BAGAMOYO: NYONGO AFUNGUA MLANGO WA SERIKALI KUTATUA KERO ZA ARDHI
BAGAMOYO: NYONGO AFUNGUA MLANGO WA SERIKALI KUTATUA KERO ZA ARDHI
Na Albert Kawogo
BAGAMOYO, PWANI: Wananchi wa Bagamoyo wenye changamoto mbalimbali, ikiwemo zinazohusu ardhi, wamepewa nafasi ya kuwasilisha kero zao moja kwa moja kwa Serikali, huku Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Stanslaus Nyongo, akisisitiza kuwa hakuna sababu ya wananchi kubaki na matatizo bila kuyafikisha kwenye mamlaka zinazohusika.
Akizungumza Oktoba 7, 2026 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Halmashauri ya Mji wa Bagamoyo, Mhe. Nyongo alisema ofisi yake iko wazi kwa wananchi wanaohitaji msaada katika kutatua changamoto zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku.
Alisema wananchi wanapaswa kutumia fursa zilizopo za kuwasilisha malalamiko na changamoto zao kwa Serikali ili ziweze kufanyiwa kazi kwa wakati, badala ya kuendelea kuzibeba bila kupata ufumbuzi.
Kauli hiyo imekuja wakati suala la ardhi likiendelea kuwa miongoni mwa maeneo yanayohitaji usikivu wa karibu katika baadhi ya maeneo ya Bagamoyo, kutokana na ongezeko la shughuli za makazi, biashara, kilimo, uwekezaji na miradi mikubwa ya maendeleo.
Kwa miaka kadhaa, mabadiliko ya matumizi ya ardhi na ongezeko la thamani ya maeneo katika wilaya hiyo yameifanya ardhi kuwa suala muhimu kwa wananchi, wawekezaji na Serikali.
Hali hiyo imeongeza umuhimu wa kuwa na mifumo ya utatuzi wa migogoro, utoaji wa taarifa sahihi kuhusu umiliki na matumizi ya ardhi, pamoja na ushirikishwaji wa wananchi katika masuala yanayogusa maeneo yao.
Katika mkutano huo, Mkuu wa Mkoa alipokea na kusikiliza hoja mbalimbali kutoka kwa wananchi, akisisitiza kuwa wale wanaokutana na changamoto hawapaswi kuwa na hofu ya kufika kwenye ofisi za Serikali na kueleza matatizo yao.
“Milango ya ofisi yangu iko wazi kwa wananchi,” alisema Mhe. Nyongo,huku akiwataka wananchi kutumia njia rasmi zilizopo kufikisha changamoto zao ili Serikali iweze kuzifanyia kazi.
Mbali na kusikiliza kero za wananchi, ziara ya Mhe. Nyongo Bagamoyo imehusisha pia ukaguzi wa shughuli za maendeleo na uwekezaji, ikiwemo viwanda vinavyotekelezwa katika eneo la uwekezaji la TISEZA pamoja na mradi wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo.
Miradi hiyo inaifanya Bagamoyo kuwa eneo lenye umuhimu mkubwa katika mipango ya uwekezaji na maendeleo, jambo linaloifanya Serikali kuwa na jukumu la kuhakikisha ukuaji wa shughuli za kiuchumi unaenda sambamba na usimamizi mzuri wa ardhi na maslahi ya wananchi.
Kwa wananchi, ujumbe uliotolewa na Mkuu wa Mkoa unalenga kuimarisha mawasiliano ya moja kwa moja kati yao na Serikali, hasa katika masuala yanayohitaji ufafanuzi, uamuzi au hatua za mamlaka.
Mhe. Nyongo amewataka wananchi na Serikali kuendelea kushirikiana katika kubaini changamoto na fursa zilizopo, akisisitiza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kuhakikisha Bagamoyo inanufaika na uwekezaji na miradi ya maendeleo inayoendelea katika eneo hilo.
Awali kwenye mkutano wa ziara hiyo Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo Mheshimiwa Subira Hamisi Mgalu(CPA) alielezea jitihada kubwa iliyofanywa na serikali katika kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye jimbo hilo ikiwemo ile huduma za jamii hasa afya na elimu.

Comments
Post a Comment