Tuesday, July 16, 2024

MABASI 100 MWENDOKASI YANAKUJA

 

Na Mwandishi wetu 



SERIKALI iko mbioni kuleta mabasi 100 ya mwendokasi nia ikiwa ni kuongeza nguvu kwenye eneo la huduma ya usafiri kwa Jiji la Dar es Salaam 


Msajili wa Hazina Nehemiah Kyando Mchechu amesema hayo jana kwenye kikao maalum na Wahariri kuwa mabasi 100 yatanunuliwa kwa fedha za mkopo kutoka Benki ya NMB.

 


Mchechu amesema kwa kipindi cha miezi miwili amekuwa akifanya vikao na Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART), Kampuni ya Mabasi Yendayo Haraka (UDART), Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) na sasa wamefikia ukingoni.


"Nimekuwa na vikao nao vya mara kwa mara na wadau hawa ili kuokoa hii hali  maana tumeona inaenda kuleta crisis (maafa) na kuathiri taswira nzuri ya Serikali kwenye mradi huu” amesema Mchechu.


Kwa mujibu wa Mchechu mabasi hayo yatakuwa yamewasili nchini ndani ya miezi sita ijayo ili kusaidia kutatua changamoto ya usafiri wa mabasi yaendayo kasi kwa mkoa wa Dar es Salaam.


Kauli ya Mchechu imekuja wakati kukiwa na malalamiko kwa wadau na wananchi juu ya ubora wa mabasi hayo kutokana na mrundikano wa watumiaji pamoja na uchache wa usafiri huo kulinganisha na mahitaji yaliyopo.


Mbali na changamoto hizo baadhi ya mabasi hayo pia ni machakavu na pia yapo katika mfumo wa kizamani kwa  kutokidhi mahitaji ya watumiaji ikiwemo wenye ulemavu na wazee.


Pia msajili wa hazina amesema ni muhimu sana kwa mji kama Dar es Salaam kuwa na kampuni za usafiri zaidi ya moja zitakazosaidiana kutoa huduma hiyo kwa wananchi.


Mwaka jana Oktoba 24, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed  Mchengerwa aliuelekeza uongozi wa Dart kuongeza watoa huduma ili kuboresha huduma ya usafiri huo.


Aidha, Mchechu ameitaka Dart ifikapo Agosti mwaka huu kuhakikisha wametengeneza mifumo ya ukusanyaji fedha ili kudhibiti mapato na kupunguza wizi. 


“Kuna wizi mwingi unafanyika kwenye cash, mimi huwa nasema ni ‘headache’ kusimamia huu mradi kwenye suala la malipo. Tumekubaliana na Dart kuwa hadi Agosti 2024 wawe wamekamilisha mfumo wa nauli kwa njia ya mtandao.” amesema Mchechu


No comments:

Post a Comment