Monday, April 30, 2018

BAGAMOYO YAZINDUA CHANJO YA SARATANI YA MLANGO WA KIZAZI.

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga akiandaa sindano kwaajili ya uzinduzi wa chanjo ya Saratani ya Mlango wa kizazi kwa wasichana wenye umri wa miaka 14.
   
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga akizungumza kabla ya kuzindua chanjo ya Saratani ya Mlango wa kizazi kwa wasichana wenye umri wa miaka 14.
.......................................
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga amesema mtu atakaekwamisha zoezi la chanjo ya Saratani ya shingo ya Kizazi atachukuliwa hatua za kisheria.

Mkuu huyo wa wilaya ametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti katika Halmashauri za Bagamoyo na Chalinze wakati wa uzinduzi wa chanjo ya Saratani ya mlango wa kizazi.

Alisema serikali inapanga mikakti ya kuboresha Afya za wananchi wake ili waweze kutumikia taifa pamoja na kuihudumia wenyewe na familia zao.

Aliongeza kuwa, Bagamoyo ina mikakati ya kukuza uchumi kwa kujenga viwanda hivyo ni wazi kuwa wanaotakiwa kufanya kazi katika viwanda hivyo ni watu wenye afya nzuri isoyokuwa na mgogoro.

Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekuwa ikitoa chanjo za magonjwa mbalimbali lengo likiwa ni kuhakikisha afya za wananchi zinakuwa salama.

Katika hatua nyingine mkuu huyo wa wilaya ameigiza Halmashauri ya Chalinze kuangalia madeni ya madaktari na kuwalipa ili kuwaondolea manung'uniko ambayo yanaweza kuzorotesha utendaji kazi wao.

Alisema yapo malalamiko kwa madaktari ambao hawalipwi fedha za kuitwa kazini kwa matukio ya dharula nje ya muda wa kazi (On-call Allowance) ambayo ni haki yao kimsingi.

Ameitaka Halmshauri ya Chalinze kufanya haraka kuwalipa madaktari On-call Allowance ili waweze kuwa na moyo wa kufanya kazi muda wowote wanapohitajika.

Alisema Serikali imetenga bajeti kubwa katika wizara ya Afya ili kuboresha huduma za afya hivyo Halmashauri nazo zinapaswa kuongeza bajeti zake katika sekta ya afya ili kuwajengea mazingira rafiki madaktari na watumishi wa afya kwa ujumla. 

Aidha, alimtaka Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Chalinze Dkt. Rahim Hangai kuchukua hatua za dhati kuhakikisha zahanati ambazo hazina madaktari anapeleka madaktari ili kuwasogezea wananchi huduma za afya ambazo kwa sasa wanatembea umbali mrefu licha ya kuwepo zahanati kwenye maeneo yao.

Awali wakichangia mada katika semina elekezi iliyofanyika shule ya Kikaro Halmashauri ya Chalinze washiriki wa semina hiyo walisema wananchi wanakabiliwa na changamoto ya kufuata huduma za afya mbali na maeneo yao hali inayopelekea kushindwa kuwapatia watoto wao chanjo.

Walisema vipo baadhi ya vijiji mwananchi analazimika kutumia shilingi elfu nane ili kumpeleka mtoto akapate chanjo.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Chalinze Dkt. Rahim Hangai alisema atahakikisha anayafanyia kazi maelekezo ya Mkuu wa wilaya ili kukidhi mahitaji ya wananchi katika maeneo ambayo tayari kuna Zahanati lakini hakuna Daktari.

Alisema tatizo la upungufu wa madaktari katika Halmashauri hiyo limetokana na watumishi walioondolewa kutokana na kuwa na vyeti feki hivyo idara ya afya katika Halmashauri hiyo ni miongoni mwa wathirika ambapo mpaka sasa wanasubiri watumishi wengine watakaopangiwa na wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. (TAMISEMI) ili kuziba mapengo hayo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashuri ya Chalinze Saidi Zikatimu alisema ataiongoza Halmashauri hiyo katika kuhakikisha inatekeleza majukumu yake kwa watumishi ili nao wafanye kazi kwa moyo na bidii.

Alisema ni kweli serikali imetenga fedha kwaajili kuboresha sekta ya afya ambapo Halmashauri ya Chalinze imepoke zaidi ya shilingi milioni 440 kwaajili ya kuboresha huduma katika vituo vya afya na Zahanati na milioni 400 kwaajili ya kituo cha afya ambapo ujenzi wake unaendelea.

Chanjo ya Saratani ya mlango wa kizazi imezinduliwa rasmi hii leo jumatatu ya tarehe 30 Aprili katika Halmashauri za Bagamoyo na Chalinze ambapo walengwa ni wasichana wenye umri wa miaka 14.
 
 Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga akivaa koti la udaktari ikiwa ni maandalizi ya kuzindua chanjo ya Saratani ya Mlango wa kizazi kwa wasichana wenye umri wa miaka 14.

Watumishi wa halmashuri ya Chalinze wakifutilia kinachoendelea kwenye semina elekezi kuhusu chnjo ya mlango wa kizazi kwa wasichana iliyofanyika shule ya Kikaro kata ya Miono.
 Mwenyekiti wa Halmashuri ya Chalinze Saidi Zikatimu akizungumza katika semina hiyo.
 Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Chalinze Dkt. Rahim Hangai akitoa maelekezo kwa washiriki.



Washiriki wa semina hiyo wakifuatilia maelezo yanayotolewa.

Muwezeshaji akitoa semina kwa washiriki.
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Alhaj, Majid Mwanga akiwa na viongozi wa dini katika picha ya pamoja.


 Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Alhaj, Majid Mwanga akiwa na maafisa tarafa pamoa na viongozi wengine waandamizi katika picha ya pamoja.

No comments:

Post a Comment