Monday, November 19, 2018

MKURUGENZI AMANA BANK AZINDUA RASMI WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA.

 Mkurugenzi Mtendaji wa Amana Bank, Dkt. Muhsin Salim Masoud, akizungumza na waandishi wa Habari wakati wa uzinduzi wa wiki ya huduma kwa wateja uliofanyika katika Tawi la Nyerere Road Jijini Dar es Salaam, kulia ni Meneja Mkuu wa Biashara wa Benki hiyo, Dasu Musa, na kushoto ni Meneja wa Tawi la Nyerere Road, Aisha Awadh.
.................................

Mkurugenzi Mtendaji wa Amana Bank, Dkt. Muhsin Salim Masoud, leo Tarehe 19 Novemba 2018, amezindua rasmi wiki ya huduma kwa wateja ya Benki hiyo na kutoa wito kwa wateja na wananchi kwa ujumla kutembelea matawi yote ya jijini Dar es Salaam ili kupata huduma mbalimbali za kibenki.

Dkt. Muhsin amesema sambamba na wiki ya huduma kwa wateja, Benki hiyo pia inaadhimisha miaka saba ya kutoa huduma za kibeki hapa nchini huku ikijivunia mafanikio yaliyopatikana.

Alisema Benki hiyo ilipoanzishwa Novemba 24 mwaka 2011 ilikuwa na Tawi moja tu Kariakoo Mtaa wa Tandamti na kwamba mpaka sasa Benki hiyo ina matawi manane katika mikoa minne ambayo ni Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na Tanga.

Aliongeza kuwa tayari maandalizi yanafanyika ya kufungua tawi la tisa Zanzibar na kuongeza kuwa upo mpango wa kufungua Tawi makao makuu ya nchi Dodoma ili kusogeza huduma za Amana Bank katika makao makuu ya nchi.

Akizungumzia mafanikio waliyopata Dkt. Muhsin alisema ni pamoja na kuongezeka kwa wateja ambao mpaka sasa wamefikia elfu tisini huku fedha zilizowekwa na wateja mpaka sasa zikifikia Bilioni 192, ambapo matarajio ni kufikisha Bilioni 200 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa 2018.

Aidha, alisema mpaka sasa mikopo iliyotolewa na Amana Bank kwa wateja wake ni Bilioni 143 jambo ambalo limesaidia katika kukuza uchumi miongoni mwa watanzania mmoja mmoja, vikundi, na Taasisi huku serikali ikifaidika kwa kodi zinazotokana na wananchi waliowezeshwa kiuchumi na Amana Bank.

Alifafanua kwa kusema kuwa, mikopo hiyo imegawanyika katika makundi tofauti ambapo ipo mikopo mikubwa, mikopo ya kati na mikopo midogo midogo.

Alisema huduma mpya ya kujivunia kwa wateja wa Amana Bank katika kipindi hiki cha wiki ya huduma kwa wateja mwaka 2018 ni mikopo ya vikundi ambapo wakopaji watapewa mikopo isiyokuwa na riba bila ya dhamana kwani dhamana itakuwa ni kikundi chao tu walichokiunda na kufaidika na mikopo hiyo kuanzia shilingi laki tatu hadi milioni nne.

Akitaja miongoni mwa faida zitakazopatikana katika wiki ya huduma kwa wateja mwaka huu Mkurugenzi huyo alisema kutakuwa na punguzo maalum ya bei ya viwanja vinavyotolewa kwa njia ya mkopo na Amana Bank kwa kushirikiana na Propert International Ltd. (PIL) ambapo watakuwepo wawakilishi wa PIL katika matawi yote ya Dar es Salaam.

Aliendelea kufafanua kuwa, katika kuwajali wateja wake, Amana Bank leo imezindua rasmi kampeni maalum ya NUFAIKA NA AKIBA YAKO, katika kampeni hiyo wateja watakaoweka akiba isiyopungua milioni tano kwa kila mwezi kwa muda wa miezi mitatu mfululizo watapata nafasi ya kushinda pikipiki aina ya TVS.

