Na Daria Abdul, Hamisi Hamisi, Bagamoyo.
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mhe. Halima Okash, akishirikiana na viongozi mbalimbali wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, amefanya kikao na madereva wa pikipiki zinazobeba abiria (BODABODA) Januari 31,2024 katika ukumbi wa flexible hall Chuo cha Sanaa Bagamoyo (TASUBA), kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili katika utendaji kazi wao wa kila siku.
Mhe.Okash, amewasisitiza bodaboda kutii sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali, pia wajiepushe na matukio ya uhalifu wa kupora mali za wateja wao.
”Ndugu zangu lazima tutii sheria za usalama barabarani kwani tunawategemea ninyi vijana kuwa ndio Taifa la kesho hizo rizki tunazozipata kuna watu wanatutegemea tusipotii sheria za usalama barabarani, kutakuwa na ajali za mara kwa mara zitakazopelekea kupoteza maisha na kuleta ulemavu.” Amesema Okash
Akizungumza katika hafla hiyo Mkuu wa Usalama barabarani, Wilaya ya Bagamoyo (DTO) Azizi Zubeir, amewataka bodaboda kuhakikisha wanasajili vyombo vyao vya usafiri, leseni pamoja na bima ili wasikamatwe na vyombo vya usalama na kueleza Zaidi kuwa bima itasidia kupunguza gharama ya matengenezo ya vyombo hivyo na matibabu kwa dereva anapopata ajali.
"Ni waambie tu bodaboda ili ufanye kazi kihalali lazima usajili vyombo vyetu, tuwe na leseni ya udereva pamoja na bima ya chombo husika ili itusaidie kupunguza gharama za matengenezo na matibabu inapotokea ajali.” Amesema Zubeir
Akitoa kero yake katika hafla hiyo Mwenyekit wa Bodaboda kata ya Dunda Ndug, James Mapunda, amesema kuwa wamekuwa wakipatiwa mafunzo ya usalama barabarani na vyuo mbalimbali vikishirikiana na Jeshi la polisi Wilayani hapo na kuahidiwa kupatiwa leseni za udereva baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo, badala yake hawapewi leseni zao licha ya kulipia fedha kwa ajili ya leseni hizo.
Kwa upande wake Waziri Mohammed (BODABODA), ameeleza kuwa wamekuwa wakinyanyaswa na kukamatwa na Mgambo kwa mabavu katika vituo vyao vya kazi (vijiwe) bila ya uwepo wa askari wa Jeshi la polisi kinyume na sheria hali inayopelekea kushindwa kufanya shughuli zao usafirishaji kwa amani.
No comments:
Post a Comment