Wednesday, November 14, 2018

RC TABORA AAGIZA POLISI KUFANYA DORIA MAENEO YA SHULE ZA MSINGI ILI KUDHIBITI UOVU DHIDI YA WATOTO

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri  
 ...............................................
 
NA TTGANYA VINCENT- RS TABORA

SERIKALI ya Mkoa wa Tabora imeamua kuweka ulinzi katika shule za Msingi za Manispaa ya Tabora nyakati za masomo ili kuzuia kusije kukatolekea kwa vitendo vyovyote vya kuwazulu na kuwateka wawapo shuleni.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kufuatia vurugu kubwa zilizotokea leo katika Shule ya Msingi Chemuchemu baada ya kuwepo kwa hisia ya watoto wawili kutekwa.

Alisema hadi hivi sasa hajajulikana kama kweli kuna  watoto wa Shule hiyo waliotekwa na kupandishwa katika gari aina ya Noah.

Mwanri alisema wamejaribu kufuatilia ili kujua ni watoto gani na majina yao ya watoto waliotekwa hakuyapata na wala hakuna mzazi aliyejitokeza kusema kuwa mtoto wake amepotea.

Alitoa wito kama kuna wazazi ambapo watoto wao wametekwa watoe taarifa kwa Polisi au katika Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa ili hatua ziweze kuchukuliwa ikiwemo kuwatafuta.

“Kuanzia sasa nimeagiza Polisi kuongeza Doria katika maeneo ya shule za Msingi ili kuwaondolea hofu wazazi…na kama mtu asifahamika ataonekana maeneo ya shule achukuliwe hatua” alisema.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema vurugu hizo zilitokana na wananchi kuwa bado na kumbukumbu ya wiki iliyopita ambapo mtoto wa miaka 6 alitekwa na kuwawa katika eneo la Tambuka Reli.

Alisema Jeshi la Polisi linaendelea kulifanyia uchunguzi matukio yote na kuwataka wazazi kuwa watulivu.

WAFANYABIASHARA WATAKIWA KUENDELEA KULIPA KODI.

Mkurugenzi wa Idara ya habari Maelezo na msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbassi 
...........................................................
Na Grace Semfuko-MAELEZO

Wafanyabiashara nchini wametakiwa kuendelea kulipa kodi na kuzingatia matumizi ya mashine za kielektroniki za kukusanyia mapato (EFD) ili wasiingie katika migogoro isiyo ya lazima na serikali.

Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi wa Idara ya habari Maelezo na msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbassi katika mahojiano maalum na redio Uhuru ya Jijini Dar es Salaa, kuelezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kipindi cha miaka mitatu tangu iingie madarakani.
 
“Wafanyabiashara wale wanaokwepa kulipa kodi, tutawafikia, ni mkuhimu ulipe kodi ili iweze kufanya kazi za kuwahudumia watanzania, na kwa mawakala wa kukusanya kodi wahakikishe wanaifikisha kodi hizo serikalini kwa wakati” alisema. 
 
Dkt Abbasi amesema Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Magufuli inafanya kazi kubwa ya kuhakikisha Watanzania wanapata maisha bora, hivyo ulipaji wa kodi ni muhimu sana ili fedha hizo ziwezeshe kupatikana kwa huduma bora zaidi kwa watanzania. 
 
Aidha Dkt. Abbassi amewataka watendaji kwenye taasisi za umma kufanya kazi kwa weledi na kwa kujituma pia kuzingatia majukumu yao yaliyopo kwenye mikataba yao ya kazi ili kuleta ufanisi kwenye taasisi zao. 
 
Alisema Serikali haitasita kuwachukulia hatua za kinidhamu watendaji wote wa umma ambao hawawajibiki ipasavyo kwani wamekuwa ni mzigo kwa Serikali, na wanakwamisha jitihada kubwa zinazofanywa na Rais Magufuli.
 
“Mmeona wenyewe juzi tu Mheshimiwa Rais amefanya maamuzi magumu lakini ni sahihi kabisa ya kuwaondoa baadhi ya watendaji wasiowajibika Serikalini,haiishii kwenye ngazi ya juu tu hii ni kwa kila mtendaji wa Serikali kuanzia ngazi za chini” alisema Dkt. Abbassi. 
 
