Monday, February 19, 2024

DIVISHENI YA ELIMU SEKONDARI YAFANYA KIKAO KAZI CHALINZE.

 

Divisheni ya Elimu Sekondari katika Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo, imefanya kikao kazi kufanya tathmini ya utendaji kazi ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya matokeo ya kidato cha pili na cha nne kwa mwaka 2023 ili kuweka mikakati mbalimbali katika kuboresha utendaji kazi ili kufikia Malengo ya utendaji kazi (Key Performance Indicators).

Kikao hicho kimefanyika leo tarehe 19 Februali 2024 katika ukumbi wa Jakaya Kikwete uliopo katika Halmashauri hiyo na kuhusisha Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule za Sekondari za Serikali na binafsi na walimu wa Taaluma katika Shule zote za Sekondari katika Halmashauri ya Chalinze.

Akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi Afisa Elimu wilaya ya Chalinze, Bi Salama Ndyetabura alieleza mafanikio na Changamoto mbalimbali zinazoikabili Divisheni ya Elimu Sekondari, huku akiishukuru Halmashauri ya Chalinze kwa kuweza kujenga maabara kwa baadhi ya Shule za Sekondari katika Halmashauri hiyo

Afisa Elimu Sekondari, ametoa pongezi kwa wakuu wa Shule kwa usimamizi bora wa miradi kwa kumpongeza Mkuu wa Shule Changalikwa Mwl Benasian Ituja kwa Kusimamia ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari ya Mbwewe kwa kuisimamia kwa weledi na maarifa hata kutotengeneza hoja yoyote ya ukaguzi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Chalinze Bwana Ramadhani Possi ametoa pongezi za dhati kwa walimu wote wa Sekondari, Maafisa Elimu na Maafisa kata kwa jinsi wanavyofanya kazi kwa weledi na uadilifu katika kutoa maarifa kwa watoto wa Taifa hili.

Possi aliwapongeza kwa kukuza taaluma na kupata matokeo mazuri ya kidato cha nne na cha pili kwa mwaka 2023.

Aidha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri amewasisitiza watendaji wa kata kushirikiana na walimu ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wote waliofaulu kuingia kidato cha kwanza kuripoti kwa wakati na kuweza kuendelea na masomo.





No comments:

Post a Comment