Sunday, February 4, 2024

PWANI YAHITIMISHA SHEREHE ZA MAADHIMISHO YA MIAKA 47 YA KUZALIWA KWA CCM

 


Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Pwani leo tarehe 04/02/2024 kimehitimisha sherehe za  Maadhimisho ya miaka 47 ya kuzaliwa kwa CCM katika Kata ya  FUKAYOSI Wilaya ya  Bagamoyo huku kikiwa na matumaini makubwa ya ushindi kuelekea uchaguzi Mkuu wa Serikali za Mitaa, Vijijini na Vitongoji 2024.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika kuhitimisha maadhimisho hayo ndg. Mwinshehe Mlao amesema ili CCM iweze kuendelea kudumu lazima Viongozi waondoe ubinafsi.

Mlao amesema unapofika wakati wa uchaguzi Kila mpiga kura ahakikishe anawachagua Viongozi wa Serikali wenye nia njema ya kuongoza na ikitokea  wakawachagua Viongozi kwa ajili ya maslahi yao binafsi basi watakuwa wamepoteza haki za wengine.

Ameendelea kusema kuwa ili kushinda chaguzi zijazo kunahitajika UMOJA huku akisisitiza kuwa kama Kuna mwanachama yeyote mwenye nia ya kugombea na anaonekana kuwa na dosari aambiwe sasa wasisubiri mpaka achukue fomu ndio waseme mabaya yake huko ni kuchafuana.

" Tusikubali kusababisha migogoro isiyo na tija tunapoelekea kwenye chaguzi zijazo na wala tusikubali watu watugawe kwa ajili ya maslahi yao" amesema Mlao

Maadhimisho hayo yameambatana na ukaguzi wa Kituo Cha afya cha Fukayosi kinachojengwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 1, Uzinduzi wa ujenzi wa Ofisi ya CCM kata ya Fukayosi, ugawaji wa vifaa vya Shule kwa wanafunzi wanaoishi katika Mazingira magumu, ugawaji wa vyeti vya PONGEZI kwa Kata zilizofanya vizuri katika uingizaji wanachama wapya na usajili kwa mfumo wa kielektroniki sambamba na zoezi la upandaji wa miti.

Taarifa hii imeandaliwa na:

David Mramba
Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo CCM
Mkoa wa Pwani.


No comments:

Post a Comment