Monday, February 19, 2024

MILIONI 800 KUWASAIDIA WAHANGA WA MAFURIKO MULEBA.

 


Na Alodia Babara

 Bukoba,

Walengwa wapatao 482 walioathirika na mafuriko pamoja na upepo mkali  katika wilaya za Muleba na Manispaa ya Bukoba mwaka jana wanatarajia kupata msaada wa kibinadamu wenye malengo mbalimbali utakaoghalimu zaidi ya sh. milioni 800 kutoka taasisi zisizo za kiserikali.

Msaada  huo ambao unatolewa na Kanisa la Kiinjili la Kirutheli Tanzania KKKT Dayosisi ya Kaskazini Magharibi kwa ufadhili wa taasisis inayojihusisha na shughuli za kibinadamu kwa watu wenye majanga nchini Tanzania (TCRS) na taasisi ya Actalliance Tanzania Forum utakuwa wa mwaka mmoja utawezesha kutimiza malengo sita ambayo ni msaada wa chakula, uboreshaji wa makazi, msaada wa kisaikrojia, huduma za maji, elimu na Afya na usafi wa mazingira.

Akizindua mradi huo Februari 19, mwaka huu mkuu wa mkoa wa Kagera Fatuma Mwassa alisisitiza mambo matatu ikiwemo  matumizi ya fedha za walengwa, usimamizi mzuri pamoja na  elimu ya maafa kwa walengwa.

 Mwassa alieleza kuwa, anazo taarifa kuwa mradi huo utahusisha maswala ya fedha, akaelekeza maafisa wanaohusika na maafa upande wa Serikali kama maafisa maendeleo ya jamii, watendaji wa kata, madiwani na viongozi hadi ngazi ya wilaya kushirikiana na uongozi wa kanisa la Kiinjili la Kirutheli Tanzania dayosisi ya Kaskazini Mgharibi katika uhakiki wa walengwa ambao ni harisia ili mradi usije kunufaisha ambao siyo walengwa.

“Viongozi kuanzia ngazi ya kitongoji hadi wilaya ni lazima kushiriki kikamilifu wakati wa uhakiki na kutoa huduma kwa walengwa wanaostahili na ndiyo maana nyinyi viongozi mmehudhuria uzinduzi huu” amesema Mwassa.

Amesisitiza hilo baada ya kukumbana na changamoto wakati wa kugawa chakula kwa waathirika hao kilicholetwa na kamati ya maafa kutoka ofisi ya Waziri mkuu kwani ziliingizwa siasa na likaibuka vuguvugu wakitaka watu wote wapewe msaada huo na watu waliokuwa kwenye kata zilizokumbwa na maafa wakajitokeza wakidai wote wana shida.

Amesema tathimini ilishafanyika wenye uhitaji walishatambuliwa na kuwa viongozi wasiende kuzua la kuzua kwa kulazimisha wengine kuingia kwenye hiyo risti, kaya ambazo zitahusika baada ya uchunguzi ni 482 inajullikana na ndiyo bajeti iliyopo.

“Nitumie nafasi hii kusisitiza kuwa fedha zitakazotolewa zitumike kwa matumizi yaliyokusudiwa zisiwe chanzo cha ndoa kuvunjika na kusababisha ukatili wa kijinsia katika familia za walengwa” amesema Mwassa

Aidha aliongeza kuwa, mradi ujikite sana kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kujifunza namna ya kukabiliana na maafa, mfano wananchi waelimishwe kutojenga sehemu hatarishi zinazoweza kuhatarisha maisha yao na familia zao serikali inaposema maeneo haya hayafai kujengwa makazi basi watu wote wakubaliane na waache maeneo hayo.

Kwa  upande wake Mkurugenzi wa taasisi inayojihusisha na shughuli za kibinadamu kwa watu wenye majanga nchini Tanzania TCRS Samwel Mlay amesema kuwa, mradi utakuwa wa mwaka mmoja ulianza kutekelezwa Desemba mwaka jana na utakamilika Desemba mwaka huuu, utawezesha kutimiza malengo sita ambayo ni msaada wa chakula, uboreshaji wa makazi, msaada wa kisaikrojia, huduma za maji, elimu na afya na usafi wa mazingira.

Mlay amesema, mradi utaghalimu zaidi ya shl milioni 800 walengwa wapatao 482 walioathirika na mafuriko pamoja na upepo mkali  katika wilaya za Muleba na Manispaa ya Bukoba mwaka jana watanufaika na mradi huo ambapo katika wilaya ya Muleba ni kata mbili za Kashalunga na Kalambi na Manispaa ya Bukoba ni kata nne za Rwamishenyi, Hamugembe, Bilele na Kashai  zinatarajia kupata msaada wa kibinadamu katika nyanja mbalimbali kutoka katika  taasisi zisizo za kiserikali

Diwani wa kata ya Kashai Ramadhan Kambuga amesema kuwa, kutolewa kwa misaada hiyo kutasaidia kupunguza maumivu kwa wananchi waliokumbwa na mafuriko na upepo mkali.

 

Amesema wananchi waliokumbwa na athari za mafuriko na upepo walishatambuliwa hivyo hawatakwenda kinyume na wale waliotambuliwa kikubwa viongozi wa Serikali walishawatembelea na kuwabaini na mahitaji ya kila mmoja, hawataongeza wala kupunguza mlengwa kila mmoja alishawekwa kwenye utaratibu hivyo uadilifu, busara na hekima vitaendelea kutumika.

Hata hivyo mafuriko hayo kwa wilaya ya Muleba yalitokea Octoba 15, mwaka jana na kwa manispaa ya Bukoba yalitokea Oktoba 18, mwaka jana.


No comments:

Post a Comment