Monday, April 30, 2018

BAGAMOYO YAZINDUA CHANJO YA SARATANI YA MLANGO WA KIZAZI.

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga akiandaa sindano kwaajili ya uzinduzi wa chanjo ya Saratani ya Mlango wa kizazi kwa wasichana wenye umri wa miaka 14.
   
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga akizungumza kabla ya kuzindua chanjo ya Saratani ya Mlango wa kizazi kwa wasichana wenye umri wa miaka 14.
.......................................
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga amesema mtu atakaekwamisha zoezi la chanjo ya Saratani ya shingo ya Kizazi atachukuliwa hatua za kisheria.

Mkuu huyo wa wilaya ametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti katika Halmashauri za Bagamoyo na Chalinze wakati wa uzinduzi wa chanjo ya Saratani ya mlango wa kizazi.

Alisema serikali inapanga mikakti ya kuboresha Afya za wananchi wake ili waweze kutumikia taifa pamoja na kuihudumia wenyewe na familia zao.

Aliongeza kuwa, Bagamoyo ina mikakati ya kukuza uchumi kwa kujenga viwanda hivyo ni wazi kuwa wanaotakiwa kufanya kazi katika viwanda hivyo ni watu wenye afya nzuri isoyokuwa na mgogoro.

Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekuwa ikitoa chanjo za magonjwa mbalimbali lengo likiwa ni kuhakikisha afya za wananchi zinakuwa salama.

Katika hatua nyingine mkuu huyo wa wilaya ameigiza Halmashauri ya Chalinze kuangalia madeni ya madaktari na kuwalipa ili kuwaondolea manung'uniko ambayo yanaweza kuzorotesha utendaji kazi wao.

Alisema yapo malalamiko kwa madaktari ambao hawalipwi fedha za kuitwa kazini kwa matukio ya dharula nje ya muda wa kazi (On-call Allowance) ambayo ni haki yao kimsingi.

Ameitaka Halmshauri ya Chalinze kufanya haraka kuwalipa madaktari On-call Allowance ili waweze kuwa na moyo wa kufanya kazi muda wowote wanapohitajika.

Alisema Serikali imetenga bajeti kubwa katika wizara ya Afya ili kuboresha huduma za afya hivyo Halmashauri nazo zinapaswa kuongeza bajeti zake katika sekta ya afya ili kuwajengea mazingira rafiki madaktari na watumishi wa afya kwa ujumla. 

Aidha, alimtaka Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Chalinze Dkt. Rahim Hangai kuchukua hatua za dhati kuhakikisha zahanati ambazo hazina madaktari anapeleka madaktari ili kuwasogezea wananchi huduma za afya ambazo kwa sasa wanatembea umbali mrefu licha ya kuwepo zahanati kwenye maeneo yao.

Awali wakichangia mada katika semina elekezi iliyofanyika shule ya Kikaro Halmashauri ya Chalinze washiriki wa semina hiyo walisema wananchi wanakabiliwa na changamoto ya kufuata huduma za afya mbali na maeneo yao hali inayopelekea kushindwa kuwapatia watoto wao chanjo.

Walisema vipo baadhi ya vijiji mwananchi analazimika kutumia shilingi elfu nane ili kumpeleka mtoto akapate chanjo.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Chalinze Dkt. Rahim Hangai alisema atahakikisha anayafanyia kazi maelekezo ya Mkuu wa wilaya ili kukidhi mahitaji ya wananchi katika maeneo ambayo tayari kuna Zahanati lakini hakuna Daktari.

Alisema tatizo la upungufu wa madaktari katika Halmashauri hiyo limetokana na watumishi walioondolewa kutokana na kuwa na vyeti feki hivyo idara ya afya katika Halmashauri hiyo ni miongoni mwa wathirika ambapo mpaka sasa wanasubiri watumishi wengine watakaopangiwa na wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. (TAMISEMI) ili kuziba mapengo hayo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashuri ya Chalinze Saidi Zikatimu alisema ataiongoza Halmashauri hiyo katika kuhakikisha inatekeleza majukumu yake kwa watumishi ili nao wafanye kazi kwa moyo na bidii.

Alisema ni kweli serikali imetenga fedha kwaajili kuboresha sekta ya afya ambapo Halmashauri ya Chalinze imepoke zaidi ya shilingi milioni 440 kwaajili ya kuboresha huduma katika vituo vya afya na Zahanati na milioni 400 kwaajili ya kituo cha afya ambapo ujenzi wake unaendelea.