Dkt.Abbasi alisema kuna mjadala mkubwa duniani unaendelea kuhusu maendeleo na nini maana ya kuwekeza, ambapo Tanzania imewekeza kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo na miundombinu pamoja na watu kwa maana ya watumiaji wakuu wa miradi hiyo.
 
Kuhusu elimu amesema serikali inatoa shilingi bilioni 23.85 kila mwezi ili kugharamia elimu kwenye shule za Serikali ikiwa ni mojawapo ya mkakati wa kuimarisha elimu nchini na hasa katika utekelezaji wa sera ya Serikali ya elimu bure kuanzia ngazi ya awali mpaka kidato cha nne.
 
Fedha hizo zinapelekwa moja kwa moja kwenya akaunti za shule badala ya kupelekwa kwenye Halmashauri za Wilaya na Manispaa ambazo zilikuwa zikichelewesha fedha hizo kufika shuleni ama kutumiwa kwa matumizi yaliyokusudiwa.
 
Serikali pia imeongeza fedha za mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu katika kipindi cha miaka mitatu ya utawala wa Rais Magufuli kutoka shilingi Bilioni 380 mwaka 2015 mpaka kufikia zaidi ya bilioni 500 mwaka 2018.
 
Hatua hiyo ya Serikali inalenga kuimarisha sekta ya elimu nchini ambayo inatajwa kuwa ni msingi mkuu wa maendeleo endelevu kwenye Taifa lolote Duniani.

KOROSHO ZOTE ZIBANGULIWE NCHINI-MHE HASUNGA

Waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga
 
Na Mathias Canal-Wizara ya kilimo, Mtwara

Waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga amesema kuwa wizara yake itatekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli kuhakikisha kuwa korosho yote inabanguliwa hapa nchini.

Ameyasema hayo jana tarehe 13 Novemba 2018 wakati akieleza malengo ya ziara yake mkoani Mtwara na Lindi alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kabla ya kuanza kukagua maghala ya kuhifadhia korosho.

Hasunga alisema kuwa kuruhusu wafanyabiashara kubangulia nje ya nchi korosho za wakulima wa Tanzania ajira nyingi zilikuwa zikipotea huku watanzania wakisalia kuhangaika kutafuta ajira kwani ajira nyingi zilipelekwa nje ya nchi.

“Baada ya kujiridhisha tumeamua sasa hahutasafirisha korosho ghafi tunataka korosho yote iwe inachakatwa nchini kwenye viwanda vyetu, kwa hiyo korosho zote zilizokuwa zinachukuliwa na wafanyabiashara kwenda kubanguliwa sijui wapi huko tumezuia” Alikaririwa Mhe Hasunga

Alisema kuwa viwanda vya kubangua korosho nchini vingi vimekufa kwa sababu ya ubadhilifu wa wananchi wachache na baadhi ya hujuma za watu lakini serikali imedhamiria kuanza kubangua kwenye viwanda vilivyopo kabla ya hatua za kuanzisha viwanda vingi vya ubanguaji.

“Tunamuwezesha mkulima kwa bei ya shilingi 3300 ili imsaidie kufanya kazi zake zingine ili aweze kuongeza uzalishaji katika msimu ujao wa mwaka 2018/2019 na kuepuka kushuka kwa uzalishaji” Alisisitiza Mhe Hasunga

Alisema baada ya kukamilika uhakiki wa maghala yote ya kuhifadhia korosho serikali itaanza kulipa malipo yote stahiki kwa wakulima yatakayotolewa na Benki ya kilimo Tanzania (TADB).

“Na tumeshaandaa fedha zao tunataka wakulima walipwe haraka iwezekanavyo lakini tumeanza kumjali mkulima kwanza halafu taasisi zingine zinazofaidika na korosho zitafuata” Alisisitiza

Mhe Hasunga amewapongeza wakulima kwa kuwa wavumilivu katika kipindi hiki cha mpito wakati serikali ilipokuwa ikitafuta ufumbuzi wa zao la korosho.