Akielezea mikopo ya vikundi Meneja wa Amana Bank Tawi la Nyerere Road, Aisha Said Awadh alisema mikopo ya vikundi inawahusu kina mama, kina baba vijana na wajasiliamali wadogo wadogo ambao kwa muda mrefu ilikuwa kilio chao.

Katika uzinduzi huo wa wiki ya huduma kwa wateja ambao umefanyika Tawi la Nyere road, Mkurugenzi wa Amana Bank Dkt. Muhsin Masoud ameweza kuwahudumia wateja yeye mwenyewe katika Tawi hilo ambalo limewafurahisha watjea kwa kuwa wameweza kuuliza maswali mbalimbali na kupatiwa majibu moja kwa moja kutoka kwa Mkurugenzi mtendaji aliyekuwa katika meza ya kutolea huduma. 
 
Mkurugenzi Mtendaji wa Amana Bank, Dkt. Muhsin Salim Masoud akiwa katika picha ya pamoja na maafisa wa Amana Bank katika uzinduzi wa wiki ya huduma kwa wateja uliofanyika katika Tawi la Nyerere Road jijini Dar es Salaam.
 
Mkurugenzi Mtendaji wa Amana Bank, Dkt. Muhsin Salim Masoud(mwenye miwani) akitoa ufafanuzi kwa mteja aliyefika mezani kwake leo kupata huduma za Benki hiyo ambapo mara baada ya kuzindua wiki ya huduma kwa wateja Dkt. Muhsin alikaa mezani kuwahudumia wateja, kushoto ni Msaidizi wa Mkurugenzi wa Amana Bank, Harith Fentu.
 
Mkurugenzi Mtendaji wa Amana Bank, Dkt. Muhsin Salim Masoud (mwenye miwani) akitoa maelekezo kwa wateja waliofika mezani kwake kupata huduma leo Novemba 19, 2018 mara baada ya kuzindua wiki ya huduma kwa wateja, kushoto ni Msaidizi wa Mkurugenzi wa Amana Bank, Harith Fentu.
 
Meneja Mkuu wa Biashara wa Benki hiyo, Dasu Musa, akizungumza jambo na Meneja wa Tawi la Nyerere Road, Aisha Awadh mara baada ya kuzindua wiki ya huduma kwa wateja uzinduzi uliofanyika katika Tawi la Nyerere Road jijini Dar es Salaam.

 
Mkurugenzi Mtendaji wa Amana Bank, Dkt. Muhsin Salim Masoud (mwenye miwani) akibadilishana mawazo na meneja wa Tawi la Nyerere Road jijini Dar es Salaam, kushoto ni Msaidizi wa Mkurugenzi wa Amana Bank, Harith Fentu.
 
Kabla ya kuingia ndani unapokelewa nje kwa msaada mbalimbali wa maelezo kuhusu huduma za Amana Bank, kushoto aliyesimama ni Meneja wa Masoko wa Amana Bank, Jamali Issa akiwa tayari kupokea wateja kuwapa maelekezo kuhusu huduma za Benki hiyo katika uzinduzi wa wiki ya huduma kwa wateja uliofanyika Tawi la Nyerere Road jijini Dar es Salaam.

WAZIRI JAFO AKABIDHI RASMI VIFAA TIBA MAALUMU VYA KUTIBIA HOSPITALI YA KISRAWE

Waziri wa nchi Ofisi ya Rais  Tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo kushoto akimpatia maelezo mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe Mussa Gama  katika halfa hiyo ya makabidhiano ya mashine kwa ajili ya kutia magonjwa mbali mbali.(PICHA NA VICTOR MASANGU)
...............................................................

VICTOR MASANGU, KISARAWE

WAZIRI wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo amekemea vitendo vya upokeaji wa rushwa  vinavyofanywa na baadhi ya wauguzi,wataalamu wa afya  na madaktari  kuwataka kuachana na tabia ya kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wahakikishe wanatoa huduma ya matibabu kwa wagonjwa kwa kuzingatia misingi ya weledi ya kazi yao bila kuwa na ubaguzi wowote.


Jafo alitoa  kaul hiyo wakati  akizungumza na wataalamu wa afya, pamoja na wananchi wakati wa sherehe za kukabidhi mashine maalumu kwa ajili ya uchunguzi wa magonjwa ya aina mbali mbali katika hospitali ya Wilaya ya Kisarawe ambapo viongozi wa serikali madiwani pamoja na viongozi wa dini waliweza kushiriki katika zoezi hilo.