Chanjo ya Saratani ya mlango wa kizazi imezinduliwa rasmi hii leo jumatatu ya tarehe 30 Aprili katika Halmashauri za Bagamoyo na Chalinze ambapo walengwa ni wasichana wenye umri wa miaka 14.
 
 Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga akivaa koti la udaktari ikiwa ni maandalizi ya kuzindua chanjo ya Saratani ya Mlango wa kizazi kwa wasichana wenye umri wa miaka 14.

Watumishi wa halmashuri ya Chalinze wakifutilia kinachoendelea kwenye semina elekezi kuhusu chnjo ya mlango wa kizazi kwa wasichana iliyofanyika shule ya Kikaro kata ya Miono.
 Mwenyekiti wa Halmashuri ya Chalinze Saidi Zikatimu akizungumza katika semina hiyo.
 Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Chalinze Dkt. Rahim Hangai akitoa maelekezo kwa washiriki.



Washiriki wa semina hiyo wakifuatilia maelezo yanayotolewa.

Muwezeshaji akitoa semina kwa washiriki.
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Alhaj, Majid Mwanga akiwa na viongozi wa dini katika picha ya pamoja.


 Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Alhaj, Majid Mwanga akiwa na maafisa tarafa pamoa na viongozi wengine waandamizi katika picha ya pamoja.

WATATU WAFA NA 530 WAKUTWA NA DALILI ZA SARATANI YA MLANGO WA KIZAZI PWANI

Mganga mkuu wa Mkoa wa Pwani ,Yudas Ndungile akitoa chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi kwa mmoja wa wanafunzi, wakati wa uzinduzi wa zoezi ya chanjo hiyo kwa watoto wenye umri wa miaka 14 ,kimkoa yaliyofanyika kituo cha afya mkoani,Kibaha.
..........................

Na Mwamvua Mwinyi,Pwani

JUMLA ya akinamama 20,815 waliofanyiwa uchunguzi wa saratani ya mlango wa shingo ya kizazi mkoani Pwani katika kipindi cha miaka mitatu kati yao 530 walikutwa na dalili za awali za saratani hiyo,ambapo watatu walifariki.

Aidha kati ya akinamama hao waliofanyiwa uchunguzi akinamama 412 walitibiwa matibabu na  115 walipata rufaa ya kwenda Oceanroad na hospitali ya Taifa ya Muhimbili  kwa matibabu zaidi.

Akitoa takwimu hizo ,wakati wa uzinduzi wa zoezi la chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa shingo ya kizazi kwa watoto wenye umri wa miaka 14 ,kimkoa yaliyofanyika kituo cha afya mkoani,Kibaha,mganga mkuu wa Mkoa wa Pwani ,Yudas Ndungile alisema , ipo changamoto ya kutojua idadi ya vifo kamili kwa kuwa wengi hupata rufaa.

Pamoja na hayo ,alisema ipo haja ya kuona ukubwa wa tatizo hilo kwa kuangalia afya mapema na watoto wa mashuleni kupata chanjo.
Ndungile alisema jumla ya watoto wa kike 18,823 waliopo shule na nje ya shule mkoani hapo watapatiwa chanjo ya kukinga saratani ya mlango wa kizazi mwaka huu.

Alielezea, tayari wameshapokea chanjo na wataanza kuzitoa katika vituo mbalimbali vya huduma.

Ndungile aliitoa shaka jamii kuwa chanjo ya kukinga saratani ya mlango wa kizazi ni salama ,haina madhara na haiathiri uwezo wa binti kupata watoto hapo baadae
” Serikali imethibitisha usalama wa umadhubuti wa chanjo ya kukinga saratani ya mlango wa kizazi ndiyo maana imeiongeza kwenye mpango wa Taifa wa chanjo ili iweze kusaidia kudhibiti tatizo hilo kwa akinamama”:!
Ndungile alieleza mwaka 2018 chanjo itatolewa kwa wasichana waliofikisha umri wa miaka 14 na ili kupata kinga kamili walengwa watahitaji kupatiwa dozi mbili.

Alisisitiza chanjo hiyo huwakinga wasichana wasipate saratani ya mlango wa kizazi pindi wawapo watu wazima wakiwa na familia zao.

“Nchini Tanzania saratani ya mlango wa kizazi ni ya kwanza kwa vifo ikifuatiwa na saratani ya matiti ” Saratani hizi mbili kwa pamoja husababisha zaidi ya asilimia 50 ya vifo vyote vya wakinamama vitokanavyo na saratani”alibainisha Ndungile.

Kwa upande wake ,Mganga mkuu wa halmashauri ya Mji wa Kibaha ,Dkt.Tulitweni Mwinuka alisema ,wamezindua chanjo hiyo kwa wasichana wenye umri wa miaka 14.

