Saturday, July 20, 2019

DKT. KALEMANI AWAPA TABASAMU KYERWA NA KARAGWE.

Image may contain: 2 people, people smiling, people standing and wedding
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani akizungumza na wananchi wa kijiji cha Nyarugondo wilayani Karagwe, Mkoa wa Kagera (hawapo pichani), wakati wa hafla ya kuwasha rasmi umeme kijijini hapo.
....................................
Na Veronica Simba – Kagera

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amewasha rasmi umeme katika kijiji cha Nyakabwera wilayani Kyerwa na Nyarugondo wilayani Karagwe, Mkoa wa Kagera, tukio lililoibua furaha kwa wakazi wa vijiji hivyo.


Akiwa amefuatana na viongozi na wataalamu mbalimbali wa serikali na vyama vya siasa; Waziri aliwasha umeme katika maeneo hayo na kuzungumza na wananchi, akiwa katika ziara ya kazi, jana, Julai 18, 2019.


“Nampongeza Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli; anafanya kazi kubwa. Katika sekta ya nishati, amedhamiria kufikisha umeme katika vijiji vyote nchini,” Waziri Kalemani aliwaambia wananchi.


Kabla hajawasha rasmi umeme katika vijiji hivyo, Waziri alitoa hamasa kwa wananchi wa maeneo husika ambao hawajaunganishiwa umeme, kuchangamkia fursa hiyo kwa kujitokeza kwa wingi kulipia gharama inayohitajika ambayo ni shilingi 27,000 ili wote wawe na umeme.


Vilevile, aliwataka kulinda miundombinu ya umeme iliyopo katika maeneo yao ili kuiwezesha serikali kuendelea kuwapatia huduma hiyo kwa ufanisi.


Alisema atakayebainika kuhujumu miundombinu hiyo, atachukuliwa hatua kali za kisheria.


Pia, aliwashauri viongozi wa taasisi za umma pamoja na miradi mbalimbali ya kijamii kama vile mitambo ya maji, shule, vituo vya afya, masoko, nyumba za ibada na kadhalika, kutenga fedha za kulipia huduma ya kuunganishiwa umeme ili nishati hiyo ipelekwe katika maeneo hayo muhimu.


“Sambamba na hilo, viongozi ainisheni maeneo ambayo mmepanga kujenga miradi ya maendeleo na taasisi za umma ili mkandarasi ayapelekee umeme, ili muda wa kujenga utakapofika, kuwepo na nishati hiyo tayari,” alielekeza.


Aidha, Waziri alihamasisha matumizi ya vifaa vya Umeme Tayari (UMETA) katika kuunganisha umeme ili kuepuka gharama kubwa za kutandaza mfumo wa nyaya za umeme kwenye majengo. Aligawa vifaa hivyo bure katika vijiji vyote viwili na kumtaka mkandarasi anayetekeleza mradi wa umeme vijijini katika maeneo hayo kutowauzia wananchi vifaa hivyo hadi pale vilivyotolewa bure na serikali vitakapoisha.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi mbalimbali wa serikali na vyama vya siasa katika maeneo hayo, waliishukuru serikali kwa jitihada zake za kuwafikishia wananchi maendeleo kupitia uunganishaji umeme.


Waliomba maeneo yaliyosalia yafikishiwe huduma hiyo mapema ili wananchi wote wanufaike kwa kuanzisha biashara ndogondogo kwa ajili ya kuinua maisha yao kiuchumi.
Image may contain: 7 people, people smiling, people standing

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati), akikata utepe kabla ya kuwasha rasmi umeme katika nyumba ya Bwana na Bibi Josam Paulo ikiwa ni ishara ya uwashaji rasmi wa umeme katika kijiji cha Nyarugondo wilayani Karagwe, Mkoa wa Kagera, Julai 18, 2019. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Dkt. Tito Mwinuka na wa wa kwanza kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga.
Image may contain: 2 people, people sitting and indoor

Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Rashid Mwaimu (kushoto) akimweleza Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (kulia), hali ya upatikanaji wa umeme wilayani humo. Waziri alifika ofisini kwa Mkuu wa Wilaya Julai 18, 2019 akiwa katika ziara ya kazi.
 Image may contain: 6 people, people standing and outdoor

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani akielekea kuwasha umeme katika makazi ya baadhi ya wananchi wa kijiji cha Nyarugondo wilayani Karagwe, Mkoa wa Kagera akiwa katika ziara ya kazi, Julai 18, 2019.
 Image may contain: 2 people, crowd and outdoor
Sehemu ya umati wa wananchi wa kijiji cha Nyakabwera wilayani Kyerwa, Mkoa wa Kagera, wakimsalimu Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) kwa kuinua mikono, alipofika kuwawashia rasmi umeme na kuzungumza nao, akiwa katika ziara ya kazi Julai 18, 2019.


ADAIWA KUVUTA BANGI NA KUMUUA BIBI YAKE.

Kijana mmoja aliyejulikana kwa jina la Athuman Khamis Mkazi wa Kijiji cha Usongwa Kata ya Bukene wilayani Nzega mkoa wa Tabora anatuhumiwa kumuua kwa kumchinja bibi yake, Rahel Daud(67) mkazi wa kijiji hicho huku Sababu ikielezwa ni uvutaji wa bangi kwa kijana huyo

Tukio hilo limetokea julai 19, 2019 majira ya saa 12 jioni katika kijiji cha Usongwa kata ya Bukene wilayani Nzega Mjini 

Mkuu wa Wilaya ya Nzega Godfrey Ngupulla amesema kwa upelelezi aliofanya hadi chanzo cha mauaji hayo ni kuwa uliotokea ugomvi mdogo wa kurushiana maneno kwa bibi huyo na kijana huyo na ndipo alipomvizia ndani na kumchinja kwa kumtenganisha kiwiliwili na shingo

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya Nzega George Mgarega amesema kuwa mwili huo ulivyofikishwa hospitalini hapo ulifanyiwa uchunguzi na kuonekana ulikuwa na majeraha ya kukatwa na kitu chenye ncha kali kwa kuanzia nyuma na kwenda mbele hivyo kusababisha kuvuja kwa damu nyingi na maumivu makali na hivyo kupoteza maisha.

