Na Alodia Babara
Bukoba,
Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Abdulmalick Yahya (42) mkazi wa wilaya ya Muleba ambaye alikuwa mtunza ghala katika mradi wa ujenzi wa BAKWATA Bukoba (BAKWATA COMPLEX) amefariki baada ya kushambiliwa na wananchi wenye hasira kufuatia tukio alilofanya la kumshambulia katibu wa BAKWATA wilaya ya Bukoba na kumkata kiganja cha mkono.
Katibu wa Bakwata wilaya ya Bukoba Hamza Zakaria (43) akiwa anaendelea na matibabu katika hospital ya rufaa ya mkoa, Bukoba amesimulia alivyoshambuliwa na aliyekuwa mtunza ghala la ujenzi wa BAKWATA Complex na kuanza kumkata kwa panga kisha kutenganisha kiganja na kiwiko cha mkono wa kushoto.
"Ilikuwa ni majira ya saa 10:00 asuhuhi siku ya Tarehe 2 februali 2024 wakati nikiwa kazini kwangu nilitoka kwenda duka la jirani kuangalia viatu kwa mtu mmoja anaitwa Khalid ndipo alitokea Abdulmalick Yahya akiwa ameshika panga na kuanza kunishambulia" amesema Hamza
Ameendelea kusimulia kuwa, alipomkata panga la kwanza alikinga mkono alipotaka kumkata tena walishikana mikono na badae akajitoa kwenye mikono yake na kutaka kukimbia kutokana na kwamba alikuwa amevaa kanzu ambayo ilimtega miguu akashindwa kukimbia na badala yake alianguka chini.
"Kwa kuwa alikuwa anaendelea kunifukuza alinikuta hapo hapo chini akaanza kunikata mapanga huku nikiendelea kukinga mkono wa kushoto ndipo baadaye nilijifanya nimefariki dunia alipokata mara ya mwisho akaona sijitingishi akaondoka" ameongeza Hamza.
Amesema ndani ya dakika kama tano hivi alimuona mtu anayemfahamu akamuita wakampa msaada wa kumbeba na vijana wengine na kumpeleka hospital ya rufaa ya mkoa wa Kagera, Bukoba ambapo anaendelea kupatiwa matibabu na anaendelea vizuri.
Amesema huyo aliyemkata mapanga hakuwa na visa naye labda kama vilitokana na ujenzi uliokuwa unaendelea msikitini, siku zilizopita alikuwa ni mtunza ghala na alikuwa ni miongoni mwa watu waliokamatwa wanaiba nondo na saruji akawa amesimamishwa kuendelea kusimamia ghala hilo, sasa alihisi kuwa alichongewa na Hamza na alikuwa ni mtu wa muda mrefu pale msikitini.
Kamanda wa polisi mkoani Kagera, Blasius Chatanda, amethibitisha kutokea kwa matukio hayo mawili na kusema kuwa, Abdulmalick Yahya (42) mkazi wa wilaya ya Muleba ambaye alikuwa mtunza ghala katika mradi wa ujenzi wa BAKWATA Bukoba (BAKWATA COMPLEX) kabla hajakumbwa na umauti Februari 02,2024 majira ya saa 11:30 asubuhi katika barabara ya Kawawa karibu na ofisi za Bakwata mkoa alifika na kuanza kumkata mapanga Hamza Zakaria (43) katibu wa BAKWATA wilaya ya Bukoba.
Amesema wakati akitenda tukio hilo watu waliokuwepo walimzuia asiendelee kumshambulia bila mafanikio na walipoona anataka kuwashambulia na wao walianza kumshambulia na alibahatika kuokolewa na jeshi la polisi na kumkimbiza hospital ya rufaa ya mkoa, Bukoba ambapo wakati akiendelea kupata matibabu alifariki dunia.
Kamanda Chatanda alieleza kwamba, chanzo cha tukio hilo ni kusimamishwa kazi ya kusimamia ghala la kutunza vifaa vya ujenzi wa BAKWATA complex kwa Abdulmalick na kamati ya ujenzi Februari mosi ,2024 ambapo Abdulmalick alimtuhumu katibu wa BAKWATA, Bukoba kwamba ndiyo chanzo cha hayo yote na akaahidi kulipiza kisasi.
Amesema kuwa, alimkata mkono wa kushoto ambao kiganja chake alikitenganisha kabisa na kiwiko na alikatwa mapanga mengine mawili kichwani japo ni kwa bahati nzuri hayakuweza kupasua fuvu.
Ametoa rai kwa wananchi wa mkoa huo kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake kufuata sheria na taratibu za nchi.
No comments:
Post a Comment