Tuesday, February 6, 2024

WAFANYABIASHARA WA MAFUTA ZINGATIENI MAISHA YA WANANCHI - DKT. BITEKO

 

Na Mwandishi wetu, Dodoma

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Chama cha Waagizaji na Wasambazaji wa Mafuta nchini (TAOMAC) ambapo amewataka wafanyabiashara hao pamoja na faida wanayoipata wazingatie maslahi wananchi wa hali ya chini.

Ameyasema hayo tarehe 06 Februari, 2024 jijini Dodoma katika kikao ambacho kilijadili masuala mbalimbali ikiwemo changamoto mbalimbali ambazo wanafanyabiashara hao wanazikabili.

Amesema Serikali siku zote iko tayari kutoa ushirikiano kwa wafanyabiashara na kuwekea mazingira wezeshi ya biashara zao ili waweze kuwajibika kwa mujibu wa sheria kanuni na taratibu za usimamizi katika sekta husika.

“Tunapofanya biashara hii ya mafuta lazima tuangalie mtanzania maskini ambaye anategemea sekta hii kujikwamua kimaisha, isifike mahala kila mwisho wa mwezi watu wote wanashika vichwa wakihofia kupanda kwa bei ya mafuta… Serikali inafanya kila jitihada kupunguza makali ya bei ya mafuta hivyo nanyi mlizingatie suala hili.”amesema Dkt. Biteko

Dkt. Biteko ameishukuru TAOMAC kwa ushirikiano wao kwa Serikali katika kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na mafuta ya kutosha na kueleza kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango wao katika ukuaji wa Uchumi wa nchi.

Amesema uhusinao uliopo kati ya Serikali na TAOMAC unahitaji kuwa endelevu na pale zinapotokea changamoto zitafutwe njia za kukabiliana nazo kwa mstakabali wa Taifa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAOMAC, Kalpesh Mehta ameishukuru Serikali kwa mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara wa mafuta na utayari wa Serikali kushughulikia changamoto kadhaa zinazojitokeza katika sekta hiyo.

Akizungumzia mazingira hayo, Mkurugenzi Mtendaji, Raphael Mgaya amesema ushirikiano wa TAOMAC kwa serikali hauepukiki ili kuhakikisha nchi inapata mafuta ya kutosha hivyo wapo tayari kushirikiana na Serikali.

Kikao hicho pia kimehudhuriwa na Watendaji kutoka  Taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo Benki Kuu  ya Tanzania (BoT) Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Shirika la Uwakala wa Meli (TASAC), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba.







No comments:

Post a Comment