Aidha Waziri Jafo alibainisha kwamba lengo kubwa la serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha inaboresha sekta ya afya  kuanzia ngazi za maeneo ya vijijini kwa kuongeza ujenzi mpya wa zahanati, vituo vya afya pamoja na hospitali lengo ikiwa ni kuwaondolea adha wananchi katika suala zima la upatikanaji wa huduma ya matibabu kwa urahisi zaidi.

“Napenda kuchukua fura hii kuwambia ndugu zangu wananchi wa Kisarawe kwa kweli Rais wetu anafanya kazi kubwa sana ya kuhakikisha analeta maendeleo katika sekta mbali mbali hapa nchini na kwa sisi watu wa kisarawe tumepata bahati kubwa sana, kwa hiyo nipende kuwaambia tutaendelea kuboresha huduma ya afya katika zahanati zetu, vituo vya afya pamoja na ujenzi wa Hospitali nyingine mpya,”alisema Jafo.

Pia Jafo aliupongeza uongozi wa hospitali ya Wilaya hiyo pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe kwa kusirikiana kwa hali na mali mpaka kufanikisha kununua mashine hizo za kisasa ambazo zitaweza  kutatua changamoto za wananchi ambao hapo awali walikuwa wanapata usumbufu mkubwa kuwenda kupata vipimo katika maeneo mengine.

Naye Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jonathan Budenu alisema   hospitali ya Wilaya awali  ilikuwa inakabiliwa na changamoto mbali mbali  ikiwemo ukosefu wa  vifaa tiba pamoja na upungufu wa watumishi kwa  asilimia 36 huku akibainisha  wamefanikiwa kununua mashine maalumu  za uchunguzi wa magonjwa  ambazo zimegharimu kiasi cha shilingi milioni 119 fedha ambazo zimetokana na makusanyo ya ndani ya hospitali hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe  Jokate..amesema ataendelea kushirikiana bega kwa bega na viongozi wengine kwa lengo la kuweza  kuwaletea  mabadiliko chanya ya kimaendeleo wananchi wake hususana katika kuwaboresha huduma zaidi  ya afya katika zahanati,vituo vya afya na kuongeza kuwa mipango waliyonayo  ni kuifanya  hospitali  hiyo kuwa sehemu  ya mfano  katika nchi nzima.

“Jambo hili kwetu lina umuhimu mkubwa sana katika kuwaboreshea wananchi wetu huduma ya afya na kikubwa ni hapa tunamuunga Rais wetu Dr.John Pombe Magufuli katika kuhakikisha sekta ya afya inaboreshwa kwa kiwango cha hali ya juu ikiweo kununua vifaa tiba mbali mbali kama tulivyofanya katika hospitali yetu ya Wilaya kwa hiyo ni hatua kubwa”alisema Jokate.

Katika hatua nyingine Jokate amewataka wananchi wa Wilaya hiyo kuhakikisha wanajiunga katika bima ya afya ambayo itaweza kuwasaidia kupata matibabu kwa urahisi na kuondokana na kero ya kusumbuka kutibiwa pindi wanapokwenda hospitalini. 
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo akizungumza na wananchi hawapo pichana pamoja na wauguzi na madaktari katika halfa ya kukabidhiwa rasmi mashine maalumu kwa ajili ya kutibu magonjwa mbali mbali katika hospitali ya Wilaya ya Kisarawe..(PICHA NA VICTOR MASANGU)
  
Waziri wa chi Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) kulia Selemani Jafo akikata utepe wakati wa sherehe ya kukabidhi mashine kwa ajili ya kutibu magonjwa mbali mbali katika hospitali ya Kisarawe, kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo (PICHA NA VICTOR MASANGU)
Mganga mkuu wa Wilaya ya Kisarawe kulia Jonathan Budenu akifafanua jambo kwa Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) Seleman Jafo mara baada ya kukabidhi mashine hizo katika hospitali ya Wilaya. (PICHA NA VICTOR MASANGU)
Waziri wan chi ofisi ya Rais Tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo kulia wakiwa na baadhi ya viongozi wengine wa serikali wa kati kati ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo na kushoto kwake ni Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Kisarawe Musa Gama katika hafla hiyo ya makabishiano ya mashine za kutibu magonjwa mbali mbali. (PICHA NA VICTOR MASANGU)

SUBIRA MGALU AMWAGA VIFAA OFISI ZA UWT MKOA WA PWANI.

