Saturday, April 14, 2018

ZAIDI YA MILIONI 600 KUJENGA MIRADI YA MAENDELEO CHALINZE.

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Mh. Alhaj, Majid Mwanga akikata utepe kuashiria uwekaji wa jiwe la msingi ujenzi wa kituo cha Polisi Lunga kata ya Lugoba Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo.
  
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Mh. Alhaj, Majid Mwanga alipokuwa akiweka jiwe la msingi katika Zahanati ya Buyuni kata ya Vigwaza Halmashauri ya Chalinze, ambapo alikuwa na ziara ya wiki nzima kuweka mawe ya msingi miradi mbalimbali ya maendeleo.
..................................................................

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Mh. Alhaj, Majid Mwanga ameweka mawe ya msingi miradi ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya milioni 600 katika Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo.

Akizungumza kwa nyakati tofauti katika vijiji vya Halmashauri ya Chalinze katika zoezi la uwekaji wa mawe hayo ya msingi, Mkuu huyo wa wilaya mwenye kauli mbiu inayosema UONGOZI UNAOCHA ALAMA, alisema lengo la serikali ni kutatua kero za wananchi katika kila kijiji kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Alisema kila mwananchi anayo haki ya kupata huduma bora za Afya, Elimu, miundombinu mizuri ya Barabara, Umeme na Maji hivyo ni wajibu wa serikali kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa.

Aidha, aliwataka wananchi kutoa ushirikiano katika kufanikisha ujenzi wa miradi hiyo ili kufikia lengo la serikali ambalo ni kuwasogezea wananchi huduma muhimu za jamii.

Alisema sio dhambi kwa wananchi kuchangia ujenzi wa miradi ya maendeleo hivyo serikali inapotenga fedha kwaajili mradi fulani ni vyema wananchi wakachangia baadhi vifaa au nguvukazi ili kurahisisha utekelezaji wake.

Aliongeza kwa kusema kuwa wananchi kwa kushirikiana na serikali wanaweza kufanikisha ujenzi wa miradi muhimu kama zahanati na shule.

Mkuu huyo wa wilaya aliwataka wenyeviti wa vijiji kutoa elimu kwa wananchi juu ya ushirikishwaji wa maendeleo na kupata muafaka wa pamoja katika kuchangia maendeleo kwa hiyari ambapo serikali inaendelea kutekeleza kila kijiji.

Kwa upande wao wenyeviti wa vijiji vya Halmashauri ya Chalinze kwa nyakati tofauti wamempongeza Mkuu huyo wa wilaya kwa kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo inaleta tija kwa wananchi.

Walisema baadhi ya vijiji kwa miaka mingi vimekuwa havina huduma za Zahanati na Shule laikini kupitia uhamasishai wake wananchi wameweza kuanzisha na Halmashauri kuongeza nguvu na hatimae kufanikisha miradi kadhaa katika vijiji mbalimbali katika Halmashauri hiyo.

Katika kila kijiji wenyeviti hawakusita kumshukuru mkuu huyo wa wilaya licha ya kuwa chanzo cha ujenzi wa miradi kadhaa lakini pia ni mchangiaji wa fedha na vifaa katika kufanikisha miradi hiyo.

Miradi hiyo iliyowekwa mawe ya msingi na Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo katika halmashauri ya Chalinze na gharama zake kwenye mabano ni pamoa na Ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule ya msingi Kiwangwa kata ya Kiwangwa,(15,539,800/=) Zahanati ya Kihangaiko kata ya Msata, (30,401,400/=) Zahanati ya Buyuni kata ya Vigwaza (98,420,000/=) Madarasa 6 shule ya Msingi Vigwaza kata ya Vigwaza (198,000,000/=)

Miradi mingine ni Madarasa nane shule ya Msingi Bwilingu A na B kata ya Bwilingu (86,809,000/=) Vyumba viwili vya madarasa shule ya Msingi Lulenge kata ya Ubena ( 21,946,000/=) Nyumba ya Daktari Zahanati ya Mboga kata ya Msoga (50,000,000/=) Sekondari ya Mboga kata ya Msoga (90,000,000/=) Vyumba viwili vya madarasa shule ya Msingi Changa kata ya Msoga (20,000,000/=)  Kituo cha Polisi Lunga kata ya Lugoba (60,000,000/=)

Miradi yote hiyo imetekelezwa kwa ushirikiano wa serikali, wananchi, wafadhili na wadau mbalimbali wa maendeleo wa kata husika na wilaya kwa ujumla.

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo alitoa wito kwa wadau wa maendeleo wilayani Bagamoyo kujitokeza kuchangia miradi hiyo ambayo baadhi yake haijakamilika.

Aidha, aliwataka wananchi wazaliwa wa Bagamoyo popote walipo kuchangia maendeleo ya vijiji walivyotoka ikiwa ni njia ya kuenzi vjiji vyao huku wakiisaidia serikali katika kuleta maendeleo.
 
 Muonekano wa jengo la kituo cha Polisi Lunga kata ya Lugoba Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo ambapo Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo ameweka jiwe la msingi ili kukamilisha kituo hicho cha Polisi zinahitajika Milioni 30.

 
Muonekano wa Zahanati ya Buyuni kata ya Vigwaza Halmashauri ya Chalinze, ambayo imekamilka kwa sasa zinahitaika samani za ndani ili kuanza kazi rasmi.
 
 Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Mh. Alhaj, Majid Mwangaakiweka jiwe la msingi nyumba ya Daktari katika Zahanati ya Mboga iliyopo kata ya Msoga Halmashauri ya Chalinze.

No comments:

Post a Comment