Tuesday, February 4, 2020

KITONGOJI CHA UKUNI BAGAMOYO WATENGA VIWANJA VYA MICHEZO

Na Omary Mngindo, Bagamoyo.

Kitongoji cha Ukuni, Kata ya Dunda wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani wetenga eneo lenye ekari zaidi ya tatu kwa ajili ya viwanja vya michezo.

Hayo yamebainishwa na diwani wa Kata hiyo Dickson Makamba, mbele ya Mwenyekiti wa Kitongoji hicho Dawson Shigera katika mkutano Mkuu uliogubikwa na changamoto lukuki ikiwemo ubovu wa miundombinu ya barabara maeneo yaliyotelekezwa.

Kauli ya diwani Makamba ilitanguliwa na malalamiko ya udogo wa uwanja unaotumika na vijana kitongojini hapo, hali inayotokana na eneo hilo kuwa na ardhi ya kutosha lakini walioyanunua wameyaacha hivyo kuwa mapori.

"Naomba nizungimzie malalamiko ya Dkt. Omary kuhusiana na ufinyu wa eneo la vijana kushiriki michezo, Kitongoji chetu kina eneo lenye ukubwa wa zaidi ya ekari tatu zilizotengwa kwa ajili ya viwanja vya michezo, ambapo pia tunaweza kuweka mabembea ikawa sehemu ya vyanzo vya mapato," alisema Makamba.

Awali Dkt. Omary alielezea masikitiko yake kuhusiana na changamoto hiyo ya ukosefu wa uwanja wa michezo, huku akiuelezea uwanja uliopo eneo hilo ambalo ndio linalofanyikia mikutano kuwa finyu, ukilinganisha na mipangilio mizuri iliyopo.

"Kitongoji cha Ukuni kina eneo kubwa na mji wake kuwa katika mipango iliyobora, lakini cha kusikitisha ni kukosekana kwa viwanja vya michezo kwa vijana wetu, huku sehemu kubwa ya mji ukiwa umezungukwa na mapori yanayomilikiwa na watu waliopo nje ya Ukuni," alisema Dkt. Omary.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kitongoji hicho Shigera alianza kuwapongeza watangulizi wake kwa namna walivyokisimamia katika nyanja mbalimbali, huku akiwaomba wana-Ukuni kuwapatia ushirikiano ili kwa pamoja wakipatie maendeleo Kitongoji chao.

"Maendeleo tunayoyataka hayawezi kufikiwa kama sisi wananchi tutakuwa wagumu kufika kwenye mikutano, tumezungumzia viwanja vya michezo sekta inayoongoza kuwapatia ajira wa-Tanzania waliowengi," alimalizia Mwenyekiti huyo.

MASHIRIKA YA KISHERIA LINDI YALALAMIKIA TOZO KUBWA SERIKALINI.

NA HADIJA HASSAN, LINDI

WASAIDIZI WA KISHERIA Manispaa ya Lindi Mkoni humo wameiomba serikali kupunguza mrundikano wa tozo zinazotozwa katika mashirika mbali mbali ya usaidizi wa kisheria hapa nchini.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Msaada wa Kisheria Mingoyo (SHIMKIMI) Manispaa ya Lindi Mkoani humo Nuhu Mkapanda alipokuwa anazungumza na BAGAMOYO KWANZA BLOG hivi karibuni ofisini kwake.

Mkapanda alisema awamu ya kwanza mashirika hayo ya usaidizi wa Kisheria hapa Nchini yalikuwa yanasajiliwa na wizara ya Afya jinsia, wazee na watoto ambapo walikuwa wanalipa pesa elfu 50 kwa ajili ya usajili kila baada ya miaka mitatu na shilingi elfu 50 kwa ajili ya ada kila mwaka.

Mkapanda aliongeza kuwa kuanzia mwaka jana 2019 Mashirika hayo pamoja na kusajiliwa katika Wizara hiyo pia wamelazimika kusajiliwa tena kwenye Wizara ya katiba na Sheria ambapo wanatakiwa kulipia tena shilingi elfu 60 kwa ajili ya usajili wa shirika kila baada ya miaka mitatu na elfu 60 kwa ajili ya ada kila mwaka huku wasaidizi wa kisheria wakitakiwa kulipa elfu 30 kwa ajili ya usajili wa kwao binafsi pamoja na elf 30 kwa ajili ya kulipia ada.

