....................................
Na Omary Mngindo, Ruvu.
TAASISI ya Lions Club ya jijini Dar es Salaam imekabidhi matenki 8 ya kuhifadhia maji katika shule za msingi na Sekondari ndani ya Kata ya Vigwaza Halmashauri ya Chalinze Mkoani Pwani.
Matanki hayo yanalenga kuwaondolea adha wanafunzi kwenye shule hizo, yamekabidhiwa kwa Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Chalinze, Ramadhani Possi, aliyewakilishwa na Miriam Kihiyo Afisa Elimu Msingi.
Muntazir Bharwan alisoma taarifa ya taasisi kwa niaba ya Mwenyekiti wa Lions Host Kaniz Naghavi, iliyoeleza kuwa kukabidhiwa kwa matenki hayo kumetokana na diwani wa Kata hiyo Mussa Gama kuelezea uwepo wa changamoto kwenye shule hizo.
Hafla hiyo iliyotumika pia kumkaribisha Gavana wa Tanzania District 411C Happiness Nkya, matenki hayo yanakwenda katika shule za Msilale, Chamakweza, Sekibwa, Ruvu, Mnindi, Kitonga na Kwazoka.
"Baada ya kupokea maombi ya diwani Gama tukawasiliana na Kampuni ya Refuelling Solutions (T) Limited na wadau wengine wakiwemo wanachama wa Lions ambao tumefanikisha upatikanaji huu," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Gavana wa taasisi hiyo Nkya alisema kwamba kwa sasa wana wanachama 620 na Club 23, wakati Dar es Salaam zikiwa 14, na kwamba wamekuwa wakisaidia maeneo tofauti wakisaidiana na makampuni mengine.
Kwa upande wake diwani Gama ameishukuru Taasisi hiyo, huku akieleza kuwa imekuwa ikisaidia maendeleo katika nyanja mbalimbali ikiwemo vifaa katika Zahanati ya Ruvu Darajani, madaftari kwa wanafunzi ikiwemo matenki hayo.
"Club ya Lions imekuwa na msaada mkubwa sana kwetu wanaVigwaza, kwani wanasaidia kutatua matatizo kwenye kata yetu kwa kushirikiana na wadau wengine kutupatia misaada ya fedha na vitu katika sekta mbalimbali," alisema Gama.
Afisa Elimu awali na Msingi wa Halmashauri ya Chalinze, Mariam Kihiyo akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi hiyo, aliishukuru taasisi hiyo, kwa misaada inayoendelea kuipeleka inayolenga kupunguza vikwazo kwa wanaVigwaza.
"Kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Chalinze, Alhaj Ramadhani Possi, tunawashukuru sana ndugu zetu wa Lions Club kwa namna mnavyojitoa mkishirikiana na wadau wenu, wanaChalinze tunatambua na kuthamini mchango wenu mkubwa kwetu," alisema Kihiyo.
Samwel Mjema Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Ruvu Darajani alisema matenki hayo yatasaidia kutunza maji pindi yanapokatika, huku akiahidi utunzwaji yaweze kudumu kwa muda mrefu.
No comments:
Post a Comment