Msimamizi wa uchaguzi jimbo la Bagamoyo Shauri Selenda, amewataka makarani waongozaji katika uchaguzi mdogo wa kata ya Fukayosi Halmashauri ya Bagamoyo, kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa mafunzo watakayopewa.
Selenda ameyasema hayo alipokuwa akifungua mafunzo kwa Makarani waongozaji wa uchaguzi mdogo kata ya Fukayosi Haashauri ya Bagamoyo ambapo alisema makarani wanapaswa kuzingatia kanuni na sheria za uchaguzi katika kutekeleza majukumu yao kama watakavyoelekezwa katika mafunzo hayo.
Alisema kazi ya ukarani wa uchaguzi inahitaji uvumilivyu, subira na busara katika utendaji wake kwani kazi hiyo inawakutanisha na watu tofauti ambao wanahitaji kusikilizwa, kuelekezwa na kuongozwa juu ya kile wanachopaswa kufanya katika kutekeleza haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi.
Makarani hao walikula kiapo cha kutekeleza majukumu hayo tayari kwaajili ya uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Machi 20, 2024.
Kiti cha udiwani kata ya Fukayosi kimebaki wazi baada ya aliyekuwa Diwani wa kata hiyo kufariki dunia kwa maradhi ya shinikizo la damu mnamo mwezi Novemba mwaka 2023.
Akizungumza kwa niaba ya Makarani wenzake, Athumani Hassan Fundi, amesema watahakikisha wanazingatia kile wanachofundishwa ili kutekeleza majukumu yao kwa weledi
Alisema nia wameipokea kazi hiyo kwa moyo mmoja na wapo tayari kufuata maelekezo kwa mujibu wa sheria za uchaguzi ili kufanikisha kazi hiyo muhimu.
No comments:
Post a Comment