MTANZANIA ACHAGULIWA URAIS CHUO CHA PATRICE LUMUMBA NCHINI URUSI

Mtanzania Mohamed Mansour mkazi wa Kijiji cha Ruvu, Kata ya Ruvu Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani, akiwa katika picha Mara baada ya kimalizika kwa uchaguzi uliomchagua kuwa Rais wa Chuo Kikuu cha Patrice Lumumba kilichopo nchini Urusi.
........................................

Na Omary Mngindo

UMOJA wa Wanafunzi na Vijana wa Kiafrika Chuo Kikuu cha Urafiki cha Patrice Lumumba kilichopo nchini Urusi, wamemchagua Mtanzania Nassoro Mansour kuwa Rais katika chuo hicho.

Uchaguzi huo uliofanyika mwishoni mwa wiki nchini humo, Mansour ambaye hakuwa na mpinzani, alipigiwa kura za ndio 23 kati ya 25 hatua iliyotokana na kukidhi vigezo katika mchakato wa mchujo.

Akizungumza kwa njia ya simu, Mansour alisema kuwa uchaguzi huo ulioshirikisha mataifa mbalimbali, Makamu wa Rais wa chuo hicho amechaguliwa Mahamat Muqaddam wa Chad, Katibu Mkuu Diouf Daur wa Senegal huku Naibu Katibu Mkuu akiwa amechaguliwa Dju Orlindo automation kutoka Guinea Bissau.

Mansour alisema kuwa, Patrice Lumumba ni Chuo Kikuu cha Urafiki cha Watu wa Urusi, kilichoanzishwa mwaka 1960, kikapewa jina la Patrice Lumumba University kuanzia 1961-1992.

"Chuo hiki kina mataifa zaidi ya 155 na tamaduni za watu wa dini zote duniani ambao ni wastaarabu, pia kina walimu na wahadhiri na maprofesa kutoka nchi mbalimbali duniani lakini zaidi ni Warusi wenyewe," alisema Mansour.

Aliongeza kuwa nafasi ya Urais katika chuo hicho inagombewa kila mwaka, na kwamba mgombea hawezi kurudia tena nafasi hiyo baada ya kumaliza kipindi chake cha mwaka mmoja.

Mansour alisema kuwa yeye ni Mhadhiri Msaidizi katika chuo hicho, Kitivo cha Uchumi, Idara ya Jiografia na Uchumi wa Kikanda, pia ni Mwanafunzi wa Stashahada ya Uzamivu na kwamba ndio mara ya kwanza kushika wadhifa huo.

Ametanabaisha kuwa hiyo ndio mara ya kwanza kwa Mtanzania kuwa rais katika chuo hicho, kwa mwaka wa 2018/2019 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1960.

"Nimeshika nafasi hii baada ya Mwanadada Alice Lafara kutoka nchini Madagasca kumaliza muda wake wa Uraisi ambaye alichaguliwa kwenye uchaguzi wa mwaka 2017/2018," alisema Rais hiyo.

Mansour alisema kuwa nchi zilizopiga kura kumchagua Raisi zilikua 45, kupitia Wawakilishi na Maraisi wa Wanafunzi wa nchi hizo ambapo waliowania nafasi hiyo walikuwa watatu.

"Mimi ni kijana wa pili kutoka Afrika Mashariki kushika nafasi hii, aliyetangulia ni Mwanadada Lilian kutoka nchini Kenya miaka kadhaa iliyopita, nawashukuru walionipogia kura," alisema Mansour.

Aidha Mansour amewashukuru wa- Tanzania wote waliomuombea dua wakati anaingia katika kinyang'anyiro hicho, huku akimalizia kwa kusema kwamba nafasi hiyo imekua ikishikwa na vijana wa Kiafrika kutoka Afrika ya Magharibi hasa Nigeria
Mtanzania Mohamed Mansour aliyefunga Tai akiwa katika picha ya pamoja na wanachuo wenzake katika ukumbi wa mkutano wa Chuo Kikuu cha Urafiki cha Patrice Lumumba kilichopo nchini Urusi.
Pichani wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Chuo Kikuu cha Patrice Lumumba kilichopo nchini Urusi, wakiwa kwenye ukumbi wa tayari kwa zoezi hill, lililomchagua Mohamed Mansour kuwa Rais wa chama hicho.

