Sunday, October 20, 2024

MTAALAMU BINGWA WA NYONGA NA MAGOTI KUTOKA UINGEREZA AWASILI DAR.





Atashirikiana na wataalamu wa Mloganzila

Na Mwandishi Wetu


MTAALAMU bingwa wa upasuaji wa nyonga na magoti  kutoka hospitali ya Queen Elizabeth ya Uingereza Profesa Mamoun AbdelGadir, amewasili jijini Dar es Salaam kwaajili ya kambi ya matibabu ya siku tano kwa watanzania.

Daktari huyo kwa kushirikiana na wataalamu wa ndani atafanya upasuaji huo kwenye kambi itakayofanyika katika hospitali ya Muhimbili Mloganzila  kuanzia Jumatatu 21,Oktoba 2024.

Aliwasili leo  katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ambapo alipokelewa na wafanyakazi wa Global Medicare ambao wameratibu kambi hiyo kwa kushirikiana na Muhimbili Mloganzila.

 Akizungumza kwenye mapokezi hayo, Meneja Mkuu wa Global Medicare, Daniel Lazaro,  alisema wamefurahi kuona amefika salama nchini Tanzania na kwamba ujio wake utakuwa wa manufaa makubwa kwa watanzania wenye matatizo ya nyonga na magoti.

“Tumefurahi kuona umefika salama na tunatarajia watanzania wengi watanufaika na ujio wako kwenye kambi hii ya siku tano itakayoanza katika hospitali ya Muhimbili Mloganzila kuanzia Jumatatu,” alisema

Naye Profesa Gadir aliishukuru serikali ya Tanzania na taasisi ya Global Medicare kwa kuratibu vyema safari yake ya kuja nchini Tanzania na aliahidi kutoa huduma bora kwa wagonjwa watakaojitokeza kwenye kambi hiyo.

 

“Natarajia tunashirikiana vizuri sana na wataalamu wenzangu wa hapa nchini kwenye kambi hii ya siku tano na kwa huduma hii natarajia tutaongeza chachu ya ushirikiano wa nchi zetu na tutabadilishana uzoefu wa kufanya upasuaji wa aina hii kwa wataalamu wetu,” alisema

 

Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Upasuaji wa hospitali ya Mloganzila, Goodlove   Mfuko, alisema hivi karibuni kuwa maandalizi yote yamekamilika na kwamba kwenye kambi hiyo watashirikiana na mtaalamu huyo.

“Mtaalamu huyu atashirikiana na madaktari bingwa ambao ni wataalamu wa mifupa na ajali hapa Mloganzila, hii itakuwa mara ya pili kutoa huduma  kama hii kwani mara ya kwanza tuliwafanyia upasuaji wa kubadilisha nyonga na magoti wagonjwa 170 kwa mafanikio makubwa,” alisema

“Kwa hiyo kwenye kambi hii ambayo ni ya pili  tutashirikiana na daktari huyu mbobezi kutoka Uingereza kupata uzoefu ili tuweze kuboresha zaidi huduma zetu hapa Muhimbili Mloganzila,” alisema

Aliwashauri watu wenye matatizo ya nyonga na magoti wafike Mloganzila kwaajili ya kupewa hiyo huduma ya kubadilisha nyonga na magoti kutoka kwa mtaalamu huyo wa Uingereza .

Aron Mwamyanda ambaye alifanyiwa upasuaji wa goti kwenye kambi iliyopita Mloganzila alisema aliugua magoti kwa miaka mitatu na alizunguka hospitali nyingi bila mafanikio.

“Nilienda hadi kwa waganga wa jadi lakini sikufanikiwa lakini mtoto wangu mmoja aliposikia kuna wataalamu wa magoti na nyonga hapa Mloganzila alinileta. Nilikuja wakanipiga wakasema hali yangu ni mbaya wakanipa gharama wakanitibia,” alisema

“Baada ya kunifanyia upasuaji hali yangu imekuwa tofauti kabisa kwasababu naweza kufanya mambo mengi ambayo awali sikuwa na uwezo wa kuyafanya na natarajia nitarejea kwenye hali yangu ya kawaida,” alisema

TRA KAGERA YAWAPA ELIMU YA KODI WAANDISHI WA HABARI.

 

Afisa uhusiano mkuu kutoka mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) Hudson Kamoga, akizungumza katika mafunzo hayo.

..............................................

Na Alodia Dominick, Bukoba


Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) nchini imeendelea kusisitiza wananchi wanaponunua bidhaa yoyote kudai risit na wanapouza kutoa risit kwa kufanya hivyo pande zote zitakuwa zimechangia ulipaji kodi inayosaidia katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini.