“Hali hii inatufanya kwa upande wa Mashirika yenyewe peke yake tuanatakiwa kulipia kiasi cha shilingi 110,000 kwa ajili ya ada kwa wizara zote mbili tulizosajiliwa, na kwa mfano sisi hapa SHIMKIMI tupo wasaidizi wa Kisheria tisa ambapo tanatakiwa kulipia 270,000 sawa na jumla ni 380,000” alisema Mkapanda

“Hii inatuwia mzigo mkubwa kwetu sisi wasaidizi wa kisheria kwa sababu sisi hatulipwi mshahara kutoka sehemu yoyote kazi zetu ni zakujitolea pesa hizi tunazitoa wapi? Na ukizingatia lengo kubwa la kuanzisha mashirika haya ni kusaidia jamii hivyo endapo kama haya mashirika yatafungwa kutokana na michango mikubwa basi tujue kwamba watakaoathirika zaidi ni jamii” Alifafanua mkapanda


Kwa upande wake Victoria Mtemo Msaidizi wa kisheria kutoka katika shirika hilo la usaidizi wa kisheria mingoyo (SHIMKIMI) alisema kwamba fedha hiyo kubwa ambayo inayotumika kulipa Serikalini ingekuwa inabaki Katika mashirika yenyewe ingeweza kusaidia kupanua wigo wa kutoa elimu ya kisheria katika maeneo mbali mbali ambayo mashirika hayo hayajayafikia.

“Kwa mfano huku kwetu Lindi maswala ya Elimu ya ukatili wa kijinsia , ukatili wa watoto wanajamii walio wengi bado hawajapata kabisa na bado hawajui wapi wapeleke malalamiko yao, mathalani sasa hivi kunashida sana ya wababa kuwatelekeza watoto hasa wale wanaochepuka nje ya ndoa kuanzia mimba mpaka mtoto anapozaliwa hivyo hawa wote tunahitaji kuwafikia na kuwapa misaada ya kisheria” alisema.

Mtemo Rehema maluma ni miongoni mwa wateja waliwahi kupata huduma katika shirika la msaada wa kisheria Mingoyo alisema kuwa uwepo wa mashirika hayo ya usaidizi wa kisheria umekuwa msaada mkubwa hasa kwa wananchi wenye uwezo wa chini kwa kuwa mashirika huduma zake hutolewa Bure bila malipo 


“Wananchi wengi tunaweza kufikisha malalamiko yetu hapo tofauti na maeneo mengine ambapo inaweza kukulazimu kulipia kiasi Fulani cha fedha ili uipate haki yako mathalani ukianza kumtafuta wakili moja kwa moja lazima utalipia fedha lakini endapo utayatumia mashirika haya uwezi kulipia fedha yoyote ” alisema Maluma.

KAWAMBWA ASHUHUDIA MRADI WA MAJI CHOMBE JUU

Na Omary Mngindo, Bagamoyo.

WAKAZI wa Vijiji na Vitongoji vilivyomo ndani ya Kata zinazounda Jimbo la Bagamoyo Mkoa wa Pwani, wanatarajia kunufaika na usambazaji wa maji kutoka kwenye vyanzo vilivyopo kweye maeneo yao.

Hayo yamebainishwa na Mbunge wa Jimbo hilo Dkt. Shukuru Kawambwa, akizungumza na wakazi wa Kitongoji cha Chombe Juu Kata ya Yombo, aliposhuhudia matofali na mabomba yatakayojenga kituo cha kuchotea maji sanjali na mabomba ya kusambazia kwenye vituo vitatu.

Mbele ya James Kionaumela Mhandisi wa Maji (RUWASA), Makamu Mwenyekiti wa halmashauri Mohamed Usinga ambaye ndie diwani wa Kata hiyo na Hassani Wembe diwani wa kata ya Kiromo, Dkt. Kawambwa alisema kuwa juhudi hizo za serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli, zimedhamiria kuwakomboa wananchi.

"Niliwahi kuwaleta marafiki zangu hapa kuchimba visima viwili kwa thamani ya zaidi ya shilingi milioni 9, lakini kwa bahati mbaya maeneo hayo moja halikuwa na maji kabisa, lingine maji yake hayakuwa katika ubora, yalikuwa na rangi sana," alisema Dkt. Kawambwa.

Kwa upande wake Mhandisi Kionaumela aliishukuru serikali kwa kuanzisha chombo kinachoitwa RUWASA, kinacholenga kushugbulikia usambazaji wa maji kutoka kwenye vyanzo na kuwasambazia wananchi, lengo ni kumtua ndoo mwanamke.

"RUWASA tumepewa jukumu la kuwasambazia maji wananchi, kutoka katika visima tusambaza mabomba ili maji hayo yawafikie wananchi, hapa Chombe Juu leo tumeleta matofali na mabomba kwa ajili ya kazi hiyo," alisema Kionaumela.

Makamu Mwenyekiti Usinga alisema kuwa juhudi hizo zinalenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji, huku akimshukuru Mbunge Dkt. Kawambwa kwa juhudi zake za kuwatafuta marafiki kwa ajili kuchimba visima vya maji.