Katibu wa mbunge wa viti maalum mkoa wa Pwani ambaye pia ni Naibu waziri wa Nishai Subira mgalu akikabidhi vifaa vya ofisi kwa mwenyekiti wa UWT mkoa wa Pwani Farida Mgomi.
..............................................

Na Shushu Joel,  Mlandizi
NAIBU waziri wa Nishati Subira Mgalu ambae pia ni Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Pwani, amemwaga vifaa kwa ajili ya matumizi ya ofisi kuanzia ngazi ya matawi mpaka kata kwa lengo la barua zote ziwe katika mfumo wa kiofisi na wepesi wa kutambulika kwa barua hizo kule zitokako kirahisi

Akikabidhi vifaa hivyo katika mkutano wa jumuiya ya wanawake mkoa wa Pwani uliofanyika katika wilaya ya Kibaha, katibu wa mbunge huyo Rehema Kawambwa  alisema kuwa kutokana na majukumu ya kitaifa Mgalu ameshindwa kufika lakini uwepo wa katibu ni sawa na kuwepo kwake, vifaa tumevikabidhi ili viweze kuanza kutumika katika ngazi zote ambazo Naibu waziri huyo amezilenga kwa ajili ya kupata vifaa hivyo.

“Uwepo wa vifaa katika maofisi yetu ya jumuiya ya wanawake yatasaidia kupunguza changamoto nyingi lakini kubwa ni utambulisho wa barua kule zitokako ili hata wanaozipokea waweze kuzitambua kwa urahisi na kuzifanyia kazi kwa haraka”Alisema katibu wa Naibu waziri wa Nishati. 

Aliongeza kuwa vifaa hivyo vina thamani ya zaidi ya milioni 2 kwani ni vifaa vingi ambavyo vinahitajika katika kuendesha shughuli zote za kiofisi ili ofisi iweze kutambulika,kata hizo ni mtongani,kilangalanga,magimbi,janga,dutumi,soga,book,mlandizi,mtambani na nyingine zote ikiwa na madhumini ya kuwasaidia wanachama katika utambulisho wa barua zao zote.

Aidha aliongeza kuwa vifaa hivyo vitakuwa ni chachu ya kuigwa kwa sehemu zingine hapa nchini kutokana na  ofisi nyingi za chama zimekuwa zikisaulika sana na huku chama ndio kilichoshika dola,hivyo  pia vifaa hivyo vitachangia kuwafanya kinamama kuunda vikundi na kuwezeshwa kupata mikopo kupitia halmashauri zetu.

Akipokea vifaa hivyo Mwenyekiti wa umoja wa wanake mkoa wa Pwani Farida Mgomi amesema kuwa Mgalu amekuwa kiongozi wa pekee katika jumuiya hiyo kwani amekuwa akijitolea katika ufanikishaji wa vitu mbalimbali kwenye jumuiya hiyo.

Hivyo Mgomi amewataka viongozi wengine kuiga mfano wa Subira Mgalu ili kuhakikisha jumuia hiyo inakuwa ya kuigwa katika jumuia zote hapa nchini na hata nje ya nchi.

Aliongeza kuwa kwa kipindi hiki jumuiya ya wanawake imekuwa ni ya kuigwa kutokana na jinsi jumuiya hiya inavyojitolea katika ufanikishaji wa maendeleo mbalimbali katika mkoa wa Pwani.
 Katibu wa mbunge wa viti maalum Mkoa wa Pwani, Rehema Kawambwa akizungumza mara baada ya kukabidhi vifaa hivyo.

WAFUGAJI WATEMBEZA KIPIGO KIJIJI CHA NYANI KISARAWE.

