Wednesday, July 10, 2024

WAFUNGWA/MAHABUSU ZAIDI YA 7,000 WANUFAIKA NA KAMPENI YA MAMA SAMIA LEGAL AID.

 

Na Mwandishi Wetu


 


KAMPENI ya msaada wa kisheria ya Mama Samia Legal Aid imeanza kuzunguka kwenye magereza mbalimbali hapa nchini kuwapa msaada wa kisheria wafungwa na mahabusu na mpaka sasa imeshawahudumia zaidi ya  7,000.


 


Hayo yamesemwa julai 09, na Kaimu Mkrugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Ester Msambazi wakati akizungumza kwenye banda la Mama Samia Legal Aid Campain katika maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaama (DITF) yanayoendelea barabara ya Kilwa wilayani Temeke.


Alisema wameamua kwenda magerezani kwani wanaamini kwamba kuna watu wanaweza kujikuta kwenye mazingira hayo kwa kukosa tu wakili au watu wa kuwaongoza kwenye mashauri yanayowakabili.


“Kuna watu wako mahabusu kwasababu tu wamekosa mwongozo wa kisheria na wakipata mwongozo wanaweza kutoka kwa dhamana au suala linalomkabili likazungumzwa na pande zote mbili na likafikia mwisho,” alisema


Kuhusu wafungwa, alisema kuna watu wanaweza kuwa wamefungwa kifungo cha ndani lakini kupitia kampeni hiyo wanaweza kumsaidia akapata kifungo cha nje kwa kufanyakazi za kijamii au kukata rufaa mahakama za juu.


“Kwa hiyo huduma ya msaada wa kisheria kwa watu walioko kizuizini ni muhimu sana na huwa tunaenda kwenye vituo vya polisi na kwenye magereza na tunapokwenda magerezani tunatoa elimu ya haki jinai kwa watu walioko gerezani,” alisema


Alisema wamekuwa wakitoa elimu kuhusu ukamataji upelelezi uendeshaji wa mashauri, haki na wajibu wa mahabusu na wafungwa wanapokutwa na hatia kwenye kesi mbalimbali za jinai na kupewa kifungo cha ndani.


Alisema wamekuwa wakitoa elimu kuhusu namna ya kupata dhamana na kukata rufaa kwa wale ambao wamehukumiwa lakini hawajaridhishwa na hukumu walizopewa kwenye Mahakama mbalimbali nchini.


“Kupitia kampeni hii tunatoa ushauri kwa mfungwa au mahabusu mmoja mmoja tunakwenda na wanasheria wanaitwa mmoja moja wanashauriwa wanachotakiwa kufanya na wanaandaliwa nyaraka kwasababu wengine wamekaa mahabusu muda mrefu inabidi waandaliwe kila kitu,” alisema


Alisema timu ya wanasheria imekuwa ikiambatana na watu kutoka Ofisi ya Raifa ya Mashtaka, Wizara ya Katiba na Sheria, Jeshi la Polisi Makao Mkuu, Jeshi la Magereza Makao Makuu, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.


“Kwa mfano tukikuta mtu amekaa ndani muda mrefu shauri lake linapigwa dana dana, ushahidi haukamiliki kwa wakati anayehusika hapo atakuwa anayetoka ofisi ya mashitaka kwa hiyo atawajibika kufuatilia kujua kesi imekwamia wapi na kisha ataikwamua na itaanza kusikilizwa na kwenda haraka ili mtu apate haki,” alisema.


Alisema timu hiyo pia imekuwa ikimshirikisha Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Mkoa na vyombo vingine vya utoaji wa haki ngazi ya mkoa wakati wa kusikiliza mashauri hayo ya wafungwa na mahabusu.


“Kuna wafungwa na mahabusu wanapewa msaada wa kisheria na  wanatoka kabisa mahabusu au jela na kuna wengine tunawapa elimu tu ya namna ya kudai haki zao wanapoona zinakiukwa  kwa hiyo wengi wameshanufaika na kampeni hii ambayo imefika mikoa saba,” alisema



Alisema Mama Samia Legal Aid Campaign pia imekuwa  ikiwapa msaada wa kisheria wahamiaji haramu ambao kesi zao zimeshasikilizwa na kutolewa maamuzi warejeshwe nchini kwao lakini wanakosa namna ya kuondoka.


Alisema wamekuwa wakiwasaidia kuhakikisha wanakwenda nchini mwao kwani baadhi ya wahamiaji hao wamekuwa wakishindwa kurudi kwao kutokana na kukosa fedha za kuwafikisha kwenye nchi zao.






No comments:

Post a Comment