Alielezea ,kiwilaya wamezindua chanjo hiyo kwa wasichana 100 kituoni hapo na wanatarajia kufanikisha na kuleta matokeo kutokana na chanjo hiyo .
Akizindua zoezi hilo ,kwa niaba ya mkuu wa Mkoa wa Pwani,mkuu wa wilaya ya Kibaha Assumpter Mshama aliwataka wanafunzi wa kike kuacha kujiiingiza kwenye vitendo vya ngono mapema ili kujiepusha kuingia kwenye hatari ya kupata magonjwa ya zinaa,ukimwi na hata saratani ya mlango wa kizazi.

Alisema moja ya sababu zinazosababisha saratani hiyo ni kuwa na wanaume wengi ,kuvuta sigara ,wenye mitala, na kuanza mapema kufanya ngono.
“Acheni kujiingiza kwenye mapenzi mapema ni hatari katika maisha yenu, ukivua sketi ,na mwanaume akavua suruali jua kuna hatari ya kuhatarisha maisha yako kwa magonjwa yanayosababishwa kutokana na ngono”
“Jizuieni hadi hapo mtakapoolewa ,msikimbilie ngono za haraka,mtapata saratani”: alisisitiza Mshama.

Mshama aliwahimiza wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao wa kike wenye umri wa miaka 14 kupata chanjo hiyo kwani haina madhara.

TEDDY MALKIA WA NGUVU 2018.

Malkia wa nguvu 2018 Teddy Davis kutoka Bagamoyo akionyesha tuzo yake ya Malkia wa nguvu katika Ukumbi wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo, TaSUBa.
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga akizungumza wakati wa hafla za kumtangaza Malkia wa nguvu 2018 iliyofanyika Ukumbi wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo, TaSUBa.
........................................
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga amewataka wanawake kushirikiana ili kujiletea maendeleo kupitia vikundi vya ujasiliamali.

Majid aliyasema hayo wakati wa sherehe za kumtangaza Malkia wa Nguvu 2018 Teddy Davis  ambae ametoka wilayani Bagamoyo.

Alisema ushindi  wa Teddy kuwa Malkia wa nguvu ni wazi kuwa wanawake wakifanya juhudi wananweza kufanikiwa hivyo ni vyema wakawa na ushirikiano ili kuonyeshana njia.

Aliongeza kwa kusema kuwa, Halmashauri za Bagamoyo na Chalinze zinatenga asilimia tano kwa wanawake na vijana ili waweze kujikwamua kiuchumi kupitia vikundi vyao.

Aidha, Mkuu huyo wa wilaya alisema Serikali ya wilaya Bagamoyo itashirikiana na wanawake wote wilayani humo wenye kuonyesha nia ya kujikwamua kiuchumi kwa kujishughulisha na mambo mbalimbali ya uzalishai mali kupitia vikundi vyao.

Nae katibu Mwenezi wa CCM wilaya ya Bagamoyo, John Francis (Bolizozo) alisema wanawake wanapaswa kuiwekea malengo ya maendeleo kwakuwa wao ndio dira ya familia.

Alisema kuna baadhi ya wanawake waba tabia ya kujiuza miili yao hivyo aliwataka kuacha tabia hiyo na badala yake wafanye shughuli zitakazowaingizia kipato kwa njia ya halali.

Aliongeza kwa kusema kuwa ili mwanamke awe na thamani katika jamii na kuweza kupata msaada wa kitaalamu anapaswa kwanza kujiheshimu yeye mwenyewe na kujitambua thamani yake.

Bolizozo alikemea tabia ya wanawake wanaovaa mavazi ya kujidhalilisha pamoja vijana wakiume ambao huiga tamaduni zisizo na maadili.

Alimpongeza Teddy pamoa na ukwaa zima la uwezeshai wanawake Bagamoyo kwa kuikita katika shughuli za kujiletea maendeleo na kuongeza kuwa hayo ndio matunda ya CCM.

Kwa upande wake Mshindi wa Malkia wa Nguvu 2018 Teddy Davis alisema anaishukuru serikali ya wilaya ya Bagamoyo kwa kumuunga mkono yeye na wanawake wenzie katika shughuli za uasiliamali.

Teddy ambae ni Mwenyekiti wa Jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi wilayani Bagamoyo aliwashukuru watu wote waliompigia kura ili kupata nafasi hiyo ambayo hakuitarajia.

Jukwaa analoliongoza la uwezeshaji wanawake kiuchumi ni agizo la makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la kuundwa kwa Majukwaa hayo nchi nzima ili wanawake wapate fursa za kujiajiri na kujiwezesha kiuchumi.