Afisa uhusiano mkuu kutoka mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) Hudson Kamoga ameyasema hayo Oktoba 19,2024 wakati akizumgumza na waandishi wa habari katika mafunzo yaliyoandaliwa na mamlaka hiyo.


Kamoga amesema, waandishi wa habari ni sehemu ya kuchochea maendeleo ya nchi yao na wanao wajibu wa kuelimisha jamii juu ya faida zinazopatikana kutokana na ulipaji kodi kwani asilimia 70 ya mapato ya serikali inatokana na kodi huku asilimia inayosalia ikitokana na wahisani mbalimbali.


"Unaponunua bidhaa ukadai risit unatimiza wajibu wako, risit ni ulinzi kwa bidhaa uliyoinunua unaweza kununua bidhaa ikiwa na changamoto usipokuwa na risit huwezi kurudishiwa bidhaa hiyo, inapotokea ulinunua simu bila risit ikatokea kuna mtu mwingine aliibiwa simu inayofanana na ya kwako mtu akasema hii ni simu yangu unajiteteaje kwamba hiyo simu ni ya kwako na siyo ya mtu yule anayedai" amesema Kamoga 


Kamoga ameongeza kuwa, unaponunua bidhaa ukadai risit unaisaidia serikali kukusanya mapato yake na kuwa yule aliyekuuzia bidhaa kama hajakupa risit unamsaidia kukwepa kulipa kodi hivyo wananchi waone umuhimu wa kudai risit ili kuisaidia serikali kusonga mbele.


"Unaweza kununua kitu dukani bila kudai risit alafu ukafika nje wakasema kuna kibaka ameiba kama huna risit wewe ukikamatwa kama mwizi hautaweza kujitetea, wananchi waone kudai risit ni wajibu wa kisheria lakini ni wajibu wao wa kizalendo kwa nchi yao na ni ulinzi wa bidhaa anayoinunua" ameeleza Kamoga 


Kwa upande wake, meneja msaidizi huduma kwa mlipa kodi mkoa wa Kagera Estomih Mossi ameeleza kwamba, elimu ya kodi imekuwa endelevu na walipa kodi inabidi waipate kutoka kwa waandishi wa habari kupitia vyombo vyao vya habari kwani wao ni kiunganishi kwa TRA na wananchi.


Amesema mamlaka hiyo kwa mwaka 2023/2024 walikusanya mapato zaidi ya trioni 28  na mwaka 2024/2025 wanapaswa kukusanya trioni 30.4


Akitoa mada ya elimu kwa waandishi wa habari afisa elimu na mahusiano TRA Kagera Rwekaza Rwegoshora amesisitiza utunzaji wa kumbukumbu kwa wafanyabiashara kwani itawaondolea kulipa kodi kubwa tofauti na mitaji yao ikiwemo kupata adhabu ya faini au kifungo.


Aidha alisisitiza kila mwananchi mwenye miaka 18 na kuendelea kuwa na namba ya utambulisho ya mlipa kodi (TIN namba) awe anafanya biashara au hafanyi na kuwa sheria hiyo ilifanyiwa maboresho mwaka 2023 ya mtanzania yeyote kuanzia umri huo anapaswa kuwa na namba ya tin 

kwani itamsaidia kupata huduma mbalimbali.


Alitolea mfano mtu anaponunua chombo cha moto kutumia namba hiyo ya utambulisho kupata leseni ya udereva au anaponunua chombo cha moto kutoka nje ya nchi ili ukifanyie usajili lazima uwe na namba ya utambulisho ya mlipa kodi (TIN)


Ashura Jumapili mwandishi wa habari gazeti la majira alishauri mamlaka hiyo kufuatilia hata wafanyabiashara waliopo nje ya mji ili nao waweze kulipa kodi kwani unakuta baadhi ya wafanyabiashara hao wanazo biashara kubwa hadi bidhaa nyingine ipo stoo lakini hawalipi kodi.


Ikumbukwe kuwa, TRA Kagera imekuwa ikikaa mara kwa mara na waandishi wa habari kwa lengo la kuwapa elimu ili nao wakaelimishe jamii inayowazunguka juu ya umuhimu wa kulipa kodi kwa maendeleo ya nchi hii.

