Wednesday, July 17, 2024
Tuesday, July 16, 2024
MABASI 100 MWENDOKASI YANAKUJA
Na Mwandishi wetu
SERIKALI iko mbioni kuleta mabasi 100 ya mwendokasi nia ikiwa ni kuongeza nguvu kwenye eneo la huduma ya usafiri kwa Jiji la Dar es Salaam
Msajili wa Hazina Nehemiah Kyando Mchechu amesema hayo jana kwenye kikao maalum na Wahariri kuwa mabasi 100 yatanunuliwa kwa fedha za mkopo kutoka Benki ya NMB.
Mchechu amesema kwa kipindi cha miezi miwili amekuwa akifanya vikao na Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART), Kampuni ya Mabasi Yendayo Haraka (UDART), Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) na sasa wamefikia ukingoni.
"Nimekuwa na vikao nao vya mara kwa mara na wadau hawa ili kuokoa hii hali maana tumeona inaenda kuleta crisis (maafa) na kuathiri taswira nzuri ya Serikali kwenye mradi huu” amesema Mchechu.
Kwa mujibu wa Mchechu mabasi hayo yatakuwa yamewasili nchini ndani ya miezi sita ijayo ili kusaidia kutatua changamoto ya usafiri wa mabasi yaendayo kasi kwa mkoa wa Dar es Salaam.
Kauli ya Mchechu imekuja wakati kukiwa na malalamiko kwa wadau na wananchi juu ya ubora wa mabasi hayo kutokana na mrundikano wa watumiaji pamoja na uchache wa usafiri huo kulinganisha na mahitaji yaliyopo.
Mbali na changamoto hizo baadhi ya mabasi hayo pia ni machakavu na pia yapo katika mfumo wa kizamani kwa kutokidhi mahitaji ya watumiaji ikiwemo wenye ulemavu na wazee.
Pia msajili wa hazina amesema ni muhimu sana kwa mji kama Dar es Salaam kuwa na kampuni za usafiri zaidi ya moja zitakazosaidiana kutoa huduma hiyo kwa wananchi.
Mwaka jana Oktoba 24, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa aliuelekeza uongozi wa Dart kuongeza watoa huduma ili kuboresha huduma ya usafiri huo.
Aidha, Mchechu ameitaka Dart ifikapo Agosti mwaka huu kuhakikisha wametengeneza mifumo ya ukusanyaji fedha ili kudhibiti mapato na kupunguza wizi.
“Kuna wizi mwingi unafanyika kwenye cash, mimi huwa nasema ni ‘headache’ kusimamia huu mradi kwenye suala la malipo. Tumekubaliana na Dart kuwa hadi Agosti 2024 wawe wamekamilisha mfumo wa nauli kwa njia ya mtandao.” amesema Mchechu
WAZIRI MKUU AZINDUA MITAMBO YA KISASA YA KURUSHIA MATANGAZO.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Julai 15, 2024 amekagua na kuzindua mitambo na vifaa vipya vya kurushia matangazo vya kampuni ya Azam Media Limited.
Vifaa hivyo ni pamoja na Magari ya kisasa ya kurushia matangazo (OB Van), kamera za kisasa pamoja na mfumo wa kusaidia maamuzi viwanjani (VAR).
Vifaa hivyo vilivyogharimu shilingi bilioni tano vitatumika katika kurushia matangazo ya mpira wa miguu wa ligi Kuu Tanzania bara na Zanzibar pamoja na michezo mingine.
