Sunday, January 12, 2020

RAIS DKT. MAGUFULI AHUDHURIA KILELE CHA SHEREHE ZA MIAKA 56 ZA MAPINDUZI MATUKUFU YA ZANZIBAR MJINI UNGUJA JANUARI 12, 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ally Mohamed Shein mara baada ya kuwasili katika sherehe za maadhimisho ya Miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyofanyika katika uwanja wa Amani Unguja. Januari 12, 2020.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akipokea salamu ya heshima kutoka katika paredi maalum ya vyombo vya ulinzi na usalama wakati wa sherehe za maadhimisho ya Miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyofanyika katika uwanja wa Amani Unguja. Januari 12, 2020.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Bi. Fatuma Karume mke wa muasisi na Rais wa kwanza  Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Hayati Abeid Karume mara baada ya kuwasili katika sherehe za maadhimisho ya Miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyofanyika katika uwanja wa Amani Unguja. Januari 12, 2020.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Waziri mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Edward Lowassa baada ya kumalizika kwa sherehe za maadhimisho ya Miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyofanyika katika uwanja wa Amani Unguja. Januari 12, 2020



WAZIRI LUGOLA AMUAGIZA MKUU WA NIDA KUTOA VITAMBULISHO KILA SIKU.

NA HADIJA HASSAN, LINDI.

WAZIRI wa mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Vitambulisho vya Taifa NIDA Arnold Kihaule pamoja na Menejmenti yake kufika ofisi za Wizara hiyo siku ya jumatatu wakiwa na mpango kazi unaoonyesha uhalisia wa kumaliza changamoto ya wananchi kupata namba za Vitambulisho kabla ya tarehe 18, January mwaka huu.


Lugola ametoa maagizo hayo jana katika mkutano wa hadhara na wanachi wa Mkoa wa Lindi uliofanyika katika Viwanja vya Ilulu Manispaa ya Lindi Mkoani humo.


Maagizo hayo ya lugola yamekuja baada ya kubaini kuwepo kwa namba 17,447 za NIDA kutoka Mkoa wa Mtwara na Ruvuma ambazo zimekamilika zikiwa bado ofisini pasipo kuwasilishwa kwa wahusika na Vitambulisho 88,000 kati ya 117000 vilivyotengenezwa katika Mkoa wa Lindi vikiendelea kubaki katika ofisi za NIDA.


"Pamoja na maagizo hayo ninakutaka Mkurugenzi wa NIDA ugawe Mikoa kwa Wakurugenzi wako na wazunguke katika hiyo Mikoa kila siku na watakapomaliza watengeneze taarifa za kila Mkoa ambazo watakuwa wanazituma kwa katibu wa Wizara kila siku ili tuone mwenendo wa uzalishaji na ugawaji wa namba unavyofanyika" alisema Lugola.


Alisema ili kukimbizana na muda uliobaki wafanyakazi wa NIDA wanatakiwa kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha wananchi wote ambao hawajapata namba za vitambulisho wanapata namba hizo kabla ya tarehe ya mwisho kufika bila kujali mapumziko ya juma ama siku za siku kuu.


Maagizo mengine aliyoyatoa Waziri huyo wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola kwa Mkuu wa NIDA ni kuhakikisha ofisi za NIDA Zote hapa Nchini zinaongezwa wafanyakazi wa ziada, ofisi zote za NIDA hazitakiwi kufungwa Mpaka pale mwananchi wa mwisho aliyopo ofisini anapomalizika kupewa huduma bila kujali wingi wa watu waliopo

WAAJIRI WASIOLIPIA WAFANYAKAZI MIFUKO YA HIFADHI KUSHTAKIWA.

Happy Lazaro, Arusha.

Naibu waziri wa kazi, Vijana, Ajira na Ulemavu , Antony Mavunde ameiagiza Mifuko ya hifadhi ya jamii nchini kuwachukulia hatua kali ya kuwafikisha mahakamani waajiri wote wasiopeleka michango ya wafanyakazi wao kwenye mifuko hiyo na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wafanyakazi pindi wanapoacha ama kuachishwa kazi.


Mavunde ametoa kauli hiyo jijini Arusha wakati alipokuwa akiongea na wafanyakazi wa hoteli za Naura springs na Impala za jijini Arusha ambapo wafanyakazi hao walimweleza changamoto mbalimbali ikiwemo ya suala la michango ya mifuko ya Hifadhi ya jamii.


Naibu waziri amesema kuwa kumekuwepo na malalamiko mengi kwa baadhi ya waajiri nchini kutopeleka michango ya wafanyakazi wao kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii jambo ambalo alionya ni kinyume cha sheria na kuitaka mifuko hiyo kuwakamata waajiri hao na kuwafikisha mahakamani.


Akiongelea changamoto za wafanyakazi katika hoteli hizo,Mavunde ameitaka menejimenti ya hoteli hiyo kuboresha utendaji wake wa kazi na kuhakikisha wanakuwa kitu kimoja na wafanyakazi wao kwani serikali inawahitaji wawekezaji wa mahoteli katika kuimarisha sekta ya utalii na ajira.


Naibu waziri amempongeza mkurugenzi wa hoteli hiyo,Randy Mrema kwa kukubali kumaliza changamoto ya malimbikizo ya mishahara ya wafanyakazi wake ndani ya miezi mitatu kuanzia sasa hadi ifikapo Machi 31 mwaka huu. 


Kwa upande wake Mkurugenzi wa hoteli hizo Randy Mrema alimweleza Naibu waziri kuwa yupo tayari kumaliza changamoto za wafanyakazi wake na kuahidi pindi ifikapo Januari 31 mwaka huu atalipa mishahara ya miezi miwili na kwamba ifikapo Machi 31 mwaka huu atamaliza madai yote ya wafanyakazi hao.


Awali wafanyakazi hao walimweleza Naibu waziri kuhusu madai ya kutolipwa mishahara ya miezi sita pamoja na baadhi yao waliopunguzwa kazi hivi karibuni kutolipwa stahiki zao ikiwemo mishahara ya kuvunja mkataba.


Wamedai kuwa hali hiyo imewafanya waishi katika mazingira magumu na kushindwa kumudu maisha ikiwemo kuwasomesha wao ,kodi za pango pamoja na mahitaji mengine ya kujikimu.


Hata hivyo wameahidi kuendelea na kazi bila kuwa na kinyongo huku wakisubiri ahadi ya mwajiri wao ya kuwalipa mishahara katika kipindi cha miezi mitatu alichoahidi.