Afisa elimu na mahusiano TRA Kagera Rwekaza Rwegoshora akitoa mada ya elimu kwa waandishi wa habari
Meneja msaidizi huduma kwa mlipa kodi mkoa wa Kagera Estomih Mossi akifungua mafunzo kwa waandishi wa habari na mamlaka hiyo

Baadhi ya waandishi wa habari mkoani Kagera waliohudhuria mafunzo yaliyotolewa na mamlaka ya mapato Tanzania TRA

Sunday, October 13, 2024

HOSPITALI YA SHIFAA YAZINDUA KITUO CHA TIBA NA UTAFITI WA SARATANI DAR

 






Picha mbalimbali wakati Waziri wa Afya,  Jenista Mhagama alipozindua kituo cha tiba na utafiti wa saratani katika hospitali ya Shifaa iliyoko Kinondoni barabara ya Msese jijini Dar es Salaam Ijumaaa Tarehe 11 Oktoba 2024.
.......................................
Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Afya, Jenista Mhagama amezindua Kituo cha Tiba na Utafiti wa Saratani cha Shifaa na kuahidi kuwa serikali itaendelea kuongeza bajeti ya dawa za saratani kila mwaka kutokana na ongezeko kubwa la wagonjwa wa saratani.


Waziri Mhagama aliyasema hayo Ijumaa jioni jijini Dar es Salaam wakati akizindua kituo hicho kilichopo kwenye hospitali ya Shifaa barabara ya Msese Kinondoni jijini Dar es Salaam.


Alisema wakati idadi ya wagonjwa ikiongezeka wagonjwa wengi wanaougua ugonjwa huo hawana uwezo wa kugharamia matibabu hivyo wanahitaji kusaidiwa.


Alisema kwa mwaka huu wa fedha pekee serikali imetenga shilingi bilioni 10 kwaajili ya kununua dawa za saratani na kwamba kila bajeti mpya kiasi hicho kitakuwa kikiongezeka.


Alisema uwepo wa kituo hicho utaongeza upatikanaji wa huduma muhimu sana za kiuchunguzi na kitabibu kwa matatizo yanayohusu ugonjwa wa saratani nchini.


Alisema saratani imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka na takwimu za kila mwaka zinaonyesha kuwa na ongezeko na mwaka 2022 wagonjwa wapya wa saratani walikuwa 45,000.


“Wagonjwa wa saratani wasipowahi kupata matibabu inawasababishia vifo kwa hiyo unapokuwa na wagonjwa 45,000 nchi lazima iweke mipango ili kuokoa uhai wa wananchi hao kwa kupata tiba mapema,” alisema.


Alitaja saratani zinazoongoza kuwa ni saratani ya mlango wa kizazi inayochukua asilimia 24.2, saratani ya tezi dume inachukua asilimia 10.7, saratani ya matiti inayochukua asilimia 10, saratani ya koo inayochukua asilimia 7.9, saratani ya utumbo mpana inayochukua asilimia 4.9 ya aina zote  za saratani nchini.


Waziri Mhagama alisema saratani zote hizo zinachukua asilimia 42 ya idadi ya wagonjwa wote wanaougua saratani nchini na saratani zinazoathiri zaidi wanawake nchini ni ile ya mlango wa kizazi na saratani ya matiti.


“Ndiyo maana serikali imeamua kuchukua jitihada za kukinga wananchi wake dhidi ya saratani na pale ambapo mtu anapata saratani apate matibabu na leo Shifaa wanapounga mkono juhudi za serikali kuokoa wagonjwa wa saratani na kuwarejeshea furaha tunawashukuru sana,” alisema Mhagama.


 Alisema serikali imeendelea kutoa elimu na kufanya kampeni maalum za uchunguzi na utambuzi wa mapema wa maradhi ya saratani na kupanua huduma za uchunguzi kwenye mikoa mbalimbali nchini.


Alisema lengo ni kuhakikisha kunakuwa na vituo vingi vya utoaji wa huduma hizo na hasa kwa wanawake na serikali imeimarisha huduma za uchunguzi a kimaabara na huduma za radiolojia kwa kuhakikisha inakuwa na mashine 85 za  CT SCAN za kutosha  na MRI.


Mkurugenzi Mtendaji wa  hospitali ya Shifaa, Bashir Haroon aliipongeza serikali kwa uwekezaji mkubwa inaofanya kwenye sekta ya afya.


Alisema hospitali ya Shifaa ni uwekezaji ambao umegharimu dola za Marekani milioni 60 kama jitihada za kuwawezesha wananchi kupata matibabu bora yanayokwenda na wakati.