"Tulikuja kutoa ahadi ya maji katika eneo hili, leo tumefika hapa chini ya Mkuu wetu wa msafara Dkt. Shukuru Kawambwa anayefanyakazi kubwa ya kuwatafuta marafiki kwa ajili ya kuendeleza mradi wa maji uliopo kwnye eneo hill," alisema Usinga.

Nae Wembe hakusita kuanza kumpongeza Dkt. Kawambwa kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha wananchi wake wanaondokana na changamoto ya maji katika maeneo yao.

Monday, February 3, 2020

WANANCNH LINDI WATAKIWA KUTUMIA WIKI YA SHERIA KUPATA ELIMU YA SHERIA.I


NA HADIJA HASSAN, LINDI.

WANANCHI Mkoani Lindi wametakiwa kuitumia wiki ya sheria kupata Elimu mbali mbali inayohusiana na mambo ya Sheria na haki zao kupitia vituo mbali mbali vilivyotengwa na mahakama kwa ajili ya kutoa elimu.

Wito huo umetolewa na Hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya Mkoa wa Lindi Elimo Masawe kwenye ufunguzi wa wiki ya Sheria uliofanyika mwishoni mwa wiki katika viwanja vya mahakama ya mkoani humo.

Wiki hiyo ya sheria huanza february 1 na kuhitimishwa february 6 kila mwaka ikiwa ni ishara ya kuanza rasmi kwa shughuli za mahakama hapa nchini ambapo kwa mwaka huu 2020 Kauli mbiu ya wiki ya sheria ni “uwekezaji na biashara wajibu wa mahakama na wadau kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji”

Masawe alisema katika Mkoa wa Lindi na wilaya zake kwa ujula imetenga vituo zaidi ya 50 kwa ajili ya kutoa elimu kwa umma juu ya masuala ya sheria Alisema elimu hiyo ya kisheria itatolewa kwa kushirikiana na wadau wengine wa mahakama kama vile, jeshi la polisi, magereza, mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) Shirika la kuhudumia viwanda vidogo (SIDO) pamoja na wadau wengine.

Akielezea vituo vya kutolea elimu, alisema kuwa vituo hivyo vimewekwa katika maeneo yenye misongamano wa watu kama vile masoko makubwa na madogo, vituo vya mabasi pamoja na kutoa elimu katika shule za msingi na sekondari, makundi ya wajasiriamali wadogo na wakati, wafanya Biashara ,vyuo vya ufundi pamoja na makundi ya madereva bajaji na boda boda.

“Lengo kubwa la kutaka kufikia makundi haya yote tunataka jamii ituelewe sana kwa sababu jamii ikishatuelewa itakuwa na nafasi ya ujasiri wa kusimamia haki zao kwani kitendo cha mtu kuijua haki yake ni sawa na kuongeza ujasiri wa maisha”

Nae mwenyekiti wa kamati ya elimu , Hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya Wilaya ya Lindi, Maria Batulaine alisema kuwa miongoni mwa mambo watakayowafundisha wananchi kwenye vituo hivyo kuhusiana na sheria ni pamoja na kujua sheria za jinai na madai, kuwajulisha shughuli zinazofanywa na mahakama, huduma zinazotolewa na mahakama na mambo mbali mbali ya kisheria.

Akizindua wiki hiyo ya sheria katibu tawala wa wilaya ya Lindi Tomas Safari kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya Hiyo Shaibu Ndemanga, aliwataka wadau wa mahakama kudumisha mshikamano ili kuhakikisha haki ya mwananchi inapatikana kwa wakati.

Saturday, February 1, 2020

ULINZI NA USALAMA WA MTOTO NI JUKUMU LA JAMII NZIMA



 
Devotha Ndunguru Ofisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Songea akisisitiza jambo
 NA Joyce Joliga


Wanawake Mkoani Ruvuma wameshauriwa kuwa walinzi  namba moja kwa watoto wao wachanga  na wale wenye umri mdogo wa miaka 3-8 kwa  kujenga tabia ya kukagua nguo za ndani za watoto wao pamoja na kuwakagua mara kwa mara ilikujua kama wamefanyiwa vitendo vya ukatili.

Kwa mujibu wa  Ofisa ustawi wa Jamii Manispaa ya Songea Devotha Ndunguru anasema matukio ya watoto kufanyiwa vitendo vya ukatili ni mengi Songea  hivyo Suala la Ulinzi na Usalama wa Mtoto ni jukumu la jamii nzima ili kuhakikisha ustawi  wa mtoto ili aweze kukua akiwa mwenye afya njema,furaha , na Amani