Wakati huo huo Jeshi la Polisi wilayani Nzega linaendelea kufanya uchunguzi wa kumtafuta kijana huyo aliyefanya mauaji hayo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, ambae ni Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Mh. Godfrey Ngupulla  akielezea jinsi tukio la Mauaji hayo  lilivyotokea.

OMARI MGUMBA AWATOA HOFU WAKULIMA WA PAMBA MWANZA

Naibu Waziri wa Kilimo, Omari Mgumba, akizungumza na wakulima wa pamba wilayani Kwimba. Kulia ni Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza Salum Kalli na kushoto ni Mbunge wa Kwimba Shanif Mansoor.
...............................


NA BALTAZAR MASHAKA, KWIMBA

SERIKALI imewatoa hofu wakulima wa zao la pamba na kuwataka wasirubuniwe na walaghai, wapeleke pamba yao sokoni kwani fedha zipo, watalipwa na hakuna mkulima atadhulumiwa.

Pia imewahakikishia wanunuzi wa pamba kuwa hawatapata hasara baada ya serikali kuridhia kutoa ruzuku ya kuwafidia endapo bei ya pamba haitapanda kwenye soko la dunia ifikapo Agosti 15, mwaka huu.


Kauli hiyo ilitolewa na Naibu wa Waziri wa Kilimo Omari Mgumba alipozungumza na wakulima wa vijiji vya wilaya za Magu na Kwimba na baadhi ya wanunuzi wa pamba kwenye wilaya hizo juzi kwa nyakati tofauti.



Mkumba ambaye aliambatana na Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza Salum Kalli alisema kutokana na mdodoro wa bei ya pamba kwenye soko la dunia, msimamo wa serikali wakulima wauze pamba yao kwa bei dira ya sh. 1,200 kwa kilo na si vinginevyo.



Alisema imekubaliana na wanunuzi wanunue kwa bei hiyo na waichambue na kuihifadhi kisha waiuze kwa bei ya itakayokuwa sokoni lakini ikifika Agosti 15 mwaka huu, haijapanda wauze pamba yao na endapo wataiuza pungufu ya senti 69.4 USD serikali itawafidia.



“Licha ya wanunuzi kusuasua kutokana na mdororo wa bei na fedha zilizopo kutokidhi mahitaji ya mzigo uliopo sokoni, msirubiniwe kuwa pamba haina soko la hasha.Kilo ni sh. 1,200 na tunataka wakulima wapate tija kwa sababu wanatumia nguvu nyingi kulima pamba hadi wavune,”alisema Mkumba.


Alieleza kuwa awali wanunuzi walisita kununua pamba kutokana na changamoto ya bei kubwa kulingana na mikataba waliyoingia na wanunuzi wakubwa hivyo waliona wanapata hasara.


Naibu waziri huyo alisema malalamiko ya wakulima kuwa hakuna fedha baada ya kuuza pamba yao yalitokana na benki kugoma kuwakopesha wanunuzi zikihofia kuzamisha fedha za watanzania, lakini serikali ilipoingilia kati zimeamua kuwakopesha wafanyabiashara ili waingie sokoni.


“Wanunuzi walikuwa hawana uhakika wa biashara na mitaji yao.Sasa serikali imebeba dhamana hiyo na yote hayo ni kumjali mkulima.Hivyo wakulima mnapaswa kumuunga mkono Rais John Magufuli kwa kuchapa kazi kwa ajili ya maendeleo ambayo hayaji bila kufanya kazi,”alisema Mkumba.


Pia aliwasisitiza wakulimakulipa madeni ya pembejeo ili mwakani waondokane na uhaba wa viaududu na mbegu ili walime kwa tija zaidi na kujiongezea kipato na kubadilisha maisha yao kiuchumi.


Aidha, Katibu wa CCM, Kalli alisema Rais Magufuli analala na kuamka na shida za wananchi na kuwataka wakulima wasikubali kubabaishwa na kurubuniwa na wadanganyifu kwani serikali imewadhamini wanunuzi wa pamba licha ya bei kushuka kwenye soko.


“Wapo wapo vishoka waliingia kuwatisha wakulima kuwa pamba Mwanza ni siasa ili wauze kwa bei chee, lakini serikali imeingilia jambo hili kuwanusuru wakulima kwa kulipa fidia endapo watauza pamba kwenye soko chini ya senti Dola 68.Tuwatie shime wanunuzi wapate idea ya serikali waingie sokoni,”alisema Kalli.


Naye Mbunge wa Kwimba Shanif Mansoor alisema serikali kutoa ni faraja kwa wakulima baada ya serikali kutoa ruzuku kwenye pamba kwani kwa mara ya kwanza hiyo ni historia na ni vizuri wakulima wakaelezwa ili wanununuzi wasiwaonee.


“Nimefarijika kuona Serikali ya Rais John Magufuli ikitoa ruzuku kwenye pamba, wanunuzi watapata fidia na hakuna hasara na nadhani wataingia sokoni baada ya benki kukubali kutoa fedha.Lakini wanunuzi nao watoe bei halali,”alisema Mbunge huyo wa Kwimba.