“Ujenzi wa hospitali hii umefanywa kama sehemu ya kuunga mkono jitihada za serikali katika sekta ya afya na tunafurahi kuona maboresho makubwa yakiendelea kwenye sekta ya afya na navipongeza vituo binafsi vya afya kwa kazi kubwa wanayofanya,” alisema


Haroon alisema ugonjwa wa saratani umekuwa tatizo kubwa sana duniani na hapa Tanzania na ndiyo sababu yeye aliona umuhimu wa kuanzisha kituo cha tiba ya saratani ili kuwapunguzia mzigo wa gharama wagonjwa wa Tanzania wanaokwenda India kutibiwa.

Friday, October 11, 2024

WANANCHI 10,378 WAFIKIWA NA HUDUMA YA AFYA YA MACHO LINDI.





NA HADIJA OMARY, LINDI.


Jumla ya Wananchi 10,378 kutoka halmashauri sita za Mkoa wa  Lindi  wamefikiwa na huduma ya Afya ya macho ambapo kati yao 9690 wamefanyiwa vipimo na kupatiwa matibabu 



Hayo yameelezwa na Dokta Sharifu Hamza kwa niaba ya Mganga Mfawidi wa hospital ya Rufaa MKoa wa Lindi Sokoine, Jana oktoba 10 wakati wa maadhimisho ya Afya ya macho yaliyofanyika kimkoa Katika hospital hiyo ya Rufaa Sokoine huko Manispaa ya Lindi .



Zoezi hilo la utoaji Elimu ya Afya ya macho sambamba na vipimo na matibabu limeendeshwa kwa ufadhili wa mashirika ya  Heart to Heart foundation,  CBM pamoja na Korea church .


Amesema  zoezi hilo lililoendeshwa kwa siku saba kuanzia oktoba 4 hadi 10 wataalamu walipita katika shule mbalimbali kwa halmashauri zote sita kutoa elimu pamoja na kutoa matibabu kwa wananchi walioonekana na changamoto ya afya ya macho.


maadhimisho hayo ya Afya ya macho  yanayohimiza vijana na watoto kupenda macho yao na  kuitaka dunia kuongeza umakini katika upatikanaji wa huduma bora za macho kwa vijana, ambapo amesema kuwa ni faraja kubwa kwa mkoa huo ambapo zoezi hilo limefanyika kwa ufanisi mkubwa 


Hata hivyo Dokta Sharifu Ameeleza kuwa  huduma hiyo ya macho inaendelea kutolewa Katika hospital hiyo Hata baada ya wiki hiyo ya Afya ya macho kumalizika.


Edward Aloyce Afisa mradi kutoka shirika la  heart to heart foundation amesema shirika lao limekuwa likifanya mradi wa macho katika Mkoa wa Lindi wakilenga kupata watoto 20 wenye changamoto ya mtoto wa jicho ambao watanufaika kufanyiwa oparesheni Bure 


"Tumesukumwa kwa sababu watoto ndio wanapata changamoto kubwa katika tatizo la macho na tumefanya kwa ushirikiano pamoja na hospitali hii ya Lindi Sokoine lakini pia tutafanya na hospitali ya taifa ya muhimbili kwa kuleta madaktari bingwa baada ya watoto hao kuweza kuainishwa kutokana na changamoto zao za magonjwa ya macho"


Aidha  Aloyce alitoa wito kwa Wazazi na walezi Mkoani humo kujenga tabia ya kuwahimiza watoto kufanya uchunguzi wa changamoto ya macho katika hospitali ya sokoine ili kuweza kuwasiliana na wataalam hao wa hospitali ya muhimbili



Dokt Mwacha Machaja  Ni mtaalamu wa magonjwa ya macho Hospital ya Rufaa ya Lindi Sokoine amesema zipo sababu mbalimbali zinazopelekea matatizo ya macho ambapo miongoni kwa sababu hizo ni umri, ajali, lishe duni , maambukizi  na sababu za  kuzaliwa, 



Hata hivyo Amesema  sababu kubwa inayowafanya baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Lindi wamekuwa wakipata changamoto ya macho kutokana na kukosa lishe bora hali inayopelekea kuathirika kwa macho


" wakazi wengi wa Lindi wanaopata changamoto ya macho inatokana na kutokula vyakula vinavyolinda macho uwenda kwa kujua ama kutokujua kula mboga za majani zilizoiva sana ama pengine kutokula kabisa".



Nae Asha Matola mkazi wa Lindi amesema amefika hospitalini hapo kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi baada ya kuugua macho kwa muda mrefu na kwamba imani yake atapata matibabu mazuri .


 

Tuesday, October 8, 2024

WAANDIKISHAJI WAPIGA KURA NACHINGWEA, WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA WELEDI.

 



Na Hadija Omary, Lindi.