Akizungumza na wafanyakazi wa Azam Media pamoja na wadau wa michezo Mheshimiwa majaliwa amesema manunuzi ya vifaa hivyo ni mapinduzi makubwa katika tasnia ya habari kwani kunaifanya Tanzania kuwa nchi ya kipekee kuwa na vifaa vya kisasa vya aina yake katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Majaliwa pia ameshuhudia uzinduzi wa chaneli mpya ya Azam 4 HD ambayo itatumika kurusha ligi kuu ya Ufaransa (Legue 1) na ligi kuu ya Ujerumani (Bundesliga)
MCHINJITA AWAVUNA VIGOGO CHADEMA LINDI KUHAMIA ACT
NA HADIJA OMARY
JUMLA ya wanachama 45 wa chama cha Demockasia na Maendeleo CHADEMA na viongozi wao Mkoani Lindi wamekihama chama chao na kujiunga na chama cha ACT wazalendo
Wanachama hao wamejiunga na chama cha Act kwa kurejesha Kadi zao za uanachama na kupewa Kadi mpya za ACT, zoezi lililoongozwa na makamu Mwenyekiti wa chama cha ACT Wazalendo bara Bwana Isihaka Mchinjita
Viongozi waliojiunga ACT ni pamoja na aliekuwa Mwenyekiti Mkoa wa Lindi, Zainab Lipalapi; Mwenyekiti BAVICHA Mkoa wa Lindi, Said Mzee; Katibu wa Jimbo, Musa Rwegoshora; Mwenyekiti wa Wazee Jimbo, Bakari Likaku; Mweka Hazina wa Jimbo, Mohamed Mandoyo; na Mwenyekiti BAVICHA Jimbo, Doa Omari.
Akizungumza mara baada ya kuwakabidhi Kadi zao mpya za ACT wazalendo Mchinjita amewapongeza wanachama kwa uamuzi wao wa kujiunga na chama hicho na kwamba wamechagua jukwaa sahihi
Nae Bwana Mussa Rwegoshora ambae alikuwa katibu wa chama cha Demockasia na Maendeleo CHADEMA Wilaya ya Lindi amesema, wameamua kujiunga na ACT kwa ajili ya kuunganisha nguvu ya pamoja ili kutetea maslah na Maendeleo ya Wana Lindi hivyo ni wajibu wao kuwa na jukwaa la pamoja la upinzani
" Sisi wote tumeamua kujiunga na ACT kwa ajili ya ukombozi wa Jimbo la Lindi na wala haya hayakuja kwa ghafla ni mpango wa mwenyezimungu, wakati tunaendelea kudhoofika na madalali wa siasa mungu akasema hili haliwezekani ngoja wenya haki wakae huku na wenye dhulma waendelee kudhulumu wenzao"
TFCG YAWEZESHA UPATIKANAJI WA HATI MILIKI ZA KIMILA 738 HALIMASHARI YA MTAMA
Na Hadija Omary
Katika kuiwezesha jamii kwenye usimamizi shirikishi wa misitu ya asili na kuondoa migogoro ya umiliki wa Aridhi shirika la kuhifadhi misitu Tanzania (TFCG) limewezesha upatikanaji wa hati miliki za kimila 738 kwa wananchi wa vijiji 10 vya halmashauri ya Mtama Mkoani Lindi
Kijiji cha mihima ni miongoni mwa vijiji 10 vya halmashauri ya Mtama vilivyopo kwenye mradi wa kuongeza usimamizi shirikishi wa misitu chini ya shirika la kuhifadhi misitu Tanzania (TFCG) baadhi ya wananchi walinufaika na hati miliki za kimila wanaeleza faida na manufaa ya hati hizo
Yahaya mtonda ni meneja mradi wa kuongeza usimamizi shirikishi wa misitu kutoka TFCG amesema malengo ya utoaji wa hati hizo ni kuiwezesha jamii kuzingatia misitu ya hifadhi ya vijiji kutoingiliwa na matumizi mengine
Victor shao ni mkuu wa kitengo cha maliasili na uhifadhi wa mazingira halmashauri ya Mtama amesema tangu mwaka 2020 tfcg ilipoanzisha mradi wa kuongeza usimamizi shirikishi wa misitu katika halmashauri hiyo vijiji hivyo vimeweza kuanzisha sheria ndogo ndogo ili kuhakikisha wananchi hawavamii misitu hiyo
Thursday, July 11, 2024
