Monday, March 23, 2026

SERIKALI YAHIMIZA MELI YA NEW MV MWANZA KUKUZA UCHUMI, UTALII KANDA YA ZIWA.

 



Serikali imetoa wito kwa wafanyabiashara, wasafirishaji na wawekezaji mbalimbali kutumia fursa ya meli mpya ya MV New Mwanza kibiashara na kiutalii ili kukuza uchumi wa Kanda ya Ziwa.

Itakumbukwa meli hiyo imejengwa kwa zaidi ya Tsh. Bilioni 120, ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo, magari makubwa matatu na madogo, ambapo itafanya safari zake katika bandari zote zinazozunguka Ziwa Victoria ikiwemo Kisumu (Kenya), Port Bay (Uganda) na Kemondo (Bukoba).

‎Akizungumza Jumapili Machi 22, 2026 na waandishi wa habari katika bandari ya Mwanza Kusini jijini Mwanza ilipoegeshwa meli hiyo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema kutokana na uwekezaji huo wakazi wa Kanda ya Ziwa, wawekezaji na wafanyabiashara wakubwa na wadogo wanapaswa kuitumia kwenye shughuli zao na kuleta tija ya uwekezaji huo mkubwa.

‎Amesema Serikali imetimiza jukumu lake la kutekeleza wajibu wa kujenga mazingira mazuri ya biashara, uwekezaji na ustawi wa jamii, hivyo mpira sasa unahamia kwa wananchi kuitumia ili kulinufaisha taifa na malengo yaliyokusudiwa yafikiwe.

‎"Nawaombeni mkiiona New MV Mwanza, oneni suluhuhisho la uhakika la usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo, oneni fursa muhimu na adhimu ya utalii" amesema Msigwa na kuongeza;

‎"Serikali inategemea kuona utalii unakua kwa kasi hapa Mwanza, Bukoba na kwingine, watalii waje hapa Mwanza kisha waingie Serengeti, waende Rubondo, Burigi- Chato na kwingineko" amesema.

‎Ameongeza kuwa, wafanyabiashara na wawekezaji wanapaswa kuiona meli hiyo kama suluhisho la uhakika la kukua kwa biashara mbalimbali za madini, samaki, pamba, nyama na maziwa.

‎"Katika kanda ya Ziwa, amkeni mkamate biashara za maeneo yote ambayo yanazungukwa na Ziwa Victoria - Tanzania, Kenya, Uganda na kote ambako uwepo wa meli unarahishisha mambo, pia fursa zilizopo DRC, Sudan Kusini, Rwanda, Burundi" amesisitiza Msigwa.

‎Kwa mujibu wa Msigwa, mafanikio ya ujenzi wa meli hiyo ni moja ya mambo makubwa ya kujivunia kwa watanzania wakiwa na kila sababu ya kutembea kifua mbele kwa kuwa na serikali yenye maono na dhamira ya kuwekeza katika mambo makubwa ambayo yatatoa mchango mkubwa katika mageuzi ya kiuchumi.   

‎"Hii inafanya meli hii sio tu kuwa kubwa kuliko zote katika ziwa Victoria na maziwa makuu bali pia hii ndiyo meli kubwa kuliko zote katika maji baridi barani Afrika" amesema



No comments:

Post a Comment