Msimamizi wa Uchaguzi wa Wilaya ya Nachingwea Mkoani Lindi Mhandisi chionda kawawa ametoa Rai kwa Waandikishaji wa wapiga Kura kuzingatia kanuni za uchaguzi wakati wa zoezi hilo linalotarajia kuanza oktoba 11 hadi 20 mwaka 2024


Chionda ametoa Rai hiyo alipokuwa anazungumza wakati wa Mafunzo kwa Waandikishaji wapiga Kura kutoka Katika vitongoji vyote vya halmashauri hiyo yaliyofanyika Katika ukumbi wa TTC Wilayani Nachingwea 



Katika mafunzo hayo Jumla ya Waandikishaji 525 walipatiwa Mafunzo ambapo Kati ya hao 15 ni Waandikishaji wa akiba huku 36 wakiwa ni wasimamizi wa Uchaguzi Katika Ngazi ya Kata 



Waandikkshaji hao wameapa mbele ya hakimu wa Wilaya Nachingwea na wako tayari kwa kuanza zoezi la uandikishaji, 



Aidha, Mhandisi Chionda amewapongeza waandikishaji hao kwa kuteuliwa kufanya kazi hiyo na kuwaahidi kuwapa ushirikiano pale watakapohitaji, pia amewataka kufanya kazi kwa juhudi ili kufikia malengo na kufanya wananchi wengi kushiriki kupiga kura siku ya tarehe 27 Novemba 2024.



Afisa Uchaguzi ndugu Robert Mmari amewasihi waandikishaji hao kufuata kuzingatia mambo mbalimbali waliyofundishwa na kuuliza pale wanapokosa majibu na sio kufanya kwa utashi.


"Serikali za Mitaa, Sauti ya Wananchi, Jitokeze kushiriki Uchaguzi"


WAJASIRIAMALI WANAWAKE BUKOBA WAPATIWA ELIMU.

 



Na Alodia Dominick, Bukoba


Wanawake wajasiriamali katika mji wa Bukoba wamepata elimu ya ujasiriamali, na kutakiwa kujiamini, kujithamini, kujiheshimu na kutojikweza.


Mafunzo hayo yametolewa na kampuni ya Stein Group inayojihusisha na shughuli za kijamii na  mafunzo hayo yamefanyika Octoba 06, 2024 katika manispaa ya Bukoba.


Meneja wa  Kampuni ya Stein Group mkoa wa Kagera Exavery Kyatwa ametaja lengo la kutoa mafunzo hayo kuwa ni kuwaelimisha wanawake wajasiriamali waliopo Manispaa ya Bukoba ili watoke hatua moja na  kwenda hatua nyingine kwa kujiendeleza kiuchumi.


Naye Mkurugenzi wa taasisi hiyo Taifa Mayamba Mbilinyi amesema, wameanza na wajasiriamali wa manispaa ya Bukoba yenye kata 14 na wajasiriamali wanawake wapatao 200 na baadaye wanatarajia kuwafikia zaidi ya wajasiriamali 1,000 katika wilaya nyingine za mkoa wa Kagera kwa kutoa elimu ya ujasiriamali.


“Sisi tumelenga akina mama ili tuwajengee uwezo wa kujiamini katika kufanya biashara zenu, msiendelee kuwa tegemezi, na muache omba omba, baba akileta sukari mama ulete chunvi msaidiane katika familia” amesema Mbilinyi.


Mwenyekiti wa chama cha wafanyabiashara mkoa wa Kagera, Tanzania Women Chamber of Commerce (TWCC) Ivona Bajumuzi amesema kuwa, wanahitaji wanawake wote wawezeshwe kiuchumi kwani mwanamke anapofanya biashara inamfanya ajiamini.


Ameeleza kuwa, wasiendelee kuitwa wajasiriamali wadogo wadogo wakue nao wawe wajasiriamali wa kati na wakubwa.


Akitoa mada ya wewe ni wa juu Grace Victor alisema mtaji mkubwa ni mtu mwenyewe kwani anavyo viungo vya mwili kama macho, masikio mikono na miguu vinavyomuwezesha kufanya shughuli mbalimbali za kujiingizia kipato.


“Wewe mwanamke kama unataka kuwa mjasiriamali lazima ujiamini, ujithamini, ujiheshimu na usijikweze na lazima uwaze kile unachotaka kukifanya kama kitazaa matunda” amesema Victor


Amesisitiza mwanamke anapopanga kufanya biashara asitazamie biashara ya wengine bali utashi utoke rohoni mwake kwamba anakwenda kufanya biashara fulani ili apate faida, na kuwa wanapoanza biashara wasikate tamaa wakomae nazo ili waone kama zitawapa faida au la.