KITUO CHA UTAFITI RUANGWA KAMPASI YA UDSM KUKAMILIKA NDANI YA MIEZI 18
NA HADIJA OMARY
Naibu makamu mkuu wa chuo kikuu cha Dar es salaam ambae ni mratibu wa Mradi wa elimu ya juu kwa mageuzi ya uchumi (HEET) Profesa Benadeta Kiliani amesema watahakikisha ujenzi wa kituo cha utafiti wa sayansi ya Kilimo na chakula cha chuo kikuu cha Dar es salaam unaofanyika katika kijiji cha Likunja wilayani Ruangwa unakamilika ndani ya miezi 18
Profesa kiliani Ameyasema hayo katika kikao kazi cha uzinduzi wa kamati ya "kasema" ambayo ni sehemu ya ulinzi na usalama wa mradi huo na yenye jukumu la kuweka kumbukumbu za kile kinachoendelea katika mradi
Profesa kilian ametoa wito kwa kamati na wananchi wa Ruangwa kutoa ushirikiano wakati wa utekelezaji wa mradi huo
Kamati hiyo ya " kasema " Ina wajumbe watano na inalengo la kukusanya na kushughulikia maoni au malalamiko ya wananchi katika eneo la mradi husika
Jukumu lingine la kamati hiyo ni kuweka kumbukumbu za kile kinachoendelea na kufanyika katika mradi huku ikiwa sehemu ya ulinzi na usalama katika utekelezaji wa mradi
Kwa upande wake Naibu mratibu wa Mradi huo wa Elimu ya juu kwa mageuzi ya uchumi ( HEET) Liberato Haule amesema mradi huo unaotekelezwa na chuo kikuu cha Dar es salaam umedhaminiwa na serikali kupitia fedha ya mkopo kutoka benk ya dunia ukilenga kuboresha huduma za Elimu ya juu nchini ili iweze kuchangia maendeleo ya uchumi.
Amesema mradi huo unatekelezwa katika maeneo mapya 14 ambapo mpaka sasa maeneo mapya matatu tayari yameshafikiwa ambayo ni pamoja na Ngongo (Manispaa ya Lindi), Likunja Wilayani Ruangwa pamoja na Halmashauri ya Bukoba mkoani Kagera
Mwenyekiti wa Halmashari hiyo Andrew Chikongwe anatumia fursa hiyo kuitaka kamati hiyo kutimiza wajibu wao kwa maslah ya halmashauri hiyo
Baadhi ya viongozi na watendaji walioshiriki katika uzinduzi wa kamati hiyo wamepokea kwa shauku na matumaini makubwa na kwamba kituo hicho kitakuwa msaada kwa wakulima na kuongeza fursa za kiuchumi
Wednesday, July 10, 2024
WAFUNGWA/MAHABUSU ZAIDI YA 7,000 WANUFAIKA NA KAMPENI YA MAMA SAMIA LEGAL AID.
Na Mwandishi Wetu
KAMPENI ya msaada wa kisheria ya Mama Samia Legal Aid imeanza kuzunguka kwenye magereza mbalimbali hapa nchini kuwapa msaada wa kisheria wafungwa na mahabusu na mpaka sasa imeshawahudumia zaidi ya 7,000.
Hayo yamesemwa julai 09, na Kaimu Mkrugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Ester Msambazi wakati akizungumza kwenye banda la Mama Samia Legal Aid Campain katika maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaama (DITF) yanayoendelea barabara ya Kilwa wilayani Temeke.
Alisema wameamua kwenda magerezani kwani wanaamini kwamba kuna watu wanaweza kujikuta kwenye mazingira hayo kwa kukosa tu wakili au watu wa kuwaongoza kwenye mashauri yanayowakabili.
“Kuna watu wako mahabusu kwasababu tu wamekosa mwongozo wa kisheria na wakipata mwongozo wanaweza kutoka kwa dhamana au suala linalomkabili likazungumzwa na pande zote mbili na likafikia mwisho,” alisema
Kuhusu wafungwa, alisema kuna watu wanaweza kuwa wamefungwa kifungo cha ndani lakini kupitia kampeni hiyo wanaweza kumsaidia akapata kifungo cha nje kwa kufanyakazi za kijamii au kukata rufaa mahakama za juu.
