Ndugu
Wanahabari,
Serikali
kupitia Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto imekuwa
ikitoa taarifa ya mwenendo wa mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu na hatua
zinazochukuliwa kudhibiti ugonjwa huu Kuanzia Januari hadi kufikia tarehe 31
Machi 2018, jumla ya wagonjwa 1448, wametolewa taarifa, na kati ya hao 27
wamepoteza maisha.
Kwa
kipindi cha Januari wagonjwa 365 na vifo 9 walitolewa taarifa, Februari
wagonjwa 996 na vifo 18 na Machi wagonjwa 87 bila kifo. Mwenendo wa takwimu
hizi za ugonjwa wa Kipindupindu zinaonyesha kuwa idadi ya wagonjwa na vifo
imepungua kwa kiasi kikubwa. Aidha, Mkoa wa Dodoma
umeongoza kwa kipindi cha Januari hadi Machi kwa kuripoti jumla ya wagonjwa 583
kati ya 1,448 walioripotiwa nchi nzima sawa na asilimia 40.3%, ikifuatiwa na Ruvuma 374 (25.8%), Rukwa 276 (19.1%), Iringa 88 (6.1%),
Morogoro 56 (3.9%), Songwe 37 (2.6%), Kigoma 25 (1.7%) na Manyara 9 (0.6%).
Kwa
mwezi Machi 2018, jumla ya wagonjwa 87 bila kifo wametolewa taarifa, ambapo ni
pungufu kubwa sawa na asilimia 91.3% ukilinganisha na mwezi Februari 2018
ambapo kulikuwa na jumla ya wagonjwa 996 na vifo 18. Kwa mwezi Machi mikoa na
halmashauri ambazo zimeendelea kutoa taarifa ya ugonjwa wa Kipindupindu nchini
ni Dodoma (Mpwapwa-35, Chamwino-15, Dodoma
Mjini-6, Kongwa-5), Ruvuma (Nyasa-18,
Mbinga-5), Rukwa (Sumbawanga Vijijini-5), na Iringa (Kilolo-2).
Ukilinganisha
idadi ya wagonjwa waliotolewa taarifa mwezi Februari na ule wa mwezi Machi,
mikoa imeweza kufanikiwa kudhibiti ugonjwa huu kwa kiasi kikubwa. Mfano mkoa wa
Morogoro umefanikiwa kudhibiti kikamilifu kutoka wagonjwa 56 mwezi Februari na
kutokuwa na wagonjwa wowote mwezi Machi. Mikoa mingine iliyofanikiwa kupunguza
idadi ya wagonjwa kwa sehemu kubwa katika kipindi cha mwezi mmoja ni Iringa
(punguzo la asilimia 97.7%), Rukwa (punguzo la asilimia 96.1%) na Ruvuma (punguzo la asilimia 92.7%). Mkoa wa Dodoma pia umefanikiwa
kupunguza idadi ya wagonjwa kwa takribani asilimia 83% katika kipindi cha mwezi
mmoja.
Wizara
inatoa pongezi kwa Mikoa kwa jitihada mbalimbali walizozichukuwa kudhibiti
ugonjwa huo ambayo imepelekea kupunguza kwa sehemu kubwa kuenea kwa ugonjwa huu
katika kipindi cha mwezi wa Machi.
Ndugu
Wanahabari,
Ingawa
takwimu hizi zinaonyesha kuwa ugonjwa umepungua, bado uwezekano wa kuenea kwa
ugonjwa wa Kipindupindu na kupata maambukizi mapya ni tishio hata kama ni
Halmashauri moja tu itakuwa na wagonjwa wa Kipindupindu. Tishio hili
inaongezeka katika msimu huu wa mvua ambapo inaweza kuongeza kasi ya kuenea kwa
maambukizi ya Kipindupindu. Hivyo tunahitaji kuzidisha juhudi za kuzuia ugonjwa
huu, kwa kusimamia kikamilifu maelekezo na miongozo stahiki inayotolewa.
Ni
dhahiri kuwa ushirikishwaji wa sekta zote kwa ngazi mbalimbali na jamii kwa ujumla
ni muhimu sana
katika kukabiliana na ugonjwa wa Kipindupindu. Wizara inasisitiza kuwa
wadau wote wapewe nafasi katika mapambano haya kupitia vikao mbalimbali za
kujadili udhibiti wa ugonjwa wa Kipindupindu kwenye Halmashauri na Mikoa.
Viongozi wa dini, watu mashuhuri na waganga wa tiba mbadala pia wasaidie
kuhamasisha jamii zao kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huu.
Ndugu
Wanahabari,
Wizara
inaendelea kuwasihi wananchi kuungana na Halmashauri, Mikoa, hasa iliyotoa
taarifa kipindi cha Januari hadi Machi, pamoja na Wizara katika juhudi za
kupambana na kuenea kwa ugonjwa wa Kipindupindu. Jamii izingatie kanuni
za usafi binafsi na usafi wa mazingira, ikiwa ni pamoja na:
1.
Kujenga
na kutumia vyoo bora katika maeneo tunayoishi.
2.
Kunawa
mikono kwa maji yanayotiririka na sabuni kabla ya kula,
baada ya kutumia choo,
na baada ya kumsafisha mtoto aliyejisaidia.
3.
Kunywa
maji safi na salama yaliyotakaswa kwa dawa (kama vile water guard) au
yaliyochemshwa na kupoa.
4.
Kuzingatia
ushauri na elimu sahihi kuhusu ugonjwa wa Kipindupindu, ili jamii iondokane na
imani potofu kuhusu Kipindupindu.
5.
Kufikisha
wagonjwa wa Kipindupindu mapema katika vituo vya kutolea huduma ili wawahi
kupata matibabu.
6.
Kutotiririsha
maji taka ovyo
Vile
vile, Wizara inasisitiza yafuatayo yasimamiwe kwenye Halmashauri na Mikoa yote
nchini,
1.
Utoaji
wa taarifa sahihi za ugonjwa wa Kipindupindu na kwa wakati kwa kufuata miongozo
iliyopo.
2.
Usimamizi
wa utekelezaji wa miongozo katika kuzuia na kudhibiti ugonjwa ni pamoja na;
- Usimamizi wa utekelezaji wa sheria ndogondodo za usafi wa mazingira ili kuimarisha matumizi ya vyoo.
- Usafi wa mazingira pamoja na udhibiti wa biashara za chakula na pombe za kienyeji katika mitaa.
- Kuzingatia agizo la Mheshimiwa Rais la kufanya usafi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi.
1.
Kuimarisha
mifumo ya upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo yote mijini na
vijijini hasa wakati wa mlipuko wa Kipindupindu. Hii ni pamoja na:
- Mamlaka za maji katika ngazi zote ziweke mkazo wa kuwepo kwa vyanzo mbadala vya maji.
- Utakasaji wa maji ya bomba kwa njia ya kutumia klorini ufanyike kama miongozo inavyotaka na ufuatiliaji wa ubora wa maji ufanyike kulingana na miongozo.
Hitimisho
Wizara
kwa ukaribu itaendelea kufuatilia mwenendo wa ugonjwa wa Kipindupindu nchi
nzima. Aidha, Wizara inawashukuru wadau wote wa sekta mbalimbali, wataalamu na
watumishi, waandishi wa habari na wananchi kwa michango yao mbalimbali katika
mapambano dhidi ya ugonjwa wa Kipindupindu nchini.
Asanteni
sana
No comments:
Post a Comment