Akitoa mada ya mama amka Anold Kikoyo amesema wanawake wanayo nguvu kubwa ya kufanya biashara na biashara zao zikakua nguvu hiyo ambayo ni uwezo wa kuatamia, hamasa, mlango wa sita wa fahamu, kujitolea katika jamii na uwezo wa kujadili hisia za wengine.


Kikoyo almewataka kuzingatia mahusiano sahihi, afya ya akili, kusimamia maamuzi ya ndoto zao bila kuangalia wengine wanasema nini, kuacha tabia ya kuahirisha mambo na vipaumbele vya matumizi sahihi ya muda.


Aidha kwa upande wake mtoa mada ya maswala ya uchumi Hamis Kashirima amewasihi wajasiriamali kuacha kuishi maisha feki na kuishi maisha halisi kutokana na kipato chao na wajiwekee malengo ya baadaye.


Amesema ili waweze kukua kiuchumi watengeneze mapato na matumizi ya kila mwezi katika familia zao, wajiwekee akiba na watakapoanzisha miradi wasitegemee chanzo kimoja cha mapato kwani kitakapo kwama kuendelea watakuwa wamerudi nyuma kiuchumi.      


Mada mbalimbali zizilizotolewa kwa wanawake hao ni pamoja na wewe ni wa juu, mama amka pamoja na mada ya maswala ya uchumi.

DC MWANZIVA NSSF: LINDI ONGEZENI KUTOA ELIMU KWA WANACHI UMUHIMU WA KUJIUNGA NA MFUKO NA FAIDA ZAKE

 





Na Hadija Omary, LINDI.


MKUU wa Wilaya ya Lindi Mkoani Humo Bi.Victoria Mwanziva  amewataka watumishi WA Mfuko wa hifazadhi ya Jamii (NSSF) Mkoa wa Lindi kuendelea kutoa Elimu kwa wananchi wengi juu ya Umuhimu wa kujiunga na mfuko huo na faida zake


Mwanziva ametoa Rai hiyo oktoba 07/2024 wakati akizungumza na watumishi na wanachama wa Mfuko huo wa NSSF Mkoa wa Lindi Katika uzinduzi wa wiki ya huduma kwa wateja uliofanyika huko manispaa ya Lindi .


Mwanziva Amesema wakati huu ambao Mfuko umeboresha mfumo wa sekta isiyo rasmi kwa wanachama waliojiajiri na kuandaa skimu maalumu kwa wafanyakazi walio Katika sekta rasmi ili kuweza kuchangia kwa hiari kupitia skimu hiyo ya (NISS NA SS)  pamoja na mambo mengine zinalenga kupanua wigo wa huduma za hifadhi ya Jamii hivyo ni wajibu wao kuendelea kutoa Elimu kwa wananchi .


Mifuko hii ya Watu kujichangia wenyewe ebu twendeni tukaongeze Elimu kwani tuna wananchi wengi Sana ambao wamejiajiri wafanyabiashara, wajasiriamali tuweke mpango kabambe Katika wiki hii ya huduma kwa wateja kuwafikia wengi na kuwaelimisha  namna ya kujichangia na faida za kujichangia .


Kwa kutumia wiki hii ya huduma kwa wateja wanaweza kuwavutia wananchi wengi ambao huwenda mpaka sasa bado hawafahamu faida za mifuko hii ya hifadhi ya Jamii kuanza kuchangia kwa  hiari .



Katika hatua nyingine Mwanziva pia aliwakumbusha wanachama  kuhakiki taarifa za michango wanapokuwa kazini ili kuepuka usumbufu wa kufuatilia michango wanapokuwa tayari kustaafu au nje ya ajira .


Kwa upande wake meneja wa NSSF Mkoa wa Lindi Juma Namuna Amesema Mfuko umekuwa unaweka mikakati ya kuongeza uandikishaji mwaka Hadi mwaka ambapo kwa mwaka 2023/2024 Mfuko huo uliweza kuandikisha wanachama wapya 291,266 huku mwaka 2024/2025 ukilenga kuandikisha wanachama wapya 324,321.


"Lakini pia kwa upande wa ukusanyaji wa michango tulikuwa tunalengo la kukusanya  Bilioni mbili Milioni miatisa na sitini na tatu  na tuliweza kukusanya Bilioni mbili milioni miatano na themanini na  saba sawasawa na ufanisi wa asilimia 87.30%"


Baadhi ya wanachama wa Mfuko huo wamesifu huduma wanazozipata kutoka Katika Mfuko na kuwasihi wananchi wenzao kujiunga ili waweze kupata manufaa.


