Monday, August 26, 2019

MGALU ATOA ONYO KWA MKANDARASI WA UMEME VIJIJINI KILIMANJARO

Image may contain: 1 person, crowd and outdoor
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, akizungumza na wananchi wa Kata ya Ngarenairobi, Wilaya ya Siha, Mkoa wa Kilimanjaro alipokuwa katika ziara ya kazi, Agosti 25, 2019.
...................................

Na Veronica Simba – Kilimanjaro.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu ametoa onyo kali kwa Mkandarasi Urban & Rural Engineering, ambaye anatekeleza mradi wa umeme vijijini awamu ya tatu mkoani Kilimanjaro, kwa kumwambia asiijaribu serikali kwa kutikisa kibiriti kwani njiti zimejaa na kitawaka.


Alitoa onyo hilo kwa nyakati tofauti Agosti 25, 2019 akiwa katika ziara ya kazi kwenye Wilaya za Hai na Siha, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi na viongozi wao kuwa kasi ya mkandarasi huyo hairidhishi.


Akizungumza katika mkutano na wananchi wa Hai, Naibu Waziri Mgalu alikiri mbele yao kuwa utendaji kazi wa mkandarasi husika unasuasua na zaidi ameonesha vitendo vya utovu wa nidhamu kwa serikali kwa kutoitikia wito alipoitwa kushiriki kwenye ziara hiyo pasipo kutoa sababu yoyote.


Akielezea zaidi, Naibu Waziri alisema yeye binafsi alijaribu kuwasiliana na mkandarasi huyo kwa njia ya simu pasipo mafanikio na hata ujumbe mfupi wa maandishi aliomtumia kumtaka apokee simu, haukujibiwa; kitendo ambacho alikiita ni dharau.


“Sasa mimi nataka nitoe salamu kwake. Mkandarasi Urban & Rural Engineering naona unatikisa kibiriti, unataka ujue kama kina njiti au hakina, na kama njiti zimejaa au zina baruti. Nataka nikwambie kibiriti kimejaa, njiti zina baruti na kitawaka.”


“Ulichokifanya ni dharau na unatupelekea tufanye maamuzi ya kuanza mapitio; na ni kweli nathibitisha ameshindwa kazi,” alisema Naibu Waziri.


Kufuatia hali hiyo, alimwagiza Msimamizi wa Mradi husika kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kumjulisha mkandarasi huyo kwenda Dodoma mara moja kushiriki katika kikao kitakachofanya mapitio ya suala hilo ili ikibidi hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.


“Kama ameshindwa kazi, tutawapatia wakandarasi wengine au hata TANESCO wanaweza kumalizia kazi husika.”


Awali, Meneja wa TANESCO wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Mahawa Mkaka, alimweleza Naibu Waziri kuwa, Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu mkoani Kilimanjaro unagharimu kiasi cha shilingi za kitanzania takribani bilioni 12.


Alisema, Mradi unahusisha ujenzi wa kilomita 150 za msongo wa umeme wa kilovoti 33, ujenzi wa kilomita 334 za msongo wa umeme wa kilovoti 400 na ufungaji wa mashine umba (transfoma) 132 na kwamba unatarajiwa kuunganishia umeme jumla ya wateja 3,572 katika vijiji 75 ndani ya mkoa.


Aliongeza kuwa, kwa ujumla utekelezaji wa mradi husika mkoani humo umefikia asilimia 43 hadi sasa.


Katika ziara hiyo, Naibu Waziri aliwasha umeme katika shule za msingi za Roo na Msamadi zilizopo wilayani Hai, pamoja na eneo la viwanda Mwangaza na shule ya msingi Gararagua wilayani Siha. Pia, alizungumza na wananchi wa Kata ya Ngarenairobi wilayani Siha.
Image may contain: 2 people, people standing, hat and outdoor
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akiwasha rasmi umeme katika shule ya msingi Gararagua, iliyopo wilayani Siha, Mkoa wa Kilimanjaro akiwa katika ziara ya kazi, Agosti 25, 2019.
 Image may contain: one or more people and outdoor
Umati wa wananchi wakishuhudia tukio la uwashwaji rasmi wa umeme katika shule ya msingi Msamadi iliyopo wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro. Tukio hilo lilifanywa na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani), akiwa katika ziara ya kazi, Agosti 25, 2019.


AMUIBA MTOTO WA MIEZI 3 NA KUTOWEKA NAE.

Mtu asiyejulikana amemuiba mtoto wa miezi mitatu aitwae Swaum Saidi na kutoweka nae kusikojulikana.
Akitoa Taarifa kwa waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi, (ACP) Wankyo Nyigesa, alisema tukio hilo limetokea Tarehe 25 agosti 2019 majira ya saa saba mchana maeneo ya Msongola wilaya ya kipolisi Mlandizi.


Alisema mama wa mtoto huyo aliyejulikana kwa jina la Mariam Shomari mwenye umri wa miaka 25 aligundua kuibiwa mtoto wake baada ya kurejea nyumbani kutoka kuomba kibiriti nyumba ya jirani.