Na Omary Mngindo, Kisarawe

WAFUGAJI jamii ya Wasukuma Kitongoji cha Kimeremeta Kijiji cha Nyani Kata ya Mafizi Kisarawe Pwani, wametembeza kichapo na kuvunja mlango nyumbani kwa Mohamed Rashid, kisa kizuiliwa wasiingize mifugo shambani.

Tukio hilo limetokea Nov 13 katika Kitongoji hicho baada ya wafugaji hao kuingiza mifugo kwenye shamba ambalo limeshalimwa kwa trekta wakisubili mvua tayari kwa kupanda.

Kitendo hicho kinachoelezwa ni cha kinyama, watuhumiwa hao baada ya kuzuiliwa wasiingize mifugo, walianza kumshambulia mdogo wake Rashid kwa fimbo sehemu za mwili, alipofika mwenyewe nae alipigwa mikononi na mgongoni.

"Usiku wa kuamkia Nov 14 alfajili walikuja wakavunja mlango kama mnavyouona, wamebomoa ukuta wa nyumba, wamechukua fedha kisha wakasema watakuja tena usiku kuendeleza vipigo," alisema Rashid.

Nae Amina Salum mke wa Rashid alisema kwamba usiku wa kuamkia Nov 15 walilazimika kukimbia nyumba wakihofia vipigo kwani wafugaji hao walifikia kutamka wataua mtu, kwanini wanakatazwa wasiingize mifugo.

"Tumelala mbali na Kitongoji chetu kuhusuru maisha yetu kwa kuhofia maisha yetu, walipomaliza kufanya fujo kuna mmoja wa wananchi waliwaomba wasifanye fujo ndio wakaondoka," alisema Amina.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyani Selemani Mnandi alisema kuwa baada ya kutokea hali hiyo, aliwasiliana na Polisi Kituo cha Mzenga ambapo walifika na kuwachukua aliyejeruhi na kujeruhiwa kwa ajili ya mahojiano.

Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Kamishna Msaidizi wa Polisi, (ACP) Wankyo Nyigesa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo cha tatizo hilo.


Sunday, November 18, 2018

AMANA BANK YAFANYA USAFI NA WAKAZI WA MBAGALA.

 Amana Bank leo Tarehe 18, Novemba 2018 imeshirikiana na wananchi wa eneo la Mbagala kufanya usafi wa mazingira ikiwa ni sehemu ya kuwa pamoja na wateja wao.

Pamoja na kufanya usafi huo wa mazingira uliowashirikisha wananchi mbalimbali wa eneo hilo wakiongozwa na Umoja wa Madereva wa Kusini mwa Tanzania (UMAKUTA) Benki hiyo pia ilikabidhi vifaa vya kufanyia usafi na kuhifadhia taka kwa UMAKUTA.

Akizungumza mara baada ya kumaliza kufanya usafi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Amana Bank, Dkt. Muhsin Salim  Masoud amesema Amana Bank ni kawaida yao kujitolea katika shughuli mbalimbali za kijamii.

Alisema wameamua kufanya usafi huo wa mazingira kama utangulizi wa kuadhimisha wiki ya huduma kwa wateja ambayo inaanza rasmi kesho Tarehe 18 Novemba 2018.

Aliongeza kuwa, katika wiki ya huduma kwa wateja ambayo inakwenda sambamba na maadhimisho ya miaka saba sasa toka Benki hiyo ianze kutoa huduma za kibenki Tarehe 24 Novemba 2011.

Aliongeza kwa kusema kuwa, Amana Bank ambayo ni Benki pekee inayofuata misingi ya sheria za kiislamu hapa nchini na kutoa huduma bora za kibenki kwa watu wote, inathamini umuhimu wa usafi wa mazingira katika juhudi za kujenga jamii bora.

Aidha, alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wateja wake na jamii kwa ujumla kwakuwa pamoja toka Benki hiyo ilipoanza kutoa huduma hapa nchini.

Amewaomba wateja wa Amana Bank na watanzania kwa ujumla kutembelea katika matawi ya Benki hiyo katika kipindi hiki cha huduma kwa wateja ili waweze kujipatia huduma mbalimbali za kibenki ikiwemo zawadi mbalimbali, fursa ya kuhudumiwa na Mkurugenzi mtendaji, mameneja wakuu  na wakuu wa idara mbalimbali katika Benki hiyo.