Sunday, October 6, 2024

WAZEE WAASWA KUWA MBELE KATIKA KUHAMASISHA USHIRIKI WA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA

 




NA HADIJA OMARY, LINDI.


Wazee wa Nachingwea wameaswa kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha wananchi kujitokeza kushiriki kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Vijiji unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba mwaka huu 2024.


Wito huo  umetolewa na Afisa Uchaguzi wa Wilaya ya Nachingwea Robert Mmari alipokuwa akizungumza na wazee maarufu wa Wilaya hiyo ambapo amesisitiza   kuwa maandalizi yanaendelea vizuri na msaada wa wazee utahakikisha zoezi linafanikiwa



Afisa Uchaguzi (W) ya Nachingwea ndugu Robert Mmari pia ameeleza kuwa sifa za mgombea na mpiga kura zimesha ainishwa, kwamba Mpiga kura lazima awe na akili timamu, awe na umri wa miaka 18 au zaidi, na awe mkazi wa kitongoji husika Wananchi wote wanatakiwa kupiga kura kwenye vitongoji walivyojiandikisha, huku zoezi la kuchukua fomu za kugombea likipangwa kuanza Novemba 1


Aidha, Msaidizi wa uchaguzi Joshua mnyang'ali Amesema kuwa kwa mwananchi  kushindwa kujiandikisha  kwa wakati uliopangwa, atapoteza haki ya kupiga kura 


Hata hivyo Alisisitiza kuwa Halmashauri imejipanga vyema kuhakikisha wananchi wanapata elimu kuhusu uchaguzi na umuhimu wa kushiriki katika zoezi hilo


Kwa upande wake, Chief Nakotyo alibainisha kuwa kutakuwa na tukio maalum lenye ujumbe kuhusu maadili na hamasa ya uchaguzi litakalofanyika tarehe 7 na 8 Novemba na aliwataka wazee kuendelea kuhamasisha wananchi ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa mafanikio Vilevile, Joyce Chipanda, mkazi wa Kilimani Road, amewaasa wananchi kutopotosha wenzao na badala yake kujitokeza kwa wingi kupiga kura ili kulinda usalama na amani ya nchi


Thursday, October 3, 2024

BASHE AWAHAKIKISHIA WAKULIMA WA KOROSHO KUPATA BEI NZURI

 




NA HADIJA OMARY,  LINDI.

Waziri wa kilimo Hussain Bashe Amewahakikishia wakulima wa korosho kuwepo kwa bei nzuri ya zao Hilo Katika msimu wa mauzo 2024/2025 unaotarajiwa kuanza November 11 mwaka huu

Waziri Bashe ameyasema  hayo  November 02, 2024 akiwa Mkoani Lindi wakati anazungumza na Wadau wa kilimo ambapo Amesema kuwa kutokana  na mfumo rafiki unaotumika Katika uuzaji wa mazao wa Soko la Bidhaa (TMX) Hana Shaka kuwepo kwa bei zinazoridhisha Katika minada

" Tunaamini mwaka huu bei za korosho zitakuwa nzuri na kwa mara ya kwanza kwenye mfumo huu wa TMX tumeona makampuni ya kigeni ambayo yamejaribu kununua na zimepokea mzigo kama walivyotaka"

''Yaan wameshiriki wameiona katalog wameomba na kununua wakiwa huko huko nje na wameweza kupokea sasa maana yake   hamu imekuwa kubwa wanaweza kuuamini mfumo"

Hata hivyo Bashe ameviagiza Vyama vikuu vya ushirika Mkoa wa Lindi kufanya utambuzi wa maghara ya kuhifadhia korosho kabla ya msimu mpya wa mauzo ya zao Hilo kuanza rasm ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa korosho kwenye maghala 


"Nimewaagiza jukumu la usimamizi na uendeshaji wa maghala ni lakwao kwa sababu katalogi inatengenezwa na chama cha ushirika , sasa kama unatengeneza katalogi kwa nini kesho unapotokea upungufu Mimi siusiki?"

Amesema ili uingie mzigo hewa Katika ghala ni lazima uanzie kwenye chama cha msingi AMCOS ili kupata uthubitisho kutoka chama kikuu cha ushirika na mwendesha ghala hivyo ili kukabiliana na Hilo lazima vyamavikuu vikasimamia na endapo kutatokea udangajifu  wa Aina yoyote na wao watahusika 

MAAFISA KILIMO KATA KARAGWE WAPATIWA PIKIPIKI.