“Kwa hiyo huduma ya msaada wa kisheria kwa watu walioko kizuizini ni muhimu sana na huwa tunaenda kwenye vituo vya polisi na kwenye magereza na tunapokwenda magerezani tunatoa elimu ya haki jinai kwa watu walioko gerezani,” alisema
Alisema wamekuwa wakitoa elimu kuhusu ukamataji upelelezi uendeshaji wa mashauri, haki na wajibu wa mahabusu na wafungwa wanapokutwa na hatia kwenye kesi mbalimbali za jinai na kupewa kifungo cha ndani.
Alisema wamekuwa wakitoa elimu kuhusu namna ya kupata dhamana na kukata rufaa kwa wale ambao wamehukumiwa lakini hawajaridhishwa na hukumu walizopewa kwenye Mahakama mbalimbali nchini.
“Kupitia kampeni hii tunatoa ushauri kwa mfungwa au mahabusu mmoja mmoja tunakwenda na wanasheria wanaitwa mmoja moja wanashauriwa wanachotakiwa kufanya na wanaandaliwa nyaraka kwasababu wengine wamekaa mahabusu muda mrefu inabidi waandaliwe kila kitu,” alisema
Alisema timu ya wanasheria imekuwa ikiambatana na watu kutoka Ofisi ya Raifa ya Mashtaka, Wizara ya Katiba na Sheria, Jeshi la Polisi Makao Mkuu, Jeshi la Magereza Makao Makuu, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.
“Kwa mfano tukikuta mtu amekaa ndani muda mrefu shauri lake linapigwa dana dana, ushahidi haukamiliki kwa wakati anayehusika hapo atakuwa anayetoka ofisi ya mashitaka kwa hiyo atawajibika kufuatilia kujua kesi imekwamia wapi na kisha ataikwamua na itaanza kusikilizwa na kwenda haraka ili mtu apate haki,” alisema.
Alisema timu hiyo pia imekuwa ikimshirikisha Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Mkoa na vyombo vingine vya utoaji wa haki ngazi ya mkoa wakati wa kusikiliza mashauri hayo ya wafungwa na mahabusu.
“Kuna wafungwa na mahabusu wanapewa msaada wa kisheria na wanatoka kabisa mahabusu au jela na kuna wengine tunawapa elimu tu ya namna ya kudai haki zao wanapoona zinakiukwa kwa hiyo wengi wameshanufaika na kampeni hii ambayo imefika mikoa saba,” alisema
Alisema Mama Samia Legal Aid Campaign pia imekuwa ikiwapa msaada wa kisheria wahamiaji haramu ambao kesi zao zimeshasikilizwa na kutolewa maamuzi warejeshwe nchini kwao lakini wanakosa namna ya kuondoka.
Alisema wamekuwa wakiwasaidia kuhakikisha wanakwenda nchini mwao kwani baadhi ya wahamiaji hao wamekuwa wakishindwa kurudi kwao kutokana na kukosa fedha za kuwafikisha kwenye nchi zao.
Thursday, June 27, 2024
ETDCO YAENDELEA KUJENGA MIUNDO MBINU YA KUSAFIRISHA UMEME MRADI WA TABORA - KATAVI 132kV
Kaimu Meneja Mkuu Kampuni ya ETDCO CPA Sadock Mugendi, Amesema Wanaendelea kujenga miundo mbinu ya Umeme Nchini ikiwemo Njia ya kusafirisha umeme kutoka Tabora hadi Katavi ambao ni mradi wa kusafirisha Umeme na tayari Mradi Umefkia Asilimia 67.
Mugendi amesema ETDCO ni kampuni Tanzu ya Shirika la Umeme Tanzania na ni suluhisho la miundo mbinu ya umeme kwani ipo kwa ajili ya kujenga na kukarabati miundo mbinu ya kusafirisha na kusambaza umeme.
