ASKOFU MKUU TAG ACHANGIA MIL 10 UJENZI KANISA LA KCC
ASKOFU MKUU TAG ACHANGIA MIL 10 UJENZI KANISA LA KCC Na Allan Kitwe, Tabora ASKOFU Mkuu wa Kanisa la TAG Dkt Barnabas Mtokambali amechangia kiasi cha shilingi milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa la Kitete Christian Centre (KCC) la Mjini Tabora ambalo ni Makao Makuu ya Jimbo jipya la Tabora Kati. Askofu Mkuu ameahidi kutoa mchango huo kwenye ibada maalumu ya uzinduzi wa Jimbo jipya la Tabora Kati lililopo Mjini Tabora baada ya kufurahishwa na kazi nzuri ya ujenzi wa kanisa hilo la kisasa linalojengwa na Kanisa la KCC. Ameeleza kuwa kanisa linalojengwa kwenye Makao Makuu hayo ya Jimbo jipya ni la kiwango cha juu, linavutia sana, hivyo akaahidi kuwaunga mkono ili kufanikisha maono hayo ya kujengwa kanisa la kisasa ambalo sasa limefikia asilimia 70. Dkt Mtokambali amebainisha kuwa jengo hilo litaleta heshima kwa TAG na kuheshimisha Makao Makuu wa Jimbo ambayo yamezinduliwa rasmi katika ibada hiyo iliyohudhuriwa na Viongozi wa serikali, Maaskofu, wachungaji na waumini. ...