Aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Mobhare
Matinyi, akiwa katika picha ya pamoja na Mfalme wa Sweden, Carl XVI Gustaf,
wakati alipokwenda kumuaga katika Jumba la Kifalme jijini Stockholm, tarehe 19
Machi, 2026 (Picha kwa hisani ya Jumba la Kifalme).
.......................................................
Mfalme Carl XVI Gustaf wa Sweden, amemuaga aliyekuwa Balozi
wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Mobhare Matinyi, katika hafla fupi iliyofanyika
kwenye Jumba la Kifalme jijini Stockholm, jana tarehe 19 Machi, 2026.
Katika mazungumzo yao mafupi, viongozi hao walijadiliana
namna ya kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizi mbili katika sekta
za nishati, mazingira, kilimo, utalii, miundombinu, madini na teknolojia.
Mfalme Gustaf aliipongeza Tanzania kwa kuweka utulivu nchini
na kubuni mipango thabiti ya kutafuta maendeleo na kukuza uchumi wake licha ya
changamoto nyingi zinazoikabili dunia nzima hivi sasa.
Balozi Matinyi alimshukuru Mfalme Gustaf kwa ushirikiano
mzuri alioupata katika kipindi alichohudumu nchini Sweden ambapo Tanzania
imefaidika katika sekta za nishati, kilimo, miundombinu, teknolojia na elimu ya
juu.
Hii ilikuwa mara ya tatu kwa Balozi Matinyi kukutana na
Mfalme Gustaf tangu awasili nchini Sweden mwezi Mei 2025. Mara ya kwanza
ilikuwa wakati wa kukabidhi hati zake za utambulisho tarehe 12 Juni, 2025, na
tarehe 9 Desemba, 2025, kwenye mazungumzo ya kibalozi ya mwisho wa mwaka.
Imetolewa na Ubalozi wa Tanzania, Stockholm, Sweden,
19 Machi, 2026.

No comments:
Post a Comment