ya umeme.

Hayo aliyasema wakati alipokuwa kwenye ziara ya Kukagua na
kuangalia utekelezaji wa mradi wa usambazaji umeme vijijini  Wilayani Chato.

Ambapo Diwani wa kata ya Iparamasa Amos Jiji ,amemweleza Waziri wa
nishati ambaye pia ni mbunge wa Jimbo hilo matatizo ambayo yameendelea kujitokeza kutokana na kukosekana  kwa umeme kwenye  kata yake  na kwamba kwa sasa kuna nguzo ambazo zimekaa
kwa muda wa miezi mitatu bila ya kusambazwa kwa wananchi ambao wanashida na huduma hiyo.

 Mmoja kati ya wananchi wa kata hiyo ,Bw Peter Mabula ameelezea
kukosekana kwa umeme ni chanzo kikubwa ambacho kinakwamisha utendaji kazi hususani kwa upande wa biashara kutokana na wengi wao kutegemea nishati hiyo ili waweze  kuendesha  biashara zao.

Aidha kutokana na maombi hayo kutoka kwa Diwani pamoja na wananchi
Mbunge wa Jimbo la Chato na waziri wa nishati Dk Kalemani alitoa maagizo
kwa Mkandarasi kuhakikisha nguzo ambazo zimelala ndani ya miezi mitatu zisimame na kufikia siku ya alhamisi vijiji hivyo na kata hizo ziwe zimepata umeme.
“Nimesikia kuwa nguzo zimelala tu chini ndani ya miezi mitatu na kwamba mkandarasi alivyosikia nakuja ndio ameanza kazi sasa namwagiza kuwa ahakikishe alhamisi wiki ijayo awe amewasha umeme kwenye kata ya iparamasa na vijiji vyote na mimi siondoki hapa nitahakikisha namsimamia”Alisisitiza Kalemani.

Mradi wa usambazaji wa umeme vijijini  Mkoani
Geita,unatekelezwa na mkandarasi  wa Shirika la White City
International ambapo unatarajia kufanyika ndani ya miezi  16 kwenye
jumla  vijiji  220 vilivyopo  mkoani humo na jumla ya fedha ambazo
zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza mradi huo ni  Sh Bilioni 78.56.

MADIWANI BAGAMOYO WAIKATAA TAARIFA YA UTEKELEZAI WA ILANI.


Diwani wa kata ya Yombo, Mohamed Usinga akitoa msimamo kwa Mwenyekiti wa Halmashauri kuhusu kuiktaa Taarifa ya utekelezaji wa ilani.
............................................

Madiwani wa Halmashauri ya Bagamoyo wameikataa taarifa ya utekelezaji wa ilani ya 2017 kufuatia taarifa hiyo kuwa na mapungufu kadhaa.

Madiwani hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo, Ally Ally Issah wameikataa taarifa hiyo mara ilipofika katika utekelezai wa miradi inayohusu idara ya uvuvi ambapo miradi iliyoainishwa ndani ya taarifa hiyo haipo katika maeneo husika jambo liliwatia hasira madiwani hao na kuamua kuirudisha Taarifa yote kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ili ifanyiwe marekebisho.

Akitoa maamuzi ya Baraza Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo, Ally Ally alisema wanairudisha taarifa yote ka Mkurugenzi ili ipitiwe upya na kunyiwa marekebisho katika maeneo ambayo madiwani hawakuridhika nayo.

Kabla ya Mwenyekiti wa Halmashauri kutoa msimamo huo wa Baraza, madiwani hao walisema ifike wakati sasa wataalamu wa Halmashauri wafanye kazi kwa kuzingatia sheria na kanuni za kazi ili kila mmoja achunge mipaka yake.

Walisema katika kikao cha Baraza kuleta tarifa inayokwenda kinyume na uhalisia katika utekelezaji wa miradi ni kukiuka sheria, na kwamba baraza halitasita kumuwajibisha mtumishi yeyote anaekiuka sheriaa kwa kushindwa kutoa taarifa sahihi za utekelezaji wa ilani.

Walisema madiwani ni viongozi wanaochaguliwa na wananchi kwa lengo la kusimmamia utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa manufaa ya wananchi hivyo si vyema wataalamu wa Halmashauri wanaposhindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo ni wazi kuwa wanawatengezea mazingira magumu madiwani ambao watarudi kwa wananchi kuomba kura kwaajili ya kurudi tena madarakani.

Aidha, Madiwani hao waliwataka wataalamu wa Halmashauri wanapofika katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye maeneo mbalimbali wawasiliane na viongozi wa kata husika ili kuleta ushirikiano kati ya wataalamu hao na viongozi wa kata wakiwemo watendai wa kata na madiwani ili kuondoa sintofahamu inayoweza kujitokeza siku ya kuwasilisha taarifa.

Katika taarifa hiyo idara ya uvui imetaja kujenga kwa mabwawa ya samaki katika baadhi ya maeneo huku madiwani wakishangaa kwakuwa hawajawahi kuyaona mabwawa hayo kwenye maeneo yao.
 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo, Fatuma Latu amekiri kupokea taarifa hiyo na kwenda kuifanyia marekebisho na wataalamu wake ili baadae iwasilishwe ikiwa imekamilika.
Wakati huohuo Katibu wa CCM wilaya ya Bagamoyo, Salum kamote amewaonya wakuu wa idara ambao wanatabia ya kutoa taarifa zisizo sahihi kwani kwa kufanya hivyo wanachangia kuidhoofisha chama tawala katika mikakati yake ya kusimamia utekelezaji wa ilani uchaguzi jambo linaidhoofisha serikali iliyopo madarakani kwa ujumla.