Dkt. Muhsin, alisema Amana Bank katika kuhakikisha inawapatia wateja wake huduma bora za kibenki imekuja na huduma mpya ya mikopo kwa vikundi ambapo wakopaji watakopa bila ya kuwa na dhamana kwani dhamana itakuwa kikundi chao weneyewe.

Katika wiki ya huduma kwa wateja, Dkt. Muhsin alisema wateja watapata punguzo maalum la bei ya viwanja vinavyotolewa kwa njia ya mkpo usiokuwa na riba kupitia Amana Bank kwa kushirikiana na Property International Ltd. (PIL) ambao watakuwepo katika matawi yote ya Dar es Salaam ili kuonesha viwanja vilivyopo katika miradi malimbali.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Umoja wa Madereva wa Mabasi ya Kusini mwa Tanzania, (UMAKUTA) Yusuf Malabe ameishukuru Benki hiyo kwa kushiriki zoezi la usafi katika eneo hilo na kuwakabidhi vifaa vya kufanyia usafi.

Malabe alisema Amana Banki ni Benki ya kwanza kuonyesha mfano huo toka walipoanza shughuli zao katika kituo hicho mabasi Mbagala.

Alisema kwa kitendo walichokifanya Amana Bank ni wazi kuwa Benki hiyo inawajali wateja wake na jamii kwa ujumla hivyo wana kila sababu ya kuwaunga mkono kwa kufungua Akaunti katika Beniki hiyo.

Amana Bank imekabidhi Vifaa vya kufanyia usafi katika eneo la kituo cha mabasi Mbagala ambavyo ni Ndoo za kuhidhia taka 20, Reki za kukusanyia taka, Fagio na Buti zitakazovaliwa wakati wa kufanya usafi.

Katika zoezi hilo la usafi huduma za kibenki zilikuwa zikiendelea ambapo watu mbalimbali waliweza kufungua Akaunti zao, kuuliza maswali na kupewa miongozo kuhusu mikopo ya aina zote inayotolewa na Amana Bank bila ya riba.
 
Mkurugenzi Mtendaji wa Amana Bank, Dkt. Muhsin Salim  Masoud, akizungumza na waandishi wa Habari mara baada ya kumaliza zoezi la usafi kituo cha mabasi Mbagala leo Novemba 18, 2018.
   
Mkurugenzi Mtendaji wa Amana Bank, Dkt. Muhsin Salim  Masoud,(kulia) akifurahia jambo pamoja na wafanyakazi wa Amana Bank eneo la Magala jijini Dar es Salaam mara baada ya kumaliza kufanya usafi wa mazingira leo Novemba 18, 2018.

 
Wafanyakazi wa Amana Bank, wakiwa na nyuso za furaha mara baada ya kumaliza shughuli ya kufanya usafi wa mazingira kituo cha mabasi Mbagala leo Novemba 18, 2018.
 Wafanyakazi wa Amana Bank wakiwa pamoja na wakazi wa Mbagala wakijiandaa kufanya usafi mapema asubui ya leo Novemba 18, 2018.


 Usafi ukiendelea katika eneo la Mbagala

 
Meneja Mkuu wa Biashara wa Amana Bank, Dasu Musa (kulia) akiwa na Meneja wa Tawi la Tandamti, Juma Yamlinga wakiendelea na ukaguzi wa maeneo waliyosafisha kuona kama kuna uchafu umebaki.
Meneja Mkuu wa Biashara wa Amana Bank, Dasu Musa, akibadilishana mawazo na Meneja wa Masoko wa Benki hiyo, Jamali Issaeneo la Mbagala mara baada ya kumaliza kufanya usafi eneo la Mbagala.
 
Umoja wa Madereva wa Mabasi ya Kusini mwa Tanzania, (UMAKUTA) wakiwa na vifaa vya kufanyia usafi walivyokabidhiwa na Amana Bank leo Novemba 18, 2018.
Pamoja na usafi uliofanyika eneo la Mbagala, wafanyakazi wa Amana Bank waliweza kuendelea na majukumu yao ya kuwahudumia wateja hapo hapo kama wanavyoonekana wakiwafungulia Akaunti wateja wapya.