Monday, April 23, 2018

TAKUKURU BAGAMOYO YATOA SOMO SHULE ZA SEKONDARI.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Pwani, Suzana Raimond kulia akizungumza katika Tamasha la klabu za wapinga rushwa shuleni, kushoto ni Mkuu wa TAKUKURU wilaya ya Bagamoyo, Raimond Katima.
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Alhaj, Majid Mwanga akifungua Tamasha la klabu za wapinga rushwa shuleni. 
.................................
Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilaya ya Bagamoyo imeandaa Tamasha la klabu za kupinga rushwa katika shule za sekondari.

Katika Tamasha hilo lililofanyika Shule ya Sekondari ya Baobab iliyopo Mapinga wilayani Bagamoyo, Mgeni Rasmi alikuwa Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga ambapo aliwataka wanafunzi kujifunza kuchukia rushwa ili kuwa raia wenye uzalendo na nchi yao.

Alisema vijana ni kundi muhimu linalopaswa kutambua ubaya wa rushwa kwakuwa hao ndio wanaondaliwa kuwa viongozi wa baadae hivyo kutambua ubaya wa rushwa kwao kutapelekea nchi kupata viongozi wenye uzalendo watakaoiletea nchi yao maendeleo.

Aidha, ameipongeza TAKUKURU wilaya ya Bagamoyo kwa kufanya kazi vizuri na kupelekea vitendo vya rushwa kupungua wilayani humo na kulinda haki za watu katika idara mbalimbali.

Aliwapongeza TAKUKURU kwa utaratibu wao wa kutoa elimu katika kila idara ili kuelezea ubaya wa rushwa na namna ya kuiepuka.

Kwa upande wake Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Pwani, Suzana Raimond alisema klabu za wapinga rushwa shuleni zimesaidia kwa kiasi kikubwa kazi kupambana na rushwa kwakuwa wananfunzi wamekuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu kwa njia ya maigizo na kutambua ubaya wa rushwa.

Alisema TAKUKURU mkoa wa Pwani imefanikiwa kukamata watu kupitia taarifa zinazotolewa na klabu za wapinga rushwa shuleni na kwamba hiyo imesaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa vitendo vya rushwa shuleni.

Nae Mkuu wa TAKUKURU wilaya ya Bagamoyo Raimond katima ambao ndio waandaaji wa Tamasha hilo alisema vitendo vya rushwa vinasababishwa na mmomonyoko wa maadili katika jamii kuanzia ngazi ya chini.

Alisema maadili yanapaswa kujengwa kwenye familia, mashuleni na katika kila maeneo yanayohusiana na malezi ili kuwajenga watoto na vijana kutambua umuhimu wa kuwa na maadili mema ikiwa ni pamoja na kutambua ubaya wa rushwa.

Aliongeza kwa kusema kuwa kiongozi au mtumishi wa uma anapokuwa na vitendo vya rushwa ni wazi kuwa vitendo hivyo vimeanzia chini.

Alisema nchi inakabiliwa na rushwa hivyo ni vyema wananchi wakatambua kuwa rushwa inasababisha kurudisha nyuma maendeleo

Aliwataka wananchi kushirikiana na TAKUKURU ili kubaini wale wote wanaojihusisha na vitendo vya rushwa ili hatua za kisheria zichkue mkondo wake.

Wanfunzi wa klabu za wapinga rushwa shuleni walisema wamefaidika na elimu wanayopata kupitia klabu hizo ambapo kwa sasa wamefahamu vyema madhara yatokanayo na kupokea na kutoa rushwa.

Walisema taasisi nyingi hapa nchini kuna vijna hivyo kuwajengea uelewa vijana wakiwa shuleni ni jambo la msingi na kwamba wakitoka watatoa elimu hiyo katika jamii.
Wanfunzi wa klabu za wapinga rushwa shuleni kutoka shule za sekondari sita wilayani Bagamoyo wakifuatilia Tamasha hilo.

No comments:

Post a Comment