Alisema ni vyema taarifa ikawa wazi kama kuna mradi haujatekelezwa ili chama kijue wapi kwenye madhaifu ili nguvu zielekezwe hapo na kuhkikisha miradi hiyo inateekelezwa kuliko kutoa taarifa za uongo.
Aidha, katibu huyo wa CCM wilaya ya Bagamoyo amewapongeza madiwani Halmashauri ya Bagamoyo kwa uwasilishaji mzuri wa taarifa za kata na hatua waliyochukua kuikataa taarifa ya utekelezaji wa ilani.

Alisema Madiwani ndio wasimamizi wa miradi hivyo wanapaswa kuwa imara katika kuhakikisha miradi yote iliyopangwa na kutengewa mafungu inatekelezwa kwa ukamilifu wake ili kujenga imani kwa wananchi ambao ndio walipewa ahadi za kutekeleza mambo mbalimbali.

Kikao hicho cha Baraza la madiwani Halmashuri ya Bagamoyo kimeanza leo jumatano February 14 ambapo kimejadili taarifa za robo ya pili ambapo madiwani waliweza kuwasilisha taarifa za kata zao.
 Madiwani wa Halmashauri ya Bagamoyo wakifuatilia kwa karibu uwasilishwaji wa taarifa za kata pamoja na kupokea taarifa ya utekelezaji wa ilani ambayo baadae waliikataa kwa pamoja na kumrudishia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo Fatuma Latu kwaajili ya Marekebisho.

 Madiwani wa Halmashauri ya Bagamoyo wakifuatilia kwa karibu
 uwasilishwaji wa taarifa za kata pamoja na kupokea taarifa ya utekelezaji wa ilani ambayo baadae waliikataa kwa pamoja na kumrudishia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo Fatuma Latu kwaajili ya Marekebisho.

BIL. 161.9 ZIMETUMIKA KUBORESHA VITUO VYA AFYA 170.



WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imetumia sh. bilioni 161.9 kuboresha vituo vya afya 170 nchini pamoja na kugharamia huduma ya Afya ya Mama na Mtoto kwa lengo la kuokoa maisha yao.

Amsema Serikali itaendelea kukarabati na kupanua miundombinu ya kutolea huduma pamoja na kununua vifaa vya kisasa katika Hospitali za Mloganzila, Benjamini Mkapa, Dodoma na Hosptali za Rufaa katika Mikoa na Kanda.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Februari 14, 2018) wakati akizindua jengo  jipya la mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa-Amana iliyopo wilayani Ilala jijini Dar es Salaam.

Jengo hilo la ghorofa mbili limejengwa kwa ufadhili wa kundi la kampuni za AMSONS na lina thamani ya sh bilioni 1.2.

Amesema uzinduzi wa jengo hilo  unakwenda sambamba na azma ya Rais Dkt. John Magufuli za kuimarisha sekta ya afya na kuifanya kuwa miongoni mwa sekta za kipaumbele.

Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha inasogeza huduma za afya karibu na wananchi. “Mfano, Hospitali za Rufaa za Amana, Mwananyamala na Temeke, zimeendelea kuhudumia wagonjwa kutoka Zahanati, Vituo vya Afya vya Serikali, binafsi na vya dini kutoka mikoa jirani ya Pwani, Morogoro na Lindi.

Pia amesema Serikali itaendelea kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 – 2020, kuhusu kuwapatia wananchi huduma bora za afya pamoja na kujenga hospitali nyingine za Rufaa kwa ajili ya Kanda ya Kusini, Kati na Magharibi.

Akizungumzia kuhusu changamoto ya idadi ndogo ya watumishi na ukosefu wa huduma za uangalizi maalumu (ICU) katika hospital ya Amana, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kufanyia kazi changamoto zote zilizopo katika sekta ya afya zikiwemo n aza hospital hiyo. 

Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuthamini na kutambua mchango wa wadau mbalimbali pamoja na kuendelea kushirikiana nao katika kuhakikisha kuwa huduma za afya nchini zinaboreshwa.

Hivyo, alitumia fursa hiyo  na kulipongeza kundi la kampuni za AMSON’s lililoamua kujenga jengo la mama na mtoto katika hospital hiyo kwa ushawishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Paul Makonda.

Awali, Mganga Mkuu Hospitali ya Rufaa ya Mkoa – Amana, Dkt. Meshack Shimwella alisema wazazi wanaolazwa katika hospitali hiyo kwa siku ni 180 hadi 250 na uwezo wa hospitali ni vitanda 353, ambapo vitanda 250 vinatumika wodi ya wazazi.

Alisema idadi hiyo hailingani na idadi ya wagonjwa, hivyo kusababisha wakati mwingine wagonjwa kulala zaidi ya mmoja kwenye kitanda kimoja kutokana na kasi ya ongezeko wa wagonjwa wanaolazwa hususani wodi ya watoto na akinamama.

Dkt. Shimwella alisema wamefanikiwa kuongeza jingo la kutolea huduma ya mama na mtoto lenye ghorofa mbili ilililojengwa kwa ufadhili wa AMSONS lenye uwezo wa vitanda 100, ambalo ndilo liliongeza idadi ya vitanda kutoka 253 hadi kufikia 353.

“Kutokana kukamilika kwa jengo hilo kwa sasa akinamama wanaonyonyesha wanalala wakiwa mmoja mmoja, watoto wachanga wanahudumiwa katika mazingira mazuri yanayofanana na viwango Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.”

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Makonda aliwashukuru wafadhili waliojenga jengo hilo kwa sababu si kila mtu anayekwenda hospitali na kukuta changamoto na akaamua kuzifanyia kazi.

Bw. Makonda alisema awali akinamama walikuwa wanalala hadi watatu katika kitanda kimoja, hivyo madhumuni ya ujenzi wa jego hilo ni kupunguza msongamano katika wodi ya wazazi.