 


Na Alodia Dominick, Karagwe


Halmashauri ya wilaya ya Karagwe mkoani Kagera yenye maafisa kilimo wa kata wapatao 33 tayari wote wamepatiwa usafiri wa pikipiki kutoka Wizara ya kilimo ili kuwawezesha kufanya kazi zao kwa ubora.


Maafisa kilimo hao wamepatiwa pikipiki kwa nyakati tofauti na Oktoba mosi, mwaka huu maafisa kilimo wapatao tisa ambao wameajiriwa hivi karibuni wamepatiwa pikipiki kama mwendelezo wa maafisa kilimo 24 ambao walitangulia kupata pikipiki hizo.


Akizungumza katika halfa hiyo ya makabidhiano Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Karagwe Happiness Msanga ameishukuru serikali kupitia Wizara ya kilimo kwa kuendelea kuwakumbuka watumishi wa wilaya ya Karagwe hususani maafisa kilimo ngazi ya kata ambao shughuli zao kwa kiasi kikubwa zinategemea usafiri kutokana na ukubwa wa maeneo na umbali ili kuwafikia wananchi kwa wakati.


"Nichukue nafasi hii kuwasisitiza maofisa wote ambao mmekabidhiwa pikipiki kwa ajili ya kufanikisha kazi zenu mzitunze na kuzitumia kama ilivyokusudiwa, sitegemei kuona mnazitumia kufanya biashara ya usafirishaji (bodaboda) badala ya kufanya shughuli za kuwatumikia wananchi ambao ndio walengwa"


Pia amewakumbusha  kuwa, wahakikishe wanakuwa na leseni halali na wahudhurie mafunzo ya udreva kwa wale ambao hawajui kuzitumia ili pikipiki hizo zisiwe sababu ya ajali, na kuwa zitumike kwa matumizi salama na wazingatie sheria za usalama barabarani ili kuepukana na ajali zisizo za lazima


Aidha Afisa kilimo wilaya ya Karagwe Adamu Salum amezitaja kata hizo tisa ambazo maafisa kilimo wamekabidhiwa pikipiki kuwa ni kata ya Kanoni, Igurwa, Kihanga, Nyaishozi, Kituntu, Nyakahanga, Kayanga, Ihembe na Chonyonyo.


Naye afisa kilimo kata ya Kayanga  Fatuma Hashimu ambaye ni miongoni mwa waliopokea pikipiki hizo ameishukuru serikali kwa kuwapatia pikipiki ambazo zitawasaidia kuwafikia wakulima kwa haraka zaidi na kutatua changamoto zao kwa wakati.


Amesema awali walikuwa wanapata adha kuwafikia wakulima kutokana na changamoto ya usafiri na wakati mwingine wanashindwa kufika kwa wakati ili kuwahudumia lakini baada ya kupata usafiri huu wanatarajia kutoa huduma bora kwa wakulima na kuwafikia kwa wakati ukilinganisha na mwanzo ambapo hawakuwa na chombo cha usafiri.


Hata hivyo, serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania inayoongozwa na Dkt Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha mazingira ya kufanya kazi kwa watumishi wa umma katika kuongeza ufanisi na ubora katika kutimiza majukumu yao ya kila siku.

NACHINGWEA KUFANYA BONANZA LA KUTOA ELIMU YA MPIGA KURA

 

Na Mwandishi wetu, Lindi.


Kuelekea Uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji unaotarajiwa kufanyika November 27 mwaka huu Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea Mkoani Lindi inatarajia kufanya bonanza la kuhamasisha wananchi kujitokeza kushiriki kikamilifu Katika uchaguzi huo



Akizungumza na mwandishi wetu, kaimu mkurugenzi  halmashauri hiyo Joshua Mnyang'ali alisema kuwa bonanza hilo litafanya siku ya jumamosi 5/10/2024 katika uwanja wa majengo ambao michezo mingi itafanyika huku kukiwa na  wasanii mbalimbali wakipamba jukwaa la burudani kwa wakazi wa wilaya ya Nachingwea.


Amesema bonanza hilo linalenga kutoa elimu ya kushiriki kikamilifu uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji katika wilaya ya Nachingwea, kuhamasisha maswala ya Amani pamoja na kuelezea shughuli mbalimbali za Maendeleo zilizofanywa na serikali


Mwenyekiti wa halmashauri ya Nachingwea Adinani mpyagila ametoa wito kwa wananchi wa Nachingwea pamoja na wa Maeneo jirani kujitokeza kwa wingi kushiriki bonanza Hilo kubwa