Tuesday, January 30, 2018

MAHAKAMA MPYA YA WILAYA BAGAMOYO YAZINDULIWA.


 Muonekano wa mbele wa Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo 
Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamisi Juma (kulia) na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo (kushoto) wakifungua kitambaa kuashiria uzinduzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo ambalo limejengwa Kitongoji cha Ukuni kata ya Dunda.  
 Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamisi Juma (kulia) na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo (kushoto) wakipeana mikono baada ya kuzindua jengo la Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo ambalo limejengwa Kitongoji cha Ukuni kata ya Dunda. 
 Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamisi Juma (katikati) akizungumza katika uzinduzi wa Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo, Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo.
............................................
Huduma za Mahakama katika ngazi mbalimbali hapa nchini bado haziwafikii wananchi zaidi milioni 25 kutokana na  changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa majengo ya mahakama.

Hayo yamebainishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Juma alipokuwa akizindua Mahakama ya wilaya ya Bagamoyo.

Alisema uboreshaji wa majengo ya Mahakama utasaidia huduma za mahakama kuwafikia wananchi wengi zaidi na kupunguza changamoto zinazoikabili mahakama za Taznaznia ikiwemo uchakavu wa majengo.

Alisema upatikanaji wa haki kwa wakati ndio jambo wanalotarajia wananchi hivyo serikali inayo wajibu wa kusogeza huduma za mahakama karibu na wananchi na kuzisimamia katika utekelezaji wake.

Aliongeza kwa kusema kuwa, katika kutoa haki kwa wakati ni pamoja na kuzingatia maadili ambapo wananchi wanataka kuona ngazi zote ili kuwajengea imani na vyombo vyao vya sheria ikiwemo Mahakama.

Prof. Ibrahim Juma aliwataka Mahakimu, na wafanyakazi wote katika mahakama ya wilaya ya Bagamoyo kufanya kazi inayoendana na hadhi ya jengo hilo kwa kutoa huduma bora kwa wakati huku akiwataka kuepuka kabisa rushwa.

Aidha, alisema jengo hilo la kisasa ni utekelezaji wa mpango mkakati wa mahakama uliozinduliwa rasmi Tarehe 21 Septemba 2016 huko Kibaha Mkoani Pwani na Waziri Mkuu wa Tanzania Kasim Majaliwa kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Jaji Mkuu Prof. Ibrahim Juma alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo kwa kuwezesha upatikanaji wa maeneo katika mkoa wake kwaajili ya ujenzi wa Mahakama.

Alisema kufuatia juhudi hizo za Mkuu wa Mkoa wa Pwani, tayari wilaya tatu za mkoa huo zimepata Mahakama tatu za kisasa ambazo ni Kibaha, Bagamoyo na Mkuranga.

Jaji Mkuu aliwataka viongozi wengine kwenye mikoa yote na wilaya nchini kutoa nafasi katika maeneo yao ili kuona namna ya kusogeza huduma za mahakama karibu na wananchi. 

Awali akizungumza mbele ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo alizitaka mahakama mkoani humo kufanya haraka kusikiliza na kumaliza kesi ili kuepuka manunung'uniko kutoka kwa wananchi.

Alisema Mkoa wa Pwani unakabiliwa na migogoro ya wafugaji na wakulima hivyo ni vyema mahakama zikasimamia haki, usawa na uadilifu katika kutoa hukumu ili aliyekosa apate adhabu stahiki kulingana na kosa lake na hatimae kila mwananchi aweze kusimama kwenye utii wa sheria.

Alivitaka vyombo vinavyosimamia sheria mkoani Pwani kusimamia vyema utoaji wa haki ili kuepuka kutoa fursa kwa wananchi kujichukulia sheria mikononi.

Mkoa wa Pwani una jumla ya wilaya 7 ambapo mahakama za wilaya zilizopo ni sita tu na kufanya upungufu wa mahakama moja ya wilaya.

Aidha, Wilaya ya  Bagamoyo yenye jumla ya kata 26 ina Mahakama za Mwanzo 7 tu ambazo mbili kati ya hizo ndio zenye majengo ya kisasa huku kata tano zina majengo chakavu na kata 19 zikiwa hazina kabisa majengo ya mahakama za Mwanzo.

Mahakama mpya ya wilaya ya Bagamoyo imejengwa Kitongoji cha Ukuni kata ya Dunda ambapo awali Mahakama ya wilaya ya Bagamoyo ilikuwa jirani na jengo la Halmashauri ya Bagamoyo.

Kukamilika kwa Mahakama hiyo ya kisasa ya wilaya ya Bagamoyo kutasaidia katika utunzaji wa nyaraka ukilinganisha na jengo lile la zamani ambapo kutokana na uchakavu wake baadhi ya nyaraka zimekuwa zikinyeshewa na mvua au kuliwa na mchwa.

Friday, January 26, 2018

WAZIRI WA AFYA AFUNGUA MASHINE YA CT-SCAN HOSPITALI YA RUFAA BUGANDO



waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ameahidi kuwaletea mashine ya uchunguzi ya MRI katika hospitali ya rufaa ya kanda ya ziwa Bugando mwaka huu.

Waziri Ummy Mwalimu ameyasema hayo wakati akifungua mashine ya  CT-scan ambayo itakua inapima magonjwa mbalimbali iliyogharimu shilingi za kitanzania bilioni 1.6 ambazo zinetokana na vyanzo mbalimbali vya hospitali hiyo.

Aidha,Waziri Ummy ameahidi ndani ya miaka mitatu kuanzisha taasisi ya moyo ili kuweza kupunguza gharama kwa wananchi wa kanda ya ziwa na magharibi wanaopata matatizo ya moyo kwenda kuoata vipimo na matibabu kwenye taasisi ya moyo ya  JKCI ya jijini Dar es Salaam.


Waziri Ummy mwalimu akiongea na watumishinwa hospitali ya rufaa ya kanda ya ziwa ya bugando wakati wa uzinduzi wa mashine ya CT-scan
Mkurugenzi wa hospitali ya rufaa ya bugando dkt.Abel Makubi akitoa shukrani mara baada ya uzinduzi wa mashine hiyo

Askofu wa Jimbo la Geita Baba Flavian Kasala akiongea wakati wa ufunguzi huo



Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongela akiongea wakati wa ufunguzi wa mashine hiyo,ambapo aliomba kuanzishwa kwa taasisi ya moyo katika hospitali hiyo ili kuwasaidia wananchi wa kanda ya ziwa
Mtaalamu wa Mionzi wa hospitali ya Bugando akimpatia maelezo Waziri wa Afya mara baada ya ufunguzi wa mashine hiyo.

Licha ya ufunguzinwa mashine hiyo ,waziri Ummy pia aliwajulia hali wagonjwa waliofika hospitalini hapo kupata matibabu.