WAZIRI WA VIWANDA ATOA WIKI MBILI KWA KAMPUNI ZINAZOMILIKI VIWANDA VILIVYOBINAFSISHWA KUWASILISHA MIKAKATI YAO WIZARANI.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Joseph Kakunda akizungumza leo Novemba 14, 2018 Mkoani Lindi.
 ..........................................................
NA HADIJA OMARY-LINDI

Serikali Nchini Tanzania imetoa wiki mbili kwa  Kampuni au Taasisi zinazomiliki viwanda vilivyobinafsishwa na serikali bila kuviendeleza ama kubadilisha matumizi viwanda hivyo  kuwasilisha mipango mikakati  wizara ya viwanda, ya kuviendeleza viwanda hivyo kabla ya serikali haijachukuwa hatu dhidi yao

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa  na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Joseph Kakunda  alipofanya Zihara ya siku moja katika Mkoa wa Lindi ambapo aliweza kukagua kiwanda kinachotarajiwa kubangua korosho cha Bucco kilichopo manispaa ya lindi pamoja na ghara la kuifadhia mazao la Ilulu Wilayani Nachingwea

Kakunda amesema katika kulisimamia jambo hilo kama Wizara  tayari ameshamuagiza katibu Mkuu wa viwanda bihashara  na Uwekezaji   kuandaa taarifa ya uchambuzi kwa Nchi mzima  ili kubaini viwanda vyote  vidogo, vikubwa na vyakati  kwa vile vilivyobinafsishwa ili kubaini kama vinafanya kazi yake ya msingi iliyokusudiwa

Alisema kuwa baada ya taarifa hiyo kuwasilishwa  Wizarani  itapitiwa ili kuona  ni Viwanda vipi vinafanya kazi iliyokusudiwa na vipi vilivyobadilishwa matumizi ambapo  vile  vitakavyobainika kuwa vimebadilishwa matumizi ama kutoendelezwa  hatua za haraka zitachukuliwa na serikali  ya kuona viwanda hivyo vinaendelezwa

“natoa taadhari kwa mtu yeyote ama kampuni yoyote ambayo ilichukuwa  kiwanda  akabinafsishiwa , kilikuwa cha Serikali sasa kimekuwa cha binafsi huyo mtu au kampuni  tangu alipopewa kazi hiyo na akaacha hiyo kazi ya msingi  akafanya kazi nyingine , kama serikali watu hao tunawafanyia kazi

Akizungumzia juu ya urejeshwaji wa kiwanda cha Bucco  Naibu waziri wa kilimo Innocent Bashungwa alisema kuwa  serikali ilipoamua kiwanda hiko kukikabidhi kwa jeshi la kujenga taifa (JKT)  nia ilikuwa ni  kuiongezea thamani korosho ndani ya nchi kutoka moja kwa moja kwa wakulima  ambapo inaweza kukuza pato la taifa pamoja na kuleta ajira kwa wananchi wake

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Lindi Godfrey Zambi  alisema kuwa kiwanda hiko cha Bucco toka kubinafsishwa kwake kutoka kwa serikali kiliweza kufanya shughuli ya ubanguaji wa korosho kwa mwaka mmoja wa 2007 hadi 2008 pekee hata hivyo alisema kuwa baada ya hapo kiwanda hiko kiligeuzwa ghara la kuifadhia korosho mpaka hivi sasa
 

MAGAZETI YA LEO NOVEMBA 14, 2018.

Tuesday, November 13, 2018

RAIS MAGUFULI AKUTANA NA ROSTAM AZIZ IKULU JIJINI DAR ES SALAAM.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akifurahia jambo na Mfanyabiashara Rostam Aziz mara baada ya mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es Salaam. PICHA NA IKULU

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika mazungumzo na Mfanyabiashara Rostam Aziz Ikulu jijini Dar es Salaam.
 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza jambo na Mfanyabiashara Rostam Aziz Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Mfanyabiashara Rostam Aziz mara baada ya mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es Salaam.