Kamanda Nyigesa aliendelea kusema kuwa, mama wa mtoto huyo alienda kuomba Kibiriti kwa jirani yake umbali wa mita mia mbili na kwamba baada ya kurejea nyumbani hakumkuta mtoto wake ambae alimuacha chumbaani.


Alisema mwizi huyo wa mtoto alitumia mbinu ya kumdanganya mtoto mdogo wa miaka mitatu3, Fatma Saidi aliyebaki na mtoto huyo kwa kumwambia ametumwa kumchukua mtoto ili ampeleke kwa mama yake.


Mwizi huyo wa mtoto alifanikiwa kutekeleza kitendo hicho kiovu cha kuiba mtoto na kutokomea kusikojulikana.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linaendelea na msako mkali wa kumtafuta mwizi huyo wa mtoto.


Kamanda wa Mkoa wa Pwani, anatoa wito kwa viongozi wa serikali za mitaa, watendaji wa kata, wenyeviti wa vitongoji na vijiji na wananchi wote kwa ujumla, kutoa taarifa iwapo watamtilia mashaka mtu watakaemuona na mtoto ili akamatwe.
  

DKT. KALEMANI AAGIZA WAKANDARASI KUKAMATWA.

Image may contain: 1 person, on stage, standing and outdoor
Na Hafsa Omar, Katavi.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ametoa agizo kwa vyombo vya usalama mkoani Katavi kuwakamata wakandarasi waliopewa kazi ya kusambaza umeme vijijini mkoani humo kutoka kampuni ya CRCBEG baada ya kusuasua katika utekelezaji wa kazi.


Alitoa agizo hilo jana Agosti 25, 2019 wakati akielekea kwenye kijiji cha Ntibiri wilayani Mlele, Mkoa wa Katavi ili kukagua kazi ya usambazaji umeme, mara baada ya kuwasha umeme katika kijiji Kirida wilayani humo.


Waziri wa Nishati pia alitoa agizo la kushikiliwa kwa hati za kusafiria za wakandarasi hao mpaka watakapomaliza kazi zao za usambazaji umeme walizopangiwa na Serikali.


“ Nilitoa mwezi mmoja eneo lote la kilometa 27 muwe mmeshawasha umeme lakini bado, Kijiji cha Majimoto bado hamjawasha, leo nimepita hapa sijaona vibarua wakihangaika, na wala nguzo hazijafika, nimefika Shule ya Sekondari kule nguzo hazijafika na wala hamjasambaza popote.”alisema Dkt. Kalemani.


Waziri Kalemani, pia aliwaagiza Mameneja wa TANESCO kutoondoka katika eneo hilo ili kuhakikisha kazi ya usambazaji umeme inafanyika kwa kasi zaidi, “ninataka umeme ufike Kijiji cha Majimoto, ifikapo tarehe 5 mwezi ujao na mameneja wote mtabaki hapa kusimamia kazi.”
Akizungumza na Wananchi wa kijiji cha Ntibiri, Dkt.


Kalemani aliwaeleza wananchi hao kuwa, Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 89 kwa ajili ya usambazaji umeme mkoani Katavi na kuwahakikishia kuwa, mkoa mzima utapata umeme.


“Leo nimetoa maelekezo kuwa, eneo la Ntibiri na maeneo ya jirani, wakandarasi watamaliza kazi mwezi wa 12 mwaka huu, hakuna kijiji kitakachobaki, sasa kama eneo lako halijapitiwa na umeme, kuanzia sasa litapitiwa.” Alisema Dkt Kalemani.


Akiwa wilayani Mlele, Waziri wa Nishati, pia aliwasha umeme katika Kijiji cha Society katika eneo la wachimbaji wadogo wa dhahabu hali itakayopelekea wachimbaji hao kufanya shughuli zao kwa tija.

AKAMATWA KWA KUBAKA MTOTO WA MIAKA 3 MLANDIZI.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani, limemkamata mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Dismas Siyvester mwenye umri wa miaka 35, kwa kosa la kubaka mtoto wa miaka mitatu 3, jina linahifadhiwa.


Akitoa Taarifa kwa vyombo vya habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi, (ACP) Wankyo Nyigesa, alisema tukio hilo limetokea Tarehe 19, agosti 2019 majira ya saa tisa alasiri huko Mlandizi "A" kata ya Mlandizi tarafa ya Mlandizi wilaya ya Kipolisi Mlandizi mkoani humo.


Alisema mtuhumiwa aliiba mtoto huyo na kwenda nae vichakani kisha kumfanyia kitendo cha ubakaji.


Aidha, aliongeza kuwa, mara baada ya taarifa kutolewa, jeshi la polisi kwa kushirikiana na raia wema lilimkamata mtuhumiwa akiwa na mtoto huyo (aliyebakwa) katika mashamba ya mboga mboga Vichakani, na kwamba mara baada ya uchunguzi imebainika kuwa, mtoto huyo ameingiliwa kimwili.   