Teddy ni mjasiliamali anaejishghulisha na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zitokanazo na Lozela huku akiwaonyesha wanawake wenzie fursa za kujikwamua kiuchumi kupitia bidhaa za kutengeneza kwa mikono na ubunifu wa aina mbalimbali.

Akizungumzia namna ya mchakato wa kumpata Malkia wa nguvu, Muwakilishi kutoka Clouds Media Group, Amani Maltin ambao ndio waandaai wa shindano la Malkia wa nguvu alisema kura zimepigwa kutoka kwa wasikilizaji wa Clouds fm na Clouds tv ambapo majina ya washiriki yalitoka nchi nzima.

Maltin Alisema miongoni mwa sifa za kumpata Malkia wa nguvu ni pamoja na kujishughulisha kwake na mambo ya kimaendeleo yeye wenyewe pamoja na kushirikiana na wanawake wenzie sehemu anayoishi na ni kwa jinsi gani anakubalika katika jamii.
 
 Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga pamoa na kamati ya ulinzi na Usalama wakipiga makofi kumkaribisha Malkia wa nguvu wakati akiingia ukumbini.

 Mshindi wa Malkia wa Nguvu 2018 Teddy Davis akiingia Ukumbini.
 

 Mshindi wa Malkia wa Nguvu 2018 Teddy Davis akizungumza katika sherehe hizo.
 
Diwani wa Kata ya Dunda, Dckson Makamba akimkaribisha Mgeni rasmi Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo ili kuzungumza katika sherehe hiyo.

 Katibu Mwenezi wa CCM wilaya ya Bagamoyo, John Francis (Bolizozo) akizungumza katika sherehe hiyo.
 Mshindi wa Malkia wa Nguvu 2018 Teddy Davis akikata keki katika sherehe hizo.
 Mshindi wa Malkia wa Nguvu 2018 Teddy Davis akimlisha keki mama yake mzazi, kulia na kushoto ni watoto wake.
 Katibu Mwenezi wa CCM wilaya ya Bagamoyo, John Francis (Bolizozo)kimlisha keki Malkia wa nguvu 2018, Teddy Davis.
 
 
Malkia wa nguvu 2018, Teddy Davis, akimkabidhi zawadi ya kanzu kofia na tasbih Mgeni rasmi Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga.
 
Picha ya pamoja Mgeni rasmi, Malkia wanguvu, Kamati ya ulinzi na usalama na viongozi wengine waandamizi pamoja na watoto wa Malkia wa nguvu waliochuchumaa chini na Katibu mwenezi wa CCM wilaya Bolizozo.

MAGAZETI YA LEO 30 APRIL 2018.

RAIS MHE. DKT. MAGUFULI AFUNGUA BARABARA YA IRINGA-DODOMA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Mwakilishi wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB Jeremy Aguma wa pili kutoka kulia  wakivuta utepe kwenye jiwe la msingi kuashiria ufunguzi wa Barabara ya Iringa-Dodoma katika sehemu ya Iringa-Migori-Fufu Km 189 iliyokamilika kujengwa katika kiwango cha lami. Sherehe hizo za ufunguzi zilifanyika katika kijiji cha Ndolela kilichopo Isimani nje kidogo ya mji wa Iringa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Mwakilishi wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB Jeremy Aguma, Balozi wa Japan Masaharu Yoshida wakikata utepe kuashiria ufunguzi wa Barabara ya Iringa-Dodoma katika sehemu ya Iringa-Migori-Fufu Km 189 iliyokamilika kujengwa katika kiwango cha lami. Wengine katika picha ni Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Waziri wa Ujenzi Profesa Makame Mbarawa , Spika wa Bunge Job Ndugai pamoja na viongozi wengine wa Serikali na wageni kutoka nje ya nchi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi katika sherehe za ufunguzi wa Barabara ya Iringa-Dodoma katika sehemu ya Iringa-Migori-Fufu Km 189 iliyokamilika kujengwa katika kiwango cha lami.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili Isimani Mkoani Iringa.
Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli akiwa jukwaa kuu pamoja na Balozi wa Japan Masaharu Yoshida, Waziri wa Ardhi Wiliam Lukuvi, pamoja na Waziri wa Mambo ya nje Balozi Dkt. Augustine Mahiga wakifatilia sherehe za ufunguzi wa barabara ya ya Iringa-Dodoma katika sehemu ya Iringa-Migori-Fufu Km 189 iliyokamilika kujengwa katika kiwango cha lami.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi wa Iringa mjini waliofika kumpokea mara baada ya kuwasili akitokea Isimani mkoani Iringa.


PICHA NA IKULU