Kaimu Meneja Mkuu CPA Sadock Amesema Mradi wa Kutoka Tabora kwenda Katavi wenye Urefu wa kilometa 383 wa msongo wa 132kV ambao Unatarajiwa kumalizika Mwaka huu kupelekea Mkoa wa Katavi kupata Umeme wa Uhakika pia Kuipunguzia Gharama Tanesco za Kununua Mafuta ya Dizeli kwajili ya Jenereta ili kuzalisha Umeme kwenye Mkoa Wa Katavi.
CPA Sadock Ameipongeza Serikali kuendelea kuwekeza kwenye Sekta ya Nishati ili Kuhudumia Wananchi wake vizuri, Amesema Hayo Wakati Akitembelea Mradi wa Kimkakati wa Tabora kwenda Katavi wenye msongo wa 132kV.
Wednesday, June 26, 2024
KIKWETE MWENYEKITI WA BARAZA LA WAZEE WA SADC YUKO LESOTHO
Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, leo tarehe 26 Juni, 2024, yuko katika Ufalme wa Lesotho kwa nafasi yake kama Mwenyekiti wa Jopo la Wazee wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Jopo hili la Wazee wa SADC ambalo Makamu Mwenyekiti wake Mheshimiwa Paramasivum Pillay B. Vyapoory, Makamu wa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Mauritius, limekutana na Serikali na wadau mbalimbali ndani ya Ufalme wa Lesotho, kama mwendelezo wa juhudi ya kusaidia upatikanaji wa utulivu wa kisiasa katika Ufalme huo.
Jopo limekutana na Mhe. Ntsokoane Samuel Matekane, Waziri Mkuu wa Ufalme wa Lesotho; Mhe. Nthomeng Justina Majara, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Sheria na Masuala ya Bunge; Mhe. Mamonaheng Mokitimi, Mwenyekiti wa Seneti; Viongozi wa Vyama vya Upinzani; Mhe. Constance Seoposengwe, Balozi wa Afrika Kusini nchini Lesotho na wadau mbalimbali.
WAZIRI MKUU AZINDUA VITABU VYA HISTORIA YA BUNGE
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua vitabu vya historia ya Bunge ambavyo vitasaidia kuhamasisha tafiti na kujua zaidi kuhusu mchango wa Bunge katika maendeleo ya jamii nchini.
Amesema kuwa vitabu hivyo pia vitakuwa kielelezo cha mafanikio na changamoto ilizopitia Bunge la Tanzania katika kudumisha demokrasia na utawala wa sheria. “Historia yetu ni sehemu ya mchango wetu kwa jumuiya ya kimataifa katika kukuza amani, utulivu na maendeleo.”
Amesema hayo leo (Jumatano, Juni 26, 2024) wakati wa uzinduzi wa vitabu viwili vya historia ya bunge katika ukumbi wa Pius Msekwa, Jijini Dodoma.Vitabu vilivyozinduliwa ni Kitabu cha Historia ya Bunge kutoka 1926-2024 na Wabunge wa Tanzania na nafasi zao kuanzia mwaka 1965-2023
“Kumbukumbu za historia ya Bunge zinaweza kuchochea utafiti wa kitaaluma na maendeleo ya nadharia za kisiasa na utawala. Watafiti wanaweza kutumia taarifa hizi kujenga ufahamu mpya na kupendekeza mifumo bora ya kisiasa.”
Kwa upande wake Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson amepongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa sehemu ya maono ya bunge ikiwemo kuridhia kulikabidhi bunge maeneo yote yanayozunguka jengo la bunge.
“Tunatarajia kujenga makumbusho ya bunge ambayo yatakuwa ni makubwa kwa nchi nzima ili mtu anapokuja bungeni apate historia ambayo tumeipitia kama nchi lakini pia historia ya bunge letu”





.jpeg.jpg)





.jpeg.jpg)





