Sunday, August 25, 2019

DC BAGAMOYO AWAONYA WENYEVITI WA VITONGOJI NA VIJIJI KUHUSU KUKARIBISHA WAFUGAJI WAGENI.

 
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, zainabu kawawa, akizungumza na wananchi wa kata ya Kiwangwa alipofanya ziara kusikiliza kero za wananchi, katikati ni Katibu tawala wilaya ya Bagamoyo, Kasilda Mgeni.
................................
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, zainabu kawawa amewaonya wenyeviti wa vitongoji na vijiji wilayani humo kuacha tabia ya kuwakaribisha wafugaji wageni ili kuepuka migogoro ya wafugaji na wakulima wilayani humo.


Mkuu huyo wa wilaya ambae ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya, ameyasema hayo katika ziara yake aliyoifanya kwenye vijiji vya kata za Kiwangwa na Fukayosi iliyolenga kusikiliza kero za wananchi.


Katika ziara hiyo ambayo alipata nafasi ya kufanya mikutano ya hadhara na kuwapa nafasi wananchi kueleza kero zao ambapo wakulima wamelalamikia wafugaji kuingiza mifugo yao kwenye mashamba yenye mazao hali inayopelekea wakulima kushindwa kuvuna kile walichopanda.


Wakulima hao walimueleza Mkuu wa wilaya kuwa, wenyeviti wa vijiji na vitongoji wamekuwa chanzo cha migogoro hiyo kwakuwa wanawakaribisha wakulima wageni ambao hawafuati taratibu zilizowekwa katika vijiji hivyo.


Akitoa majibu mbele ya Mkutano wa hadhara, Mkuu huyo wa wilaya alisema wenyeviti wa vitongoji wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya sheria ili kuepuka kuleta migogoro kwa wananchi.


Alisema mwenyekiti yeyote wa kitongoji au kijiji atakaehusika kuwakaribisha wafugaji wageni atamchukulia hatua za kisheria na kinidhamu kwani kitendo hicho kinachangia migogoro.


"Kama umeshindwa kuwahudumia wananchi kwenye kitongoji chako mpaka uchukue chochote kitu kutoka kwa wafugaji ili uwakaribishe na hali unajua huna eneo kwenye kitongoji chako, nikianza operesheni yangu ya kuondoa wafugaji wageni nitaanza na wewe Mwenyekiti wa Kitongoji, Alisema Mkuu huyo wa wilaya.


Aliongeza kwa kusema kuwa kitendo hicho ni kuniharibia mazingira yangu ya kazi na kwamba yeye hayuko tayari kuharibiwa kazi na wenyeviti wa vitongoji au vijiji.


Alisema wilaya ya Bagamoyo tayari ina wafugaji ambao wamesajiliwa katika vijiji vyao na kutengewa maeneo kupitia mpango wa matumizi bora ya ardhi hivyo si vyema kuleta wafugaji wageni ambao hawana maeneo ya kupeleka mifugo yao.


Aidha, amewaonya pia wafugaji kuacha kuwakaribisha wafugaji wenzao kutoka maeneo mengine ili kuepuka migogoro ya wafugaji na wakulima ambayo imebainika inasababishwa na wageni.


Kwa upande wao wafugaji wamesema watashirikiana na serikali kuwaondoa wafugaji wageni kwakuwa hata wao wanapata madhara kutoka kwa wafugaji wageni.


Wamesema kuwepo kwa wafugaji wageni kumekuwa na madhara ya aina nne kwenye maeneo yao ambayo ni wafugaji wageni huvamia kwenye malisho ya wenyeji na kufanya wenyeji kukosa sehemu ya kulisha, wizi wa mifugo, kuleta magonjwa ya kuambukiza ya wanyama na pia wafugaji wageni wamekuwa na tabia ya kubaka mabinti wenyeji wa maeneo husika.


Kufuatia hali hiyo, Mkuu wa wilaya amemuagiza Mkuu wa polisi wilaya ya Bagamoyo, kuchukua maelezo ya Mwenyekiti wa kitongoji cha Segwa na katibu wake ili kuwabaini wale walifanya vitendo viovu kwenye eneo hilo na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
 
Wenyeviti wa vitongoji kata ya Kiwangwa wakisikiliza maelekezo kutoka kwa Mkuu wa wilaya.
 
Baadhi ya wafugaji wakimsikiliza Mkuu wa wilaya katika mkutano wa hadhara uliofanyika kata ya Kiwangwa.
 
 Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya ya Bagamoyo, wakifuatilia mazungumzo ya Mkuu wa wilaya hiyo alipofanya mkutano wa hadhara kata ya Kiwangwa.
Baadhi ya wananchi wakisikiliza mazungumzo ya Mkuu wa wilaya alipokuwa akizungumza katika mkutano wa hadhara kata ya Kiwangwa.