Thursday, February 1, 2024

WALENGWA WA TASAF WATAKIWA KUTUMIA FEDHA ZA TASAF KUJIENDELEZA KIMAISHA.

 

Mkurugenzi wa uratibu  wa shughuli za serikali ofisi ya makamu wa pili wa Rais, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Siajabu Suleiman Pandu akizumgumza na wanufaika wa mpango wa TASAF Manispaa ya Bukoba hawako pichani.

..........................................

Alodia Babara,

Bukoba.

WALENGWA wa mpango wa kunusuru kaya maskini nchini, TASAF wametakiwa kuzitumia fedha za mpango huo kama sehemu ya ukombozi, kuimarisha ndoa na familia zao kwa lengo la kuondoa umaskini.

Hayo yamesema Januari 31, mwaka huu 2024, na Mkurugenzi wa uratibu wa shughuli za serikali ofisi ya makamu wa pili wa Rais Zanzibar Siajabu Pandu wakati wadau mbalimbali wa mpango huo walipotembelea walengwa katika manispaa ya Bukoba mkoani Kagera kwa lengo la kukusanya maoni na changamoto zinazowakabili walengwa, ambazo baada ya kuzibaini zitawawezesha wadau hao kuboresha mpango unaofuata.

“Serikali tunaamini fedha hii iwe ni sehemu ya ukombozi, kwa hiyo ninawaomba muishi katika ndoa njema, familia nzuri ni sehemu ya ukombozi, fedha ni matokezeo tu sasa tuzitumie hizi fedha kuimarisha ndoa zetu, ndoa si chochote ni subira, tunapaswa kuvumiliana kuhakikisha kwamba tunaishi na watoto wetu kwa pamoja na familia zetu ili kuondoa hali hii ya umaskini” amesema Pandu

Katika ukusanyaji maoni na kusikiliza changamoto za walengwa wadau hao wamegundua kuwa, baadhi ya kaya za walengwa wametelekeza familia zao na kumuacha mzazi mmoja wapo, baba/mama, akiangalia majukumu ya kulea watoto peke yake.

Aidha baadhi ya walengwa wa mpango huo katika mtaa wa Kabale ka Ngaiza manispaa ya Bukoba wakati wakitoa hadithi zao mbele ya wadau hao imeonekana kuwa kuna baadhi ya walengwa ambao ni watoto walishindwa kuendelea katika mpango baada ya wazazi wawili mke na mme kutengana na hivyo watoto kuhamishwa eneo la mtaa husika bila kuwepo mawasiliano na mratibu wa mpango na hivyo kusababisha watoto kuondolewa katika mpango.

Esther Peter mkazi wa mtaa wa Kabale Ka Ngaiza mwenye wategemezi sita, watoto wake wanne na wadogo zake wawili amesema kuwa, yeye anakabiliwa na changamoto mbili mtaji wake kuwa mdogo tofauti na mahitaji yake pamoja na sehemu ya kuishi kwani anaishi kwenye nyumba za kupanga.

Amesema kutokana na changamoto za ndoa watoto waliingizwa kwenye mpango baadaye baba yao akawachukua kuishi nao eneo jingine na hivyo kutokana na kwamba hakuwa na mawasiliano naye watoto waliondolewa kwenye mpango na sasa baada ya kuanza kuishi nao tena anafanya utaratibu wa kuwarudisha kwenye mpango.

“Nashukuru mpango huu wa TASAF na namshukuru Rais wa nchi yetu mama Samia Suluhu Hassan mimi kabla sijaingia  katika mpango huu nilikuwa naishi kwa kuomba omba chakula na nguo kwa watu lakini baada ya kuingia kwenye mpango huu kwa sasa naweza kumudu chakula milo mitatu naweza kuvaa nguo nzuri na kuwanunulia wanangu pia na nimepata mtaji kidogo nafanya biashara ya kuuza samaki” amesema Peter

Amesema, kipindi hicho alikuwa na mdogo wake yuko kidato cha pili lakini kwa sasa amemaliza chuo cha maendeleo ya jamii ingawa bado hajapata ajira na mdogo wake yuko chuo kikuu anasomea sheria.

Aidha walengwa hao wameiomba serikali waendelee kuwa walengwa katika mpango wa kunusuru kaya maskini kwani wapo baadhi yao wamekumbwa na changamoto mbalimbali na hivyo kusababisha kutoinuka kiuchumi na kubaki wakiwa maskini.

Mwenyekiti wa mtaa wa Kabale ka Ngaiza Longino Goerge ametoa maombi kadhaa kwa wadau hao kuwa, ni pamoja na TASAF kuunda dawati la usuluhishi kwa wanandoa, kuwaingiza wazee kwenye mpango na kutoa ajira kwa vijana waliotokana na mpango.

Akijibu maswali ya mwenyekiti Kaimu mkurugenzi wa mifumo , mawasiliano na ufuatiliaji TASAF makao makuu Peter Lwanda amesema kuwa, wanaendelea kutengeneza mpango mwingine ambao utaendelea.

Kuhusu ajira ameeleza kuwa, TASAF ilikuwa inafuatilia wale wanaomaliza darasa la saba na kidato cha nne  ambao hawaendelei ofisi ya waziri mkuu inawapeleka vyuo vya ufundi na kuwa serikali bado inaangalia matatizo ya ajira na kuyafanyia kazi.

Lwanda akijibia swala la wazee kuingizwa kwenye mpango ameeleza kuwa, watalichukua na kulifanyia kazi mpango ujao.

Ikumbukwe kuwa mkoa wa Kagera una walengwa wa TASAF wapatao 80,563 ambapo tangu mpango ulipoanza mwaka 2015 hadi sasa zaidi ya shilingi bilioni 57.2 zimeishatolewa kwa walengwa hao.





Walengwa wa mpango wa kunusuru kaya masiki mtaa wa Kabale Ka Ngaiza

No comments:

Post a Comment