MBUNGE, KOKA ACHANGIA MLIONI 3 UJENZI WA KIVUKO KWA WANANCHI WA MTAA WA MUHEZA NA LUMUMBA

Mbunge wa jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka akizungumza na baadhi ya wananchi wa mtaa wa  Muheza na Lumumba iliyopo kata ya maili moja katika mkutano wake wa adhara baada ya kufanya ziara yake ya kutembelea miradi mbali mbali ya maendeleo (PICHA NA VICTOR MASANGU)
..................................................



VICTOR MASANGU, KIBAHA
 
WANANCHI WA  wa mitaa  miwili ya Lumumba na Muheza kata ya Pangani ,katika halmashauri ya  mji Kibaha mkoani Pwani wameanza jitihada za  kujitolea kuanza ujenzi wa  kivuko cha kutembea kwa miguu katika mto Mpiji kwa lengo la  kuepukana na maafa ya kujeruhiwa na kuliwa  na mamba kutokana na kero kubwa ya ukosefu wa kivuko cha kudumu .

Hayo yamebainika baada ya Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka kufanya ziara yake kwa ajili ya kutembelea na kukagua miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwemo kusikiliza changamoto na kero ambazo zinawakabili wananchi wake hususan tatizo lililopo la kukosa kivuko cha kudumu na kupelekea baadhi ya wananchi kuliwa na mamba.

Katika kuliona hilo  Koka ambaye alifika na kujionea adha hiyo ameamua kuungana na wananchi hao na kuchangia kiasi cha shilingi milioni tatu kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa muda wa kukitengeneza kivuko cha watembea kwa miguu.

“Wananchi kweli kwa sasa wanateseka sana hasa katika kipindi cha mvua na mimi tayari nilishatoa fedha nyingine kujenga kivuko hicho lakini mafuriko yalipokuja yalikisomba kwa hivyo nimetoa tena shilingi milioni tatu ambazo zitaweza kuanza utekelezaji wa kujenga kivuko hiki na nawapongeza wananchi kwa ushirikiano wao wa kujitolea kwa ahali na mali na mimi nitaendelea kuchangia zaidiili kuondokana nah ii hali,”alisema Koka.


Pia Koka alibainisha  kuwa ,serikali  ya awamu ya tano kupitia wakala wa barabara zamijini( na vijijini  TARURA )imetenga sh.mil 500 kwa ajili ya ujenzi wa kivuko hicho kwa mwaka wa fedha 2018/2019 ili kujenga kivuko kikubwa na cha kudumu ambacho kitaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kuwaunganisha wananchi  mbali mbali wa Wilayani Kibaha pamoja na maeneo ya Kibwegere Jijiini Dar es Salaam .

Mwenyekiti wa mradi huo ,Jerome Munisi alisema wameungana mitaa ya Lumumba ,Muheza na Kibwegere (LUMUKI)kukabiliana na tatizo hilo baada ya watu kujeruhiwa na mamba.

Alielezea, mchango wa kaya wametoa mil 3.9,kanisa katoliki 530,000,chemchem ya uzima 750,000 jumla mil. 5.250 hivyo kwasasa mahitaji ya mafundi bado ni milioni 20 ambazo zitasaidia kujenga kivuko hicho .


Hata hivyo ,Koka alikagua kivuko kingine cha Mkombozi kinachojengwa kwa kushirikiana na Jeshi kwa kushirikiana na wananchi na serikali ambapo yeye alishachangia milioni 11 na  kuahidi kuendelea kuwahimiza wajenzi wa daraja ambao ni jeshi na kwamba atawasiliana na makao makuu ya jeshi ili kuweka msukumo kitako cha daraja kipelekwe kabla ya mvua kubwa kunyesha. 

Mbunge wa jimbo la Kibaha mjini Silvestry koka akiangalia mradi wa ujenzi wa shule ya msingi muheza ambao unatakuwa na vyumba vitatu vya madarasa ambapo ukikamilika utaweza kusaidia wanafunzi kutotembea umbari mrefu kwenda kufuata huduma ya masomo.(PICHA ANA VICTOR MASANGU)
Mmoja wa wazee maarufu akizungumza jambo wakati wa mkutano huo wa adhara ambao ulifanyika katika mtaa wa muheza (PICHA NA VICTOR MASANGU)